012-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kitu Gani Hutumika Kustanjia?

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

012-Kitu Gani Hutumika Kustanjia?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Inatosheleza kustanji kwa moja ya vitu viwili:

 

 

1- Mawe na mfano wake kati ya kila kitu kigumu chenye  kuondosha najsi na kisicho na thamani kubwa.

 

Ni kama karatasi, vitambaa, mbao na vyote vyenye kutakasa najsi.

Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 ((إذا ذهب احدكم إلى الغائط فليستطب بثلاثة احجار فإنها تجزيء عنه))

((Anapokwenda mmoja wenu haja, basi astanji kwa vijiwe vitatu, kwani hivyo humtosheleza)). [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (40), An Nasaaiy (1/18), Ahmad (6/108 – 133) kwa Sanad Dhwa’iyf. Kuna Hadyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine yenye kuitilia nguvu. Angalia Al- Irwaa (44)].

Haijuzu kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu, kwa kauli hizi zenye nguvu:

 

(a)  Ni kwa Hadiyth ya Salmaan, amesema:

 

"Hakika alitukataza sisi (yaani Rasuli (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuelekea Qibla wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, au kustanji kwa mkono wa kulia, au kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu, au kustanji kwa kinyesi au mfupa".[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (262), An-Nasaaiy (1/16), At-Tirmidhiy (16) na Abuu Daawuud].

 

 (b) Imepokelewa toka kwa Jaabir, amesema:  

 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا استجمر أحدكم فليستجمر ثلاثا))

 

((Anapostanji mmoja wenu kwa vijiwe, basi astanji mara tatu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad, Ibn Abu Shaybah, na Ibn Khuzaymah. Al Huwayniy Allaah Amhifadhi anasema kwamba Sanad yake ni Swahiyh katika kitabu cha Badhl Al Ihsaan]. 

 

(c) Imepokelewa toka kwa Khilaal bin As-Saaib toka kwa baba yake ikiwa ni Marfu’u:

 

((إذا  دخل أحدكم الخلاء فليتمسح بثلاثة أحجار))

 

((Anapoingia mmoja wenu msalani, basi ajipanguse kwa vijiwe vitatu)). [Hadiyth Hasan kutokana na yaliyotangulia. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (7/6623). Angalia Al-Badhl (1/352)].

  

 

Ninasema (Abuu Maalik): "Ikiwa patasafika kwa vijiwe vitatu, basi ni vyema. Na kama si hivyo, itabidi kuongeza zaidi ya vitatu mpaka pasafike".

 

Haifai kustanji kwa mifupa au kinyesi cha mnyama kutokana na Hadiyth ya Ibnu Mas'uud kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

(( لا تَسْتَنْجُوا بِالرَّوْثِ وَلا بِالْعِظَامِ فَإِنَّهُ زَادُ إِخْوَانِكُمْ مِنَ الْجِنِّ ))

 

((Msistanji kwa kinyesi cha mnyama wala mifupa, kwani hivyo ni masurufu ya ndugu zenu katika majini)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (682), At-Tirmidhiy (18) na Ahmad (1/436)]  

 

Na imepokelewa toka kwa Ibnu Masu'ud, amesema:

"Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda haja, akaniamuru nimletee vijiwe vitatu. Nilipata viwili na nikatafuta cha tatu lakini sikukipata. Nikachukua kinyesi cha mnyama nikamletea. Alivichukua vijiwe viwili na akakitupa kinyesi. Akasema:

((هذا ركس))

 

((Hii ni najsi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (156) na wengineo. Imeshatajwa nyuma].   

 

 

2- Maji

 

Imepokelewa toka kwa Anas, amesema:

 

"Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiingia msalani, na mimi na kijana pembeni mwangu tunabeba ndoo ya maji na kiegemeo, na yeye (Rasuli) akistanji kwa maji".[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (151), Muslim (270, 271) na wengineo].

 

Na kustanji kwa maji ni bora zaidi kuliko kustanji kwa mawe, kwani Allaah Mtukufu Amewasifu watu wa Qubaa kwa kustanji kwa kutumia maji.

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Allaah Amridhie) ikiwa marfu'u:

"Aayah hii iliteremka kwa watu wa Qubaa:

(( فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُواْ))

 

(( Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa)).[At Tawbah ( 9:108)].

 

Akasema: "Walikuwa wakistanji kwa maji, na Aayah hii  ikateremka kuwazungumzia wao". [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (44), At-Tirmidhiy (3100) na Ibn Maajah kwa Sanad Dhwa’iyf. Kuna Hadyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine yenye kuitilia nguvu. Angalia Al-Irwaa (45)]. 

 

At-Tirmidhiy anasema (1/31): “Hili ndilo ambalo Wanachuoni wanalolifanya. Wamekhitari kustanji kwa maji ingawa kustanji kwa mawe kunawatosheleza. Wamependelea kustanji kwa maji na wamelionelea hilo ni bora zaidi. Na hayo hayo ameyasema Sufyaan Ath-Thawriy, Ibn Al-Mubaarak, Ash-Shaafi'iy, Ahmad na Is-haaq na wengineo”.

 

 

Mtu Hastanji Kwa Kutokwa na Upepo, Na Si Lazima Kustanji Kabla ya Kutawadha

 

Si lazima kustanji kwa mtu aliyetokwa na upepo au aliyeamka toka usingizini. Ibnu Qudaamah anasema:

" Hatujui katika hili mahitilafiano yoyote".

Abuu ‘Abdullah anasema:

"Hakuna katika Kitabu cha Allaah wala katika Hadiyth za Rasuli Wake kwamba mtu astanji kwa kutokwa na upepo, bali linalompasa ni kutawadha".

 

Na imepokelewa toka kwa Zayd bin Aslam katika Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

((إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ))

((Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah, basi osheni nyuso zenu)). [Al Maaidah (5:6)].

 

..akisema: "Mnapotoka usingizini, na Hakuamuru jingine zaidi. Hivyo basi, inaonyesha si lazima, kwa kuwa la wajibu hubainishwa na shariyah. Na hapa Aayah haikutaja kustanji, wala kustanji huko hakuko katika maana iliyoelezewa, kwani kustanji kumewekwa kwa ajili ya kuondosha najsi, na hapa hakuna najsi.." [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/206)].   

 

Kustanji si lazima kuungamane na wudhuu, hilo halikusuniwa na wala halikupendezeshwa kama wanavyodhani watu wengi, bali hiyo ni ‘ibaadah peke yake kando. Makusudio yake ni kupatakasa mahali kutokana na najsi. Na wala hakuna yeyote aliyenukuu kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akistanji kila anapotawadha au aliamuru hilo.

 

 

Share