01-Ruqyah Ya Shariy'ah Na Hukmu Zake

 

 Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah

 

Ruqyah Ya Kishariy’ah Na Hukmu Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Maradhi  na  madhara yoyote yale hayamsibu mtu isipokuwa kwa majaaliwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini kwa rahmah Yake ‘Azza wa Jalla, Amejaalia shifaa (poza) kwa kila maradhi na kila dhara, kwa kutumia ruqyah pamoja na tiba ya Sunnah, na pia kutokana miti na majani kadhaa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amejaalia kuwa ina tiba ndani yake kwa dalili:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَا أَنْزَلَ اللَّهُ دَاءً إِلاَّ أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً)) رواه البخاري   

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Hakuteremsha maradhi isipokuwa Ameyateremshia shifaa)) [Al-Bukhaariy]

 

Pia:

وعَنْ جَابِرٍعَنْ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم؛ أَنَّهُ قَالَ: ((لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءٌ، فَإِذَا أُصِيبَ دَوَاءُ الدَّاءِ بَرَأَ بِإِذْنِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ)‏) رواه مسلم  

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kuna dawa kwa kila maradhi, na pindi dawa inapotumiliwa katika maradhi huponyesha kwa idhini ya Allaah ‘Azza wa Jalla)) [Muslim katika Kitaab As-Salaam]

 

Pia:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابن مَسْعُدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يُنْزِلْ دَاءً إلاَّ  أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً عَلِمَهُ مَنْ عَلِمَهُ، وَجَهِلَهُ مَنْ جَهِلَهُ))

Kutoka kwa Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla) Hakuteremsha maradhi ila Ameteremsha pamoja nayo shifaa, amejifunza aliyejifunza na amekuwa jahili aliyekuwa jahili kwayo)) [Musnad Ahmad (6/121) kwa isnaad Swahiyh. Taz. Majmuw’ Fataawa Ibn Baaz (1/171), (6/290)]

 

 

Imekatazwa kutumia dawa za haraam kwa dalili:

 

عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه)  قَالَ:  قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((إِنَّ اللَّهَ أَنْزَلَ الدَّاءَ وَالدَّوَاءَ، وَجَعَلَ لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءً، فَتَدَاوَوْا ولاَ تَدَاوَوْا بِحَرَامٍ))

Kutoka kwa Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah Ameteremsha maradhi na dawa zake, Akajaalia kwa kila maradhi kuna dawa yake, basi jitibuni wala msijitibu kwa yaliyo haraam)) [Abuu Daawuwd, Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy ameipa daraja ya Hasan, Taz. Takhiryj Mishkaat Al-Maswaabiyh (4/272), Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (1762) au (2390)]

 

Inafaa kusoma Suwrah au Aayah ambazo imepatikana dalili zake, lakini Qur-aan nzima ni shifaa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾

Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rahmah kwa Waumini; na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara. [Al-Israa: 82]

 

Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini. [Yuwnus: 57[

 

'Ulamaa wamejuzisha ruqya pindi ikipatikana masharti matatu ambayo ameyanukuu Al-Haafidhw Ibn Rajab (Rahimahu-Allaah):

  1. Iwe kwa maneno ya Allaah (Ta’aalaa) au kwa Majina Yake na Sifa Zake.
  2. Isomwe kwa lugha ya Kiarabu.
  3. Aitakidi kwamba si ruqya pekee ndiyo itakayomponyesha bali aitakidi kwa uwezo wa Allaah (Ta’aalaa).

Pia zifutazo ni nukta muhimu Muislamu azingatie kabla ya kufanya ruqyah:

 

1-Uitakidi moyoni mwako kwamba njia yoyote uitumiayo ikiwa ni ruqyah, au kutumia dawa, hakupatikani shifaa isipokuwa kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kwa hiyo uanze kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee ili Akutakabalie ruqyah yako.

 

 

2-Unaweza kutumia Aayah na du’aa za Qur-aan na Sunnah madamu tu hutozitumia kwa kuziwekea idadi maalumu, au wakati maalumu ambavyo haikupatikana dalili, au kutumia njia nyinginezo kama kuweka kwenye hirizi, au kutundika mahali n.k. ambapo itakuingiza katika shirki. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya hayo aliposema:

 

عَنْ عَوْفِ بْنِ مَالِكٍ الأَشْجَعِيِّ قَالَ: كُنَّا نَرْقِي فِي الْجَاهِلِيَّةِ فَقُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ، كَيْفَ تَرَى فِي ذَلِكَ؟ فَقَالَ: ((اعْرِضُوا عَلَيَّ رُقَاكُمْ لاَ بَأْسَ بِالرُّقَى مَا لَمْ يَكُنْ فِيهِ شِرْكٌ))

Kutoka kwa ‘Awf bin Maalik Al-Ashja’iyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Tulikuwa tunafanya ruqyah katika zama za jahiliyyah, tukasema: Ee Rasuli wa Allaah,  unaonaje katika hayo (ruqyah yetu]? Akasema: ((Nionyesheni ruqyah yenu, hakuna ubaya katika ruqyah madamu tu haitokuwa na shirki)) [Muslim katika Kitaab As-Salaam, Abuu Daawuwd katika Kitaab Atw-Twibb]

 

3-Akipenda mtu, anaweza kubakia katika kutawakkal kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee bila ya kujizingua au kuomba kufanyiwa ruqyah kama ni mojawapo ya fadhila za kumuingiza mtu Jannah bila ya kuhesabiwa kama alivyosema  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مِنْ أُمَّتِي سَبْعُونَ أَلْفًا بِغَيْرِ حِسَابٍ: هُمْ الَّذِينَ لاَ يَسْتَرْقُونَ ولاَ يَتَطَيَّرُونَ وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ))

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wataingia Jannah kati ya Ummah wangu watu elfu sabini bila ya hesabu; hao ni wale ambao hawaombi kufanyiwa ruqyah, wala hawatabirii nuksi au mkosi, wala kujitibu kwa moto, bali wanatawakkal kwa Rabb wao tu.)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

​Tunaona kwenye Hadiyth hiyo kuwa, ni bora zaidi mtu kujizuia kuomba kufanyiwa ruqyah -  japo ni jambo lenye kuruhusiwa-, lakini ni bora zaidi kuacha kuomba kufanyiwa ruqyah na kuwa ni mwenye kutawakkal kwa Allaah, kwa sababu hiyo ni katika sababu ya kupata Pepo.

 

 

4-Ujiepushe  na kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kinyume chake ni kudumisha Tawhiyd ya Allaah (kumpwekesha) kwa Ar-Rubuwbiyyah (Uola), Al-Uluwhiyyah ('Ibaadah), na Asmaa wasw-Swifaat (Majina na Sifa Zake).

 

5- Ujiepushe na maasi na ubakie katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

5-Udumishe Adhkaar za asubuhi na jioni, na Adhkaar za kulala kwa mfululizo bila ya kuacha  hata baada ya kupata tiba ili ujikinge kutokurudiwa tena kudhuriwa na viumbe viovu na shari zao.

 

 

6-Uvute subira na ukumbuke fadhila za kuvuta subira ili zikusaidie kuvumilia madhara yaliyokusibu.

 

 

7-Uanze kusoma ruqyah kwa thanaa - kumtukuza na kumsifu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kufuata adabu za kuomba du’aa  ili itakabaliwe ruqyah yako.

 

 

 

Share