090-Aayah Na Mafunzo: Hatua Za Uharamisho Wa Pombe, Laana Ya Allaah Na Adhabu Zake

Aayah Na Mafunzo

Al-Maaidah

Hatua Za Uharamisho Wa Pombe, Laana Ya Allaah Na Adhabu Zake

Na Sababu Ya Kuteremshwa Aayah

 

Alhidaaya.com

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo mpate kufaulu. [Al-Maaidah: 90]

 

Mafunzo:

 

 

 

 

 Hatua Za Uharamisho Wa Pombe Na Kikomo Chake:

 

Rejea Al-Baqarah (2 :219), An-Nisaa (4 :43).

 

Hatua ya kwanza kuhusu pombe ni swali alouliza Swahaba na jibu lake katika Suwratul-Baqarah (2:219):

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ

Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake. [Al-Baqarah (2:219)]

 

Hatua ya pili ilikuwa ni kukatazwa pombe katika nyakati za Swalaah kwa sababu Swahaba walikosea kusoma Qur-aan katika Swalaah kutokana na kulewa. Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah katika Suwrah An-Nisaa (4:43):  

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ  

Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema [An-Nisaa (4:43)]

 

Hatua ya tatu ndipo ilipofutwa hukmu hizo na ikabakia pombe kuwa ni haraam nyakati zote kwa kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo mpate kufaulu.

 

إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ ﴿٩١﴾

Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kumdhukuru Allaah na Swalaah, basi je mtakoma? [Al-Maaidah (5:90-91)]

 

Baada ya kuteremshwa Aayah hizo za Suwrah Al-Maaidah (5:90,91), hapo hapo Swahaba wakaacha moja kwa moja kulewa ikawa ndio kikomo cha kunywa pombe.

 

 

Hadiyth Za Matahadharisho Na Uharamisho Wa Pombe, Laana Ya Allaah Na Adhabu Zake:

 

 

Watu Kumi Wamelaaniwa Wanaohusika Na Pombe:

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amelaani aina ya watu kumi wanaohusika na pombe amesema: “Mwenye kugema pombe, mwenye kutaka afanyiwe, mwenye kunywa, na mwenye kubeba, mwenye kubebewa, mwenye kunywesha, mwenye kuuza, mwenye kula thamani yake, mwenye kununua, na mwenye kununuliwa.” [At-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida nyenginezo kuhusu matahadharisho ya pombe, uharamisho wake, laana na adhabu zake:

 

04-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Al-Huduwd (Adhabu): Mlango Wa Adhabu Ya Mnywaji Pombe Na Kubainisha Kileo (Ni Nini)

 

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Pia Aayah za Suwrah Al-Maaidah (5:90,91), zimeteremshwa kuwazungumzia makabila mawili katika Answaar. Walikunywa pombe mpaka wakalewa mno kisha wakagombana na kuchafuana baadhi yao kwa baadhi mpaka athari zikawa zinaonekana katika nyuso zao. Kisha pale ulevi ulipowaondokea na akili zao zikawarejea, viliingia vinyongo katika nyoyo zao, hapo zikateremka Aayah hizi zinazoharamisha pombe moja kwa moja:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo mpate kufaulu. [Al-Maaidah (5:90)]

 

إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ ﴿٩١﴾

Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kumdhukuru Allaah na Swalaah; basi je mtakoma? [Al-Maaidah (5:90-91)]

 

 

[Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) – amepokea Ibn Jariyr]

 

 

 

Share