Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kuhusiana Na Qur-aan – 03

 

Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Kuhusiana Na Qur-aan – 03

 

Je, Qur-aan Imeumbwa?

 

Abuu Rabiy'

 

 

 

Hili ni swali ambalo kalamu za watu wengi sana zinashindana kulijibu na hasa hasa hawa watu waliopinda, kwani wanajitahidi sana kudalilisha juu ya ubatili wao kuwa Qur-aan imeumbwa. Sasa nachotaka hapa ni kunukulu hoja zao kisha kuzijibu moja moja na namuomba Allaah Anipe auni katika hili.

 

 

Hoja Yao Ya Kwanza:

 

 Bila shaka kila Muislamu anatakiwa kujua kuwa hakuna kitu kinachotoka nje ya hukumu mbili; ima kiwe ni kiumbe au kisiwe kiumbe. Kila Muislamu anatakiwa kujua kuwa aliyekua si kiumbe ni yule aliyeumba tu, naye ni Allah mtukufu, na vilivyobakia vyote ni viumbe vyake.

 

 

Majibu Yetu:

 

Naam sisi tunakubaliana kuwa hukmu ni mbili tu na wala hakuna ya tatu.

Kuwa kilichopo ima awe muumba au muumbwaji. Hii ni hukmu ya haki kabisa na kuwa Muumba ni Allaah na asiyekuwa Allaah ni kiumbe.

 

Lakini tatizo ni pale ambapo mnapoithibitisha dhati yake. Kwani tunasema kuwa hakuna chochote kilichopo lazima kiwe na sifa, kwa hiyo hakuna kwenu ila mojawapo ya mambo mawili:

 

1. Kuithibitisha dhati pasina kuwa na sifa na hii ni muhaal.

2. Kuithibitisha dhati yenye sifa na hii ndio sawabu.

 

Sasa kumthibitishia Allaah sifa ya kuzungumza na wakati huo huo mnathibitisha kuwa maneno Yake yameumbwa huu ni mchezo!

 

Kwa sababu kama alivyokuwa mmoja katika dhati Yake na katika uumbaji Wake pia ni mmoja katika majina yake na sifa zake.

 

Kama alivyokuwa yeye hakuumbwa bali Yupo pasina kuwa na mwanzo pia sifa Zake kwa sababu sifa Zake si mwengine bali zinafungamana na dhati Yake. Sasa haiwezekani kuizungumzia dhati Yake ambayo haina sifa ya kuumbwa na pia haiwezekani pia Allaah kuziumba sifa Zake.

 

Kusifika na sifa ya kuzungumza na wakati huo huo maneno Yake Ameyaumba, huo ni mchezo na wala haingii akilini!

 

Na hapa hatusemi kuwa sisi tunatanguliza akili mbele ya dalili, bali ifahamike kuwa akili iliyosalimika haigongani na dalili iliyokuwa sahihi.

 

Bila shaka tunakubaliana kuwa bubu ni mtu ambae Allaah Amemnyima uwezo wa kuzungumza imma kwa maradhi au kwa sababu nyingine. Je, bubu akiweza kujielezea kwa kutumia maandishi sifa yake ya ububu itakuwa imeondoka?

 

Mkisema hapana tutauliza kwanini na wakati ameweza kuyaweka maneno yake kwenye karatasi?

 

Na wala shaka ububu wake upo pale pale kwasababu sharti ya kuzungumza ni kutamka herufi na kutoa sauti.

 

Na Allaah Ana mfano uliokuwa juu kabisa.

 

Na hii yote ni kwa sababu haya makundi mapotofu kwanza kabisa yamemfananisha Allaah na viumbe Wake katika sifa Zake, kisha baada ya kuona kuwa Allaah Hafanani na yeyote wakamkanushia sifa Zake!

 

Wakasahau kuwa hizi ni dhati mbili tofauti, dhati ya Muumba ambayo ina sifa Zake na majina Yake na dhati ya kiumbe ambayo ina majina yake na sifa zake.

 

Sasa uungwana ni kila dhati kuithibitishia yale yanayofungamana nayo pasina kufananisha na dhati nyingine.

 

Wa-Allaahi, wangefanya hivi wangestarehe sana kama walivyokuwa Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah.

 

 

Hoja Yao Ya Pili:

 

Qur-aan ni kitu, yaani kilichopo au kuwepo na kilichopo hakitoki kati ya hukmu mbili; ima awe Allaah au kiwe kiumbe, na Qur-aan si Allaah; inalazimu kuwa kiumbe.

 

Na pia madaam Qur-aan ni kitu Allaah Anasema:

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ ﴿٦٢﴾

“Allaah ni Muumbaji wa kila kitu, Naye juu ya kila kitu ni Mdhamini.” [Az-Zumar: 62]

 

Neno "Kullu", ni katika matamko yanayojulisha ujumla katika maneno.

Na neno "Shay-in" Ni nakirah (neno linaloenea katika jinsi).

 

Sasa katika Aayah hii, Allaah Ametumia neno"Kullu", na ametumia neno "Shay-in" katika uumbaji Wake. Kwa maana Allaah Ameumba kila kitu kidogo na kikubwa na Qur-aan ni katika kitu, kwa hiyo itakuwa imeumbwa.

 

 

Majibu Yetu Juu Ya Hoja Hii:

 

Ukiisoma kwa makini hii Qur-aan utaona kuwa Allaah Ametofautisha kabisa katika ya uumbaji na amri Zake, kwa maana uumbaji ni kitu kingine na amri ni kitu kingine kabisa.

 

Allaah Anasema ndani ya Qur-aan:

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗتَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٥٤﴾

“…Uumbaji ni Wake Pekee na kupitisha amri. Tabaaraka-Allaah, Amebarikika Allaah Rabb wa walimwengu.” [Al-A’raaf: 54]

 

Utaona kuwa katika Aayah hii, Allaah Ametofautisha kabisa kati ya uumbaji na amri. Sasa ni katika jambo la ajabu wewe usitofautishe kati ya mawili haya!

 

Anasema Imaam Ibn Abil-'Izz Al-Hanafiy (Allaah Amrehemu):

 

"ففرق بين الخلق والأمر، فلو كان الأمر مخلوقا، للزم أن يكون مخلوقا بأمر آخر، والآخر بآخر، إلى مالا نهاية له، فيلزم التسلسل وهو باطل"

"Akatofautisha kati ya kuumba na amri, na laiti amri ingekuwa imeumbwa ingelazimika kuumbwa na amri nyingine, na amri nyingine na nyingine mpaka kutokufikia mwisho, ingelazimisha kufuatana; nayo ni batili."

Sasa Allaah Mwenyewe Aliyekuwa juu, Amejaalia Qur-aan ni katika amri Yake si katika uumbaji Wake!

 

Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا ۚ ﴿٥٢﴾

“Na hivyo ndivyo Tulivyokuletea Ruwh (Qur-aan) kutoka amri Yetu.” [Ash-Shuwraa: 52]

 

Sasa Aayah hii inajulisha kuwa hii Qur-aan ni katika amri Yake Allaah na wala si katika uumbaji Wake.

 

Hili ni jambo la kwanza, jambo la pili ni kuwa si kila kitu kinaingia katika huu ujumla, anasema Allaah Aliyekuwa juu ‘Arshi Yake:

قُلْ أَيُّ شَيْءٍ أَكْبَرُ شَهَادَةً ۖ قُلِ اللَّـهُ ۖ ﴿١٩﴾

“Sema: “Kitu gani ushahidi wake ndio mkubwa zaidi?” Sema: “Allaah;…” [Al-An’aam: 19]

 

Ikajulisha kuwa Allaah ni kitu, na twakubaliana sisi kuwa Allaah hakuumbwa, na pia sifa Zake hazikuumbwa.

 

Kwa hiyo Aayah hii ambayo inasema kuwa Allaah ni Muumba wa kila kitu tunakubali kabisa, lakini tunasema kuwa Allaah Hakuiumba dhati Yake na pia Hajaziumba sifa Zake kwa sababu sifa Zake zimefungamana na dhati Yake sasa vipi ziwe zimeumbwa?

 

Na Qur-aan Allaah Ameizungumza na Jibriyl amemsikia Allaah Akizungumza na pia ni katika amri Zake, na mwenyewe Ar-Rahmaan. Ametofautisha kati ya amri na uumbaji, sasa nyie vipi mjaalie hii Qur-aan kuwa ni katika uumbaji Wake?

أَأَنتُمْ أَعْلَمُ أَمِ اللَّـهُ ۗ ﴿١٤٠﴾

“Je, nyinyi mnajua zaidi au Allaah?”

 

Hamna zaidi ya moja ya majibu mawili:

Kwamba nyie ni wajuzi kuliko Allaah Ambaye Amejaalia hii Qur-aan ni katika amri Zake na nyie mnajaalia katika uumbaji Wake.

 

Au nyie si wajuzi bali mwamsemea Allaah uongo.

 

 

Hoja Yao Ya Tatu:

 

Lugha ya Kiarabu inathibitisha kuwa Qur-aan ni kiumbe.

 

Ukiwauliza ehe kivipi?

 

Wanajibu hivi:

Kitendo "Ja'ala" kina maana ya "Kuumba". Na Allaah Anasema ndani ya Qur-aan:

 

إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٣﴾

“Hakika Sisi Tumefanya Qur-aan ya Kiarabu ili mpate kutia akilini.” [Az-Zukhruf: 3]

 

 

Majibu Yetu:

 

Ni kweli kabisa kuwa kitendo "Ja'ala" Kuna wakati kinajulisha maana ya kuumba, lakini ni wakati gani kinajulisha hivyo?

 

Mkisema kuwa wakati wote kinajulisha maana ya kuumba, tutawaambieni kuwa tafsirini Aayah hizi ambazo zipo mbele yenu:

 

 

1. Anasema Allaah Mtukufu:

 

وَأَوْفُوا بِعَهْدِ اللَّـهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلَا تَنقُضُوا الْأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا وَقَدْ جَعَلْتُمُ اللَّـهَ عَلَيْكُمْ كَفِيلًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ ﴿٩١﴾

“Na timizeni ahadi ya Allaah mnapoahidi, na wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha; na …………. Allaah kuwa ni Mdhamini wenu.  Hakika Allaah Anajua yale mnayoyafanya.” [An-Nahl: 91]

 

Hapo kwenye vidoti twawataka muweke neno "Kuumba"!

Kama maneno hayatakuwa yana ukafiri!!

 

Maana itasomeka hivi:

"Na mmemuumba Allaah"!!

 

Kutakasika na sifa mbaya ni kwa Allaah Aliyekuwa juu.

 

 

2. Anasema Allaah:

وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا ۚ ﴿١٩﴾

 

Na hapo sijui watatafsiri vipi? Kwa sababu wakiweka kitendo cha kuumba maana yake wao wamewaumba Malaika!!

 

Bila Shaka Aayah hizi na mfano wake, zinawapa wakati mgumu sana hawa watu wanaosema kuwa Qur-aan imeumbwa kisha wakadalilisha kwa kitendo "Ja'ala" Moja kwa moja pasina ya kupambanua na kuweka wazi.

 

Sasa wakifasiri kitendo Ja'ala katika Aayah hizi kwa maana ya kuumba!! Wa-Allaahi huu ni ukafiri!!

 

Lakini upi usahihi kuhusiana na hiki kitendo "Ja'ala"?

 

Hili ni somo la lugha ya Kiarabu, na nawaombeni radhi kwa kutumia lugha ya kitaalamu kwa sababu lazima tubainishe ukweli wa mas-alah haya.

 

Sasa tunasema hivi:

Kitendo katika lugha ya Kiarabu hakitoki katika hali hizi zifuatazo:

1. Laazim: Nacho ni kitendo ambacho hakina uwezo wa kumfikia mtendewa ila kwa msaada.

Mfano kitendo "Jalasa" kwa maana "Amekaa".

 

Utasema hivi katika lugha ya Kiarabu:

Jalasa Muhammadun 'alaal Kursiyyi.”

Maana: “Amekaa Muhammad juu ya kiti.”

 

Hapa unaona kuwa kitendo hiki "Jalasa" kimeshindwa kumfikia mtendewa ambaye ni kiti ila kwa msaada wa “'alaa”.

 

Na mfano mwingine:

Kitendo "Dhahaba, chenye maana “amekwenda”, utasema katika lugha ya Kiarabu:

Dhahaba Abuu Bakr ilaa Ssuuqi.”

Maana yake: “amekwenda Abuu Bakr sokoni.”

 

 Unaona wazi kabisa kuwa kitendo hiki hakijamfikia mtendewa ila kwa msaada wa “'ilaa”.

 

Sasa vitendo kama hivi kitaalam huwa vinaitwa "Af'aalul-Laazim."

 

 

2. Muta'diy: Maana yake kitendo hiki kinamfikia mtendewa bila ya msaada wowote. 

 

Mfano: kitendo "Akala" (amekula).

Utasema katika lugha ya Kiarabu:

Akala waliydun tuffaahatan.”

Maana yake: “amekula Waliyd tofaa”.

 

Umeona kuwa kitendo hiki kimemfikia mtendewa pasina msaada wowote.

 

Sasa hivi vitendo vyagawanyika sehemu kuu mbili:

 

1. Kinachomfikia mtendewa mmoja. Kama vile: “Akala”.

Kwani mfano huu upo wazi:

Akala Waliydun tuffaahatan

Akala” = kitendo.

Waliyd” = mtendaji.

Tuffaahatan” = mtendewa.

Hapa unaona kuwa mtendewa ni mmoja tu.

 

 

2. Kinachowafikia zaidi ya mtendewa mmoja.

Mfano:

A'twaa Zaydun ‘Aliyyan Kitaaban.”

Maana yake: “Zayd alimpa Aliyy kitabu”.

 

Hapo utaona kuwa:

A'twaa” = kitendo.

Zaydun” = mtendaji.

’Aliyyan” =Mtendewa namba moja

Kitaban” = Mtendewa namba mbili.

 

 

Sasa baadhi ya hivi vitendo inakuwa hivi katika hukmu:

Ikimfikia mtendewa mmoja, maana yake kadhaa. Na ikimfikia mtendewa zaidi ya mmoja maana yake inakuwa kadhaa.

 

Mfano kitendo "Ja'ala", kikimfikia mtendewa mmoja maana yake ameumba.

Mfano kauli yake Allaah:

…وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ ۖ… ﴿١﴾

Kwa sababu gani tumefasiri "Ja'ala" Kwa maana ya kuumba?

Kwa sababu katika Aayah hii, kitendo hiki kimemfikia mtendewa mmoja tu ambaye ni kiza.

 

Kwa sababu:

Ja'ala” = kitendo.

Dhwulumaat” = mtendewa.

 

Mfano mwingine kauli yake Allaah:

وَجَعَلْنَا فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ ﴿٣١﴾

 

 

Lakini kitendo hiki kikimfikia zaidi ya mtendewa mmoja maana yake si kuumba, bali itakuwa maana yake ni kufanya, kuteremsha au kuitakidi n.k.

Kama Allaah Alivyosema:

إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٣﴾

“Hakika Sisi Tumefanya (Tumeteremsha) Qur-aan ya Kiarabu ili mpate kutia akilini.” [Az-Zukhruf: 3]

 

Kwanini tumefasiri kufanya badala ya kuumba?

Kwa sababu hapa kitendo kimemfikia zaidi ya mtendewa mmoja ambayo ni Qur-aan na Kiarabu.

 

Na kwa maana hii, ndio zile Aayah ambazo niliwalazimisha wale wanaosema kuwa Qur-aan imeumbwa na kudalilisha (kutolea dalili) kwa “Ja'ala” zitakuwa zitatafsiriwa hivyo.

 

 

Fuatana na Mimi katika hoja yao namba nne.

 

 

Share