172-Asbaabun-Nuzuwl: Aal-'Imraan Aayah 172: الَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ مِن بَعْدِ مَا أَصَابَهُمُ الْقَرْحُ

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

Aal-‘Imraan 172-Wale waliomwitikia Allaah na Rasuli baada ya kuwasibu majeraha

 

 

الَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ مِن بَعْدِ مَا أَصَابَهُمُ الْقَرْحُ ۚ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا مِنْهُمْ وَاتَّقَوْا أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿١٧٢﴾

172. Wale waliomwitikia Allaah na Rasuli baada ya kuwasibu majeraha. Kwa wale waliofanya ihsaan miongoni mwao na wakawa na taqwa watapa ujira adhimu.

 

الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ﴿١٧٣﴾

173. Wale walioambiwa na watu: “Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni.” Lakini hili liliwawazidishia iymaan wakasema: “Hasbuna-Allaah! Allaah Anatutosheleza, Mzuri Alioje Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.”

 

فَانقَلَبُوا بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ لَّمْ يَمْسَسْهُمْ سُوءٌ وَاتَّبَعُوا رِضْوَانَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ ذُو فَضْلٍ عَظِيمٍ ﴿١٧٤﴾

174. Basi wakarudi na neema kutoka kwa Allaah na fadhila; halijawagusa ovu lolote; na wakafuatilia radhi za Allaah. Na Allaah ni Mwenye fadhila adhimu.

 

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Aayah hii mpaka Aayah 174 (3:172–174) zimeteremka pale washirikiana waliporudi Makkah kutoka Uhud.  Walipofika wakasema: “Hamjamuua Muhammad wala hamkuteka wanawake, ubaya ulioje mliofanya, rudini mkawamalize na kuwasagasaga! Ikamfikia khabari hii Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), akaamrisha jeshi la Waislamu litoke (ili kuwaogopesha washirikina na kuwaonyesha kuwa Waislamu bado wako imara na wana uwezo mkubwa wa kukabiliana nao pamoja na kwamba wana majeraha ya vita). Wakatembea pamoja na maumivu na majeraha yao mpaka wakafikia (sehemu fulani ya) Hamraa Al-Asad au Bi-ir Abiy ‘Uyaynah.   Na hapo Allaah (عزّ وجلّ) Akateremsha:

 

الَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ مِن بَعْدِ مَا أَصَابَهُمُ الْقَرْحُ

Wale waliomwitikia Allaah na Rasuli baada ya kuwasibu majeraha.

 

Na Abu Sufyan alimwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “Miadi yako ni msimu wa Badr ulipowauwa Swahaba wetu.” Basi waliokuwa waoga walirejea, ama walioshujaa  walijiandaa kwa vita  na biashara, wakamwendea lakini  hawakumkuta yeyote pamoja naye, wakafanya manunuzi, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha:

فَانقَلَبُوا بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ لَّمْ يَمْسَسْهُمْ سُوءٌ

Basi wakarudi na Neema kutoka kwa Allaah na Fadhila; halijawagusa ovu lolote. (3:174) [Atw-Twabaraaniy kwa Isnaa Swahiiyh].  

 

 

 

 

Share