Kuishi Nchi Za Kikafiri: Hukmu Yake

 

 

SWALI:

 ASSALAAM ALAYKUM.

Suala langu hili ni kwa sheikh ABDULLAH ALY MUHSIN ambaye ametupa mawaidha juu ya mada ya hapo juu. (Kuhusu hukmu ya kuishi nchi za kikafiri) na Masheikh wengineo kwa ujumla. SUALA; 

WANGAPI KATI YA WAISLAM WALIOKO NDANI YA MIJI YA KIISLAM HAWAFATI AMRI ZA MWENYEZIMUNGU (WAMEKUFURU) NA WANGAPI KATIKA MIJI YA KIKAFIRI WANAFATA AMRI ZA MWENYEZIMUNGU. NA WANGAPI WANAOISHI  KATIKA MIJI YA KIISLAM NDIO WAKUMBATIAJI WAKUBWA WAMAKAFIRI, NA WANGAPI WANAOISHI  KATIKA MIJI YA KIKAFIRI NDIO WAPIGANIAJI WA UISLAM  SIULIZII IDADA YA WATU ILA NAULIZIA UWEZEKANO (WAMEJENGA MISKITI, MADRASA, WAMEWEZA HATA KUWAVUTIA MAKAFIRI KATIKA UISLAM KWA MWENENDO WAO NA WAMEANZISHA UTAMADUNI WA KIISLAM NDANI YA MIJI YA  KIKAFIRI. WAISLAM KUISHI KATIKA MIJI YA KIKAFIRI NI NJIA MOJA YA KUUENEZA UISLAM WALA SIO KUWAKUMBATIA MAKAFIRI AU UKAFIRI. AMA SIVYO? (WAMEANZISHA NA KUUKUZA UISLAM NDANI YA MIJI YA KIKAFIRI. INSHAALLAAH MUNGU AUPE NGUVU UISLAAM NDANI YA MIJI YA KIKAFIRI KWA NJIA HII AU NYENGINE. "ALLAAHU A`LAM. WAISLAM WANAOISHI KATIKA MIJI YA KIISLAAM WAKAWA WANAENDESHEWA AU WANAENDESHA MAMBO YAO KWA MUJIBU WATAKAVYO MAKAFIRI AU KUWAHUSISHA MAKAFIRI KATIKA MAMBO YAO NDIKO KUWAKUMBATIA MAKAFIRI UA UKAFIRI. AMA SIVYO? ZAIDI. NINGEPENDA NIFAFANULIWE AYA YA QUR`AAN SURA YA 66 AYA YA 9 NA 10 (A`TTAHRIIM) NA KISA CHA UTOTO WA NABII MUSA (A.S.).

ASSALAAM ALAYKUM WARAHMATULLAHI WA BARAKAATUHU.

 

JIBU:Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa maelezo mazuri ya uhakika na yenye ukweli unaofahamika na wengi miongoni mwetu. Hii ndio hali halisi ya mambo na hakika isiyopingika ni kuwa nchi za Waislamu zimezorota kwa kiwango kikubwa hata zimeshinda nchi za ukafiri kwa unyanyasaji wa Uislamu na Waislamu. Tunisia ni nchi moja ambayo kwa zaidi ya miaka 40 sasa imekuwa ikiwafunga Waislamu wenye kutaka Uislamu uhukumu maisha yao hapa duniani. Wengi wao wamekaa gerezani kwa muda mrefu na upo wakati katika miaka ya themanini ambamo zaidi ya Waislamu 30,000 walikuwa ndani. Morocco, Misri, Libya, Algeria, na Jordan nazo hali kadhalika.

 

Pia kupigwa marufuku kwa wanawake kuvaa hijabu na nguo za sitara. Na kanuni mpya ni kuwa anayeonekana barabarani amevaa vazi hilo basi polisi wana haki ya kumvua kwa nguvu na kumtilisha saini katika waraka wa kuahidi kuwa hatafanya tena hivyo. Uturuki nayo ni dola nyingine ambayo imepiga marufuku uvaaji huo wa hijabu katika shule za serikali na maofisi pia. Pakistan nayo tumeona inavyoendeshwa na makafiri na kutii yote yale yenye malengo ya kuumaliza Uislam kama kufunga Madrasah na kuzuia wanafunzi kutoka nje kusoma Dini huko!

 

Ukitazama Iraaq na Afghanistan zimefikia hali hiyo ya kutekwa na kutawaliwa na wasiokuwa Waislamu kwa sababu ya majirani zao Waislamu ambao wameshirikiana na kuwasaidia makafiri kutoka mbali kabisa kuvamia! Pamoja na wanafiki waliojaa katika nchi hizo ambao wako tayari kuuza Dini yao kwa thamani ndogo kabisa za kidunia. Inna Lillaahi wa Inna Ilayhi Raaji’uun.

 

Tukirudi katika ufafanuzi wa ayah ya 9 hadi 10 katika Suratut Tahriym (66) Insha Allaah tutajaribu kutazama Mufassirina tofauti na kauli zao kuhusu ayah hizo. Na kwa Allaah ndio tunaelekea na kutaka usaidizi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema katika ayah hizo: “Ewe Nabii! Pambana (pigana Jihadi) na makafiri na wanafiki, na kuwa mgumu kwao! Na makazi yao ni Jahanamu. Na hayo ni marejeo mabaya. Allaah Amewapigia mfano waliokufuru: mke wa Nuuh na mke wa Luut. Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini wakawakhini waume zao, nao wasiwafae kitu. Na ikasemwa: Ingieni Motoni pamoja na wanaoingia!

 

1.    Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhiym ya Ibn Kathiyr, Mjalada wa 4: Allaah Aliyetukuka Anamuaru Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) apigane Jihadi dhidi ya makafiri na wanafiki. Hao wa awali (makafiri) ni kwa kutumia silaha na hao wa pili kwa kuanzisha juu yao sheria ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Na kauli: “Na uwe mgumu/ mkali kwao”, yaani katika maisha haya.

 

Allaah Amepiga mfano wa wale waliokufuru”. Hii ina maana ya wale makafiri walioishi hapa duniani na Waislamu, kwa kutangamana nao haitawasaidia makafiri, wala haitawafalia chochote mbele ya Allaah, mpaka mioyo yao itakapo jawa na Imani. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amepiga mfano, “Mkewe Nuuh na mkewe Luut, walikuwa chini ya waja wetu wema wawili”.

Hii inamaanisha hao walikuwa masahibu zao mchana na usiku, wakila na kulala nao, kama maingiliano ya ndoa yoyote baina ya wanandoa. Hata hivyo, “Wote waliwafanyia khiyana”, kumaanisha katika Imani, kwa kuwa wao hawakufuata Imani iliyoletwa kwa waume zao wala hawakukubali risala zao. Hivyo, ilimu nyeti na muhimu hazikuwafaidisha wala kuwazuia na adhabu. Kwa hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Waume zao hao hakuweza kuwasaidia chochote mbele ya Allaah”. Hii ina maana kuwa wake zao walikuwa makafiri. “Pakasemwa”, kwa hao wake wawili, “Uingieni moto pamoja na hao wanaouingia”.

 

Sehemu ya ayah hiyo inasema: “Wote waliwafanyia khiyana”, hii haina maana ya kuwa walizini, bali ni kukataa kuikubali Dini. Hakika ni kuwa wake za Mitume wote walikingwa kuzini kwa ile heshima ambayo Allaah Aliyetukuka Aliwapatia Mitume Yake. Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhuma) anasema: “Waliwafanyia khiyana kwa kutofuata Dini.

Mke wa Nabii Nuuh alikuwa akitoa siri za mumewe kwa kuwajulisha watu wake madhalimu pindi anaposilimu mtu kwa Nabii Nuuh.

 

Ama kuhusu mkewe Luut alikuwa akiwajulisha watu wa mji wa Sodom, waliokuwa wakitenda kitendo kiovu cha liwati, pindi mgeni alipokuwa akikirimiwa na mumewe”. Adh-Dhwahhaak amehadithia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhuma) aliyesema: “Hakuna mke wa Mtume yeyote aliyezini”. Hiyo ndiyo iliyokuwa kauli ya Ikrimah, Sa‘iyd bin Jubayr, adh-Dhwahhaak na wengineo.

 

2.    Taysiir Al-Kariim Ar-Rahmaan Fiy Tafsiyr Kalaam Al-Mannaan cha Shaykh ‘Abdur-Rahman Naaswir As-Sa‘diy, ukurasa 874: Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anamuamuru Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) apigane jihadi dhidi ya makafiri na wanafiki na awe mgumu kwao katika hilo. Hii imekamilika kwa kupambana nao kwa kuwasimamishia hoja na kwa kuwalingania kwa mawaidha mazuri. Pia kuvunja kila aina ya upotevu na kupigana nao kwa silaha kwa anayekataa kukubali ulinganizi wa Allaah na kufuata hukumu Zake. Huyu anapigana nao kwa kuwa mgumu kwao. Ama nafasi ya kwanza ni kwa njia iliyo bora na nzuri zaidi. Makafiri na wanafiki watakuwa na adhabu kali hapa duniani kwa Allaah kuwasalitisha na Mtume Wake na kipote chake dhidi yao kwa kupigana nao. Hivyo hivyo, watakuwa na adhabu kali ya Moto Siku ya Qiyaamah na hayo ni mashukio mabaya sana.

 

Mifano hii miwili ambayo Allaah Ametupatia ya Waumini na makafiri. Hii ni kubaini kuwa kuwasiliana baina ya kafiri na Muumini na kuwa karibu naye haitomfaidi chochote. Maingiliano baina ya Muumini na kafiri haitomdhuru chochote pamoja na kusimamia wajibu. Kama kwamba katika hilo ipo ishara ya kuwaonya wakeze Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wasiyaendee maasiya na mahusiano yao na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayatowafalia chochote wakiwa ni waovu.

 

Hawa wake za Nuuh na Luut walifanya khiyana katika Dini, kwani hawakuwa katika Dini za waume zao. Hilo ndio kusudio la khiyana na wala sio khiyana katika zinaa. Hakika ni kuwa hakuzini mke wa Nabii yeyote yule, na Allaah hakujaalia hilo kwa mke yeyote miongoni mwa wake za Manabii.

 

3.    Al-Jaami‘u Liahkamil Qur-aan cha Abu ‘AbdAllaah Muhammad bin Ahmad Al-Answaariy Al-Qurtwubiy, mjalada 17-18, ukurasa 1312 – 132: Kauli Yake Aliyatukuka: “Ewe Nabii! Pambana (pigana Jihadi) na makafiri na wanafiki, na kuwa mgumu kwao!” ni katika mas-ala moja nayo ni kuwa mgumu na mkali katika Dini ya Allaah. Hivyo akamuamru apambane na makafiri kwa silaha (upanga), mawaidha mazuri na kumuomba Allaah. Ama wanafiki basi awe mgumu kwao na kuwasimamishia hoja thabiti. Pia kuwajulisha makazi yao Akhera. Kuwa wao hawana nuru yakuweza kupita kwenye sirata (njia nyembamba atakayepita kila mmoja kuelekea Peponi) pamoja na Waumini. Amesema Al-Hasan: “Pambana nao kwa kusimamisha adhabu juu yao kwani wao walikuwa wakifanya mambo yanayowajibisha hadd (adhabu). Na ilikuwa hadd ikisimamishwa kwao”. “Na makazi yao ni Jahanamu”, nayo inarudi kwa makundi yote mawili. Anamalizia Allaah Aliyetukuka ayah hii ya 9: “Na hayo ni marejeo mabaya”.

 

Allaah Aliyetukuka Ametupigia mfano kama kutukumbusha kuwa hakuna hata mmoja atakayefaidi Akhera kwa sababu ya ujamaa au nasaba ikiwa watatofautiana Dini. Amesema mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): “Hakika Jibril alishuka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumpa habari kuwa jina la mkewe Nuuh lilikuwa Waaghilah na mkewe Luut Waalihah.

 

Wakawakhini waume zao”. Amesema adh-Dhwahhaak na ‘Ikrimah: “Kwa ukafiri”. Amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma): “Alikuwa mkewe Nuuh akisema kuwa mumewe ni mwenda wazimu. Na alikuwa mkewe Luut akitoa habari za wageni wa mumewe”. Ijmaa ya Mufassirina wamesema kuwa kukhini kwao ni katika Dini kwani wote walikuwa mushirikina. Allaah Anaendelea kusema: “Nao wasiwafae kitu”, yaani hawakuweza Nuuh na Luut (‘Alayhimas Salaam) pamoja na utukufu wao kuwatetea kwa Allaah, pindi walipoasi wake zao ili wasiadhibiwe. Hili ni kututanabahisha kuwa adhabu huondoshwa na utiifu na wala sio wasila. Pamesemwa: “Makafiri wa Makkah walifanya istihzaa kwa kusema: ‘Hakika Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atatuombea’. Hapo Allaah Aliyetukuka Akabainisha shafaa hiyo haitawafaa kitu makafiri wa Makkah japokuwa wako karibu kiujamaa (na Mtume), kama vile haikufaa shafaa ya Nuuh na Luut kwa wake zao.

 

 

Ama kuishi katika dola ya kikafiri, msingi wa Kiislamu ni kuwa hilo ni haramu kwa Muumini ikiwa kutakuwa na dola ya Kiislamu na ikawa ni rahisi kwake kuhamia. Katika hali hiyo inafaa kwake ahame huko. Hii ndio hali iliyokuwa kwa waliosilimu pindi kulipokuwa na dola ya Kiislamu Madiynah. Wengi waliokuwa wameshikwa Makkah kabla ya kutekwa mji huo walikuwa wakifanya juhudi kukimbilia katika mji wa Madiynah. Mifano ni juhudi za kina Abu Jandal, Abu Baswir na wengineo (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Ni hakika kuwa mwenye kuishi katika nchi ya kikafiri anasongwa na mazingira mabaya katika nyanja ya Akhlaaq, adabu na udini. Mara nyingi anakuwa ni mwenye kutekwa na fikra za makafiri ambao wamemzunguka kila upande.

 

Yapo masharti mawili ya msingi kwa mtu kuweza kukaa katika nchi ya kikafiri. Masharti yenyewe ni kama yafuatayo:

 

La kwanza: Anapaswa mtu awe na dhamana ya kushikilia Dini yake kwa kuwa na ilimu tosha ya Uislamu, Imani na uwezo wa kupambana na kasumba mbaya, maadili mabovu na changamoto nyinginezo. Hivyo kuwa na msimamo thabiti na kutahadhari ili asiwe ni mwenye kupotea njia. Asiwe ni mwenye kufanya nao urafiki wa karibu wala kuwapenda kwani mambo hayo yanakwenda kinyume na Imani. Hata hivyo awe na muamala nao mzuri kama wanaadamu ili aweze kuwafikishia ujumbe wa Uislamu kwa usahali zaidi. Allaah Aliyetukuka Ametutahadharisha kuwapenda wala kuwafanya wao ni awliyaa’ wetu (marafiki wa karibu) kama Anavyotueleza:

“Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala ya Waumini. Na anaye fanya hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Ila ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu” Al-‘Imraan: 28

 

“Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa” Al-Mujaadilah: 58

 

“Enyi mlio amini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa ni marafiki. Wao ni marafiki wao kwa wao. Na miongoni mwenu mwenye kufanya urafiki nao, basi huyo ni katika wao. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu” Al-Maaidah: 51

 

“Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema: Tunakhofu yasitusibu mabadiliko. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake wakawa wenye kujuta kwa waliyo yaficha katika nafsi zao” Al-Maaidah: 52

 

“Na lau wangeli kuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu, na huyu Nabii, na yaliyoteremshwa kwake, wasingeliwafanya hao marafiki. Lakini wengi katika wao ni wapotofu” Al-Maaidah: 81

 

La pili: Anatakiwa aweze kutekeleza mambo ya Dini yake bila pingamizi yoyote, kama kuzuiliwa kuswali, kutoa Zakah, kufunga, kutekeleza amali ya Hajj na ‘Ibaadah nyinginezo ambazo anatakiwa atekeleze. Ikiwa hataweza kutimiza hayo basi hatoruhusiwa kukaa huko, katika nchi hizo.

 

Inatakiwa tufahamu kuwa sisi kuishi katika nchi za kikafiri tuwe na lengo la kufanya Da‘wah au kusomea masomo ambayo kwenye nchi zetu hayapo na masomo yenyewe yawe ni ya manufaa na faida kwa Umma wetu. Lau tutakwenda kwa lengo lingine lolote hatutakuwa na thawabu aina yoyote. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema: “Hakika vitendo huzingatiwa kwa nia, na kwa hakika kila mmoja atalipwa kwa nia yake. Mtu ambaye kuhama kwake ni kwa ajili ya Allaah na Mtume Wake, basi kuhama kwake ni kwa ajili ya Allaah na Mtume Wake. Ama yule ambaye kuhama kwake ni kwa ajili ya kuupata ulimwengu au mwanamke wa kumuoa, basi kuhama kwake ni kwa lile alilohamia” (Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

 

Lakini kwa kiasi kikubwa wengi wenye kuhamia katika nchi za kikafiri ni kwa ajili ya kutafuta pato la kidunia, posho na usaidizi, uraia na kipato kizuri hata kama hufanyi kazi. Kuhama kwa namna hii hakukubaliki kisheria. Mara nyingi huwa tunasema nchi hizi zina uhuru mkubwa zaidi kuliko nchi za Waislamu zote. Nadharia yetu ikiwa ni hiyo, je, hizi nchi zetu zitabadilishwa na nani ili ziwe nzuri? Inabidi sisi tuwe ngangari na kuishi katika nchi hizo zetu au kurejea au kuweka nia ya kurejea ili tulete mabadiliko na mageuzi, na hilo ni sahali sana kwa Allaah Aliyetukuka ikiwa sisi tuna azma hiyo insha Allaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share