10-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Twahaarah: Mlango Wa Hedhi

 

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتابُ الطَّهارَة

Kitabu Cha Twahaarah

 

بَابُ اَلْحَيْضِ

10-Mlango Wa Hedhi

 

 

 

 

116.

 

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {إِنَّ فَاطِمَةَ بِنْتَ أَبِي حُبَيْشٍ كَانَتْ تُسْتَحَاضُ، فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم  "إِنَّ دَمَ اَلْحَيْضِ دَمٌ أَسْوَدُ يُعْرَفُ، فَإِذَا كَانَ ذَلِكَ فَأَمْسِكِي مِنَ اَلصَّلَاةِ، فَإِذَا كَانَ اَلْآخَرُ فَتَوَضَّئِي، وَصَلِّي"} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ، وَاسْتَنْكَرَهُ أَبُو حَاتِمٍ

وَفِي حَدِيثِ أَسْمَاءَ بِنْتِ عُمَيْسٍ عِنْدَ أَبِي دَاوُدَ: {لِتَجْلِسْ فِي مِرْكَنٍ، فَإِذَا رَأَتْ صُفْرَةً فَوْقَ اَلْمَاءِ، فَلْتَغْتَسِلْ لِلظُّهْرِ وَالْعَصْرِ غُسْلاً وَاحِدًا، وَتَغْتَسِلْ لِلْمَغْرِبِ وَالْعِشَاءِ غُسْلاً وَاحِدًا، وَتَغْتَسِلْ لِلْفَجْرِ غُسْلاً، وَتَتَوَضَّأْ فِيمَا بَيْنَ ذَلِكَ }

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: Fatwmah bint Abiy Hubaysh alikuwa na hedhi ya kudumu[1], Rasulu wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Damu ya hedhi ni nyeusi inatambulika, kwa hivyo ikiwa ndiyo hiyo, jizuie kuswali, na ikiwa ni nyingine (iliyopauka), basi tawadha na uswali.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy, wakaisahihisha Ibn Hibbaan na Al Haakim, na akaiita Munkar (si ya kawaida) Abuu Haatim]

Na katika Hadiyth ya Asmaa bint ‘Umays[2] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) iliyopokewa na Abuu Daawuwd, amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “(Mwanamke) Akae ndani ya bafu lenye maji, na akiona rangi ya njano hivi juu ya maji, basi afanye ghuslu moja kwa Swalaah ya Adhuhuri na Alasiri na afanye ghuslu moja tena kwa Swalaah ya Magharibi na ‘Ishaa, na afanye ghuslu kwa Swalaah ya Alfajiri, na baina ya nyakati hizi atawadhe.”

 

 

 

117.

 

وَعَنْ حَمْنَةَ بِنْتِ جَحْشٍ قَالَتْ: {كُنْتُ أُسْتَحَاضُ حَيْضَةً كَبِيرَةً شَدِيدَةً، فَأَتَيْتُ اَلنَّبِيَّ  صلى الله عليه وسلم أَسْتَفْتِيهِ، فَقَالَ: "إِنَّمَا هِيَ رَكْضَةٌ مِنَ اَلشَّيْطَانِ، فَتَحَيَّضِي سِتَّةَ أَيَّامٍ، أَوْ سَبْعَةً، ثُمَّ اِغْتَسِلِي، فَإِذَا اسْتَنْقَأْتِ فَصَلِّي أَرْبَعَةً وَعِشْرِينَ، أَوْ ثَلَاثَةً وَعِشْرِينَ، وَصُومِي وَصَلِّي، فَإِنَّ ذَلِكَ يُجْزِئُكَ، وَكَذَلِكَ فَافْعَلِي كَمَا تَحِيضُ اَلنِّسَاءُ، فَإِنْ قَوِيتِ عَلَى أَنْ تُؤَخِّرِي اَلظُّهْرَ وَتُعَجِّلِي اَلْعَصْرَ، ثُمَّ تَغْتَسِلِي حِينَ تَطْهُرِينَ وَتُصَلِّينَ اَلظُّهْرَ وَالْعَصْرِ جَمِيعًا، ثُمَّ تُؤَخِّرِينَ اَلْمَغْرِبَ وَتُعَجِّلِينَ اَلْعِشَاءِ، ثُمَّ تَغْتَسِلِينَ وَتَجْمَعِينَ بَيْنَ اَلصَّلَاتَيْنِ، فَافْعَلِي.‏ وَتَغْتَسِلِينَ مَعَ اَلصُّبْحِ وَتُصَلِّينَ.‏ قَالَ: وَهُوَ أَعْجَبُ اَلْأَمْرَيْنِ إِلَيَّ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا النَّسَائِيَّ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَحَسَّنَهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Hamnah bint Jahsh[3] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: Nilikuwa na hedhi yangu ilikuwa nyingi mno na kali, kwa hivyo nilikwenda kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kumtaka fatwa, akasema: “Hii ni athari ya shaytwaan, kwa hivyo wewe zingatia hedhi yako kwa siku sita au saba, kisha fanya ghuslu na ukitwaharika, swali kwa siku ishirini na tatu au ishirini na nne, na ufunge na uswali, kwani hiyo itakutosheleza wewe, na ufanye hivyo hivyo kila mwezi kama wanavyopata hedhi wanawake wengine.  Lakini ukiwa na nguvu[4] unaweza kuakhirisha Swalaah ya Adhuhuri na kutanguliza Alasiri, kisha fanya ghuslu na uswali Adhuhuri na Alasiri pamoja kisha akhirisha Magharibi na kutanguliza ‘Ishaa, fanya hivyo, na ufanye ghuslu na ukusanye baina ya Swalaah mbili, fanya hivyo na fanya ghuslu asubuhi na uswali Alfajiri.” Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mimi hii ninaipendelea zaidi, (yaani kufanya ghuslu kwa kila Swalaah).” [Imetolewa na Al Khamsah (Maimaam watano wa Hadiyth) ila An-Nasaaiy. Na akaisahihisha At-Tirmidhiy, na akaipa daraja la Hasan, Al-Bukhaariy]

 

 

 

118.

 

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا; {أَنَّ أُمَّ حَبِيبَةَ بِنْتَ جَحْشٍ شَكَتْ إِلَى رَسُولِ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم اَلدَّمَ، فَقَالَ: "اُمْكُثِي قَدْرَ مَا كَانَتْ تَحْبِسُكِ حَيْضَتُكِ، ثُمَّ اِغْتَسِلِي" فَكَانَتْ تَغْتَسِلُ كُلَّ صَلَاةٍ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

وَفِي رِوَايَةٍ لِلْبُخَارِيِّ: {وَتَوَضَّئِي لِكُلِّ صَلَاةٍ} وَهِيَ لِأَبِي دَاوُدَ وَغَيْرِهِ مِنْ وَجْهٍ آخَرَ.

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Ummu Habiybah bint Jahsh[5] alimshtakia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) damu (iliyokuwa ikitoka zaidi ya kipindi cha hedhi); akasema: “Kaa kadiri ilivyokuwa hedhi yako inakuzuia kuswali, kisha fanya ghuslu.” Akawa anafanya ghuslu kila Swalaah[6]. [Imetolewa na Muslim]

 

Na katika Riwaayah ya Al-Bukhaariy: “Tawadha kwa kila Swalaah.” [Pia ameipokea na Abuu Daawuwd na wengine kwa namna nyingine.]

 

 

 

119.

 

وَعَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كُنَّا لَا نَعُدُّ اَلْكُدْرَةَ وَالصُّفْرَةَ بَعْدَ اَلطُّهْرِ شَيْئًا} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ، وَأَبُو دَاوُدَ وَاللَّفْظُ لَهُ

Kutoka kwa Ummu ‘Aatwiyyah[7] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Hatukuwa tukihesabu unjano na ukahawia kuwa ni chochote (majimaji yanayotokea ukeni[8]) baada ya Twahaarah.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy na Abuu Daawuwd, na tamshi hili ni lake]

 

 

 

120.

 

وَعَنْ أَنَسٍ  رضى الله عنه  {أَنَّ اَلْيَهُودَ كَانُوا إِذَا حَاضَتْ اَلْمَرْأَةُ لَمْ يُؤَاكِلُوهَا، فَقَالَ اَلنَّبِيُّ  صلى الله عليه وسلم  "اِصْنَعُوا كُلَّ شَيْءٍ إِلَّا اَلنِّكَاحَ"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Mayahudi walikuwa hawali na mwanamke wakati ana hedhi, kwa hivyo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Fanyeni kila kitu (na wake zenu) isipokuwa kujamiiana.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

121.

 

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم يَأْمُرُنِي فَأَتَّزِرُ، فَيُبَاشِرُنِي وَأَنَا حَائِضٌ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiniamrisha kuvaa Izaar[9] (gagulo) kisha ananipapasa kwa mahaba[10] wakati nina hedhi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

122.

 

وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، عَنِ اَلنَّبِيِّ  صلى الله عليه وسلم فِي اَلَّذِي يَأْتِي اِمْرَأَتَهُ وَهِيَ حَائِضٌ قَالَ: {يَتَصَدَّقُ بِدِينَارٍ، أَوْ نِصْفِ دِينَارٍ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ وَابْنُ اَلْقَطَّانِ، وَرَجَّحَ غَيْرَهُمَا وَقْفَهُ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema kuhusu mume anayejamiiana na mkewe akiwa na hedhi: “Atoe dinari moja au nusu dinari kama Swadaqah.” [Imetolewa na Al-Khamsah (watano). Wakaisahihisha Al-Haakim na Ibn Al-Qatwaan, na wengine waliita kuwa Mawquwf[11]]

 

 

 

123.

 

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ  رضى الله عنه  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم {أَلَيْسَ إِذَا حَاضَتْ لَمْ تُصَلِّ وَلَمْ تَصُمْ؟} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ فِي حَدِيثٍ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Je si kweli kuwa mwanamke aliye katika hedhi haswali wala hafungi[12]?” [Al-Bukhaariy, Muslim na ni sehemu ya Hadiyth ndefu]

 

 

 

124.

 

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {لَمَّا جِئْنَا سَرِفَ حِضْتُ، فَقَالَ اَلنَّبِيُّ  صلى الله عليه وسلم  "اِفْعَلِي مَا يَفْعَلُ اَلْحَاجُّ، غَيْرَ أَنْ لَا تَطُوفِي بِالْبَيْتِ حَتَّى تَطْهُرِي"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ فِي حَدِيثٍ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Tulipofika mahali paitwapo Sarif, mimi nilipata hedhi, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaniambia: “Wewe fanya analolifanya Haji isipokuwa usifanya twawaaf (kutufu Ka’bah) mpaka ukishatwahirika.” [Al-Bukhaariy, Muslim, na ni sehemu ya Hadiyth ndefu]

 

 

 

125.

 

وَعَنْ مُعَاذٍ  رضى الله عنه  {أَنَّهُ سَأَلَ اَلنَّبِيَّ  صلى الله عليه وسلم مَا يَحِلُّ لِلرَّجُلِ مِنِ اِمْرَأَتِهِ، وَهِيَ حَائِضٌ؟ قَالَ: "مَا فَوْقَ اَلْإِزَارِ"} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَضَعَّفَهُ

Kutoka kwa Mu’aadh (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kitu gani halali kwa mwanamume kwa mkewe wakati ana hedhi? Akasema: “Kilicho juu ya Izaar[13].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaidhoofisha]

 

 

 

126.

 

وَعَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَتِ اَلنُّفَسَاءُ تَقْعُدُ فِي عَهْدِ رَسُولِ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم بَعْدَ نِفَاسِهَا أَرْبَعِينَ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا النَّسَائِيَّ، وَاللَّفْظُ لِأَبِي دَاوُدَ

وَفِي لَفْظٍ لَهُ: {وَلَمْ يَأْمُرْهَا اَلنَّبِيُّ  صلى الله عليه وسلم بِقَضَاءِ صَلَاةِ اَلنِّفَاسِ} وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa Ummu Salamah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Wanawake wenye nifaas zama za Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) walikuwa wakikaa (bila kuswali) kwa siku arubaini[14].” [Imetolewa na Al Khamsah isipokuwa An-Nisaaiy, na tamshi hili ni la Abuu Daawuwd]

 

Na katika Riwaayah nyengine ya Abuu Daawuwd anasema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakumuamrisha (mzazi) alipe Swalaah alizoacha wakati wa nifaas yake.” [Aliisahihisha Al Haakim]

 

 

 

[1] Istihaadhwah (damu imtokayo mwanamke ukeni) ni damu inayodumu muda mrefu na inaweza kuwa ni damu ya uzazi au ya hedhi, na huhesabika kuwa ni kutokwa na damu kati kati ya vipindi. Kipindi cha hedhi, kwa mujibu wa ‘Ulamaa ni kutoka siku moja mpaka siku kumi na tano; na kwa mujibu wa wengine ni kutoka siku tatu mpaka siku kumi. Uzoefu unaonyesha kuwa huo usemi wa pili ni sahihi zaidi. Kila mwanamke huwa anafahamu vipindi vyake, na akitokwa damu zaidi ya wakati wake, basi hiyo ni Istihaadhwah.

 

 

[2] Asmaa alikuwa mke wa Ja’far bin Abiy Twaalib (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ). Alihajiri pamoja naye hadi Habashah (Abyssinia   Ethiopia), na alimzalia watoto watatu, na kati ya hao ni ‘Abdullaah. Baada ya Ja’far (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kufa Shahidi katika vita vya Mut’a, Abuu Bakar Swiddiyq (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimuoa Asmaa ambaye alimzalia mtoto mmoja Muhammad. Na baada ya kufariki Abuu Bakar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ), ‘Aliy bin Abiy Twaalib (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimuoa Asmaa ambaye alimzalia Yahyaa. ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alizowea kumuuliza Asmaa tafsiri ya ndoto. Alikufa baada ya kifo cha ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ).

 

 

 

[3] Hamnah bint Jahsh ni dada wa “Mama wa Waumini”, Zaynab bint Jahsh. Alioelewa na Musw’ab bin ‘Umayr ambaye alikufa Shahidi katika  vita vya Uhud, na baada ya hivyo akaolewa na Twalhah bin ‘Ubaydillaah.

 

 

[4] Katika Hadiyth hii Hamnah aliamriwa kuoga mara tatu kila siku. Aoge mara moja kwa ajili ya Swalaah za Adhuhuri na Alasiri, na aoge mara ya pili kwa Swalaah za Magharibi na ‘Ishaa, na aoge mara ya tatu kwa Swalaah ya Alfajiri. Katika Hadiyth iliyopita, Faatwimah binti Abiy Hubaysh aliamuriwa achukue wudhuu tu kabla ya kila Swalaah. Hii inamaanisha kuwa, kwa mwanamke anayekuwa na Istihaadhwah kuoga siyo lazima, lakini kuchukuwa wudhuu ni lazima kwa kila Swalaah. Kuoga ni bora ikiwa hali ya afya na ya hewa itaruhusu, vinginevyo hakuna haja ya kuoga.

 

 

[5] Habiybah bint Jahsh alikuwa dada mwingine wa “Mama wa Waumini” Zaynab bint Jahsh, naye aliolewa na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf. Mulsim alisimulia kuwa alikuwa na damu iliyodumu miaka saba. Alifariki mnamo mwaka wa 44 A.H.

 

[6] Ilikuwa ni hatua ya hiari na ya tahadhari tu kwa Umm Habiybah kuoga kwa kila Swalaah. Uamuzi sahihi kuhusu kadhia hii ni kuoga baada ya hedhi na atawadhe. Kuhusu kutokwa damu kwa muda mrefu mno, ipo amri ya kuosha damu na kuchukua wudhuu katika kila Swalaah.

 

[7] Ummu ‘Atwiyyah ni jina la Nusaybah Ka’b bint Al-Haarith Al-Ansariyya. Alikuwa ni miongoni mwa Swahaba wa kike maarufu, na alikuwa akiongozana na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) vitani akiwauguza wagonjwa na kuwatibu majeruhi. Alipigana katika Vita vya Uhud kama shujaa. Alishuhudia kuoshwa kwa maiti ya binti wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ambako alieleza na alitusimulia, na Swahaba, Taabi’, ‘Ulamaa wa Basra walirikodi kutoka kwake. Hadiyth yake inahesabika kuwa ndiyo msingi wa kuosha maiti. Alikuwa mmoja wa Swahaba wa kike waliolowea kule Basra.

 

[8] Katika usimulizi wa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) majimaji ya rangi ya njano au na vumbi yanahesabika kuwa ni damu ya hedhi, lakini Hadiyth hii inasema: “Tuliyahesabu kuwa siyo kitu.” Hadiyth hizi mbili zaelekea kujipinga, lakini zote mbili ni sahihi katika muktadha wa kila moja. Ikiwa majimaji ya rangi ya njano au ya vumbi yatajitokeza wakati wa kipindi cha hedhi, yatahesabika kuwa ni “damu ya hedhi.” Lakini yakijitokeza baada ya kipindi cha hedhi basi si chochote kama maneno ya Kiarabu ya بَعْدَ اَلطُّهْرِ yanavyodokeza.

 

 

[9] Vazi linalovaliwa kutoka kiunoni kuenda chini kama gagulo au sketi.

 

[10] Wale ambao hawazisadiki Hadiyth, yaani wakanushaji wa Sunnah, wanaleta utata na mashaka hapa, na wanawafanya watu wazishuku Hadiyth. Wanasema kuwa tendo la ndoa katika kipindi cha hedhi limekatazwa na Qur-aan lakini kwa mujibu wa Hadiyth hii Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alifanya wakati ule, kwa hiyo Hadiyth hiyo siyo sahihi. Maana ya maneno ya ‘Mubaasharat’ ni kugusa na kuukanda mwili kwa mwili, na kwa kifumbo maana yake ni kufanya tendo la ndoa. Katika Hadiyth imewekwa wazi kwamba tendo la ndoa limekatazwa wakati ya hedhi ya mwanamke. Kwa hivyo ni udanganyifu tu kutafsiri neno hilo ‘mubashaarat’ kuwa ni ‘tendo la ndoa’ badala ya kulitafsiri kuwa ni ‘kushikashika kwa mahaba’ na kuleta mashaka.

 

[11] Hii ni Hadiyth dhaifu, kwa hivyo wengi wa ‘Ulamaa hawadhani kuwa ni lazima kufidia, ingawa baadhi ya ‘Ulamaa hudhani inafaa kufidia, lakini rai ya kwanza ni sahihi kwa kuwa amri hiyo ni kwa kuhamasisha Swadaqah.

 

[12] Hii ni sehemu ndogo tu ya Hadiyth ndefu. Alipokuwa akitoa khutbah kwa wanawake Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwaambia kuwa dini yao haijakamilika. Walipouliza kwa namna gani, kwa kusema maneno yanayomaanisha kuwa wanawake walio na hedhi wasiswali wala wasifunge Swawm.

 

[13] Kila kilicho juu ya Izaar (Nguo inayovaliwa chini ya kiuno) inaweza kuwa na maana mbili: kwanza inaweza kuwa na maana ya jimai. Kwa maneno mengine, kila kitu kinaruhusiwa isipokuwa jimai. Pili: ina maana ya ile sehemu inayovaliwa Izaar. Ila maana hii inaweza kupingana na Hadiyth isemayo: “Fanyeni kila kitu isipokuwa jimai.” Kwa hivyo basi ni vizuri kutumia maana ya kwanza.

 

[14] Hii inamaanisha ni kile kiwango cha juu cha siku za damu ya uzazi, na hakuna kiwango chake cha chini. Laiti ikiendelea zaidi ya siku arubaini, basi itakuwa ni Istihaadhwah (damu ya ugonjwa), ambayo siyo kizuizi kwa Swalaah, wala kufunga Swawm, wala kufanya tendo la ndoa. Kila amri kuhusu damu na uzazi ni sawa na ile ya damu ya hedhi.

 

 

 

Share