18-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Du’aa Usiku Wa Laylatul-Qadr

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

18-Du’aa Usiku Wa Laylatul-Qadr

 

 

 

 

عَن عَائِشَةَ، قالَتْ: قُلْتُ: يا رَسُولَ اللهِ، أرَأيْتَ إنْ عَلِمْتُ أيُّ لَيْلَةٍ لَيْلَةُ الْقَدْرِ، مَا أقُولُ فِيها؟ قَالَ: ((قُولي: اللَّهُمَّ إنَّكَ عَفُوٌّ كَرِيمٌ تُحِبُّ العَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي)).

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba amesema: “Ee Rasuli wa Allaah! Nieleze ikiwa nitajua usiku fulani ndio wa Laylatul-Qadr, niseme nini?” Akasema: ((Sema:  Allaahumma Innaka 'Afuwwun Kariymun Tuhibbul-'Afwa fa'fu 'anniy (Ee Allaah Hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa Ukarimu Unapenda kusamehe basi Nisamehe mimi)) [At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy fiy Sunan Al-Kubraa (7712) Ibn Maajah (3850), Ahmad (25384) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3513)

 

 

Mafunzo:

 

العفو (Al-‘Afw) Ni Jina kati ya Majina Matukufu ya Allaah ('Azza wa Jalla)  yenye kuonyesha upana wa kusamehe Kwake madhambi ya Waja Wake vyovyote yawavyo kama watatubia na kurejea.

 

Na العفو “Al-Afw” asili yake ni kufuta na kuondosha kabisa athari ya kitu. Na hii ina maana kuwa Allaah ('Azza wa Jalla)  Huyafuta kabisa madhambi ya mja Wake bila kubakisha chembe ya athari.

 

 

Ama “Al Kariym”, hili pia ni Jina katika Majina ya Allaah ('Azza wa Jalla)  linaloonyesha wingi wa kuwapururia kheri waja Wake.

 

 

Katika Hadiyth hii Tukufu, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anamfundisha Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) du’aa mwafaka ya kuomba kama atabahatika kuutambua usiku fulani kuwa ni usiku wa Laylatul-Qadr. Hakumtaka aombe mali, au cheo, taqwa au kingine chochote isipokuwa msamaha wa kufutiwa kabisa madhambi yote. Kwa kuwa mambo mengine anaweza kuyaomba katika nyakati nyingine zozote ambazo humpitia mtu kila siku. Lakini usiku huu ambao ni nadra kuupata, na unakuja mara moja tu kila mwaka, du’aa hii inakuwa mwafaka zaidi kuliko du’aa nyingine yoyote.

 

 

Msamaha huu wa Allaah ('Azza wa Jalla) kama mja ataupata, basi moja kwa moja mja huyo ataingia Peponi kwa kuwa hakuna tena kizuizi cha kufika huko.

 

 

Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anayapenda Majina Yake na Sifa Zake, na Anapenda waja Wake wamwabudie kwayo, na wayafanyie kazi kwa muktadha wake na maana zake.

 

 

Madhambi na maasia ni moja kati ya sababu kubwa za kuteremka misukosuko kwetu, mitihani na naqama nyinginezo hapa duniani, na pia kuondoshewa neema ambazo Allaah ('Azza wa Jalla) Amewaneemesha waja Wake. Ama huko Aakhirah, mja kama hana madhambi basi bila shaka ataingia Peponi moja kwa moja.

 

Share