267-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 267: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ

 

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

 

Al-Baqarah Aayah 267- Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ ۖ وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلَّا أَن تُغْمِضُوا فِيهِ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿٢٦٧﴾

267. Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi. Na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa na hali nyinyi wenyewe si wenye kuvichukuwa isipokuwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba hakika Allaah ni Mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

Aayah hii:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ

Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma…” mpaka mwisho, imeteremka  kuwazungumzia baadhi ya Swahaba  ambao walikuwa wakileta chane au shada la tende kisha wanalitundika Msikitini. Na Swahabi yeyote katika Ahlus-Swufaa anapohitajia chakula, alikuwa anatungua tende iliyoiva na mbichi. Na hao Swahaba waliokuwa wakileta tende Msikitini, walikuwa ni wale wasiopenda kujitolea katika njia ya  khayr. Hivyo walikuwa wakileta chane au shada la tende ambalo lina mchanganyiko wa tende ambazo hazikuiva kutokana na matatizo ya ulimaji  wa tende, na nyinginezo zilikuwa mbovu. Na wengine huleta chane au shada ambalo limekatika katika. Hapo ndipo ikateremka hii Aayah. [At-Tirmidhiy kutoka kwa Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه), na Taz. Tafsiyr Ibn Kathiyr]  

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Kadhaali: Ibn Jariyr alinukuu kuwa Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه) alisema kuhusu sababu ya kuteremshwa hiyo Aayah: “Iliteremeshwa kuwahusu Answaar. Kila ulipowadia msimu wa kuvuna tende, Answaar walikusanya tende mbivu katika bustani zao na kuzitundika kwenye kamba iliyofungwa kati ya nguzo mbili ndani ya Masjid ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Masikini katika Muhaajiruwn walikuwa wakila tende hizo. Hata hivyo, baadhi ya Answaar waliweka tende duni katika tende mbivu zilizokomaa, walidhani kwamba iliruhusiwa kufanya hivyo, ndipo Allaah (سبحانه وتعالى)  Alipowateremshia Aayah kwa  sababu ya kufanya hivyo. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Share