000-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Utangulizi Wa Alhidaaya

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Utangulizi Wa Alhidaaya:

 

Alhidaaya.com

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

Tumekichagua kitabu hiki miongoni mwa vitabu vya Fiqhi kufasiriwa na kuwekwa kwenye tovuti hii, kwa sababu tumekiona ndicho kitabu sahihi zaidi cha Fiqhi kuliko vingine kutokana na Hadiyth zake kufanyiwa tahakiki na kuthibitishwa usahihi wake. Hiki ni tofauti na kitabu maarufu kijulikanacho kama Fiqhus-Sunnah cha mwanachuoni wa Ki-Misr, Sayyid Saabiq pamoja na kufanana kiasi majina yake. Mwandishi wa kitabu hiki, mwanachuoni wa Ki-Misr aitwaye Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayid Saalim, kakiita “Swahiyh” kwa sababu ya kuhakikisha kuwa Hadiyth zote alizotolea ushahidi humo ndani, zimethibitishwa usahihi wake na wanachuoni wakubwa wa Hadiyth.

 

 

Vilevile kitabu hiki kimepitiwa na kutolewa maoni na maelezo ya kisasa kabisa na ‘Ulamaa wakubwa; Imaam Muhammad Naaswiru-Ddiyn Al-Albaaniy ambaye ni bingwa wa elimu ya Hadiyth, na pia aliyekuwa Mufti wa Saudia  Imaam 'Abdil-'Aziyz bin Baaz, na Mwanachuoni Faqiyh  Imaam Muhammad bin Swaalih bin 'Uthaymiyn (Allaah Awarehemu wote na Awalaze kwenye pepo ya juu kabisa).

 

 

Hizo ndizo sababu kuu za kukichagua kitabu hiki kuwa ni rejea za mafunzo ya elimu ya shariy'ah za Dini kwa wana-Alhidaaya wote na Waislam kwa ujumla.

 

 

Na bila shaka hiki ndicho kitabu cha kwanza katika vitabu vikubwa (Mijalada) cha Fiqhi kwa lugha ya kiswahili. Tunaamini Waislam wengi watanufaika kwa kazi hii na yaliyomo ndani yake.

 

 

Allaah Amlipe malipo mema Shaykh Abuu Maalik Kamaal mwandishi wa kitabu, ‘Ulamaa; Imaam Al-Albaaniy, Imaam Ibn Baaz, Imaam Ibn 'Uthaymiyn na kadhalika ndugu yetu mfasiri wa kitabu hiki, Al-Akh 'Abdallaah Mu'aawiyah ambaye bado anaendelea na kazi hiyo. Tusiwasahau hao wote kwa du'aa in shaa Allaah pamoja na wahusika wa Alhidaaya ambao wameisimamia kazi hii na nyenginezo.

 

 

 

Kimehaririwa tarehe 22 Rabiy'u Al-Aakhir 1440 H (29 Decemba 2018M)

 

 

 

 

Share