002-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Aina Za Twahara

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara:

 

002-Aina Za Twahara

 

Alhidaaya.com

 

 

Maulamaa wanaigawanya twahara ya kisharia katika vigawanyo viwili:

1- Twahara halisi, nayo ni kuondosha uchafu (najsi) unaokuwepo katika mwili, nguo na mahala.

 

 

2-Twahara ya kihukmu, nayo ni kujitwaharisha kutokana na hadathi. Twahara hii  inahusiana na mwili tu, na iko aina tatu:

-Twahara kubwa, nayo ni kuoga.

-Twahara ndogo, nayo ni kutawadha.

-Na badala ya viwili hivyo vinaposhindikana, nayo ni kutayamamu.

 

 

Kwanza: Twahara Halisi

 

Makusudio Ya Najsi:

 

Najsi ni kinyume cha twahara. Ni jina la kitu chenye kuonekana kichafu kisharia. Ni lazima Muislamu ajiepushe nacho na akioshe kile kilichompata katika kitu hicho.

 

Aina Za Najsi:    

                                                                                                        

Vitu ambavyo dalili za kisharia zimethibitisha kuwa ni najsi ni:

 

1, 2- Kinyesi na mkojo wa mwanadamu

 

Viwili hivi ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa.

 

Dalili ya kinyesi kuwa ni najsi ni neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 (( إذَا وَطِئَ أَحَدكُمْ بِنَعْلِهِ الْأَذَى فَإِنَّ التُّرَابَ لَهُ طَهُورٌ ))

((Akikanyaga mmoja wenu kinyesi kwa kiatu chake, basi udongo ndio kitwaharisho chake)). [Abuu Daawuud (385) kwa Sanad Swahiyh].  

Pia zinadulisha unajsi wake Hadiyth zote zenye kuamuru kustanji ambazo zitakuja karibuni.

 

Ama mkojo, ni kwa Hadiyth ya Anas kwamba bedui mmoja alikojoa ndani ya masjid na baadhi ya watu wakamnyanyukia kutaka kumpiga. Hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

((دعوه لا تزرموه))

((Mwacheni msimkatishe)).

 

Akasema: “Alipomaliza, aliagiza ndoo ya maji  akaimimina juu yake”. [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (6025) na Muslim (284)]. 

 

 

3, 4- Madhii na wadii

 

Madhii ni maji mepesi mno yenye kunatanata yanayotoka wakati wa matamanio ya kimwili kama kuchezeana, au mtu anapokumbuka tendo la kujimai au kuwa na hamu nalo. Maji haya hayachupi au kufuatiwa na mchoko, na mtu anaweza asiyahisi yanapomtoka. Humtoka mwanamume na mwanamke, lakini wanawake ni zaidi. [Angalia Fat-hul Baariy (1/379), na Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (1/599)].

 

Nayo ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa. [Angalia Al-Majmuu cha An-Nawawiy (2/6) na Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/168)].

 

Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuuosha utupu maji hayo yanapotoka.

 

Katika Swahiyh Mbili panaelezwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aliyemuuliza kuhusu madhii:

((يغسل ذكره ويتوضأ))

((Aoshe dhakari yake na atawadhe)). [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (269) na Muslim  (303)]

Ama wadii,  haya ni maji mazito meupe yanayotoka baada ya kukojoa. Ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa.

 

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas akisema:  "Manii, wadii na madhii. Ama manii, ni yale ambayo yakitoka, ni kuoga. Ama wadii na madhii (yakitoka), basi osha dhakari yako – au nyuchi zako – na tawadha wudhuu wako wa Swalaah". [Sunan Al-Bayhaqiy (1/115). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Sunan Abuu Daawuud (190)].

 

5- Damu ya hedhi

 

Ni kwa Hadiyth ya Asmaa binti Abuu Bakr (Radwiya Allaahu 'anhuma), amesema: "Alikuja mwanamke mmoja kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Afanyaje mmoja wetu nguo yake ikiingia damu ya hedhi?” Akasema Rasuli:

((تحته ثم تقرصه بالماء ثم تنضحه، ثم تصلي فيه))

((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha ya kidole na maji, halafu ataisuuza, na kisha ataswalia)). [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (227) na Muslim (291].

 

 

6- Kinyesi cha mnyama asiyeliwa

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah ibn Mas'uud, amesema: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kwenda haja kubwa akaniambia:

((ائتني بثلاثة أحجار))

((Niletee vijiwe vikubwa vitatu)).

Nilimpatia viwili na kinyesi cha (punda). Akachukua vijiwe viwili akakitupa kinyesi na kuniambia:

 ((هي رِجْسٌ ))

((Hicho ni najsi)). [Swahiyh Al-Bukhaariy (156), At-Tirmidhiy (17), An-Nasaaiy (42), na Ibn Khuzaymah ambaye ameongeza (punda wake].

 

Kitendo hiki kinaonyesha kwamba kinyesi cha mnyama asiyeliwa ni najsi.

 

 

7- Mate ya mbwa

 

 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 (( طُهُورُ إِنَاءِ أحَدِكُمْ إِذَا وَلَغَ فِيهِ الكَلْبُ أنْ يَغْسِلَهُ سَبْعَ مَرَّاتٍ أُولاَهُنَّ بِالتُّرَابِ.))

((Utwaharisho wa chombo cha mmoja wenu mbwa akikitia ulimi ni kukiosha mara saba, ya kwanza kati yake kwa udongo)). [Swahiyh Muslim (279)].

 

Hadiyth hii inaonyesha kwamba mate ya mbwa ni najsi.

 

 

 

8- Nyama ya nguruwe

 

Ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa kwa kuelezewa wazi katika neno Lake Subhaanah:

 

((قُلْ لَا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَنْ يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنْزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ ))

(( Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hayo ni uchafu )). [Al An-Aam (6:145].

 

 

9- Nyamafu

 

Naye ni mnyama aliyejifia mwenyewe bila kuchinjwa chinjo la kisharia. Ni najsi kwa Ijma’a ya Wanazuoni kwa neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:

 (( إِذَا دُبِغَ الإِهَابُ؛ فَقَدْ طَهُرَ))

((Ngozi ya nyamafu ikisafishwa na kukaushwa kwa madawa, basi imetwaharika)). [Swahiyh Muslim (366)].

 

Haviingii katika hukmu hii:

 

(a) Maiti ya samaki na nzige.

 

Viwili hivi ni twahara kwa neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((أُحِلَّتْ لَنَا مَيْتَتَانِ وَدَمَانِ: أما الميتتان فالحوت وَالْجَرَادُ ، وأما َالدمان فالْكَبِدُ ، وَالطِّحَالُ ))

((Tumehalalishiwa mfu mbili na damu mbili. Ama mfu mbili, ni samaki na nzige. Ama damu mbili, ni ini na wengu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (3218, 3314) na Ahmad (2/97) kwa Sanad Swahiyh].

 

 

(b) Mfu wa mnyama asiye na damu ya kuchuruzika

 

Ni kama nzi, nyuki, sisimizi, chawa na kadhalika kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

 

(( إذا وقع الذباب في إناء أحدكم فليغمسه كله أو ليطرحه، فإن في أحد جناحيه داء وفي الآخر شفاء))

((Akiangukia nzi katika chombo cha mmoja wenu, basi amzamishe wote au amtupe, kwani katika bawa lake moja kuna ugonjwa na katika jingine kuna ponya)).[Swahiyh Al-Bukhaariy (3320)].

 

 

(c) Mifupa ya mfu, pembe zake, kucha zake, manyoya yake na magoya yake.

 

Hivi vyote asili yake ni twahara. Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake (1/342) ameeleza: “Amesema Az-Zuhriy - kuhusu mifupa ya mzoga wa mnyama kama vile tembo na wengineo - : Niliwakuta watu katika Maulamaa waliotangulia wakichana nywele na kujitia mafuta kwa vitu hivyo, nao hawaoni ubaya wowote kwa hilo”.

Hammaad amesema: “Hakuna ubaya kwa ugoya wa mfu”.

 

 

10- Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai

 

Kilichokatwa toka kwa mnyama hai kina hukmu ya nyamafu kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((ما قطع من البهيمة وهي حية فهو ميتة))

((Kilichokatwa kwa mnyama akiwa hai, basi ni nyamafu)).[Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1480), Abu Daawuud (2858) na Ibn Maajah (3216)].

 

11- Makombo ya maji ya wanyama mwitu na wanyama wasioliwa.

 

Unajsi wake unagusiwa na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa kuhusu maji ya jangwani (nyikani), na yale yanayonywewa mara kwa mara na wanyama mwitu na wanyama wasioshambulia akasema:

 ((إِذَا كَانَ الْمَاءُ قُلَّتَيْنِ؛ لَمْ يَحْمِلِ الْخَبَثَ))

 ((Maji yakiwa kullatayni, hayabebi uchafu (najsi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (63), An Nasaaiy (1/46), na At-Timidhiy (67). Ipo katika Swahiyh Al-Jaami’i (758)].

Ama mabaki ya paka na mfano wake, hayo ni twahara kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( إِنَّهَا لَيْسَتْ بِنَجَسٍ ، إِنَّهَا مِنَ الطَّوَّافِينَ عَلَيْكُمْ وَالطَّوَّافَاتِ ))

((Yeye si najsi, bali ni katika waume na wake wanaowazungukieni)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/303) na Aswhaab As-Sunan. Angalia Al-Irwaa (173)].

 

 

12- Nyama ya mnyama asiyeliwa

 

Hii ni kwa Hadiyth ya Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu)   amesema: "Tuliipata nyama ya punda – yaani siku ya Khaybar – na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanadi:

((إن الله ورسوله ينهاكم عن لحوم الحمر فإنها رجس، أو نجس))

((Hakika Allaah na Rasuli Wake Anakukatazeni nyama ya punda. Ni uchafu, au najsi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1940) na Ahmad (3/121). Ipo kwenye Al-Bukhaariy bila ya neno: (فإنها رجس)]

 

Na kwa Hadiyth ya Salamah bin Al Akwa'a, amesema:

“Ilipoingia jioni ya siku Khaybar imekombolewa, waliwasha mioto mingi. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

((ما هذه النار على أي شيئ توقدون))

((Moto huu ni wa nini? Mnauwashia kwa jambo gani?))

Wakasema: "Kwa ajili ya nyama". Akauliza:

((Ya mnyama gani?)).

Wakasema: “Nyama ya punda wa mjini”. Akasema:

((Imwageni na vivunjeni)).

 Akasema mtu mmoja: “Ee Rasuli wa Allaah! Je, tuimwage na tuvioshe”? Akasema:

((Au hilo)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1802)].

 

Katika Hadiyth hizi mbili, kuna dalili kwamba nyama ya punda wa mjini (kienyeji) ni najsi kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya kwanza:

((Ni uchafu, au najsi)), na katika Hadiyth ya pili kwa kukivunja chombo kwanza, kisha kuruhusu kutumika  kwa kukiosha mara ya pili.

 

 

Share