007-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nini Hukmu Ya Majimaji Yanayotoka Kwenye Utupu Wa Mwanamke Au Unyevunyevu Wa Utupu Wake?

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

007- Nini Hukmu Ya Majimaji Yanayotoka Kwenye

Utupu Wa Mwanamke Au Unyevunyevu Wa Utupu Wake?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Maulamaa wana mielekeo miwili kuhusu unyevunyevu wa utupu wa mwanamke:  [Al-Mughny (2/88), na Al-Majmu'u (1/570)].

 

Mwelekeo wa kwanza:

 

Ni najsi, kwa kuwa yako ndani ya utupu, si maji ya uzazi na yanafanana na madhii. Wametolea dalili kwa Hadiyth ya Zayd bin Khaalid kwamba alimuuliza 'Uthmaan bin ‘Affaan (Allaah Amridhie) akisema: "Nieleze, (nini hukmu) mtu anapomwingilia mkewe na wala hakumwaga manii? Akasema 'Uthmaan: "Atatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah, na ataiosha dhakari yake". 'Uthmaan akasema: "Nimeyasikia toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". [Isnadi Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (292), na Muslim (347), lakini imekuwa Mansuwkh]

.   

Na Hadiyth ya Ubayy bin Ka-'ab kwamba alisema: "Ee Rasuli wa Allaah! Inakuwa vipi mtu akimwingilia mkewe bila kumwaga? Akasema:

 

 (يغسل ما مس المرأة منه ثم يتوضأ ويصلي)

((Ataiosha sehemu aliyomgusa nayo mwanamke, kisha atatawadha, na ataswali)). [Isnadi Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (293), na Muslim (346), lakini imekuwa Mansuwkh].

 

Wamesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuamrisha kuiosha sehemu iliyogusana na utupu wa mwanamke, ni dalili juu ya unajsi wa unyevu wa utupu wa mwanamke”.

 

“Mimi ninapinga (Abuu Maalik) kwa kusema kuwa Hadiyth hizo mbili zimenasikhiwa  na Hadiyth nyingine zenye kuamrisha kuoga kama itakavyokuja katika sehemu yake inshaAllaah”. [Angalia kwenye Kitabu cha Fat-hul Baary (1/473)].

 

Na pia kuna uwezekano wa kuwa amri ya kuosha ni kutokana na madhii yanayomtoka mwanamume au mwanamke.

 

Vile vile, wametolea ushahidi juu ya unajsi wa (majimaji hayo) kwa kuwa yanatoka katika moja ya njia mbili. Na kaida inasema:

"Chenye kutoka katika njia mbili, basi ni najsi isipokuwa manii".

 

 

Mwelekeo wa pili:

 

Ni kwamba majimaji ya utupu ni twahara.  [Angalia kwenye Jaami'i Ahkaamu An-Nasaaiy (1/68) cha Shaykh wetu Mustwafa bin Al-'Adawy Allaah Amhifadhi].

 

Mwelekeo huu unatolewa dalili kwa haya yafuatayo:

 

1- Kwamba 'Aaishah - Allaah Amridhie,- alikuwa akiyakwangua manii kutoka katika nguo ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yakiwa yametokana na kukutana kimwili, kwani Rasuli kamwe hakuota kuwa anaingilia. [Hivi ndivyo alivyosema katika Al-Mughny (2/88). Na Shaykh wetu amesema: "Hili linahitajia matni toka katika Qur-aan au Hadiyth, na wala hatukuikuta matni katika mfano wa hili"]. 

Anapoingilia, hukutana na umajimaji wa utupu. Na kwa vile sisi, lau kama tungelihukumia unajsi wa utupu wa mwanamke, basi tungelihukmu unajsi wa manii yake, kwani manii hayo yanatokea kwenye utupu wake, na kwa hivyo yananajsika kwa unyevunyevu wake.

 

 

2- Kwamba majimaji haya ni jambo ambalo liko wazi, nayo huwatoka sana wanawake. Na hakuna shaka kwamba jambo hili lilikuwepo kwa wanawake katika enzi za Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo kwa wanawake wa zama zetu hizi. Na wala haikupokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha kuosha, au kutawadha kutokana na hali hiyo.

 

3- Kwamba sehemu ya kutokea majimaji haya, si sehemu ya kutokea mkojo ambao ni najsi.

 

4- Kwamba kauli ya Maulamaa isemayo: "Kila chenye kutoka kwenye njia mbili ni najsi isipokuwa manii", si kauli iliyopokelewa toka kwa Rasuli Al Ma’aswuwm (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wala kauli hii haijafanyiwa Ijma’a ya Ummah. Bali imepokelewa kwamba baadhi ya vinavyotoka kwenye njia mbili havitengui wudhuu, mfano wa damu ya istihaadhwah ambayo tutakuja kuielezea mbeleni.

 

Ninasema (Abuu Maalik): “Ninaloliona mimi lenye nguvu, ni kwa ufafanuzi huu:

"Ikiwa majimaji haya yanamtoka mwanamke wakati wa kuchezeana na mumewe, au wakati anapokuwa na hamu ya kujamiiana na mfano wa hili hasa, basi hayo ni madhii. Na mimi nimejua kwamba madhii ni najsi ambayo ni lazima ioshwe, na pia inatengua wudhuu.

 

Ama ikiwa majimaji haya yanatoka kwenye utupu wa mwanamke takriban nyakati zote, na yanazidi wakati wa ujauzito, au wakati anapofanya kazi kwa bidii, au anapotembea mwendo mrefu, basi majimaji hayo ni twahara kiasili kwa kutokuwepo dalili juu ya unajsi wake. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

Share