An-Naar (Moto Wa Jahannam)

An-Naar (Moto Wa Jahannam)

 

Imekusanywa na Ummu ‘Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

Katika Qur-aan na Hadiyth kumetajwa moto kuonesha mazingira mabaya watakayoshukiwa watu waovu, Waliompinga Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) na kuendesha maisha yao ya hapa duniani kinyume na kanuni na taratibu alizoziweka Allaah (Subhaanahu Wa Ta’alaa).

 

 

Maisha ya motoni ni kinyume na maisha ya Jannah (Peponi). Tunafahamishwa katika Qur-aan kuwa motoni kuna daraja au milango saba, na kila mlango iko sehemu iliyogawanywa Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 

وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٤٣﴾ لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَابٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ﴿٤٤﴾ 

Na hakika Jahannam ni miadi yao wote pamoja. 44. Una milango saba, na kwa kila mlango iko sehemu (makhsusi) iliyogawanywa. [Al-Hijr: 43 - 44].

 

Daraja hizi za moto zimepewa majina kama tusomavyo katika Qur-aan:

 

 

Jahannam:

 

Katika Aayah nyingi jina hili limetumiwa, Kama jina la ujumla la maisha ya Motoni. Kama katika baadhi ya Aayah hizi Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:

 

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ ﴿٩٨﴾

Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia. [Al-Anbiyaa: 98].

 

Anasema pia Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

ثُمَّ لَنُحْضِرَنَّهُمْ حَوْلَ جَهَنَّمَ جِثِيًّا ﴿٦٨﴾

Kisha Tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam wapige magoti. [Maryam: 68].

 

 

 

Lahab: Moto wenye muwako mkubwa kabisa.

 

Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ ﴿٣﴾

Ataingia na kuungua moto wenye mwako. [Al-Masad: 3].

 

 

 

Al-Hutwamah: Moto wa kuvunja vunja, unaonyambua nyambua, moto uliowashwa kwa ukali.

 

Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

كَلَّاۖ لَيُنبَذَنَّ فِي الْحُطَمَةِ ﴿٤﴾

Laa hasha! Atavurumishwa katika Al-Hutwamah (moto mkali unaonyambua nyambua). [Al-Humazah: 4].

 

 

 

Sa’iyraa: Moto ulioashwa vikali mno wa kuunguza.

 

 

Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ بِهِ وَمِنْهُم مَّن صَدَّ عَنْهُ ۚ وَكَفَىٰ بِجَهَنَّمَ سَعِيرًا ﴿٥٥﴾

Basi miongoni mwao wako waliomuamini (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na miongoni mwao wako waliomkengeuka. Na Jahannam inatosheleza kuwa ni moto uliowashwa vikali mno. [An-Nisaa: 55].

 

 

 

Saqar: Moto unaobabua.

 

Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 سَأُصْلِيهِ سَقَرَ﴿٢٦﴾

Nitamuingiza kumuunguza kwenye moto mkali mno. [Al-Mudaththir: 26].

 

 

 

Jahiym: Moto uwakao mkali mno.

 

 

Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِلْغَاوِينَ ﴿٩١﴾

Na utadhihirishwa moto uwakao vikali mno kwa wapotofu. [Ash-Shu’araa: 91].

 

Anasema pia Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

لَتَرَوُنَّ الْجَحِيمَ ﴿٦﴾

Bila shaka mngeuona moto uwakao vikali mno.  [At-Takaathur: 6].

 

Anasema pia Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِمَن يَرَىٰ ﴿٣٦﴾

Na moto uwakao vikali mno utakapodhihirishwa wazi kwa aonaye. [An-Naazi’aat]

 

 

 

Haawiyah: Moto uwakao vikali mno.

 

Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 فَأُمُّهُ هَاوِيَةٌ ﴿٩﴾

Basi makazi yake ni Haawiyah. [Al-Qaari’ah: 9].

 

 

 

Wahalifu  wataingia katika aina hizi za Moto kulingana na makosa yao. Kwa ujumla aina yoyote ya moto ulioandaliwa kwa ajili ya makafiri hata ukiwa na daraja ya chini namna gani, Utakuwa ni mkali usio na mfano na usiovumilika hata kwa muda mfupi sana kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anavyotufahamisha:

 

إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴿٦٦﴾

Hakika hiyo (Jahannam) ni mahali paovu mno pa kustakiri na mahali pa kuishi. [Al-Furqaan: 66]

 

 

Pia tuone anavyotufahamisha Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kiwango wa adhabu ya motoni.

 

 

Nuuman bin Bashiyr amesimulia kuwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema; “Hakika atakayekuwa na adhabu nyepesi kabisa katika wakazi wa motoni ni yule atakayekuwa na viatu vya moto, Kwa moto huu, (wa miguu utachemsha ubongo wake kama maji yachemkavyo kwenye birika). Haitaonekana kuna kiwango cha chini kabisa cha adhabu.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Kwa ujumla moto wa adhabu alioandaa Allaah (Subhaananu Wa Ta’ala) kwa watu waovu ni mkali sana.

 

 

Ndani ya mazingira ya motoni patakuwa na miti michungu, Na mti maarufu kwa uchungu ni “Zaqquwm”. Tunapata maaelezo kamili ya mti wa “Zaqquwm” ambao umeenea katikati ya Jahannam na watakaostahiki kuula ni katika Aayah zifuatazo:

 

 أَذَٰلِكَ خَيْرٌ نُّزُلًا أَمْ شَجَرَةُ الزَّقُّومِ ﴿٦٢﴾ إِنَّا جَعَلْنَاهَا فِتْنَةً لِّلظَّالِمِينَ ﴿٦٣﴾ إِنَّهَا شَجَرَةٌ تَخْرُجُ فِي أَصْلِ الْجَحِيمِ ﴿٦٤﴾ طَلْعُهَا كَأَنَّهُ رُءُوسُ الشَّيَاطِينِ ﴿٦٥﴾ فَإِنَّهُمْ لَآكِلُونَ مِنْهَا فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ ﴿٦٦﴾ ثُمَّ إِنَّ لَهُمْ عَلَيْهَا لَشَوْبًا مِّنْ حَمِيمٍ ﴿٦٧﴾

Je hiyo (Jannah) ni mapokezi bora au mti wa zaqquwm (motoni)? Hakika Sisi Tumeufanya (zaqquwm) kuwa ni jaribio kwa madhalimu. Hakika huo ni mti unaotoka katika kina cha moto uwakao vikali mno.  Mashada ya matunda yake kama kwamba ni vichwa vya mashaytwaan.  Basi hakika wao watakula humo na watajaza matumbo yao kwayo. Kisha hakika wao watapata mchanganyiko wa maji yachemkayo. [Asw-Swaffaat: 62 - 67].

 

 

Pia katika mazingira ya motoni patakuwa na nyoka na n’ge wakubwa wenye sumu kali watakaowauma wakazi wa humo kama sehemu ya adhabu yao kama tunavyo fahamishwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

‘Abdullaah bin Haarith bin Jaazin amesimulia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa: “Kuna nyoka huko motoni wakubwa kama ngamia, Mmoja wao akikuuma mara moja uchungu wake hubakia kwa miaka arubaini. Kuna nnge huko motoni wakubwa kama nyumba, Mmoja wao akimuuma mtu uchungu wake utabakia kwa muda wa miaka arubaini.” [Ahmad].

 

 

Kwa vyovyote itakavyokuwa maisha ya motoni yatakuwa magumu sana kwa wakazi wake. Chakula chao kitakuwa cha moto wa kuunguza kila kitu tumboni, Mavazi yao yatakuwa ya moto, Kinywaji chao cha moto kitakachochemsha matumbo yao kama maji yachemkavyo kwenye sufuria ya shaba. Picha halisi ya mazingira ya motoni, Maisha ya wakazi wake na sifa zinazowafanya wastahiki kuingia humo. Tutazame baadhi tu ya Aayah hapa:

 

 

وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الْمُجْرِمُونَ نَاكِسُو رُءُوسِهِمْ عِندَ رَبِّهِمْ رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ ﴿١٢﴾ وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿١٣﴾ فَذُوقُوا بِمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا إِنَّا نَسِينَاكُمْ ۖ وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٤﴾

Na ungeliona pale wahalifu wanainamisha vichwa vyao mbele ya Rabb wao (wakisema): Rabb wetu! Tumekwishaona, na tumeshasikia; basi turejeshe tutende mema, hakika sisi sasa ni wenye yakini.   Na Tungelitaka, Tungeliipa kila nafsi mwongozo wake, lakini imethibiti kauli kutoka Kwangu kwamba: Bila shaka Nitajaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.   Basi onjeni kwa sababu ya kusahau kwenu kukutana na Siku yenu hii. Hakika Nasi Tumekusahauni; na onjeni adhabu yenye kudumu kwa yale mliyokuwa mkiyatenda. [As-Sajdah: 12 - 14].

 

 

Na katika Suwratul Al-Nabaa Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

 

إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا ﴿٢١﴾ لِّلطَّاغِينَ مَآبًا ﴿٢٢﴾ لَّابِثِينَ فِيهَا أَحْقَابًا ﴿٢٣﴾ إِلَّا حَمِيمًا وَغَسَّاقًا ﴿٢٥﴾ جَزَاءً وِفَاقًا ﴿٢٦﴾ إِنَّهُمْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ حِسَابًا ﴿٢٧﴾ وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كِذَّابًا ﴿٢٨﴾ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ كِتَابًا ﴿٢٩﴾ فَذُوقُوا فَلَن نَّزِيدَكُمْ إِلَّا عَذَابًا ﴿٣٠﴾

 

Hakika Jahannam utakuwa wenye kuvizia. Kwa walioruka mipaka wakaasi, mahali pa kurejea. Watabakia humo dahari nyingi. Hawatoonja humo cha baridi na wala kinywaji. Isipokuwa maji yachemkayo na usaha.  Jazaa inayowafikiana kabisa.  Hakika wao walikuwa hawataraji kuhesabiwa. Na walikadhibisha Aayaat (na ishara, hoja…) Zetu kabisa! Na kila kitu Tumekitia hesabuni barabara kwa kuandika. Basi onjeni kwani Hatutokuzidisheni isipokuwa adhabu. [An-Nabaa: 21 - 30].

 

 

Na katika Suwratul Al-Fajr:

 

 

وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَۚ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٢٣﴾ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي قَدَّمْتُ لِحَيَاتِي ﴿٢٤﴾ فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ ﴿٢٥﴾ وَلَا يُوثِقُ وَثَاقَهُ أَحَدٌ ﴿٢٦﴾

Na italetwa siku hiyo Jahannam; siku hiyo mwana Aadam atakumbuka, lakini wapi atapata ukumbusho?  Atasema: Ee, laiti ningelikadimisha (mazuri) kwa ajili ya uhai wangu (wa Aakhirah).  Basi siku hiyo hakuna yeyote atakayeadhibu kama adhabu Yake. Na wala hakuna yeyote atakayefungisha (madhubuti) kama kufungisha Kwake (waovu). [Al-Fajr: 23 - 26].

 

Kama tunavyoona Aayah hizi kwa ujumla zinatilia mkazo wale watakaostahiki adhabu ya motoni ambao ni wana-Aadam na majini waovu walioendesha maisha yao hapa duniani kwa kibri kinyume na utaratibu uliowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

 

Ndugu katika Iymaan, tujilinde na adhabu hiyo kali kabisa ya moto, adhabu isiyo na mfano na moto usioweza kulinganishwa na moto wa aina yoyote uliopo hapa duniani. Tujikinge sisi na familia zetu kwa kufanya ‘amali njema zitakazomridhisha Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) na tuzitekeleze kwa njia safi na sahihi kama tulivyoelekezwa kwazo na Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa) Atukinge na adhabu ya moto, sisi na vizazi vyetu na Waislam wote kwa ujumla, Aamiyn.

 

 

 

Share