031-Aayah Na Mafunzo: Mkiwa Mnampenda Allaah Basi Mfuateni Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Mkiwa Mnampenda Allaah Basi Mfuateni Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): 

www.alhidaaya.com

 

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

31. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

 

Mafunzo:

 

Aayah hii tukufu inathibitisha kuwa mapenzi ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hayawezi kutimia isipokuwa kwa kufuta Sunnah zake. Ni hoja ya wazi pia kwa wanaodai kuwa wanampenda Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) lakini wakawa wanafanya bid’ah katika Dini kama kusoma Mawlid, Khitmah, Talqiyn, mikusanyiko ya kuomba Du’aa, kusheherekea maadhimisho na kumbukumbu za miaka, kusherehekea siku wanazosherehekea   wasiokuwa Waislamu, na yote mengineyo yasiyokuwemo katika Shariy’ah. Yeye mwenyewe Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameonya katika Hadiyth aliyosimulia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba: “Atakayetenda ‘amali isiyokuwa yetu (katika Dini yetu) basi itarudishwa.” [Al-Bukhaariy]

 

 

Na katika Hadiyth iliyopokelewa na ‘Abdu-Rahmaan bin Quraad (رضي الله عنه) kuwa “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa anatawadha, na Swahaba wakaanza kukinga maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka katika wudhuu wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), wakijifutia katika miili yao kutafuta baraka za wudhuu ule wa Nabiy.  Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akawauliza: “Kwa nini mnafanya hivi?” Wakasema; ni kwa ajili ya kumpenda Allaah na Rasuli Wake. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaambia: “Anayetaka kumpenda Allaah na Rasuli Wake, au kupendwa na Allaah na Rasuli Wake, basi aseme ukweli anapozungumza, na atekeleze amana yake anapoaminiwa, na awe jirani mwema kwa jirani yake.” [Mishkaatul Maswaabiyh – Imaam Al-Albaaniy]

 

Share