05-Imaam Ibn Baaz : Hakulipa Deni La Ramadhwaan Iliyopita Je, Itakuwa Ni Dhambi Na Je, Alipe Kafara?

 

Hakulipa Deni La Ramadhwaan Iliyopita Je, Itakuwa Ni Dhambi Na Je, Alipe Kafara?

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Aliyekuwa ana deni la Ramadhwaan iliyopita hakulipa hadi imeingia Ramadhwaan nyingine. Je, Atakuwa  na dhambi na Je, itabidi alipe kafara?

 

 

JIBU:

 

Mtu yeyote aliyekuwa na deni kutoka Ramadhwaan iliyopita, inampasa alipe kabla ya kuingia Ramadhwaan nyengine. Inaruhusiwa kuchelewesha kulipa hadi mwezi wa Sha'baan. Lakini ikiingia Ramadhwaan nyingine na yeye hakulipa Swawm zilizompita bila ya sababu yoyote, atakuwa amefanya dhambi na itabidi alipe hilo deni pamoja na kulisha maskini mmoja kwa kila siku moja ya deni. Na hivi ndivyo walivyokuwa wakifanya Maswahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kama alivyowaamrisha. 

 

Kipimo cha chakula ni nusu ya pishi (sawa na vibaba viwili au 1.5kg) ya chakula kinacholiwa sana na watu katika nchi anayoishi.  Kila siku moja ya deni alishe maskini mmoja kwa kipimo hiki. Anaweza kuwapa watu mbali mbali au hata mtu mmoja.  

 

Na kwa yule aliyekuwa anao udhuru wa kutokuweza kufunga kwa sababu ya safari au ugonjwa basi yeye inampasa swawm pekee bila ya kulisha masikini kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ  

Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah: 185]

 

Na Allaah (Ta’aalaa) Ndiye Mwenye kujaalia tawfiyq.

 

 

[Imaam Ibn Baaz - Fataawa Ramadhwaan – Mjalada  2, Uk 555, Fatwa Namba 537;
Al-Fataawa libni-Baaz - Kitaab Ad-Da'wah, Mjalada  2, Uk  158-159]

 

 

Share