07-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Twahaarah: Mlango Wa Kwenda Kujisaidia Haja Msalani

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتابُ الطَّهارَة

Kitabu Cha Twahaarah

 

بَابُ قَضَاءِ اَلْحَاجَةِ

07-Mlango Wa Kwenda Kujisaidia Haja Msalani

 

 

 

76.

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏إِذَا دَخَلَ اَلْخَلَاءَ وَضَعَ خَاتَمَهُ} أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةُ، وَهُوَ مَعْلُولٌ

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anaivua pete[1] yake akiingia msalani.” [Imetolewa na Al-Arba’ah: Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah na ina dosari]

 

 

 

77.

وَعَنْهُ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏إِذَا دَخَلَ اَلْخَلَاءَ قَالَ: "اَللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ اَلْخُبُثِ وَالْخَبَائِثِ"} أَخْرَجَهُ اَلسَّبْعَةُ

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiingia msalani anasema[2]:

اَللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ اَلْخُبُثِ وَالْخَبَائِثِ

“Allaahumma inniy a’uwdhu ‘Bika minal khubuthi wal khabaaith.” (Ee Allaah, najikinga Kwako dhidi ya mashaytwani ya kiume na ya kike).” [Imetolewa na As-Sab’ah (Maimamu Saba Wa Hadiyth: Al-Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, Ahmad)]

 

 

 

78.

وَعَنْهُ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏يَدْخُلُ اَلْخَلَاءَ، فَأَحْمِلُ أَنَا وَغُلَامٌ نَحْوِي إِدَاوَةً مِنْ مَاءٍ وَعَنَزَةً، فَيَسْتَنْجِي بِالْمَاءِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiingia msalani, mimi na ghulamu (mtoto mvulana) mwengine tukimchukulia viroba vya maji na mkuki, na anajisafisha kwa maji[3] yale.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

79.

وَعَنْ اَلْمُغِيرَةِ بْنِ شُعْبَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {قَالَ لِي اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏ "خُذِ اَلْإِدَاوَةَ".‏ فَانْطَلَقَ حَتَّى تَوَارَى عَنِّي، فَقَضَى حَاجَتَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Al-Mughiyrah bin Shu’bah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliniambia: “Chukua kiroba cha maji.” Kisha akaenda mbele hadi akanipotea[4], na ndipo akakidhi haja yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

80.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{اِتَّقُوا اَللَّاعِنِينَ: اَلَّذِي يَتَخَلَّى فِي طَرِيقِ اَلنَّاسِ، أَوْ فِي ظِلِّهِمْ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

زَادَ أَبُو دَاوُدَ، عَنْ مُعَاذٍ: {وَالْمَوَارِدَ}

وَلِأَحْمَدَ; عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ: {أَوْ نَقْعِ مَاءٍ} وَفِيهِمَا ضَعْفٌ

وَأَخْرَجَ اَلطَّبَرَانِيُّ اَلنَّهْيَ عَنْ ‏ تَحْتِ اَلْأَشْجَارِ اَلْمُثْمِرَةِ، وَضَفَّةِ اَلنَّهْرِ الْجَارِي.‏ مِنْ حَدِيثِ اِبْنِ عُمَرَ بِسَنَدٍ ضَعِيفٍ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ogopeni viwili vyenye kusababisha laana; humpata ambaye hujisaidia (kukojoa au kunya) katika njia za watu[5], na chini ya vivuli vyao.” [Imetolewa na Muslim]

 

Ameongezea Abuu Daawuwd kuwa ilisimuliwa na Mu’aadh[6] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwa: “Kujisaidia mahali pa kuchotea maji na hifadhi yake.”

 

Katika Riwaayah ya Ahmad (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alisimulia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) kuwa: “Kujisaidia palipokusanyika maji.” [Na Hadiyth zote mbili, zina udhaifu]

 

Atw-Twabaraaniy alitaja kuwa: “Imekatazwa kujisaidia chini ya miti ya matunda na kando kando ya mito inayotiririka[7].” [Imetolewa na Atw-Twabaraaniy kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar, kwa Isnaad dhaifu]

 

 

 

81.

وَعَنْ جَابِرٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{إِذَا تَغَوَّطَ اَلرَّجُلَانِ فَلْيَتَوَارَ كُلُّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا عَنْ صَاحِبِهِ، وَلَا يَتَحَدَّثَا.‏ فَإِنَّ اَللَّهَ يَمْقُتُ عَلَى ذَلِكَ} رَوَاهُ  أَحْمَدُ.‏ ‏ وَصَحَّحَهُ اِبْنُ اَلسَّكَنِ، وَابْنُ اَلْقَطَّانِ، وَهُوَ مَعْلُولٌ

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu wawili wakijisaidia pamoja, kila mmoja ajifiche na mwenzie wala wasiongee, kwani Allaah anachukia hivyo.”” [Imetolewa na Ahmad na akaisahihisha Ibn As-Sakan na Ibn Al-Qatwaan, lakini ina dosari[8]]

 

 

 

82.

وَعَنْ أَبِي قَتَادَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{لَا يُمْسِكَنَّ أَحَدُكُمْ ذَكَرَهُ بِيَمِينِهِ، وَهُوَ يَبُولُ، وَلَا يَتَمَسَّحْ مِنْ اَلْخَلَاءِ بِيَمِينِهِ، وَلَا يَتَنَفَّسْ فِي اَلْإِنَاءِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ

Kutoka kwa Abuu Qataadah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mtu yeyote asishike dhakari[9] yake kwa kulia kwake wakati anakojoa, na asijisafishe (kutokana na haja kubwa au ndogo) kwa kulia kwake, wala asipumulie katika chombo (anachonywea).” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]

 

 

 

83.

وَعَنْ سَلْمَانَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {لَقَدْ نَهَانَا رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏ "أَنْ نَسْتَقْبِلَ اَلْقِبْلَةَ بِغَائِطٍ أَوْ بَوْلٍ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِالْيَمِينِ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِأَقَلَّ مِنْ ثَلَاثَةِ أَحْجَارٍ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِرَجِيعٍ أَوْ عَظْمٍ"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

وَلِلسَّبْعَةِ مِنْ حَدِيثِ أَبِي أَيُّوبَ ‏ رضى الله عنه ‏ {لَا تَسْتَقْبِلُوا اَلْقِبْلَةَ بِغَائِطٍ وَلَا بَوْلٍ، وَلَكِنْ شَرِّقُوا أَوْ غَرِّبُوا}

Kutoka kwa Salmaan[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitukataza kuelekea Qiblah wakati wa kwenda haja kubwa au ndogo, wala tusijisafishe kwa mkono wa kulia, au kujisafisha kwa mawe yasiyotimia matatu, au kujisafisha kwa kinyesi cha wanyama au mfupa.” [Imetolewa na Muslim]

 

As-Sab’ah (Maimaam Saba wa Hadiyth) wamenukuu Hadiyth ya   Abuu Ayyuub[11] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Usielekee Qiblah[12] wakati unakwenda haja kubwa au ndogo, lakini geukia Mashariki au Mgharibi.”

 

 

 

84.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا; أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {مَنْ أَتَى اَلْغَائِطَ فَلْيَسْتَتِرْ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kwenda kujisaidia haja kubwa na ajisitiri.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd]

 

 

 

85.

وَعَنْهَا; {أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏كَانَ إِذَا خَرَجَ مِنْ اَلْغَائِطِ قَالَ: "غُفْرَانَكَ"} أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ.‏ وَصَحَّحَهُ أَبُو حَاتِمٍ، وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema tena: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akitoka msalani, anasema: “Ghufraanaka (Ee Allaah! Naomba Unighufurie).” [Imetolewa na Al-Khamsah: (Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, An-Nasaaiy, Ahmad, Ibn Hibbaan, Al-Haakim) Waliipa Hadiyth hii daraja la Swahiyh Abuu Haatim na Al Haakim]

 

 

 

86.

وَعَنِ ابْنِ مَسْعُودٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {أَتَى اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏اَلْغَائِطَ، فَأَمَرَنِي أَنْ آتِيَهُ بِثَلَاثَةِ أَحْجَارٍ، فَوَجَدْتُ حَجَرَيْنِ، وَلَمْ أَجِدْ ثَالِثًا.‏ فَأَتَيْتُهُ بِرَوْثَةٍ.‏ فَأَخَذَهُمَا وَأَلْقَى اَلرَّوْثَةَ، وَقَالَ: "هَذَا رِكْسٌ"} أَخْرَجَهُ اَلْبُخَارِيُّ

زَادَ أَحْمَدُ، وَاَلدَّارَقُطْنِيُّ: {ائْتِنِي بِغَيْرِهَا}

Kutoka kwa Ibn Mas-’uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikwenda kujisaidia na akaniamrisha nimpelekee mawe matatu, nikapata mawe mawili na sikupata la tatu. Kwa hivyo nikampelekea kinyesi cha mnyama kilichokauka. Akakirushia mbali[13] kisha akasema: “Hii ni najisi.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

Katika nukuu ya Ahmad na Ad-Daaruqutwniy imeongezewa: “Niletee kisichokuwa hiki[14].”

 

 

 

87.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏نَهَى "أَنْ يُسْتَنْجَى بِعَظْمٍ، أَوْ رَوْثٍ" وَقَالَ: "إِنَّهُمَا لَا يُطَهِّرَانِ"} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَصَحَّحَهُ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ametukataza kutumia mifupa au kinyesi kikavu cha mnyama kujisafisha, alisema: “Vitu hivi viwili havitwoharishi.”” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy na akaisahihisha]

 

 

 

88.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{اِسْتَنْزِهُوا مِنْ اَلْبَوْلِ، فَإِنَّ عَامَّةَ عَذَابِ اَلْقَبْرِ مِنْهُ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ

وَلِلْحَاكِمِ: {أَكْثَرُ عَذَابِ اَلْقَبْرِ مِنْ اَلْبَوْلِ} وَهُوَ صَحِيحُ اَلْإِسْنَادِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Jitakaseni kutoka na mkojo, kwani ni sababu kuu ya adhabu za kaburini.” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy

Na kutoka kwa Al Haakim alisimulia kuwa: “Adhabu nyingi za kaburini ni kutokana na mkojo.” [Na Isnaad yake ni Swahiyh]

 

 

89.

وَعَنْ سُرَاقَةَ بْنِ مَالِكٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {عَلَّمْنَا رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏فِي اَلْخَلَاءِ: " أَنَّ نَقْعُدَ عَلَى اَلْيُسْرَى، وَنَنْصِبَ اَلْيُمْنَى"} رَوَاهُ اَلْبَيْهَقِيُّ بِسَنَدٍ ضَعِيفٍ

Kutoka kwa Suraaqah bin Maalik[15] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitufundisha adabu za msalani: kuwa tukalie mguu wa kushoto[16] na tuusimamishe wima mguu wa kulia.” [Imetolewa na Al-Bayhaqiy kwa Isnaad dhaifu[17]]

 

 

 

90.

وَعَنْ عِيسَى بْنِ يَزْدَادَ، عَنْ أَبِيهِ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{إِذَا بَالَ أَحَدُكُمْ فَلْيَنْثُرْ ذَكَرَهُ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَه بِسَنَدٍ ضَعِيفٍ

Kutoka kwa ‘Iysaa bin Yazdaad[18] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kutoka kwa baba yake amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu akikojoa, anapaswa akung’ute dhakari yake mara tatu.”  [Imetolewa na Ibn Maajah kwa Isnaad dhaifu]

 

 

 

91.

وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا; {أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏سَأَلَ أَهْلَ قُبَاءٍ،  فَقَالَ: "إنَّ اللهَ يُثْنِي عَلَيْكُمْ، فَقَالُوا: إِنَّا نُتْبِعُ اَلْحِجَارَةَ اَلْمَاءَ} رَوَاهُ اَلْبَزَّارُ بِسَنَدٍ ضَعِيفٍ

وَأَصْلُهُ فِي أَبِي دَاوُدَ، وَاَلتِّرْمِذِيّ وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ مِنْ حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ بِدُونِ ذِكْرِ اَلْحِجَارَةِ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwauliza watu wa Qubaa akasema: “Allaah Anakusifuni.” Wakasema: “Sisi hufuatisha maji baada ya (kujisafisha kwa) mawe.” [Imetolewa na Al Bazzaar kwa Isnaad dhaifu]

Na chanzo chake ni Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy na akaisahihisha Ibn Khuzaymah Hadiyth hii kupitia kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) bila kutaja “mawe.”

 

 

 

 

[1] Pete ile ilikuwa imeandikwa mistari mitatu: “Muhammad Rasulu wa Allaah.” Hii inamaanisha kwamba, Majina ya Allaah (عز وجل) au Aayah za Qur-aan kamwe zisipelekwe chooni au unapokwenda haja yoyote.

 

[2] Kwa kawaida majini huishi sehemu chafu kama vyooni. Kwa sababu hiyo, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiomba hifadhi ya Allaah (عز وجل).   Mtu sharti aisome du’aa hii kabla ya kuingia chooni kwa sauti ya kusikika. Kwa mujibu wa usimulizi wa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) maporini na misituni, mtu sharti aisome du’aa hii kabla ya kuchuchumaa na kuenda haja. Wakati wa kuenda haja, mtu sharti aangalie mwili wake na nguo zake.

 

[3] Baadhi ya Wanazuoni hupendelea kujisafisha kwa dongo pamoja na maji.

 

[4] Tendo hili la Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) linatufundisha kuwa, wakati wa kuenda kujisaidia ni lazima kuandaa sitara (kificho) ili ufichike kwa watu wengine. Katika Hadiyth nyingine imesema kwamba, mahala palipo wazi, kijilima cha udongo au rundo la mchanga uandaliwe kwa ajili ya kujisitiri. Mtu akijisaidia mahali pa wazi kabisa, shaytwaani atayacheka matako yake na atachekwa na watu pia.

 

[5] Imekatazwa kuenda haja njiani au katika njia zilizo karibu na maeneo yenye watu wengi. Mahali penye barabara isiyotumika au magofu ya nyumba zilizohamwa zinaweza kutumika kuendea haja.

 

[6] Mu’aadh ni Answaar (wa kutoka Al-Madiynah) wa kabila la Al-Khazraj alikuwa mmoja wa Swahaba waadilifu, mtukufu na msomi mkubwa. Alishiriki katika vita za Aqabah, Badr na vita zingine kubwa. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimteuwa kuwa mwakilishi wake kule Yaman. Kisha ‘Umar akamteua kuwa Gavana wa Shaam baada ya Abuu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah. Alifariki katika mji wa Amwaas mnamo mwaka 17 au 18 A.H akiwa na umri wa miaka 38.

 

[7] Sehemu zote zinazokatazwa ni sita. Imekatazwa katika Hadiyth kuenda haja kubwa au ndogo karibu na milango ya Misikiti.

 

[8] Hii inathibitishwa na Hadiyth zingine.

 

[9] Kuushika uume kwa mkono wa kuume wakati wa kuenda haja ndogo au kuuosha, na kupumulia kwenye chombo cha kunywea imekatazwa, kwa mujibu wa wengine, na kwa mujibu wa wengine wanasema haipendezi. Kutolea pumzi ndani ya chombo kuna madhara kwa sababu hiki ni chanzo cha kuambukiza viini kutoka kwa mtu mmoja mpaka kwa mwingine. Na Hadiyth inayoagiza kuwa na mapumziko matatu wakati wa kunywa, inamaanisha kuwa kinywaji sharti kinywewe taratibu na siyo kukimeza kwa mkupuo mmoja.

 

[10] Salmaan Al-Faarisiy: Alikuwa akijulikana kwa jina la “Salmaan mkarimu”, na akapewa jina la utani la Abuu ‘Abdillaah. Asili yake alitoka Uajemi (Persia). Alisafiri akitafuta dini, na akawa Mkristo. Kisha akahamia Al-Madiynah na akamuamini Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mara tu alipowasili Al-Madiynah. Salmaan Al-Faarisy ndiye aliyetoa fikra ya kuchimbwa mahandaki katika vita vya Al-Khandaq. Alikuwa kiongozi katika Uislaam, na alifariki Al-Madiynah mnamo mwaka 50 au 32 A.H. Imetaarifiwa kwamba aliishi muda mrefu sana, ama miaka 250 au 350.

 

[11] Abuu Ayuwb jina lake ni Khaalid bin Zayd bin Kulayb. Huyu ndiye aliyemkaribisha Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipowasili Al-Madiynah mara ya kwanza. Alikuwa ni mmoja wa Swahaba wakubwa na waandamizi sana. Alishiriki katika vita vya Badr, na akafa shahidi wakati alipopigana vita dhidi ya Wabinzantina mnamo mwaka 50 A.H. Kaburi lake liko katika kuta za Istanbul linajulikana sana na watu wengi hulizuru.

 

[12] Katika kadhia hii, ‘Makatazo’ yako kwenye maeneo ya wazi. Haikatazwi ikiwa eneo hilo ni ndani ya jengo ambalo lina kuta zinazolizunguka. Kwani kuna Hadiyth ambayo ilisimuliwa na ‘Abdullaah bin ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) kwamba: “Katika nyumba ya dadangu Hafswa (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) nilikuenda ghorofani kwenye paa, nikamuona Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) anakuenda haja, ameeleka Shaam.” Hadiyth hii ni ya Sahihi Muslim.

 

[13] Hadiyth hii inatujulisha kuwa, mtu asisafishe sehemu zake za siri kwa kinyesi au samadi ya mnyama; na pia imekatazwa kujisafisha kwa mifupa.

 

[14] Hiyo nyongeza inamaanisha kwamba, kwa ajili ya usafi, hutakiwa mabonge matatu ya udongo, ingawa mawili yangetosha, lakini sharti la matatu liko pale pale. Yanaweza kutumika mabonge zaidi ya matatu, ikilazimika, lakini namba iwe Witri. Hadiyth hii pia inathibitisha kuwa kinyesi cha Wanyama hakiwezi kutumika kusafishia sehemu za siri. Na pia kujisafisha kwa mifupa pia kumekatazwa.

 

[15] Suraaqah bin Maalik bin Ju’shum Al-Mudlaj Al-Kinaan aliyepewa jina la utani la Abuu Sufyaan alikuwa Swahaba maarufu. Huyu ndiye aliyemsaka Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipokuwa akihama (kuenda zake Madiynah na Abuu Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) na mwishowe miguu ya mbele ya farasi wake ikazama ardhini mpaka magotini. Alifariki mnamo mwaka wa 24 A.H.

 

[16] Katika kila amri ya Uislaam kuna hikma, iwe tunaielewa au laa. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alituagiza sisi tuukalie mguu wa kushoto, ili kuweka uzito wa mwili upande wa kushoto kwani hata tumbo liko upande huo wa kushoto, kwa hivyo inalifanya tendo la kijisaidia liwe rahisi, na uyabisi wa tumbo, mama wa mgonjwa pia huondoshwa.

 

[17] Hadiyth hii ni dhaifu.

 

[18] ‘Iysaa na babake Yazdaad wote hawajulikani. Ibn ‘Iyn alisema kuwa: “’Iysaa na babake hawafahamiki.”

 

Share