Hukmu Ya Kusherehekea Siku Ya Mama (Mother's Day)

Hukmu Ya Kusherehekea Siku Ya Mama (Mother's Day)

 

 

www.alhidaaya.com

 

 

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu was-Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad,

 

 

Utafiti umeonyesha kwamba siku hii imeanza kutokana na sherehe za majira ya kuchipua (spring) ya Wagiriki wa kale. Sherehe hizo zilipendekezwa kwa mungu wa kike Rhea, mke wa Cronos, baba wa mungu. Rome ya kale, kulikuwa na sherehe zilizofanana na hizi zilizopendekezwa kwa kumuabudu na kumpa heshima kubwa Sybil, mungu mwingine wa kike. Hii imeanza takriban miaka 250 kabla ya kuzaliwa 'Iysaa ('Alayhis-Salaam). Sherehe hizi za kidini za Warumi ziliitwa 'Hilaria' na zilidumu kwa muda wa siku tatu kuanzia Machi 15 hadi Machi 18. 

 

 

Tarehe Za Kusherehekea Siku Hii Ya 'Mother's Day' Katika Nchi Mbali Mbali

 

Tarehe ya kusherehekea siku hii ni tofauti katika kila nchi na nchi. Norway wanasherehekea Jumapili ya pili katika mwezi wa Februari. Argentina wao ni Jumapili ya pili katika mwezi wa Oktoba. Lebanon siku ya kwanza ya msimu wa majira ya kuchipua (spring). Afrika Kusini ni Jumapili ya mwanzo katika mwezi wa Mei. Ufaransa ni Jumapili ya mwisho ya mwezi wa Mei, wao hukusanyika katika chakula cha usiku kisha humpa mama keki. Sweden huwa ni siku ya famiia Jumapili ya mwisho katika mwezi wa Mei. Jamii ya Msalaba Mwekundu wa Sweden huuza maua katika plastiki ndogo ili wawape mama zao ambao wanabakia sikukuu kulea watoto wao. Japan ni Jumapili ya pili katika mwezi wa Mei. Amerika ya Kaskazini ambako hufanywa maonyesho ya picha za watoto wenye umri wa miaka 6-14. Maonyesho hayo yanaitwa 'Mama Yangu'. Kisha maonyesho hayo husogezwa kila baada ya miaka minne na kutokeza nchi mbali mbali.

 

Nchi nyingine nyingi husherehekea ziku hii kwa tarehe mbali mbali. Nchi za Arabuni imeanza kusherehekewa Misri nayo ni tarehe 21 Machi 1956. Siku hiyo pia ni siku ya mwaka mpya wa Wakristo Wa Kikhufti (Coptic Christians) na sherehe za Nawroz za Wakurdi. Kisha tena ndio ikaenea nchi zote nyingine za kiarabu. Na wote hao walioanza kusherehekea sikukuu hii ni aidha washirikina, Mayahudi au Manaswara. 

 

 

 

Hukumu Ya Shariy'ah Ya Kiislamu Kwa Kusherehekea Siku Hii

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuonya:

 

((وَلَن تَرْضَى عَنكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ))

 

((Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao)) [Al-Baqarah: 120]

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile ametuonya:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لَتَتْبَعُنَّ سَنَنَ مَنْ كَانَ قَبْلَكُمْ شِبْرًا شِبْرًا وَذِرَاعًا بِذِرَاعٍ حَتَّى لَوْ دَخَلُوا جُحْرَ ضَبٍّ تَبِعْتُمُوهُمْ)) قُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ: الْيَهُودُ وَالنَّصَارَى؟  قَالَ: ((فَمَنْ)) البخاري ومسلم

Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyyi kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtafuata Sunnah (nyendo) za watu waliokuwa kabla yenu, kiganja kwa kiganja, mkono kwa mkono, hata wakiingia kwenye shimo la kenge mtawafuata)).  Tukasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah, je, una maanisha Mayahudi na Manaswara?" Akasema: ((Ndiyo, kwani nani zaidi ya wao?))  [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Baadhi ya watu katika Ummah wetu wa Kiislamu bado wako katika ujinga  wa kuigiza makafiri katika sikukuu zao, mila na utamaduni wao na kuacha mafunzo yetu ya Kiislamu ya thamani ambayo yana mafundisho mema zaidi na yenye manufaa kwetu katika maisha yetu ya duniani na Aakhirah.

 

 

Miongoni mwa sikukuu hizo, wanazozishereheka baadhi ya Waislamu ni 'Siku ya Baba' (Father's Day) 'Siku ya Wapendanao' (Valentine's Day) na kama siku hii ya 'Siku ya Mama' (Mother's Day) ambayo wameifanya ni siku hasa ya kumkumbuka na kumpa heshima mama. Siku hii mama hupewa zawadi, au kadi yenye maneno ya kumuamkia, kumpa pongezi na maneno ya mapenzi. Kisha baada ya siku kwisha hurudi watu katika hali yao ya kukata mawasiliano na mama au kutokumtii. Hivyo huo ulikuwa ni udanganyifu tu.

 

 

 

Uislamu Umetufunza Vizuri Zaidi Kutii Wazazi

 

Jambo la kusikitisha kwa wale wanaoigiza makafiri katika mila zao ni kwamba wamekosa kutambua kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)Ameharamisha katika Qur-aan na Sunnah kutokuwatii wazazi wetu na Am etuamrisha tuwatii na kwa kufanya hivyo Atatulipa thawabu na kutupa daraja ya juu.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa):

 

((وَاعْبُدُواْ اللّهَ وَلاَ تُشْرِكُواْ بِهِ شَيْئًا وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا))

 

((Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsaan wazazi wawili...))  [An-Nisaa: 36]

 

Na mafundisho kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kuwatii wazazi hasa mama ni mengi miongoni mwa hayo ni:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أنّه قَالَ: جَاءَ رَجُلٌ إِلَىٰ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ! مَنْ أَحَقُّ النَّاسِ بِحُسْنِ صَحَابَتِي؟ قَالَ: ((أُمُّكَ)) قَالَ:ثُمَّ مَنْ؟ قَالَ: ((أُمُّكَ)) قَالَ: ثُمَّ مَنْ؟ قَالَ:  ((أُمُّكَ)) قَالَ: ثُمَّ مَنْ؟ قَالَ: ((ثُمَّ أَبُوكَ)) متفق عليه.

Kutoka kwa Abuu Hurayrah رضي الله عنه kwamba alikuja mtu kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamuuliza: "Ee Rasuli wa Allah, nani mwenye haki zaidi mimi kumfanyia wema?". Akasema: ((Mama yako)). Akauliza: "Kisha nani?". Akasema: ((Mama yako)). Akauliza: "Kisha nani?" Akasema: (Mama yako) Akauliza: "Kisha nani?" Akasema: ((Kisha baba yako)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Vile vile:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهم عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ((رَغِمَ أَنْفُ ثُمَّ رَغِمَ أَنْفُ ثُمَّ رَغِمَ أَنْفُ)) قِيلَ مَنْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ:  ((مَنْ أَدْرَكَ وَالِدَيْهِ عِنْدَ الْكِبَرِ، أَحَدَهُمَا أَوْ كِلَيْهِمَا، ثُمَّ لَمْ يَدْخُلِ الْجَنَّةَ))

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Amekhasirika, amekhasirika, amekhasirika)) Ikasemwa: Nani yaa Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Mtu ambaye amemfikia mzazi wake mmoja akiwa katika umri wa uzee, mmojawapo au wote wawili  kisha asiingie Jannah [kwa sababu ya kutowafanyia wema])) [Muslim]

 

 

Ibn Battwaal amesema: "Hii ina maana kwamba mama afanyiwe wema mara tatu zaidi ya baba, kwa sababu ya mashaka aliyoyapata alivyobeba mimba, kuzaa na kunyonyesha. Mashaka haya yanamfika mama pekee kisha baba anasaidia katika kulea na ndio maana Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Anasema:

 

((وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَى وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ))

 

((Na Tumemuusia insani kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa katika miaka mwili; ya kwamba, unishukuru Mimi, na wazazi wako; Kwangu ndio mahali pa kuishia.)) [Luqmaan: 14]

 

Al-Qurtwubiy amesema:

"Inavyomaanisha ni kwamba Mama anastahiki zaidi kupewa heshima na mtoto na haki zake kutoka kwa mtoto zimezidi kuliko za baba inapofikia hali ya kuchagua baina ya wawili".

 

'Iyyaadhw amesema:

"Rai za 'Ulamaa wengi ni kwamba mama atangulie kupewa heshima kuliko baba katika kufadhilishwa wazazi". [Fath-AlBaari 10/402]

 

Hata kama wazazi sio Waislamu basi Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Ametuamrisha tuwafanyie wema, ila tu tusiwatii pindi wanapotuamrisha katika maasi ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa):

 

 ((وَإِن جَاهَدَاكَ عَلى أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا))

 

((Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani, na fuata njia ya anayerudi kutubia Kwangu.)) [Luqmaan: 15]

 

Kwa hiyo hali ya Muislamu katika kuwafanyia wema wazazi hasa mama ni bora kuliko makafiri ambao sisi ndio tunaowaigiza mila zao kama hizi za kumuwekea mama siku yake hasa ya kumkumbuka na kumfanyia wema. Sisi Waislamu tunatakiwa kila siku kwetu iwe ni siku ya kumkumbuka mama na kumfanyia wema na ihsani katika umri wake wote hadi anapoiaga dunia.

 

Si mama pekee, hata baba hali kadhalika anastahiki kufanyiwa wema kama mama na kukumbukwa, na wala tusiwadharau au kuchoshwa nao wanapofikia umri wa uzee na kuwaacha bila kuwashughulikia tena wala kujali hali zao au kuwavunjia heshima zao kwa kuwajibu ufedhuli kama zilivyo tabia za hao makafiri tunaowaigiza. Kisha tunasahau kwamba wao ndio waliopata tabu ya kutulea sisi hadi tukafika umri wa kuweza kusimama wenyewe na kuendesha maisha yetu. Nani basi walio bora zaidi? Wao wanaowatupa wazee wao katika majumba ya serikali ya watu wazima au sisi Waislamu tulioamrishwa tuwafanyie wema hata katika uzee wao kama Alivyotumarisha Allaah Subhaanahu Wa Ta’aalaa?

 

((وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾))

((وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾)) 

 

((Na Rabb wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima.))

 

((Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: “Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni.”)) [Al-Israa: 23-24]

 

Katika Aayah hiyo, Ameanza Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)kutuamrisha tumuabudu Yeye Pekee bila ya kumshirikisha, kisha moja kwa moja Ametuamrisha tuwatii wazazi wetu. Basi hatuoni jinsi gani kuwafanyia wema wazazi kulivyotiliwa uzito na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)?

 

 

 

Hukumu Ya Kusherehekea Siku Ya Mama (Mother's Day)

 

Sikukuu Zetu Waislamu  

 

Waislamu hatuna sikukuu zaidi ya mbili; 'Iydul-Fitwr na 'Iydul-Adhhaa. Pia Ijumaa ni katika siku tukufu, na siku zote hizi zinaambatana na ibaada kama sikukuu kubwa mbili:  

 

Katika Sunnah, Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: ''Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja Madiynah na walikuwa wana siku mbili ambazo walikuwa wakipumzika na kustarehe na kucheza. Akasema: ((Hizi ni siku gani?)) Wakasema: "Ni siku ambazo tulikuwa tukicheza na kustarehe katika Ujahiliya". Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Allaah Amekupeni zilizo bora kuliko hizo; Yawmul-Adhwhaa  ['Iydul-Adhwhaa] na Yawm Al Fitwr ['Iydul-Fitwr] )) [Abu Daawuud]

 

 

 

Kusherehekea Uzushi Kama Huu Unampeleka Mtu Katika Upotufu Na Hata Motoni

 

Siku kama hizi hazitupasi Waislamu kusherehekea kwani hazina asili ya dini yetu bali ni uzushi ambao umeharamishwa katika dini yetu. Na uzushi huu ni kama uzushi wanaozua Waislamu kama uzushi wa maulidi, khitmah, nusu ya mwezi wa Shaabani na kadhalika. Na uzushi huu ni wa dini nyingine kabisa za washirikina na makafiri. Hivyo humpeleka Muislamu aingie katika kufru na shirki. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ametuonya katika Hadiyth nyingi kuhusu mas-ala haya kama ifuatavyo:

 

Akisema katika Khutbah ya Ijumaa,

 

 ((أما بعد، فإن خير الحديث كتاب الله وخير الهدى هدى محمد صلى الله عليـه وسلم وشر الأمورمحدثاتها وكل بدعة ضلالة))

 خرجه مسلم في صحيحه 

 

((Amma Ba'ad hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu cha Allaah, na uongofu ulio bora ni uongofu wa Muhammad صلى الله عليه  وسلم na jambo la shari kabisa ni uzushi wake na kila uzushi ni upotofu)) [Muslim] na katika riwaaya nyingine ((na kila upotofu ni motoni)).

 

 

Kitendo Cha Uzushi Hakipokelewi

 

 ((من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد)) متفق عليه

 

((Atakayezusha katika jambo letu (Dini yetu) basi litarudishwa (halitokubaliwa))) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Shaykh 'Abdul-'Aziyz bin Baaz ameona kwamba kusherehekea siku hii ni kuwatia majonzi na huzuni watoto waliokuwa hawana mama. Na Uislamu umeamrisha kuwaheshimu wazazi wote. 

 

Kwa hiyo inatupasa tukhofu kuingia katika hatari za uzushi na vile vile ni wajibu wetu kuwaonya ndugu zetu wengine wasiingie na wao katika upotofu huu na turidhike na yale Aliyotufunza Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)  na  Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  katika dini yetu tukufu. Kufuata mafundisho ya dini yetu ya kumheshimu mama kila siku ni bora kuliko kuiweka siku moja iwe hasa ndio yake, kisha adharauliwe siku nyingine.

 

 

Aliyoyasema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanadhihirika kweli kwamba Ummah huu, isipokuwa Aliowahidi Allaah, wamefuata nyendo, mila na desturi nyingi za washirikina, Mayahudi na Manaswara hadi Uislamu umekuwa kama ni ugeni na mafundisho ya hao makafiri yamekuwa ni bora kuliko mafunzo ya Kiislamu mbele ya macho na fikra za watu wengi. Mema ya Kiislamu yanaonekana kuwa ni maovu, na maovu ya makafiri yanaonekana kuwa ni mema. Sunnah zimetengwa mbali na kufuatwa bid'ah na ndio umekuwa mwendo wa Waislamu wengi, kwa sababu ya ujinga wa kuigiza tu watu bila ya dalili, na kutopenda kujifunza mafunzo mema yaliyo sahihi ya Kiislamu. Mafunzo ambayo yamekamilika na kumfaa kila binaadamu popote na wakati wowote.

Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa):

 

((الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينا))

 

((Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.)) [Al-Maaidah: 3]

 

Na katika kukamilika Shariy'ah ya dini hii tukufu, kila Muislamu iwe dhaahir kwake kufahamu hikma kutokana na amri za Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)  na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Muislamu aweze kupambanua mema na maovu na awe tofauti katika kila kila mwendo, desturi na mila za makafiri ili ajihifadhi na kuingia katika upotofu na shirki kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya kuwaigiza kuwa:

 

 عن إبن عمر ((من تشبه بقوم فهو منهم)) ابن حبان - صحيح

 

Kutoka kwa Ibn 'Umar ((Mwenye kujifananisha na watu naye ni kama wao)) [Ibn Hibbaan ikiwa swahiyh]     

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta’alaa) Atuwezeshe kuifahamu dini yetu kwa kutuzidishia elimu, turekebishe hali zetu, Awahidi viongozi wetu khaswa wa dini watoe mafundisho yaliyo sahihi na siyo ya uzushi. Ajaalie Umma huu watokee watakaoeneza maneno Yake ya haki na ya  Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili Umma huu uepukane na bid'ah zote ambazo zinawapotoa Waislamu wengi na Atuthibitishe nyoyo zetu baada ya kutambua haki. Aamiyn. 

 

 

 

 

Share