14-Du'aa Za Ruqyah: Kujikinga Na Shari Ya Sehemu Mtu Anaposhukia

 

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

14-Kujikinga Na Shari Ya Sehemu Mtu Anaposhukia

 

www.alhidaaya.com

 

 

  

Imepokelewa toka kwa Khawlah binti Al-Hakiym akisema:  Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    akisema:

 

((من نزل منزلاً ثم قال: أعوذ بكلمات الله التامات من شر ما خلق لم يضره شيء حتى يرتحل من منزله ذلك))

((Mwenye kufikia mashukio (nyumba)  yoyote kisha akasema: Najilinda kwa Maneno ya Allaah yaliyotimu na shari ya Alivyoviumba, hakitomdhuru chochote mpaka aondoke kwenye mashukio yake hayo)).  [Imesimuliwa na Muslim katika Swahiyh yake toka kwa Khawlah bint Al-Hakiym]

 

 

 

Faida Na Sharh:

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipokuwa anasafiri, alikuwa hapiti kwenye mwinuko wowote ila hupiga takbiyr, na hashuki bonde lolote ila humsabihi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).    Hii ndiyo hali aliyokuwa nayo kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    ya kuwa na mwonjo wa hali ya juu wa kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika hali zote. Hili linatakiwa liwe kiigizo chema kwetu katika hali zetu zote.

 

Pia mtu anapohamia katika nyumba mpya asome du’aa hiyo na si kufanya kama wafanyao wenye kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuchinja na kukanyaga damu, au kuvunja mayai au kutundika vitu na kadhalika kwa ajili ya kinga.

 

 

Hata mtu anapokaa kufanya mkataba wa manunuzi, anapoingia kutoa darsa au muhaadharah, anapoanza mradi, anapokwenda mahakamani, anapokwenda kazini na kwenye mishughuliko yake yote ya kidunia na ki-Aakhirah, basi asisahau kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Na safari kwa hali yoyote ina mazito yake. Mazito haya yote Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ameyafanya kuwa ni sehemu ya ‘ibaadah ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kutaamuli yote anayoyaona msafiri safarini.

 

Mwana Aadam anapokithirisha kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla), basi inaundika kwake hisia ya sita inayomkumbusha daima Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kumkumbusha Uwezo Wake kwa kila anachokiona katika mazingira yanayomzunguka na anayoyapita.

 

Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  yaliyotimu kama walivyosema baadhi ya ‘Ulamaa ni:

 

سبحان الله والحمد لله ولا إله إلا الله والله أكبر

Ndani yake kuna tasbiyh, himdi, tawhiyd na takbiyr.

 

 

Kila mahala anapokwenda mtu kuna hatari. Mtu anaweza kusafiri kwenda nje ya nchi, na huko akaibiwa mkoba wake wenye kila kitu muhimu ndani yake; pasi ya kusafiria, pesa, kadi na vinginevyo muhimu. Hapo hukumbana na kila aina ya mateso. Hata kuufikia ubalozi wake kumsaidia wakati mwingine inakuwa ni kazi kubwa kwa kuwa hata pesa ya kuendea huko anakuwa hana. Hata ndani ya nchi yake, itabidi ahangaike sana mpaka aweze kuweka mambo sawa.

 

 

Wakati mwingine anapofika uwanjani sehemu ya kupokea mizigo, anakuta mizigo yake haikuwasili na ndege aliyopanda yeye. Linaibuka tatizo jingine hapo, kwa kuwa kila kitu chake kimo humo. Ndege ilipotua salama, alikuwa na furaha isiyo na kifani, kwa kuwa lau pangelitokea tatizo lolote ndege ikiwa juu, basi asingelibakia mtu. Baadhi ya watu hupiga makofi, badala ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa kuwafikisha salama. Hilo wamelianzisha wamagharibi, na sisi tunaiga kibubusa tu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    alipokuwa anawasili salama, baada ya kufanikisha vyema safari yake na kurudi salama kwa wakeze, wanawe na watu wake, alikuwa akisema:

 

الحمد لله الذي بنعمته تتم الصالحات

 

Himdi Ni Yake Allaah Ambaye kwa Neema Zake yanatimu mema matengefu.

 

Haya ni baadhi ya yanayotukabili katika safari zetu za siku hizi kwa wale wenye kusafiri safari za kawaida. Lakini kuna wasafiri wengine na hususan watafiti na wataalamu wa mambo mbalimbali wanaozamia ndani ya misitu mizito, vina virefu vya bahari, majangwa, mabonde na kadhalika, hawa hatari inakuwa kubwa zaidi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ametufundisha du’aa nyingine ya kujikinga na hatari ya haya. Inasimuliwa na  ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)  akisema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   alikuwa anaposafiri na usiku ukaingia husema:

 

يا أرض ربي وربكِ الله، أعوذ بالله من شرك وشر ما فيكِ، وشر ما خلق فيكِ، وشر ما يدب عليكِ

((Ee ardhi! Rabb wangu na  Rabb wako ni Allaah. Najilinda kwa Allaah na shari yako, na shari ya vilivyomo ndani yako, na shari ya vilivyoumbwa ndani yako, na shari ya vinavyotambaa juu yako)).  [Imesimuliwa na Abuu Daawuwd na kupokelewa toka kwa 'Abdullaah bin ‘Umar]

 

Pia alikuwa akijikinga na nge, nyoka, na wanyama wakali.

 

Alikuwa akisema:

 أعوذ بالله من أسد وأسود ومن الحية والعقرب ومن ساكن البلد ومن والد وما ولد

((Najilinda Kwako na simba, mijoka, nyoka, nge, mkazi wa nchi, na kilichozaa na kilichozaliwa)). [Imepokelewa na ‘Abdullaah bin ‘Umar]

 

 

Mkazi wa nchi hapa ni ima wana Aadam, au majini. Na kilichozaa ni Ibliys na kilichozaliwa ni mashaytwaan, au vyote vyenye kuzaa na kuzaliwa ardhini na vyenye madhara kwa mwana Aadam.

 

 

Share