Kukidhi Swalaah: Wakati Gani Swalaah Za Kukidhi Zilipwe; Kabla Ya Swalaah Ya Fardhi Au Baada Yake?

SWALI LA 1:

Vipi unasali sala zilizokupita?

 

 

SWALI LA 2:

Assalama Aleiykum,
Ningependa kujua ni wakati gani ambawo swala ya kukidhi huswaliwa wakati swala nyengine imeingia? Ni baada ama kabla ya kuswali swala ya wakati?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa maswali hayo na tutayajibu kwa pamoja hapa chini.

Zipo nyudhuru zinazokubalika kishari'ah kwa mtu kuacha Swalah kabisa au kuakhirisha Ibadah hiyo muhimu. Nyudhuru za kuacha Swalah ni:

(a) Hedhi;

(b) Nifasi;

(c) Wazimu.

Hawa wenye hali hizo Swalah haikuwalazimu. Ama kuakhirisha ni zifuatazo:

(a) Kulala; 

(b) Kusahau;  

(c) Kujumuisha Swalah mbili kwa sababu ya safari;

(d) Kukhofia kufutu Ibadah ya Hijja;

(e) Kumuokoa anayeghariki, n.k.;

(f) Kukhohofia kupasuka mwili wa maiti kwa ajili ya kuharibika;

(g) Kutotambua kuwa wakati wa Swalah umeingia mpaka ukatoka.

(h) na nyudhuru zingine zinazokubalika kishari'ah ambazo hatujazitaja hapo juu.

 

Ni wajibu kulipa Swalah kwa nyudhuru za kishari'ah. Ni muhimu sana kuilipa Qadhaa Swalah iliyokufutu kwa haraka iwezekanavyo mara tu ukumbukapo au uamkapo au ukutokapo udhuru wako.

 

Kuchunga taratibu za Qadhaa ni Sunnah. Kama imekufutu Adhuhuri na Alasiri, ni Sunnah kwanza kuilipa Adhuhuri kisha Alasiri. Lau utatanguliza Alasiri Swalah zitasihi. Kama itakubidi kulipa Qadhaa katika wakati wa Swalah mojawapo kati ya Swalah tano na hapo hapo uiswali Swalah ya wakati huo; hapo uamuzi wako utategemea wasaa wa wakati. Kama una hakika kuwa utawahi kulipa Qadhaa na kuiswali Swalah ya wakati huo bila ya kufutu wakati basi fanya hivyo. Lakini kama unaswali Jama'ah, na inaswaliwa mathalan Alasiri na wewe hujaswali Swalah ya Adhuhuri, basi weka niyyah moyoni mwako ya kuiswali Adhuhuri japo Swalah inayoswaliwa hapo Jama'ah ni ya Alasiri, kisha baada ya Swalah hiyo, wewe utaswali Alasiri mwenyewe. Hivi ndivyo Wanachuoni wengi walivyolieleza suala hili.

Hivyo, ni kutanguliza Swalah iliyokupita kwanza kisha uswali ya wakati huo. Kufuata taratibu ni bora zaidi katika kuziswali Swalah ulizokosa kuswali.

 

Qadhaa zinaweza kulipwa hata katika nyakati zilizozuiliwa kuswali.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share