017-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Sunnah Za Hulka Asilia

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

017- Sunnah Za Hulka Asilia

 

Alhidaaya.com

 

 

Nini Maana Ya Sunnah Za Hulka Asili? Ni Zipi Sunnah Hizo?

 

Sunnah za hulka asili ni mambo ambayo mtu akiyafanya, huipata hulka asili ambayo Allaah Amewaumbia kwayo waja, Atawakusanya wakiwa nayo (Siku ya Qiyaamah), na Amewapendelea waifanye ili wawe juu ya ukamilifu wa sifa na utukufu wa sura.

 

Mambo haya ni mwenendo wa kale ambao Manabii waliuchagua na sharia zote zikakubaliana juu yake. Inakuwa ni kama jambo la kimaumbile waliloumbiwa kwalo watu. [Nayl Al-Awtwaar (1/109) na Umdat Al-Qaariy cha Al’ Ayniy (22/45)].

 

Maslaha ya kidini na kidunia hufungamana na mambo ya hulka asili ambayo hudirikiwa kwa ufuatiliaji. Kati ya mambo hayo ni kuliweka umbo katika picha nzuri na kuutakasa mwili ndani na nje, na kwa mapana na marefu. [Faydh Al-Qadiyr cha Al-Minnaawiy (1/38)].

 

Baadhi ya mambo haya yamepokelewa katika haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya Abuu Hurayrah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((الفطرة خمس: الختان، والاستحداد، وقص الشارب، وتقليم الأظافر، ونتف الآباط))

((Hulka asili ni matano: Kutahiri, kunyoa kinena, kukata sharubu, kukata kucha na kunyofoa vikwapa)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5891) na Muslim (257)].

 

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

 ((عشر من الفطرة: قص الشارب، واعفاء اللحية، والسواك، واشتنشاق الماء، وقص الأظفار، وغسل البراجم، ونتف الابط، وحلق العانة، وانتقاص الماء))

((Mambo kumi ni katika hulka asili: Kunyoa sharubu, kuziachilia ndevu, kupiga mswaki, kupaliza maji puani, kukata kucha, kuosha vifupachanda, kunyofoa nywele za kwapa, kunyoa kinena na kustanji)).

 

Mus’ab mmoja wa wapokezi wa Hadiyth anasema: “Nimelisahau la kumi kama halitakuwa ni kusukutua”.[Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (261), Abuu Daawuud (52), At-Tirmidhiy (2906), An-Nasaaiy (8/126) na Ibn Maajah (293).

 

Kutokana na Hadiyth hizi mbili, tunafahamu kuwa mambo ya hulka asili hayaishilii kwenye haya kumi tu, bali yako mengineyo. Kwa ufupi mambo haya ni:

 

 

  1. Kutahiri.
  2. Kustanji.
  3. Kupiga mswaki.
  4. Kukata kucha.
  5. Kukata sharubu.
  6. Kuachilia ndevu.
  7. Kunyoa kinena (mavuzi).
  8. Kunyofoa nywele za kikwapa.
  9. Kuosha vifupachanda na sehemu ambazo uchafu hujikusanya kama kwenye mibano ya vidole, makunjano ya masikio na kadhalika.
  10. Kusukutua na kupaliza maji puani.

 

 

 

 

 

 

Share