092-Aayah Na Mafunzo: Mapendekezo Ya Kutoa Swadaqah Kitu Kilicho Kizuri

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Mapendekezo Ya Kutoa Swadaqah Kitu Kilicho Kizuri Na Mfano Wa Utoaji Wa Swahaba

Alhidaaya.com

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾

92. Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho ni Mjuzi.

 

Mafunzo:

 

 

Mapendekezo ya kutoa katika swadaqah kilicho kizuri, si kutoa kiichokuwa kibovu au kisichokuwa na thamani.  Anas bin Maalik (رضي الله عنه) kwamba: Abuu Twalhah alikuwa na mali kuliko yeyote miongoni mwa Answaar wa Madiynah na kilichokuwa kipenzi kabisa katika mali yake ni bustani ya Bayruhaa ambayo ilikuwa mbele ya Masjid Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Mara nyingine Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akienda katika bustani hiyo na kunywa maji yake baridi. Anas akaongeza kusema: Aayah hii ilipoteremka:

 

لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ

“Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda…” Abu Twalhah akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Allaah Anasema:

 

لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ

“Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda.” Na hakika bustani ya Bayruhaa ni kipenzi katika mali zangu. Kwa hiyo nataka kuitoa swadaqah kwa ajili ya Allaah nikitaraji wema wake na thawabu zake na malimbikizo kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Basi ee Rasuli wa Allaah! Itumie popote Anapokuonyesha Allaah kuwa ni bora kuitumia. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Umefanya vizuri, Ni mali yenye faida, ni mali yenye faida. Nimesikia ulivyosema na nafikiri itakuwa ni bora kuwapa walio karibu yako (jamaa zako).”  Abuu Twalhah akasema: Nitafanya hivyo ee Rasuli wa Allaah. Abuu Twalhah akagawa kwa jamaa zake na watoto wa ‘ammi yake. [Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad].

 

Share