Kusogea Kumpisha Mtu Katika Swalaah Inajuzu?

SWALI:

Haifai wakati wa kusali kumpisha mtu badala yako kama mfano ni mtu mzima?


 

JIBU:

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shaykh ibn 'Uthaymiyn يرحمه الله   amesema kwamba msingi wa sheria katika mas-ala ya kusogea (kufanya harakaat) katika Swalah ni makruuh (jambo la kuchukiza) isipokuwa imefanyika kwa sababu na akagawanya hizo sababu katika aina tano:

  1. Harakaat (mishughuliko) iliyowajibika
  2. Harakaat zilizoharamishwa
  3. Harakaat za mustahabbah (zinazopendekezeka)
  4. Harakaat zinazoruhusiwa
  5. Harakaat zilizokuwa ni makruuh (kuchukiza)

 

Harakaat zilizizowajibika

Ni zile ambazo zinategemea kuswihi kwa Swalah yenyewe. Kwa mfano mtu akiona najsi katika kofia yake, aivue kofia. Hii ni kwa sababu Jibriyl عليه السلام alikuja kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akiswalisha watu, na akamwambia kuwa kuna uchafu katika kiatu chake. Hivyo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akakivua na huku anaswali na akaendelea kuswali. [Imesimuliwa na  Abuu Daawuud na ikiwa ni sahihi kutoka kwa Shaykh Albaaniy katika Al-Irwaa]

Vile vile ikiwa mtu ameambiwa kuwa hakuelekea Qiblah basi ageuke na kuelekea Qiblah.

Harakaat zilizoharamishwa

Hizi ni zile ambazo ni kila mara zinazofanyika bila ya sababu, kwa sababu aina ya harakaat hizi zinabatilisha Swalah, na chochote kinachobatilisha Swalah hakifai kutendeka kwani ni kama kufanya mzaha na alama za Mwenyezi Mungu.

Harakaat zinazopendekezeka (Mustahabbah)

Hizi ni zile zinazotendeea kwa ajili ya kufanya vinavyopendekezeka katika Swalah, mfano kama mtu kusogea kuunga swaff (mstari) au anapoona mtu kuna uwazi katika mstari wa mbele, atasogea kujaza uwazi huo kwani hivyo ni kuifanya Swalah iwe bora zaidi na imekamilika. Ibn 'Abbaas رضي الله عنه aliposwali na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisimama kushoto kwake, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimvuta kwa kumshika kichwa chake kwa nyuma na akamfanya asogee kusimama kulia kwake. [Al-Bukhaariy na Muslim]

Harakaat zilizoruhusiwa

Ni zile ndogo ndogo zinazotokana na sababu fulani au harakaat kubwa penye kuhitajika. Harakaat ndogo kama mfano Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akiswali na huku amembeba Umaamah, mjukuu wake  kutoka kwa mwanawe Zaynab. Alipokuwa akisimama alikuwa akimbeba na alipokuwa akienda kusujudu alikuwa akimuweka chini. [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

Harakaat zinazochukiza (Makruuh

Hizi ni zote nyinginezo ambazo zisizokuwa aina ya hizo zilizotajwa juu. Na hii ni sheria ya msingi kuhusu harakati (kusogea) kwenye Swalah.

 

Hivyo tunaweza kusema kuwa kumpisha mtu mzima itakuwa ni katika harakaat za mustahabbah (zenye kupendekezeka) kwa hiyo inafaa kufanya hivyo. 

Jambo la kuzingatia ni kuhusu idadi ya harakaat hizo:

Amesema Shaykh ibn 'Uthaymiyn kuwa "Zikiwa ni harakaat nyingi itakuwa ni kama mtu asiyeswali. Kwa hiyo harakaat hizo zitabatilisha Swalah. Na ndio maana wataalamu wameeleza maana yake kuwa ni kutokana na al'urf (mazoea) na wakasema: "Ikiwa harakaat zitakuwa ni nyingi na za kuendelea basi Swalah itabatilika", bila ya kutaja idadi ya harakaat. Baadhi ya Maulamaa wametaja idadi ya harakaat kuwa ni tatu, lakini hii inahitaji dalili kwa sababu kuweka idadi yoyote lazima iweko dalili au sivyo itakuwa ni kuzua fikra mpya". [Majmuu' Fataawa al-Shaykh, 13/309-311]

 

Dalili kuwa harakaat ndogo ndogo au za kuendelea kuwa haziharibu Swalah ni ripoti kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimfungulia Bibi 'Aishah رضي الله عنها mlango uliofungwa kwa kusogea inavyosemekana kuwa ni zaidi ya harakat tatu. [Abu Daawuud, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy, Ahmad ikiwa ni Sahiyh kutoka kwa Sh Albaaniy]

Vile vile ripoti tuliyotaja juu alipombeba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  mjukuu wake wakati wa kuswali na kumuweka chini alipokuwa akisujudu.

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

 

Share