Swalaat-un-Naariyah Ni Nini? Na Je, Yafaa Kishariy'ah?

 

Swalaatun-Naariyah Ni Nini? Na Je, Yafaa Kishariy'ah?

 Abu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

  BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym

 

Kumezuka Du'aa maarufu iliyoenea iitwayo Swalaatun-naariyah, Du'aa hiyo imeenea katika jamii yetu ya Kiswahili, watu wameshughulishwa nayo. Na la kusikitisha zaidi ni kwamba inaaminiwa sana hata imekuwa ni ‘ibaadah kubwa ya kutegemewa mtu kutakabaliwa haja zake. Wanaacha kutumia du'aa zilizo sahihi na kutumia hii ambayo ni uzushi na juu ya hivyo ina maneno ya shirk.

  

Du'aa hiyo husomwa hivi:

 أللهم صلي صلاةً كاملة وسلم سلاما تاما على سيدنا محمد الذي تنحل به العقد، وتتفرج به الكرب، وتقضى به الحوائج ، وتنال به الرغائب، وحسن الخواتيم ويستسقى الغمام بوجهه الكريم وعلى آله وصحبه في كل لمحة ونفس بعدد معلوم لك

 

‘Allaahumma Swalli Swalaatan kaamilatan wa-sallim salaaman taamaa, ‘alaa Sayyidinaa Muhammad alladhiy tan-hallu bihil-‘uqadi, wa-tanfariju bihil-kurab, wa-tuqdhwaa bihil-hawaaij, wa-tunaalu bihir-raghaaib, wa-husnul-khawaatim, wa yustasqal-ghamaamu bi-wajhil-kariym, wa ‘alaa aalihi wa-swahbihi fiy kulli lamhatin wa nafsin, bi’adadi kulli ma’aluumin Lak’

 

Du'a a hii huwa yasomwa mara 4444 (Elfu nne, mia nne na arobaini na nne). Du'aa hii inaaminika kuwa imeanzia huko Bara Hindi na haswa India. Husomwa zaidi wakati mtu anapopatwa na matatizo yake ya kidunia, mikosi, majanga n.k.

 

Sasa nini hukumu yake kishariy'ah? Dini inasemaje kuhusiana na Du'aa ya mfumo huu?

 

Je, nini maana ya hayo maneno hapo juu, na je, kuna aina yoyote ya ushirikina ndani ya maneno hayo?

  

Je, kuna ubaya gani kusoma ikiwa hakuna shirki ndani yake? Kwa maana ni aina ya utajo ambao ndani yake kuna kumtaja Allaah na pia watu hukusanyika pamoja na kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ili kuondosha mitihani ya misiba na kadhalika kwa kumuomba. 

  

Jawabu Na Hukmu:

 

Kwanza maana au tarjama ya hiyo Du'aa ni hii:

 

(Ee Allaah, Mswalie  Swalaah iliyotimu bwana wetu Muhammad ambayo kwa fadhila zake, vizuizi vyote vinaondoka, mazonge (misukosuko) yanapoa, shida zote zinafarijika, na mahitaji yanakidhika, na inafikisha kwa yanayotamaniwa, na mwisho mwema wapatikana, na kwa fadhila zake yule mwenye uso mtukufu mawingu (mvua) huombwa kunyesha, na Swalah na Salaam ziwe juu ahli zake na Swahaba wake kwa kila muda na kila pumzi kwa idadi ya kadiri ya Ujuzi Wako)

 

Maana ya maneno haya kwanza yanajiweka wazi kuonyesha uzushi uliomo katika Du'aa hii.

 

Pili, Du'aa hii imekusanya maneno mengi yasiyokubalika katika Uislamu na yanayopelekea katika shirki. Ni vizuri sana mtu kujiepusha na jambo kama hili kwa sababu zifuatazo:

 

1- Du'aa hii husomwa wakati wa matatizo, nalo jambo hili halijathibiti na linahitaji dalili; kinyume chake ni uzushi.

 

2- Inasomwa kwa idadi maalum, ambayo ni mara 4444, ambao huu ni muundo potofu wa uzushi wenye idadi katika 'ibaadah.

 

3- Inatakiwa kusomwa kwa muundo wa kukusanyana watu, nalo hili ni jambo lisilokubalika na uzushi katika 'ibaadah.

 

4- Inakusanya maneno ambayo yanakwenda kinyume na Dini, na ambayo yanavuka mpaka katika kumtukuza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumpa sifa ambazo Anastahiki nazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee.

Mfano wa sifa zile zilizohusishwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye hiyo Du'aa, nazo ni:

 

kwa fadhila zake, vizuizi vyote vinaondoka, mazonge (misukosuko) yanapoa, shida zote zinafarijika, na mahitaji yanakidhika, na inafikisha kwa yanayotamaniwa, na mwisho mwema wapatikana, na kwa fadhila zake yule mwenye uso mtukufu mawingu (mvua) huombwa kunyesha

 

5- Haya yote ni mambo ambayo yanayompa Rasuli wa Allaah uwezo ambao si wake na asiostahiki.  Na sifa hizo za kuweza kuyafanya yote hayo, ni sifa tu anazoweza kuzifanya Allaah na wala si kiumbe Wake yeyote! 

 

Kwa hiyo, Du'aa hii inapelekea katika ushirikina na haifai kabisa kwa Muislam kuisoma wala kushiriki ndani yake.

 

Allaah Anasema kumwamuru Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaambie Makafiri wa Makkah:

 

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا﴿٢٠﴾قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا﴿٢١﴾قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّـهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا﴿٢٢﴾

Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi namuomba Rabb wangu na wala simshirikishi na yeyote. Sema: Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu. Sema: Hakika hakuna yeyote awezaye kunilinda na Allaah na wala sitoweza kupata mahali pa kukimbilia. [Al-Jinn: 20-22]

 

Kwa mujibu wa maneno ya Allaah ('Azza wa Jalla) tunapata ushahidi kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hana uwezo wa kumsaidia mja wala kumuongoza au kumpoteza, hayo yote yako katika uwezo wake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Pekee.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye katika kuukaripia uzushi aliposema: “Yeyote atakayezusha chochote  katika jambo letu hili (Dini ya Uislamu), basi hilo alizushalo hurejeshewa nalo mwenyewe.” [Imesimuliwa na Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa dalili hizo ndugu Waislamu, jichungeni mno na aina zote za uzushi na shirki, hakika mambo hayo yanapelekea katika maangamizi na upotofu. Tumtiini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumpenda ilivyo Nabiy wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lakini tusivuke mipaka katika mapenzi hayo tukaja kujikuta tunaingia katika shirk.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share