02-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Akijali Mno Umma Wake Na Akiwakhofia Adhabu

 

 

 

 Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

02-Akijali Mno Umma Wake Na Akiwakhofia Adhabu

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Nabiy wetu Muhammad   (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akijali mno Ummah wake huu wa Kiislamu, akikhofia na kujali Waumini wasipatwe na shari au  balaa au adhabu yoyote ile. Hadiyth ifuatayo ni dalili mojawapo ya kujali kwake kwa Ummah huu wa Kiislamu:

 

 

عنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرِو بْنِ الْعَاصِ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم تَلاَ قَوْلَ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ فِي إِبْرَاهِيم: ((‏رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِنَ النَّاسِ فَمَنْ تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي)) الآيَةَ‏.‏ وَقَالَ عِيسَى عَلَيْهِ السَّلاَمُ:((إِنْ تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ وَإِنْ تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ‏)) فَرَفَعَ يَدَيْهِ وَقَالَ" ((اللَّهُمَّ أُمَّتِي أُمَّتِي)) وَبَكَى فَقَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ: يَا جِبْرِيلُ اذْهَبْ إِلَى مُحَمَّدٍ وَرَبُّكَ أَعْلَمُ فَسَلْهُ مَا يُبْكِيكَ فَأَتَاهُ جِبْرِيلُ   عَلَيْهِ الصَّلاَةُ وَالسَّلاَمُ  فَسَأَلَهُ فَأَخْبَرَهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم بِمَا قَالَ‏.‏ وَهُوَ أَعْلَمُ‏.‏ فَقَالَ اللَّهُ يَا جِبْرِيلُ اذْهَبْ إِلَى مُحَمَّدٍ فَقُلْ إِنَّا سَنُرْضِيكَ فِي أُمَّتِكَ وَلاَ نَسُوءُكَ.

 

 

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (رضي الله عنه):  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma kauli ya Allaah (عزّ وجلّ) kuhusu Nabiy Ibraahiym:

 

رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ ۖ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي ۖ  

Rabb wangu! Hakika hao (masanamu) wamepoteza watu wengi.  Basi atakayenifuata, huyo yuko nami. [Ibraahiym: 36]

 

Na amesema ‘Iysaa (عليه السلام):

 

إِن تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ ۖ وَإِن تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١١٨﴾

Ukiwaadhibu, basi bila shaka hao ni Waja Wako, na Ukiwaghufuria basi hakika Wewe Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote [Al-Maaidah: 118]

 

Akanyanyua mikono yake akisema: “Ee Allaah! Ummah wangu! Ummah Wangu!  Akalia, kisha Allaah (عزّ وجلّ) Akasema: “Ee Jibriyl! Nenda kwa Muhammad, na Rabb wako Anajua zaidi, kisha muulize kitu kigani kinachomliza? Basi Jibriyl akamwendea (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuuliza (sababu ya kulia kwake), na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjulisha, na Allaah Anajua zaidi, Hapo Allaah Akasema: “Ee Jibriyl! Nenda kwa Muhammad na mwambie: Hakika Sisi Tutaridhia Ummah wako wala Hatutaudhika nawe.” [Muslim]

 

Imaam An-Nawawiy (رحمه الله) amesema katika Sharh Muslim: “Hadiyth hii imejumuisha aina za faida zikiwemo: Bainisho kamilifu la huruma zake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Ummah wake, na kujali kutunza maslahi yao, na kutilia hima mambo yao. Na hii ni bishara adhimu kwa Ummah huu kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ameuzidishia (Ummah) Sharaf (taadhima)  kutokana na ambayo Allaah (سبحانه وتعالى)  Amemuahidi Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم)  katika kauli Yake: “Tutaridhia Ummah wako wala Hatutaudhika nawe.”  Na hii ni Hadiyth itoayo matarajio makubwa kabisa kwa Ummah huu.

 

 

 

Share