Anasomea Uundaji Wa Kompyuta Je Halaal Kazi Hii Ikiwa Watu Wanatumia Kwa Maasi?

SWALI:

 

"ASSALAAMU ALEYKUM WARAHMATUL LAHI WABARAKATUH"

 

Sheikh nawashukuru sana kwa nasaha yenu mliotunasihi kuhusu vijana kusomea kazi zinazo kubaliwa na dini.

 

Mimi huu ndio mwaka wangu wa kwanza college na ninasomea kazi ya kutengeneza/ kujenga upya computer {technology} na kama unavyojua sheikh hichi chombo kina maasi mengi na faida nyingi pia. Je sheikh watu wakija kuitupia kutafutia maasi na balaa nyenginezo na mimi huwa nipo ndani au?

 

NAWATAKIA KILLA LA KHERI. ASSALAAMU ALEIKUM


  

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu uundaji wa Kompyuta. Hakika hili ni somo zuri katika wakati wetu wa sasa na tunahitaji Waislamu wema wajifunze na wafikie daraja ya umahiri katika ufundi huo. Hakuna tatizo lolote kwako kusomea somo hilo na baadaye kufanya kazi kwani kazi yenyewe ni halali katika Uislamu.

 

Pia ufahamu kuwa si lazima umuulize mwenye kutaka kutengeneza kompyuta yake atataka kuitumia vipi. Hiyo ni yake na Mola wake Mlezi, hata hivyo ikiwa unamjua mtu yule si mwema na ataitumia vibaya kwa ushahidi wa wazi basi hapo unatakiwa ukatae kumtengenezea chombo chake hicho.

 

Mfano huu ni kama wa muuzaji kisu. Kisu kina manufaa na madhara lakini wewe hulazimiki kumuuliza mnunuaji atatumia vipi kisu hicho. Hata hivyo, ukimjua kuwa mtu mwenyewe ni jambazi na anatumia silaha kuua watu hutomuuzia kisu hicho.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share