Riyaa (Shirki Iliyofichikana)

 

Riyaa  (Shirki Iliyofichikana)

 

Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

  BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym

 

 

Riyaa Kilugha:

 

Ni neno linalotokana na neno la Kiarabu “Ra-aa” ambalo lina maana ya kuona, kutazama au kuangalia. Na haswa makusudio yake ni kujionyesha, unafiki na udanganyifu. Katika mtazamo wa kisheria Riyaa ina maana ya ‘‘kufanya matendo ambayo ni ya kumpendezesha Allaah lakini kwa nia ya kumridhisha asiye Allaah.’’ Au ni kufanya amali njema kwa makusudio ya kuonesha watu, ili uonekane ni mzuri au mwema kuliko ulivyo, ama upate kupendeza machoni mwao au upate kilicho mfukoni mwao au cheo. Na hii Riyaa ni namna ya shirki, kadhalika ni namna ya unafiki au wizi. Hivyo basi yoyote mazuri yafanywayo kwa kutaka na kutaraji manufaa ya kilimwengu na sio kumridhisha Muumba, basi yanageuka kuwa ni matendo ya kishaytwaan.

 

Riyaa ni moja ya mafungu ya matendo hatari mno ambayo ni vigumu sana kwa wengi kuyachuja na kuyatenga mbali na matendo yao. Ni vizuri na muhimu kuweza kulichunguza tatizo hili na kulijua undani wake ili tuweze kupambana nalo na kulitibu kwa ajili ya kufikia mafanikio ya kusafisha amali zetu na kukamilika Uislam na Uchaji Allaah wetu. Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah wameelekea katika Qur-aan na Sunnah sahihi pamoja na mwelekeo wa wema waliotangulia ili kupata tiba ya ugonjwa huu hatari. Ni muhimu kuangalia hii Riyaa ilivyo tujue madhara yake na jinsi ya kutafuta kinga au ponya yake.

 

Niyyah

 

Ni muhimu sana kufahamu maana ya Ikhlaasw (utii kamili, kuitakasa niyyah) yaani kufanya jambo kwa ajili ya Allaah pekee. Hadiyth ifuatayo yatuonyesha namna gani tunapaswa kutilia umuhimu mkubwa juu ya Ikhlaasw na kuwa mbali na Riyaa. ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) kamnukuu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika matendo yanatokana na niyyah, Na kila mtu atapata (malipo) kwa kile alichonuia …" [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd].

 

Na Qur-aan vilevile inaonyesha na kueleza umuhimu wa ikhlaasw pale Allaah Aliposema:

 

وَمَا تُنفِقُونَ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ اللَّـهِ ۚ

Na hamtoi ila kutaka Wajhi wa Allaah… [Al-Baqarah: 272]

 

Kizazi cha mwanzo cha Uislam kilizingatia mno umuhimu wa ikhlaasw na jinsi ya kusafisha na kuzisahihisha niyyah zao. Tunapata mfano mzuri kutoka katika mapokezi haya ya Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyoyapokea kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ''Maneno pekee hayana faida kama hayajafuatiwa kwa vitendo, na maneno na vitendo pekee havina faida kama hadi yawe na niyyah safi. Na hayo maneno, vitendo na niyyah safi, yote hayana faida hadi yawe yamekubaliana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).'' Hivyo basi, tunaona kuna mfululizo wa masharti ambayo ndiyo yanayosababisha vitendo vikubalike na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Sharti la kwanza ni kwamba lazima kitendo kifanywe kwa ajili ya Allaah pekee. Sharti la pili kitendo hicho kiwe kimekwenda sambamba kulingana na mafunzo ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisiwe ni kitendo cha uzushi kilichoanzishwa na watu.

 

Khatari Au Madhara ya Riyaa

 

1.    Shirki iliyofichikana

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mapenzi yake makubwa mno kwa ummah wake alikuwa akichunga sana na kuchelea maafa kwa ummah wake kuliko mtu mwengine yeyote. Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) anaeleza kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakuta wakijadiliana kuhusu Dajjaal na akawaambia: ‘‘Je, niwajulisheni kile nikikhofiacho zaidi kwenu kuliko hata hatari za Dajjaal? Basi ni shirki iliyojificha. Mtu anasimama kuswali, anaipamba na kuiremba swala yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama.’’ [Sunnan Ibn Maajah, namba 3389].

 

2.    Inadhoofisha Iymaan Katika Kumpwekesha Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)

 

Kwa kufanya Riyaa, mtu huwa anaangamiza lengo kuu la uumbwaji, kwani badala ya kumuabudu Allaah, huwa anafanya ‘Ibaadah lakini kwa lengo na niyyah ya kuwaridhisha waja na kupata sifa kutoka kwa viumbe na wala si kwa ajili ya Muumba. Allaah Anasema:

 

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu. [Adh-Dhaariyaat: 56]

 

Vilevile Allaah Anawasifia wale waumini wa kweli wanaofanya matendo ya ‘Ibaadah zao kikamilifu na pekee kwa ajili yake Allaah na wala hawahitaji malipo au shukurani kutoka kwa viumbe wenzao. Anasema Allaah:

 وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka.

 

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kwenu jazaa na wala shukurani. [Al-Insaan 8-9].

 

Na pia kwa upande wa pili kinyume na hao Allaah Anawaelezea wengine kwa kusema:

 

فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ ﴿٧﴾

Basi Ole kwa wanaoswali. Ambao wanapuuza Swalaah zao. Ambao wanajionyesha (riyaa). Na wanazuia misaada ya matumizi madogodogo ya kawaida ya kila siku. [Al-Maa’uwn: 4-7].

                 

3.    Inazidisha Upotofu

 

Hakuna shaka mtu mwenye kufanya Riyaa huwa ni mwenye maradhi moyoni mwake, na kama ugonjwa huo hautotibiwa, uatapelekea kwenye matatizo mengi zaidi. Kulingana na hili Allaah Anasema:

 

يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَمَا يَخْدَعُونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾

(Wanadhani) Wanamhadaa Allaah na wale walioamini lakini hawahadai ila nafsi zao na wala hawahisi.

فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿١٠﴾

Ndani ya nyoyo zao mna maradhi na Allaah Akawazidishia maradhi, na watapata adhabu iumizayo kwa waliyokuwa wakiyakadhibisha. [Al-Baqarah: 10]

 

4.    Inapokonya Baraka Ya Matendo

 

Katika Hadiyth nyingi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaelezea kwamba Allaah Hapokei matendo yanayofanywa kwa ajili ya kuwaridhisha viumbe. Amepokea Mahmuwd bin Labiyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Allaah Mtukufu Atasema wakati Akiyahesabu matendo ya viumbe (kuwaambia waliofanya Riyaa), ‘‘Nenda kwa wale uliokuwa ukiwaonyesha matendo yako (duniani) uone kama utapata malipo yoyote kutoka kwao.’’ [Swahiyh at-Targhiyb wat-Tarhiyb namba 29].

 

5.    Inamzuia Mtu Kwenda Jannah

 

Kufanya matendo mema kwa ajili ya kusifiwa na kuridhisha watu, huenda yakapelekea kumzuia mtu kuingia Jannah. Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amemnukuu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Yeyote anayechuma elimu ambayo anapaswa kuitumia kwa ajili ya Allaah, (kisha akaitumia) kwa niyyah ya kupata manufaa ya kilimwengu, hatonusa hata harufu ya Jannah siku ya Qiyaamah." [Abu Daawuwd namba 3656, na Ibn Maajah namba 255].

 

Mambo Yanayosababisha Riyaa Kwa Ujumla

 

Kiburi

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). kasema: ‘‘Kibr ni joho langu na ukubwa (utukufu) ni kanzu yangu, hivyo yeyote anayetaka kushindana nami (katika sifa hizo), basi nitamtosa katika Jahanam’’ [Swahiyh Muslim namba 6349]. 

 

Kisha Allaah Ameeonya vikali kwa mwenye kutumbukia katika sifa hii aliposema:

 

 لَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَفْرَحُونَ بِمَا أَتَوا وَّيُحِبُّونَ أَن يُحْمَدُوا بِمَا لَمْ يَفْعَلُوا فَلَا تَحْسَبَنَّهُم بِمَفَازَةٍ مِّنَ الْعَذَابِ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٨٨﴾ 

Usiwadhanie kabisa wale wanaofurahia kwa waliyopewa na wanapenda wasifiwe kwa wasiyoyatenda. Usiwadhanie kabisa kuwa watasalimika na adhabu. Nao watapata adhabu iumizayo. [Al-‘Imraan: 188].

 

Kujionesha Na Kujisifu

 

Allaah Anasema katika Qur-aan:

 

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٤٢﴾

Hakika wanafiki (wanadhani) wanamhadaa Allaah, na hali Yeye (Allaah) Ndiye Mwenye kuwahadaa. Na wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamdhukuru Allaah isipokuwa kidogo tu. [An-Nisaa: 142].

 

Pia mtu kufanya ‘Ibaadah kwa bidii na kuiremba na utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu kwa sababu kuna watu wanamuona au kumtazama, lakini anapokua peke yake ‘Ibaadah ile huifanya kwa haraka haraka na kilegevu na uchovu kama mtu aliyelazimishwa.

 

Ama mtu anatoa msaada au sadaka pale anapoona watu wapo au  kuna mtu ambaye anamuheshimu au kumjali yupo hapo. Ni mfano wale tunaowaona wanapotoa mchango au msaada wanaita waandishi wa habari na wapiga picha na televisheni wachukue maelezo na picha wakati anapotoa ili ulimwengu wote ujue fulani katoa na ni mtu mzuri! Ajabu, yote hayo ni kwa maslaha ya kiulimwengu na hakuna nafasi ya Allaah ya kutiiwa na kuridhishwa. Allaah Hakuliacha hili pia kulikemea:

 

إِنَّهُمْ لَن يُغْنُوا عَنكَ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا ۚ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۖ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُتَّقِينَ﴿١٩﴾

Hakika wao hawatokufaa chochote mbele ya Allaah. Na hakika madhalimu ni marafiki wanaoshirkiana wao kwa wao. Na Allaah ni Mlinzi, Msaidizi wa wenye taqwa. [Al-Jaathiyah: 19].

 

 

Kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Na Hapo Hapo Huwaangushi Viumbe

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ‘‘Allaah Mtukufu Anasema: ‘‘Mimi ni mwenye kujitosheleza, sihitaji msaada wala mshirika. Kwa hiyo, yule afanyaye kitendo kwa ajili ya kumfanyia kiumbe (na hapo hapo anakifanya kwa ajili Yangu), (sitokihitaji kitendo chake hicho) nitamwachia huyo aliyemfanyia kunishirikisha Nami’’ (hatopata ujira wowote kwa kitendo hicho). [Swahiyh Muslim namba 7114].

 

Mavazi

 

Suala la mavazi linaweza kumsababishia mtu kuingia katika Riyaa, mathalan, utakuta mtu anavaa vizuri akishindana na kila mitindo mipya itokayo na akitaka watu wamuone kuwa anakwenda na wakati. Na mtu mwingine akawa anavaa ovyo ovyo (akijiweka kama hao wanaojiita madaruweshi) akionyesha watu kuwa haijali dunia bali yeye ni wa Aakhirah tu n.k. Wengine wakivaa mavazi fulani fulani yanayoonekana ya kidini ili asemwe kuwa yeye Shaykh au Mwanachuoni. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ ۖ وَإِن يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ ۖ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُّسَنَّدَةٌ ۖ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ ۚ هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ ۚ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ ۖ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ﴿٤﴾

Na unapowaona, inakupendezesha miili yao, na wanaposema, unasikiliza kauli yao, kama kwamba magogo yaliyoegemezwa; wanadhania kuwa kila ukelele unaopigwa ni dhidi yao. Wao ndio maadui, basi tahadhari nao, Allaah Awaangamize! Namna gani wanavyoghilibiwa? [Al-Munaafiquwn: 4]

 

Watu kama hao tunao katika jamii yetu, ambao kazi yao ni kutumia ulimi wao kudanganya watu na kufitinisha baina ya Waislam, na kuwazulia watu mambo kadha wa kadha ili wasiwe na thamani katika jamii! Na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba jamii inafunika maovu yao na inashirikiana nao na kuwapa nafasi katika mambo ya dini na uongozi.

 

Mambo Yenye Kuhusishwa Na Riyaa

 

Sifa Zisizokusudiwa

 

Endapo watu watahudhuria shughuli ya dini kama mhadhara n.k. ambapo kuna manufaa na kunafanywa kwa Ikhlaasw, si kunafanywa kwa malengo tofauti kama ya kujionyesha kwa watu kuwa mnaisimamia dini na hali hamna malengo yoyote wala hamjali kinachozungumzwa hapo kinafanywa kwa ikhlaasw au kwa sifa na kutaka tu watu waseme: ‘‘jamaa wanafanya harakati maa shaa Allaah.’’ Shughuli kama hiyo ikiwa ni ya Ikhlaasw na wasikilizaji wakampongeza Mhadhiri, basi pongezi hizo hazitomharibia vitendo vyake maadamu hajaigeuza au kuibadili ile niyyah yake kutoka kwa ajili ya Allaah na ikageuka ikawa ni kwa ajili ya wale wenye kumpongeza na kumsifu. Abu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘‘Ee Rasuli wa Allaah! Je, unaonaje kama mtu anafanya matendo mazuri, kisha watu wakamsifia kwa matendo yake? Akajibu: ‘‘Hiyo ni sehemu ya baraka na radhi kwa Muumini (zitakazohifadhiwa kwake siku ya Qiyaamah." [Swahiyh Muslim namba 6388].

 

Lakini awe makini mwenye kupongezwa au kusifiwa kwa matendo yake mazuri, kuwa pongezi hizo anazosifiwa akiwa ni Mhadhiri, Msomaji Qur-aan au Mdarisiji, zisije zikambadilisha niyyah yake na akawa kila mara anafanya jitihada zaidi kuremba mawaidha au kisomo chake ili azidi kusifiwa na kupata umaarufu! Kuna wengine maskini hujitahidi na kujipinda, majasho yakawatoka na koo likawakauka kuiga watu mashuhuri ili wasifiwe na kufananishwa nao. Pia wenye kumwaga sifa, nao watoe sifa au pongezi zao kwa ikhlaasw na si kinafiki. Maana utawasikia wengine wakiwaendea wenye kuwasifu na kusema ‘‘Al-Habiyb, si mchezo mawaidha ya leo, maana nakwambia watu wote walikuwa wamezimia.’’ Kama vile huyo Mhadhiri alikuwa hawaoni hao watu. Au mwengine atasema: ‘‘Muadhamu, leo ulikuwa ukitoa kama Shaykh fulani Wa-Allaahi’’!!

 

Sifa kama hizo ambazo mtoaji anazitoa na hali anajua ni kujipendekeza tu kwa huyo amsifiaye na kutaka aonekane mzuri, ni sifa za kinafiki na tabia isiyo nzuri ambayo hupelekea wale wenye kufanya matendo mazuri, wakaathirika na wakawa hawafanyi tena kwa ajili ya Allaah, bali kwa kuwafurahisha hao akina Al-Habiyb na kina  Al-Mu'adham. Na siku zikikosekana hizo sifa, basi huyo aliyezoea kusifiwa, anakuwa mnyonge na huenda pia ikapelekea hata mwisho kuacha shughuli hizo za khayr kwa ajili hakuna sifa wala kushukuriwa, au akaacha kwenda kwenye mhadhara kwa kuwa hawatokuwepo watu wengi na hatosikika. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ‘‘Ukiwaona wale wenye kuwapa watu sifa, wamwagie vumbi usoni mwao.’’ [Swahiyh Al-Bukhaariy namba 830, na Swahiyh Muslim namba 7143].

 

Mwengine ataudhiwa na watu na atasusia hata kushiriki katika shughuli hizo na kuapa, lakini baada ya muda unamuona huyoo yuko nao tena na akiulizwa vipi anadai aah nimeona nifanye maana haya ni maslahi ya Uislamu, sasa je, hayo maslahi ya Uislam hapo alipojitoa mwanzo alikuwa hayajui? Huko ni kukosa Ikhlaasw. Na matendo kama hayo yanafanya mtu asiaminike pande zote hata na hao wanaoshirikiana naye, kwani wanajua kama aliwahi kususa basi hawezi kuacha kususa tena na huko mbeleni. Maana huyo hafanyi kwa ajili ya Allaah bali ni kwa ajili ya watu. Kususa kunakokubalika ni pale watu wanapokuwa katika misimamo inayopingana na Dini kama watu wa bid'ah na wale wanaowatetea watu wa bid'ah na kushikamana nao; hao ndio wanaopaswa kususwa kama zilipokelewa kauli nyingi kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na wema waliotangulia kuhusiana na hilo.

 

Kutotaka Kuwaangusha Watu

 

Kuna wengine wana tabia ya kuridhisha watu na kutotaka kuonekana wabaya, hata kama itakuwa ni kufanya tendo lisilo kwa ajili ya Allaah au la uzushi, au tendo la khayr lakini ndani yake kumekusudiwa shari. Na watu kama hao hawataki kuwavunja wengine kwa matakwa yao, ima kwa niyyah ya kujenga urafiki, au kupata maslaha fulani au kumkomoa fulani au asichukiwe ikiwa atakataa. Kwa hiyo atafanya jambo hata kama anajua fika ndani ya jambo hilo hakuna ikhlaasw wala yeye mwenyewe haliamini kama ni sahihi. Na wakiulizwa kwanini wanafanya jambo ambalo halina Ikhlaasw ndani yake, hutoa udhuru zaidi ya sabini.

 

Kinga Na Njia Za Kujiepusha Na Riyaa

 

1.    Kuongeza Elimu

 

Mojawapo ya kinga ya matatizo mengi yanayowakabili Waislam, ni kuongeza elimu zaidi na sahihi kuhusu dini yao. Tunajua kuwa elimu chache ina matatizo na elimu kubwa isiyo sahihi nayo ni msiba. Na kuwa na elimu sahihi ndipo utakapoweza kupambanua haki na batili na yale yenye utata yaliyofichikana, na pia ndipo utakapofikia lengo la kumcha Allaah. Allaah kwa kulithibitisha hili Anasema:

 إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ

Hakika wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni ‘Ulamaa… [Faatwir: 28]

 

Ni muhimu kutambua kwamba, kutafuta elimu sahihi ni jukumu la kila Muislam mwenye kumcha Rabb wake, na wala si jukumu tu la Viongozi wa dini kama Masheikh, imaam, Maustadh n.w. Kuna wengi miongoni mwetu hawajishughulishi kusoma dini yao wala si jambo lililozoeleka kukuta katika nyumba za Waislam maktaba au hata vitabu vichache muhimu vya dini! Na sahemu nyingine kama Ulaya, utakwenda kwenye nyumba ya Muislam ukakosa hata Qur-aan! Wengine hawajui hata Qiblah kilipo.

 

2.    Du’aa

 

Katika kizuizi na chukizo kubwa la Riyaa na kilicho chepesi kukifanya ni du’aa.  Abu Bakr Asw-Swiddiyq amemnukuu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘‘Shirki iliyomo ndani yenu inajificha zaidi kuliko mtambao wa sisimizi (si rahisi kuonekana), na nitawaambia kitu, mtakapokifanya, basi kitawaondoshea ndani yenu Shirki ndogo (Riyaa) na kubwa. Sema: ‘‘Allaahumma iniy a'uwdhu bika an ushrika bika wa ana a’alam, wa astaghfiruka lima la a’alam” (maana yake: “Ee Rabb wangu, naomba unihifadhi na kutomuabudu mwengine asiyekuwa wewe (kushirikisha), na naomba msamaha kwa (kufanya) kile nisichokijua.’’ [Swahiyh Al-Jaami’. namba 3731].

 

3.    Kufikiri Juu Ya Jannah Na Jahannam

 

Jambo la tatu lenye kusaidia kumweka mtu mbali na Riyaa ni daima kuzingatia juu ya siku ya Qiyyaamah. Mazingatio ya siku ya Qiyaamah yanasaidia sana kukuza khofu ya Jahannam, na kuongeza matashi ya kuipata Jannah. Ikiwa mwanaadam atazingatia kuwa lengo kuu la kuishi kwake hapa duniani si kupata umaarufu na sifa, bali ni kujilinda na adhabu ya moto na kutaraji kuingia Jannah, atajaribu kwa kadri ya upeo wake kujiepusha kabisa na Riyaa. Allaah Anasema katika Qur-aan:

 فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake. [Al-Kahf: 110].

 

Ndugu Waislam, tujue kuwa Riyaa ni kinyume cha Ikhlaasw, palipo na Ikhlaasw hapana Riyaa, na palipo na Riyaa hapana Ikhlaasw. Tujitahidi kutazama nafsi zetu na kujihesabia matendo yetu tuyafanyayo kila siku, tunapotaka kufanya tendo lolote, ni vizuri tujiulize kwanza, ‘‘Je, nafanya hili kwa ajili ya Allaah pekee? Au kwa sababu ya fulani? Ili afurahi au aridhike n.k. Ni tatizo ambalo si rahisi mtu kuligundua katika nafsi yake ndio maana Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akalifananisha na mtambao wa mdudu chungu au sisimizi.

 

 

Wa Allaahu A’lam

 

 

Share