17-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Fadhila Za Laylatul-Qadr

 

 Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

17-Fadhila Za Laylatul-Qadr

 

 

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((مَن قام ليلةَ القدر إيمانًا واحتسابًا، غُفر له ما تقدَّم من ذنبه)) متفق عليه.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Mwenye kusimama Usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, hughufiriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii ina faida kadhaa:

 

 

1-Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameutunuku umma wetu huu usiku huu wa barka wenye sifa hizi mahsusi:

 

 

2-Ni usiku uliobarikiwa kwa kheri zake nyingi, fadhila na thawabu kochokocho. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Anasema:

 

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ﴿٣﴾

 Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa [Ad-Dukhaan: 3]

 

 

3-Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameteremsha ndani yake Qur-aan Tukufu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾

Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatil-Qadr (usiku wa Qadar). [Al-Qadr: 1]

 

 

 

4-Amali anayoifanya mja ndani ya usiku huu, malipo yake ni zaidi ya amali iliyofanywa katika miezi 1000 ambayo ni zaidi ya miaka 84 kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾

Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu. [Al-Qadr: 3]

 

 

 

5-Malaika huteremka ardhini wakibubujisha kheri, barkah na rahmah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Anatuambia:

 

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم  

Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao  [Al-Qadr: 4]

 

 

 

6-Ni usiku wa amani na usalama kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾

Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 5]

 

 

 

7-Mwenye kuswali usiku huo kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  basi hughufuriwa dhambi zake zote.

 

 

Maana Ya Al-Qadr:

 

 

 ‘Ulamaa wametofautiana kuhusu maana ya neno la القدر . Kuna kauli tatu mashuhuri.

 

 

Kauli ya kwanza inasema kuwa maana ya Al-Qadri  ni التقدير yaani makadirio (ukadirishaji). Na hapa ina maana kwamba katika usiku huu, makadirio ya mwaka ya viumbe vyote hupitishwa na kukadiriwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ﴿٤﴾

Katika (usiku) huo hupambanuliwa kila jambo la hikmah. [Ad-Dukhaan: 4]

 

 

 

Kauli ya pili inasema: Maana ya القدر   ni utukufu na uluwa wa cheo. Hii ina maana kwamba usiku huu una utukufu maalumu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

   

Kauli ya tatu inasema kwamba القدر ni kwa maana ya ufinyu au mbanano. Kwa maana kwamba kutokana na wingi wa Malaika wanaoteremka siku hiyo, ardhi inakuwa finyu.

 

 

Tafsiyr zote hizi tatu zinaonyesha ni namna gani usiku huu ulivyo na uzito kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa Malaika Wake na kwa Waumini.

 

 

Mwislamu anatakiwa afanye hima na juhudi zake zote katika mwezi mzima wa Ramadhwaan kwa jili ya kuusaka usiku huu.

 

 

 

 

Share