029-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nguzo Za Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

029-Nguzo Za Wudhuu

 

 

 

Nguzo za wudhuu ni mambo ambayo uhakika wake unajengekea kwayo kwa namna ambayo ikikosekana nguzo yoyote kati yake, basi wudhuu unabatilika na unakuwa hauzingatiwi kisharia. Nguzo hizo ni:

 

1- Kuosha uso wote:

 

Uso ni sehemu ya makabiliano. Na mpaka wake ni kutokea kwenye mapindio ya kipaji cha uso (au tokea kwenye maoteo ya kawaida ya nywele) mpaka kwenye mashukio ya ndevu na kidevu kwa urefu, na tokea kwenye sikio hadi sikio jingine kwa upana.

Kuosha uso ni nguzo kati ya nguzo za wudhuu. Wudhuu hautoswihi bila ya nguzo hii kwa neno Lake Subhaana: 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ ))

 

(( Enyi walioamini! Mnaposimama kuswali, basi osheni nyuso zenu)). [Al Maaidah 5:6]

Kila aliyehadithia sifa ya wudhuu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), amethibitisha kuoshwa uso. Na Maulamaa wote wamekubaliana juu ya hili.

 

Ni Lazima Kusukutua Na Kupaliza:

 

Kusukutua ni kusafisha mdomo na kuyazungusha maji ndani yake. Na kupaliza, ni kuyafikisha maji mpaka ndani ya pua na kuyavuta kwa pumzi hadi mwisho wake. Ama kupenga, ni kuyatoa maji puani (kwa mpumuo) baada ya kuyapaliza.

 

Kusukutua na kupaliza maji, ni mambo ya lazima wakati wa kutawadha kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi za Maulamaa. Na hii ni kwa dalili zifuatazo:

 

1- Ni kwamba Allaah Mtukufu Ameamuru kuosha uso kama ilivyotangulia. Na pua na mdomo ni sehemu ya uso, na wala hakuna chenye kuwajibisha kuhusisha nje yake bila ndani yake, kwani vyote hivyo viwili vinaitwa “uso” katika Lugha ya Kiarabu. Na kama utasema: “Tundu ya pua ina jina lake na pua ina jina lake, na hivyo haviitwi uso katika Lugha ya Kiarabu”, tunajibu tukisema: “Vilevile vitefute viwili, kipaji, mgongo wa pua, nyusi mbili na sehemu nyingine za uso, zina majina yake, na hivyo haviitwi uso! Huku ni kujikwaa kubaya, kwa kuwa kutamaanisha kwamba si lazima kuosha uso”. [Angalia Naylul Awtwaar (1/174) chapa ya Al-Jiyl na Ahkaamul Qur-aan cha Ibnul ‘Araby (2/563)].

 

 

2- Ni kwamba Allaah Mtukufu Ameamuru kuosha uso kiujumla, na Rasuli alilifasiri hilo kwa kulifanya kivitendo na kulifundisha. Akasukutua na akapaliza maji katika kila wudhuu aliotawadha. Na hakuna yeyote aliyenukulu kuwa aliacha kufanya hayo pamoja na kufupishia kwake juu ya kichache chenye kutosheleza. Na ikiwa kitendo chake kimefanyika kwa ajili ya kufuata amri, basi hukmu yake inakuwa ni hukmu ya jambo hilo katika kuhukumia ulazima. [Sharhul ‘Umdah cha Ibn Taymiyah (1/178) na At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barri (4/36)].

 

 

3- Amri ya kupaliza na kupenga imethibiti kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

((من توضأ فليستنثر))

((Mwenye kutawadha, basi apenge)).

 

Na katika riwaya nyingine:

 

  ((إذا توضا أحدكم فليجعل في أنفه ماء ثم ليستنثر))

((Anapotawadha mmoja wenu, basi aingize maji puani mwake kisha apenge)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (161), Muslim (237) na wengineo].

 

Na kauli yake:

 

(( إذا توضأ أحدكم فليستنشق..))

((Anapowatadha mmoja wenu, basi apalize maji puani)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (237)].

 

Na kauli yake:

 

(( وبالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائما..))

((na ubalighishe katika kupaliza isipokuwa kama umefunga)).[Hadiyth Swahiyh. Itakariri mara nyingi].

 

Shaykh  wa  Uislamu   anasema: “…Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa amri maalumu ya kupaliza, hakumaanishi kwamba ni muhimu zaidi kuliko kusafisha mdomo. Itawezekana vipi nailhali mdomo ndio sehemu tukufu zaidi ya kufanyia dhikri na kusoma, na mara nyingi hubadilika na kuwa na harufu mbaya?! Lakini kinachofananishwa hapa - na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi – ni kuwa, mdomo ulipowekewa usharia wa kupigwa mswaki na jambo hilo likasisitizwa, na pia kuuosha kabla na baada ya kula, itakuwa imejulikana kuwa Allaah Mtukufu Ametoa kipaumbele zaidi cha kuusafisha kinyume na pua ambayo imetajwa kwa ajili ya kubainisha hukmu yake ili isipuuzwe…”. [Sharhul ‘Umdah (1/179 – 180)].

 

 

4- Ni kwamba amri ya kusukutua imekuja vile vile katika Hadiyth nyinginezo zenye uhakika zaidi. Ni kama Hadiyth ya Laqyt bin Swabrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

(( إذا توضأت فمضمض))

((Ukitawadha, basi sukutua)).

 

Ninasema: “Na lau kama mtu atasema kwamba dalili za kuwajibisha kusukutua na kupaliza zimegeuzwa na kuelekezwa katika Sunnah kutokana na Hadiyth ya Rifa’a bin Raafi’i katika kisa cha mwenye kuswali vibaya ambaye Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

 

(( إنها لا تتم صلاة أحدكم حتى يسبغ الوضوء كما أمره الله تعالى، فيغسل وجهه ويديه إلى المرفقين ويمسح رأسه ورجليه إلى الكعبين...))

((Hakika haikamiliki Swalaah ya mmoja wenu mpaka akamilishe wudhuu wake kama Alivyoamrisha Allaah. Aoshe uso wake na mikono yake miwili hadi kwenye vifundo, na apake kichwa chake, na (aoshe) miguu yake miwili hadi kwenye vifundo…)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (859), At Tirmidhy (302), An Nasaaiy (2/20, 193) Ibn Maajah (460) na wengineo].

 

Hapa hakutaja kusukutua au kupaliza katika hayo ambayo Allaah Amemwamuru, na kwa hivyo amekwenda sawa na Aayah Tukufu. Hoja hii pia ni madhubuti na makinifu. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi".

 

 

Faida

 

Fahamu kwamba Wanazuoni wamehitalifiana juu ya hukmu ya kusukutua na kupaliza katika wudhuu na kuoga katika kauli nne.  [Ikhtilaaful ‘Ulamaa cha Al-Muruuziy (uk. 23-24), At-Tamhiyd (4/34), Al-Awsatw (1/379), At-Tahqiyq cha Ibn Al-Jawziy (1/143) na Al-Muhalla (2/50)].

 

Kauli ya kwanza:

 

Ni wajibu kusukutua na kupaliza wakati wa kuoga tu, lakini kwa wudhuu haipasi. Yamesemwa haya na Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wenzake na wengineo.

 

Kauli ya pili:

 

Ni Sunnah wakati wa kuoga na kutawadha. Haya yamesemwa na Maalik, Ash-Shaafi’iy, Al-Layth, Al-Awzaa’iy na jama‘ah.

 

Kauli ya tatu:

 

Yote mawili ni wajibu wakati wa kuoga na kutawadha. Haya yamesemwa na ‘Atwaa, Ibn Jurayj, Ibn Mubarak, Is-Haaq na riwaya iliyonukuliwa toka kwa Ahmad. Suala hili ni mashuhuri katika madhehebu ya Hanbali.

 

Kauli ya nne:

 

Kupaliza ni wajibu wakati wa kuoga na kutawadha, lakini kusukutua ni Sunnah. Yamesemwa haya na Ahmad katika riwaya, Abu ‘Ubayd, Abu Thawr na jopo la Maulamaa wa Hadiyth. Ibn Al-Mundhir ameichagua kauli hii. 

 

Kuosha Ndevu Na Nywele Nyingine Za Uso  

 

[Sharhu Fat-hil Qadiyr (1/12), Al-Mughniy (1/87) na Al-Majmuu’i (1/380)].

Ikiwa nywele zilizoota usoni (ndevu, masharubu, kilambamchuzi, kope na nyusi) ni nyingi kiasi ambacho ngozi inakuwa haionekani, basi itatosheleza kuosha juu yake tu. [Kilambamchuzi ni nywele zinazoota kati ya mdomo wa chini na kidevu].

 

Na kama ngozi inaonekana, basi itabidi ipate maji. Na ikiwa baadhi ni ndogo na nyingine ni nyingi, basi ni lazima ngozi ya nywele ndogo ipate maji na yenye nywele nyingi ioshwe juu tu.

Ama ndevu refu za singa, si lazima kuziosha zile zilizoshuka, bali inatosheleza kuosha zile tu zilizo katika mpaka wa uso, kwa vile kinachokusudiwa katika uso ni ngozi basi. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Abuu Haniyfah na riwaya toka kwa Ahmad.

 

Ama kwa mujibu wa Ash-Shaafi’iy na madhehebu ya Ahmad, ni lazima kuosha nywele singa vyovyote zitakavyokuwa zimeshuka, kwani nywele hizo zimeota katika mahali pa faradhi, na kwa ajili hiyo zinaingia katika wigo wa vyenye kuonekana. Na rai hii ina nguvu zaidi. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

 

2- Kuosha mikono miwili hadi kwenye vifundo

 

Allaah Mtukufu Anasema:

 

 (( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ))

(( Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni )).[Al Maaidah (5:6)].

 

Maulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kuwa ni lazima kuosha mikono miwili wakati wa kutawadha.

 

Fahamu kuwa herufi ya ))  (( إلىkatika Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

  (( أَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ ))

mikono yenu mpaka vifundoni

 

..ina maana ya “pamoja” kama ilivyo katika Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

  ((وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَهُمْ إِلَىٰ أَمْوَالِكُمْ ))

(( Na wala msile mali zao pamoja na mali zenu)). [An Nisaa (4:2)].

 

Na Neno Lake:

 

 ((وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ))

(( Na Atawaongezeeni nguvu pamoja na nguvu zenu)). [Huud (11:52].

 

Al Mubarrid amesema: “Ikiwa mpaka unatokana na jinsi ya chenye kuwekewa mpaka, basi nao huingia”.

 

Na kwa ainisho hili, ni lazima vifundo viwili vijumuishwe wakati wa kuosha mikono. Na haya ndio madhehebu ya Jamhuri ya Maulamaa kinyume na baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Maalik. [Al-Mabswuut (1/6), Bidaayatul Mujtahid (1/11), Al-Majmu’u (1/389), na Al-Mughny (1/90)].

 

Msimamo huu wa Jamhuri ya Maulamaa unatiliwa nguvu na kitendo cha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Imenukuliwa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba yeye alitawadha, akaosha mikono yake hata akaingia katika kipanya, na akaosha miguu yake mpaka akaingia katika miundi miwili. Kisha alisema: “Hivi ndivyo nilivyomwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (246)].

 

Kisha kaida ‘qaaidah’ (kanuni) inasema: “Lile ambalo wajibu hautimu ila kwalo, basi linakuwa ni wajibu”. Na kuosha mkono kikamilifu hakutojulikana ila kwa kuyazungusha maji kwenye vifundo viwili. [Ikhtiyaarat Ibn Qudaamah cha Al-Ghaamidiy (1/164)].

 

 

3- Kupaka kichwa

 

Allaah Mtukufu Anasema:

 

 (( وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ ))

(( Na pakeni vichwa vyenu)). [Al Maaidah (5:6)]

.

Maulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kuwa kupaka maji kichwani ni lazima. Lakini hata hivyo wamehitalifiana juu ya kiasi kinachotosheleza upakaji huo katika kauli tatu:

 

Kauli ya kwanza:

 

Ni lazima kupaka kichwa chote maji sawasawa kwa mwanamke au kwa mwanamume.

Haya ni madhehebu ya Maalik na Dhwaahir. Pia ni madhehebu ya Ahmad na kundi la wenzake, Abu ‘Ubayd na Ibn Al-Mundhir. Na Ibn Taymiyah ameuridhia msimamo huu. [Al-Mudawwanah (1/16), Al-Mughniy (1/92), Atw-Twahuur (uk. 358), Al-Awsatw (1/399) na Majmuu’i Al-Fataawa (21/123)].

 

Ushahidi wao ni haya yafuatayo:

 

1- Ni Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

   ((وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ))

((Na pakeni vichwa vyenu))

 

Hapa ب baa” ni ya kuambatisha (si ya usehemu). Kwa hiyo makadirio ya Aayah yanakuwa ni:

 

 ((وَامْسَحُوا رُءُوسِكُمْ))

Hii ni kama kuosha uso katika tayammum, kwani vyote katika Qur-aan Tukufu vimekuja kwa tamko moja. Allaah Anasema:

 

((فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُم))

((Na mwoshe nyuso zenu)). [Al Maaidah (5:6)] yaani uso wote.

 

 

2- Ni kwamba jambo hili limefasiriwa na Sunnah iliyonukuliwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kuwa, yeye alipotawadha, alikuwa akipaka kichwa chake chote. Na kati ya yanayothibitisha hili, ni Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zayd aliyesema: “Alitujia sisi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tukamtolea maji katika ndoo ya shaba. Akatawadha; akaosha uso wake mara tatu, akaosha mikono yake mara mbili hadi katika vifundo, akapaka maji kichwani kwa kupeleka mkono mbele na nyuma na akaosha miguu yake miwili”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (185) na Muslim (235)].

 

Na katika tamko jingine “akapaka kichwa chake chote”.

 

 

3- Ni Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu’ubah aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya khufu zake, mbele ya utosi wake na juu ya kilemba chake”.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (275), Abuu Daawuud (150) na At-Tirmidhy (100). Hadiyth hii imejadiliwa sana. Na Al-Albaany Allaah Amrehemu, amesema kuwa ni Swahiyh].

 

Na lau kama ingetosheleza kupukusa mbele ya utosi, basi asingelipukusa juu ya kilemba. Kwa hivyo, hilo limeonyesha kuwa ni lazima kueneza (kichwa kizima).

 

 

Kauli ya pili:

 

Inatosheleza kupaka sehemu ya kichwa.

 

Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy. [Al-Mabswuut (1/8), Al-Majmu’u (1/399), na Al-Mughny (1/92)].

 

Lakini pamoja na hivyo, wao wamehitalifiana juu ya kiasi kinachotosheleza. Wamesema ni nywele tatu, au robo ya kichwa au nusu!! Na hoja yao ni:

 

1- Kwamba “ب baa” katika Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

   ((وَامْسَحُوا برُءُوسِكُمْ))

((Na pakeni vichwa vyenu)),   

  ni ya sehemu na si ya kuambatisha.

 

2- Yale yaliyopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuwa alipaka katika utosi wake.

 

 

Kauli ya tatu:

 

Ni lazima kupaka kichwa chote kwa mwanamume tu, si kwa mwanamke.

 

Ni riwaya iliyonukuliwa toka kwa Ahmad. Amesema: “Ninataraji kupaka maji kichwani kwa mwanamke kuwe ni sahali zaidi. ‘Aaishah (Allaah Amridhie) alikuwa akipaka mbele ya utosi wake.

 

 

Ibn Qudaamah anasema: “Na Ahmad ni katika mabingwa wa Hadiyth. Na hatolei dalili kwa tukio la kitu ila kama limethibiti kwake kwa Uwezo wa Allaah”. [Al-Mughny (1/93)].

 

Ninasema: “Ninaloliona lenye nguvu katika hayo yaliyotangulia ni kuwa ni lazima kupaka maji kichwa chote wakati wa kutawadha kutokana na nguvu ya hoja zake. Ama wale waliosema kuwa ب baa” katika Aayah ni ya usehemu, basi hilo Siybawayhi amelikanusha katika sehemu kumi na tano katika kitabu chake. Na Ibn Burhan amesema: “Mwenye kudai kwamba “ب  baa” inaonyesha usehemu, basi atakuwa amewaletea mabingwa wa Lugha jambo wasilolijua. [Naylul Awtwaar (1/155) na Al-Mughny (1/87)].

 

Mbali ya hivyo, hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayoeleza kuwa yeye alifupishia kupaka baadhi ya kichwa chake tu. Lililothibiti ni kuwa yeye alipokuwa akipaka utosi wake, alikamilishia juu ya kilemba. [Majmu’u Al-Fataawa (21/122), Ahkaam Al-Qur-aan cha Ibn Al-‘Arabiy (2/571) na Subul As-Salaam (1/107)].

 

Ama mwanamke, mimi siijui dalili yoyote ya kumbagua yeye na mwanamume katika hilo. Lakini inajuzu kwake kupaka maji juu ya mtandio wake. Na lau kama amepaka utosi wake pamoja na mtandio wake, basi hilo litakuwa ni bora ili kuepukana na mvutano. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

Faida

 

Ikiwa kichwa kimepakwa hina ghafi au mfano wake, itajuzu kupaka maji juu yake. Kwani imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba yeye alikuwa akikipaka kichwa chake hina akiwa katika ihramu yake na hakuwa akijisumbua kuitoa kwa ajili ya wudhuu (kama itakavyokuja katika mlango wa Hijjah). Hii ni kwa vile kilichowekwa kichwani kinakuwa ni sehemu ya kichwa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

4- Kupaka masikio mawili:

 

Ni lazima kupaka masikio mawili pamoja na kichwa, kwani masikio ni sehemu ya kichwa. Imepokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

 

(( الأذنان من الرأس ))

((Masikio mawili ni sehemu ya kichwa )). [Hadiyth Dhwa’iyf: Ina njia nyingi na zote zina kasoro. Pia pamekhitalifiwa katika kuifanya ni Hadiyth Hasan kwa vikundi vyake. Na Mwanachuoni Mweledi Al-Albaaniy Allaah Amrehemu katika Kitabu chake cha Asw-Swahiyhah amesema kuwa huenda Hadiyth hii ikapanda kufikia ngazi ya Hadiyth Mutawaatir kwa baadhi ya Maulamaa!! Shaykh wetu (Allaah Amhifadhi), ameitolea maelezo ya kichambuzi katika Al-Nadhwaraat na akatilia nguvu udhwaifu wake, nalo ni jambo sawa kabisa. Na Shaykh Mash-huur Hasan (Allaah Amhifadhi) amesema kuwa ni Dhwa’iyf baada ya utafiti wa kina alioufanya pambizoni mwa Kitabu cha Al-Khilaafiyyaat kilichotungwa na Al-Bayhaqiy (1/448)].

 

 

Hadiyth hii ni Dhwa’iyf Marfu’u kwa kauli yenye nguvu. Lakini hata hivyo imethibiti kwa watangu wema wengi akiwemo Ibn ‘Umar. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-Daar Qutwniy (1/98), Ibn Abuu Shaybah (1/28) na wengineo].

 

Na kuna Hadiyth zinazolitolea hilo ushahidi. Ni kama ile inayoashiria kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipaka kichwa chake na masikio yake mara moja. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (133), At-Tirmidhiy (36), An-Nasaaiy (1/74), Ibn Maajah (439) na wengineo. Ina njia mbalimbali za kuifanya kuwa Swahiyh zilizonukuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas. Na asili yake iko kwa Al-Bukhaariy (157) kwa ufupi. Pia ina ushahidi toka kwa Hadiyth ya Ar-Rubayi’i binti Mu’awwidh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (126), At-Tirmidhiy (33) na Ibn Maajah (418). Vilevile imenukuliwa toka kwenye Hadiyth ya Al-Miqdaam].

 

Hadiyth hizi ni nyingi zilizonukuliwa toka kwa ‘Aliy, Ibn ‘Abbas, Ar-Rubayyi’i na ‘Uthmaan. As-Swan-’aaniy anasema: “Wote wamekubaliana kuwa kuyapaka masikio na kichwa ni mara moja tu”, yaani kwa maji hayo hayo kama inavyoonekana kutokana na tamko la “mara moja”. Kwa vile, lau kama masikio yangekuwa yanatekewa maji mapya, basi kusingelithibitishwa ya kuwa “yeye alipaka kichwa na masikio mara moja”. Na kama itachukulika kwamba mapendeleo ni kuwa yeye hakukariri kuyapaka bali aliyatekea maji mapya, basi huo ni uwezekano wa mbali”. [Subulus Salaam (1/49)].

 

Ninasema: "Na kama atateka maji mengine ya kupaka masikio, basi hapana ubaya. Kwani hilo limethibiti toka kwa Ibn ‘Umar". [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Razzaaq (29) na Al-Bayhaqiy (1/65).]

 

Angalizo

 

Hakuna usharia wowote wa kuosha shingo wakati wa kutawadha, kwa vile hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyopokelewa toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikiligusia hilo. [Majmu'u Al-Fataawa (1/56) na Zaad Al-Ma’ad (1/49). Tizama As-Silsilat Adh-Dhwa’iyfah (69-744)].

 

 

5- Kuosha miguu miwili pamoja na vifundo

 

Vifundo viwili ni mifupa miwili iliyochomoza katika pambizo mbili za mguu. Kuosha miguu miwili ni lazima kwa Jamhuri ya Maulamaa wa Ahlus-Sunnah kutokana na Neno Lake Allaah Mtukufu: 

 

((وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ))

((Na miguu yenu hadi kwenye vifundo viwili)). [Al Maaidah (5:6)].

 

Ni kwa kuweka “fat-hah” juu ya “arjulakum” kuunganishia kwenye viungo vinavyooshwa.

Na kila aliyehadithia sifa ya wudhuu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amethibitisha kwamba aliosha miguu miwili hadi kwenye vifundo viwili. Na kati ya yaliyoelezewa ni yale yanayomhusu ‘Uthmaan yanayosema: “..Kisha akaosha miguu yake miwili hadi katika vifundo mara tatu….”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (158) na Muslim (226)].

 

Na vifundo viwili hujumuishwa katika kuoshwa, kwani ikiwa mpaka unatokana na jinsi ya chenye kuwekewa mpaka, basi nao huingia kama ilivyotangulia. Na  Hadiyth ya Ibn ‘Amri (Allaah Amridhie) inaonyesha juu ya haya. Anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikawia nyuma katika safari. Kisha alituwahi nailhali alasiri imekurubia kumalizika wakati wake. Tukaanza kutawadha huku tukipaka miguu yetu. Hapo akanadi kwa sauti kubwa:  

 

((ويل للأعقاب من النار))

((Ole wao na moto kwa (kutoosha) visigino)).

Alisema mara mbili au tatu. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (161) na Muslim (241)].

 

 

Ama yale yaliyopokelewa ya kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipaka (miguu) katika wudhuu wake, linalochukuliwa ni kupaka juu ya khufu mbili, nalo ni jambo ambalo yeye aliliruhusu. Suala hili Maraafidha na Mashia wengi wamekwenda kinyume nalo wakisema kuwa ni lazima kupaka miguu miwili badala ya kuosha. Na lililo sahihi kutumiwa ni la kwanza. ‘Abdur-Rahmaan bin Abi Layla anasema: “Maswahaba wote wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wamekubaliana juu ya kuosha miguu miwili”. [Fat-hul Baariy (1/266) na Al-Mughniy (1/120)].

 

 

6-Kupachanyisha vidole vya miguu na mikono:

 

Vidole na sehemu zilizo kati yake, ni sehemu ya mahala pa faradhi. Kwa hiyo ni lazima zioshwe. Na kama haitowezekana kuoshwa ila kwa kupachanyishwa, basi ni lazima kufanya hivyo. Na kama itawezekana, basi itapendeza kama itakavyokuja.

 

 

7- Kupangilia:

 

Ni kuvitwaharisha viungo vya wudhuu kimoja baada ya kingine kwa mpangilio ambao Allaah Ameamrisha katika Aayah Tukufu. Ataosha uso, kisha mikono miwili, kisha atapaka kichwa, halafu ataosha miguu miwili. Mpangilio huu ni wajibu katika kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa. Na hayo ndiyo madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Hanbali, Abu Thawr, Abu ‘Ubayd na Adh-Dhwaahiriyya. [Al-Majmu’u (1/433), Al-Mughny (1/100), na Al-Muhalla (2/66)]. Wajibu huu wameutolea hoja kwa haya yafuatayo:

 

 

1- Ni kwamba Allaah Mtukufu Ametaja katika Aayah ya faradhi za wudhuu kimpangilio pamoja na kutenganisha miguu miwili na mikono (ambavyo ni lazima vioshwe) kwa kichwa ambacho ni lazima kipakwe. Na Waarabu hawakitenganishi kitu na chenziye ila kwa faida fulani. Na hapa Aayah inaashiria ulazima wa kupangilia. [Kama hivyo katika Al-Mughny (1/100)].

 

 

2- Ni kwamba kila aliyehadithia kuhusu wudhuu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ameuelezea ukiwa umepangika. [Maswahaba 20 wamehadithia sifa ya wudhuu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakinukulu toka kwake. Wote wameuelezea kwa mpangilio isipokuwa katika Hadiyth mbili Dhwa’iyf ambazo Al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika kitabu cha Tamaam Al-Minnah (uk.85)].

Na kitendo chake hicho kinafasiri Kitabu cha Allaah Mtukufu.

 

 

3- Ni kwa yale yaliyohadithiwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha kimpangilio kisha akasema:

 

(( هذا وضوء لا يقبل الله الصلاة إلا به))

((Huu ndio wudhuu, Allaah Haikubali Swalaah ila kwao)).

 

Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. [Hadiyth Dhwa’iyf. Angalia Al-Irwaa (85)].

 

Lakini Maalik, Ath-Thawriy na Abuu Haniyfah na wenzake, wao wanasema kuwa kupangilia ni jambo lililosuniwa na wala si wajibu. [Al-Mudawwanah (1/14), Al-Mabsuwtw (1/55), na Sharhu Fat-hil Qadyr (1/30)].

 

Hoja yao ni:

 

1- Kwamba kiunganishi kihusishi و waw” katika Aayah, hakihukumii mpangilio. Jibu la haya, liko katika yaliyotangulia.

 

2- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa ‘Aliy na Ibn Mas-’oud kwamba wamesema: “Haijalishi ni kwa kiungo gani nilichoanzia”. [Athar ya ‘Aliy. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad katika kitabu cha Al-’Ilal (1/205), Ibn Abiy Shaybah (1/55) na Ad-Daarqutwniy (1/88), Sanad yake ni Dhwa’iyf. Pia athar ya Ibn Mas-’oud iliyofanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika kitabu cha Al-Taariykh (1650) na Abu ‘Ubayd katika At Twahuur (325) kwa Sanad Hasan kwa tamko la: “Akitaka ataanza kushoto kwake katika wudhuu kama alivyosema Imaam Ahmad].

 

Hili linajibiwa kwa kauli ya Al- Imam Ahmad kama ilivyo katika “Masuala ya mwanawe ‘Abdullaah” aliposema (27-28):

“Bila shaka ina maana ya kushoto kabla ya kulia. Na hakuna ubaya kuanza kwa kushoto kwake kabla ya kulia kwake, kwani matoleo yake toka katika Qur-aan ni mamoja. Allaah Mtukufu Anasema: 

((فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ)) 

(( Basi osheni nyuso zenu na mikono yenu hadi kwenye vifundo, na mpake vichwa vyenu, na (mwoshe) miguu yenu)). [Al Maaidah (5:6)].

 

Kwa hiyo, hapana ubaya kuanza kushoto kabla ya kulia”.

 

Ninasema: “Na ingawa ubora ni kuanzia kulia kwa ajili ya kufuata Sunnah. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi".

 

 

8- Kuandamisha:

 

Ni kufuatilizia uoshaji wa viungo vya wudhuu kwa namna ambayo kisikauke kiungo kabla hajaingia kiungo kingine katika muda wa wastani.

 

Ash-Shaafi’iy katika kauli yake ya zamani na Ahmad katika Al-Mash-hur wanasema kuwa ni lazima kuandamisha. Pia Maalik anasema hivyo hivyo isipokuwa yeye ametofautisha kati ya aliyekusudia kutoandamisha na kati ya mwenye udhuru. Na haya ndiyo aliyoyachagua Shaykh wa Uislamu. [Al-Ummu (1/30), Al-Majmu'u (1/451), Kash-Shaaf Al-Qina’i (1/93), Al-Mudawwanah (1/15), Al-Istidhkaar (1/267) na Majmu'u Al-Fataawaa (21/135)].

 

Ulazima wa kuandamisha unaashiriwa na Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khattwaab kwamba mtu mmoja alitawadha akaacha sehemu ndogo ya kucha katika miguu yake. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwangalia kisha akamwambia:

(( إرجع فأحسن وضوءك ))

(( Rejea ukatawadhe vizuri)).

 

Akarejea, kisha akaswali. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (232), Ibn Maajah (666) na Ahmad (1/21). Hadiyth hii imetiwa baadhi ya dosari, lakini ina vithibitisho vyake vinavyoifanya kuwa Swahiyh bila ya shaka yoyote. Angalia katika At-Talkhiysw (1/95) na Al-Irwaa (86)].

 

 

Na katika riwaya iliyopokelewa na baadhi ya Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu mmoja akiswali nailhali juu ya mguu wake kuna sehemu nyeupe ya ukubwa wa dirham haikupata maji. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha atawadhe upya na aswali tena. [Al-Albaaniy amesema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (175) na Ahmad (3/424) kupitia kwa Buqayyah bin Al-Waliyd toka kwa Bahiyr aliyepokea toka kwa Khaalid. Buqayyah ameeleza kwamba amesikia toka kwa Bahiyr kwa mujibu wa yaliyoandikwa na Ahmad, na ambaye amesema kwamba Isnadi yake ni Hasan. Na kwa ajili hiyo, Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (86), amesema  ni Swahiyh. Ninasema: “Ni Hadiyth Hasan lau si kuhofiwa kumwadilisha Buqayyah. Hakueleza kwamba Bahiyr amesikia toka kwa Khaalid!”].

 

Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya wanasema kuwa kuandamisha si lazima. Nayo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad, na pia ni madhehebu ya Ibn Hazm. [Al-Mabsuwtw (1/56), Al-Ummu (1/30), Al-Majmuu’ (1/451) na Al-Muhalla (2/70)].

 

 

Wamesema:

 

1- Kwa vile Allaah Mtukufu Amewajibisha kuosha viungo, hivyo basi, mwenye kuviosha, atakuwa amefanya wajibu wake, ni sawa awe ameviosha kiholela bila mpangilio au akaviosha kwa mpangilio uliopangika.

 

 

2- Ni kwa aliyoyahadithia Naafi’i kwamba Ibn ‘Umar alitawadha sokoni, akaosha uso wake na mikono yake na akapaka kichwa chake. Kisha aliitwa kwenda kuswalia maiti, akaingia Msikitini, kisha akapaka juu ya khufu zake na akaswali. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (48) na kutoka kwake akapokea Ash-Shaafi’iy (16) na Al-Bayhaqiy katika Al-Ma’arifah (99)].

 

 

3- Hadiyth yenye amri ya kutawadha na kuswali upya, wanaizingatia kwamba ni Dhwa’iyf.

 

 

4- Wameliawilisha neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Rejea ukatawadhe vizuri)) kwamba makusudio yake ni kukamilisha kuosha sehemu ambayo haikupata maji mguuni.

 

 

Ninasema: “Hukmu ya mvutano wa yaliyotangulia ni Hadiyth ya Khaalid bin Mi’idaan yenye amri ya kutawadha tena na kuswali upya aliyoinukuu toka kwa baadhi ya Maswahaba wa Rasuli. Aliyeifanya kuwa ni Swahiyh, amesema ni lazima, na kama si hivyo, basi hoja zilizobakia zina uwezekano wa hili au lile. Ninaloliona mimi kuwa ni sawa, ni ulazima wa kuandamisha kutokana na Hadiyth hii. Pia, ni kwa vile wudhuu ni ‘ibaadah moja, isitenganishwe. Ama athar ya Ibn ‘Umar, inavyoonekana ni kuwa hiyo ni katika hali ya udhuru na kulazimika, na kwa hivyo, haipimiwi na hali ya kawaida. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. Lakini ikiwa patatokea mtengano kidogo katika kuosha viungo, basi hakuna ubaya. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

 

 

Share