031-Aayah Na Mafunzo: Pendekezo La Mavazi Mazuri Msikitini Na Kutokula Na Kunywa Mpaka Kushiba Sana

 

Aayah Na Mafunzo

 

www.alhidaaya.com

 

Al-A’raaf

 

031-Pendekezo La Mavazi Mazuri Msikitini

Na Kutokula Na Kunywa Mpaka Kushiba Sana

 

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu (ya mavazi ya sitara na twahara) katika kila mahala pa ‘Ibaadah. Na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu. [Al-A’raaf (7:31)]

 

 

Mafunzo:

 

Amri Ya Kuvaa Mavazi Mazuri Masafi Ya Twahara Sehemu Za ‘Ibaadah:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anaamrisha waja Wake Waumini kuvaa nguo nzuri, safi, za twahara (na siwaak) anaposwali au katika sehemu zozote zile za ‘Ibaadah kama katika Manaasik ya ‘Umrah na Hajj; katika kutufu Al-Ka’baah na kwengineko.  Na nguo bora kabisa ni ya rangi nyeupe (kwa wanaume) kama alivyohadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Vaeni nguo nyeupe kwani ndio nguo zenu bora kabisa, na kafinini kwazo maiti wenu...” [Ahmad]

 

Katazo La Kufanya Israfu:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anakataza kufanya israfu; nayo ni israfu katika kula kunywa na hata katika mavazi na upotezaji wa neema nyenginezo. 

 

 

Katika kula, kuna nasaha ya kutokula kwa wingi mno mpaka mtu ashindwe kutekeleza ‘ibaadah zake: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Bin-Aadam hajijazii chombo vibaya kama anavyojaza tumbo lake. Inamtosheleza Bin-Aadam ale kidogo tu kiasi cha kumtia nguvu uti wa mgongo wake. Lakini akitaka kula zaidi, basi thuluthi ya chakula, na thuluthi ya maji na thuluthi aache kwa ajili ya hewa.” [Amehadithia Al-Miqdaam bin Ma’diykarib (رضي الله عنه)  na imepokelewa na  Ahmad, At-Tirmidhiy]

 

 

Share