030-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Sunnah Za Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

030-Sunnah Za Wudhuu

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Kupiga mswaki:

 

Jambo hili limekwishadokezwa kuwa linapendeza katika mlango wa “Sunnah za hulka asili”.

 

 

 

2- Kupiga Bismillaah mwanzoni:

 

Kiilivyo, kupiga Bismillaahi ni jambo zuri la kisharia katika mambo yote. Kuna Hadiyth dhwa’iyf zilizopokelewa kuhusu kupiga bismillaahi wakati wa kutawadha ingawa baadhi ya Maulamaa wamesema kuwa Hadiyth ni Swahiyh. Kati ya Hadiyth hizo ni ile isemayo:

 

((ولا وضوء لمن لم يذكر اسم الله عليه))

((Hana wudhuu asiyelitaja Jina la Allaah)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (101), At-Tirmidhiy (25), Ahmad (2/418) na wengineo. Lenye nguvu ni kuwa Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. Shaykh Al-Albaaniy Allaah Amrehemu katika kitabu cha Al-Irwaai”(1/122), amesema kuwa ni Hadiyth Hasan. Shaykh Mtukufu Abuu Is-Haaq Al Huwayny – Allaah Amhifadhi – amechangia kidogo katika kuupitisha uswahiyh wake. Uswahiyh wake uko karibu zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi].

 

Na kuna Hadiyth nyingine Dhwa’iyf sana zisizofaa kabisa kutegemewa kwa hoja. Na kwa ajili hiyo, Imaam Ahmad amesema: “Siijui Hadiyth yoyote katika mlango huu yenye Isnadi Hasan”.

 

Ninasema (Abuu Maalik): “Linalotilia nguvu kutokuwepo ulazima wa kupiga bismillaahi ni kuwa watu walioelezea sifa ya wudhuu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawakutaja kuhusu bismillaahi. Na haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Maalik, Ash-Shaafi’iy na Abuu Haniyfah na wenzake. Ni riwaya toka kwa Ahmad. [Vitabu vya Fat-hul Qadiyr (1/22), Mawaahib Al-Jaliyl (1/266), Majmu'u (1/385) na Al-Insaaf (1/128)].

 

 

3- Kuosha viganja viwili mwanzoni:

 

Ni kwa yale yaliyomo katika Hadiyth ya ‘Uthmaan katika sifa ya wudhuu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). ‘Uthmaan anasema: “Akamiminia katika viganja vyake mara tatu, akaviosha…”[Hadiyth Swahiyh Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (159) na Muslim (226)].

 

 

4- Kusukutua na kupaliza maji mara tatu kwa teko moja:

 

Ni kwa yale yaliyomo katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zayd alipokuwa akifundisha namna Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akitawadha: “Kwamba yeye (Rasuli) alisukutua na akapaliza kwa teko moja. Akafanya hivyo mara tatu”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (235), At-Tirmidhy (28) na Ibn Maajah (405)].

 

 

5- Kuyakomeza maji hadi mwisho wakati wa kusukutua na kupaliza kwa ambaye hakufunga:

 

Ni kwa Hadiyth Marfu’u ya Laqiyt bin Swabrah:

 وبالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائما

((Na komeza maji hadi mwisho isipokuwa kama umefunga)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (142), An-Nasaaiy (1/66), Ibn Maajah (407) na Ahmad (4/33)].

 

 

6- Kutanguliza kulia kabla ya kushoto:

 

Katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuhusu sifa ya wudhuu wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “…kisha alichukua teko la maji akaosha kwalo mkono wake wa kulia, kisha akachukua teko jingine akaosha kwalo mkono wake wa kushoto, kisha alipaka kichwa chake maji, kisha alichukua teko la maji, akanyunyizia kwalo mguu wake wa kulia mpaka akauosha, kisha alichukua teko jingine akaosha kwalo mguu wake, yaani wa kushoto….”[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (140)].

 

Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kuanza kwa upande wa kulia wakati wa kuvaa viatu, kutembea, kujitwaharisha na katika kila jambo lake alilolifanya. [Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (168) na Muslim (268)].

 

 

7- Kuviosha viungo mara tatu:

 

Imepokelewa Hadiyth Swahiyh toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba alitawadha (akiviosha viungo) “mara moja moja”, [Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (156) toka kwa Ibn ‘Abbaas.]…na kwamba aliviosha “mara mbili mbili”. [Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (157) toka kwa ‘Abdullaah bin Yaziyd]. Na ukamilifu na utimilifu zaidi wa wudhuu ni kuviosha viungo mara tatu kama alivyofanya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mujibu wa ilivyoelezewa katika Hadiyth za ‘Uthmaan na ‘Abdullaah bin Zayd. Hadiyth hizi zimekwisha zungumziwa.

 

 

Zindushi mbili

 

(a) Kupukusa kichwa ni mara moja tu:

 

Asipukuse mara mbili au tatu kulikoelezewa kiujumla katika Hadiyth za sifa ya wudhuu wa Rasuli  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ama riwaya zinazoelezea kuwa kupukusa kichwa ni mara tatu, riwaya hizo si Swahiyh. Ama zile zinazoelezea kwamba Rasuli alipukusa mara mbili, basi hiyo ni tafsiri ya neno lake:

((فأقبل بهما وأدبر))

((Ipeleke mbele na nyuma)), kama alivyosema Ibn ‘Abdul Barri. [Al-Khilaafiyyaat cha Al-Bayhaqiy (1/336). Kimetolewa maelezo na maoni na Shaykh Mash-huur Aali Salmaan. Angalia pia At-Twahuwr cha Abu ‘Ubayd (uk 359)].

 

Kuipelekea mikono miwili mbele na nyuma wakati wa kupukusa kichwa, hakuzingatiwi kama ni kukariri, kwa kuwa kukariri kunakuwa ni kwa kuchukua tena maji upya. Kisha kukariri, kumestahabiwa tu kwa viungo vinavyooshwa na si kwa vile vinavyopukuswa. [Muqaddimaat Ibn Rushd Alal Mudawwanah (uk 16)].

 

Na kati ya dalili imara zinazoonyesha kwamba kichwa hakipukuswi zaidi ya mara moja, ni Hadiyth ya bedui aliyekwenda kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuuliza namna ya kutawadha. Rasuli akamwonyesha kila kiungo mara tatu tatu, kisha akasema:

(( هذا الوضوء، فمن زاد على هذا فقد أساء وتعدى وظلم))

((Huu ndio wudhuu. Atakayezidisha zaidi ya hivi, basi amefanya ubaya, amepetuka mipaka, na amedhulumu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na An Nasaaiy (1/88), Ibn Maajah (422) na Ahmad (2/180)].

 

Al Haafidh katika “Al Fat-h” (1/298) anasema: “Riwaya ya Sa’iyd bin Mansour, ina kiashirio kwamba alipukusa kichwa chake mara moja tu, hivyo basi, inaonyesha kwamba kupukusa kichwa zaidi ya mara moja, si jambo mustahabu. Yaliyokuja kwenye Hadiyth zinazoelezea kupukusa mara tatu – kama zitakuwa ni Swahiyh – yanaweza kuchukulika kama ni kwa lengo la kukipukusa kichwa chote kikamilifu, na si kwamba kila mpukuso na hesabu yake. Na hii ni kwa ajili tu ya kuoanisha kati ya dalili”.

 

 

Ninasema: “Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Maalik na Ahmad (katika Swahiyh kutoka kwake) kinyume na Ash Shaafi’iy Allaah Awarehemu”. [Al-Mabsuwtw (1/5), Haashiyat Ad-Dusuwqy (1/98), Al-Mughny (1/127) na Al-Umm (1/26)].

 

 

(b) Ni karaha kuzidisha zaidi ya mara tatu kwa aliyeosha viungo kikamilifu:

 

Kuosha mara tatu viungo vya wudhuu, ndio wudhuu uliokamilika na uliotimia. Ni karaha kuzidisha zaidi ya mara tatu kutokana na Hadiyth:

((فمن زاد على هذا فقد أساء وتعدى وظلم))

((Atakayezidisha zaidi ya hivi, basi amefanya ubaya, amepetuka mipaka, na amedhulumu)).

Mahala pa maneno haya, ni pale ziada inapofanywa si kwa ajili ya kukamilisha upungufu. Na kama viungo vyake vitaosheka kikamilifu mara tatu au chini yake, itakuwa ni karaha kuongeza zaidi ya mara tatu. Haya hayana mabishano kabisa. [At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barri (20/117) kwa mfano wake kwa muhtasari].

 

 

8- Kuziasulia ndevu nyingi:

 

Tumekwisha eleza kwamba kama ndevu ni nyingi zilizoficha ngozi, basi itatosha kuosha nje yake tu. Na hapa tunaongeza kusema kuwa imesuniwa kuziasulia kwa maji kutokana na Hadiyth ya Anas isemayo kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa kutawadha, alikuwa akichukua teko la maji, kisha huliingiza chini ya kaakaa na kuasulia kwalo pia. Kisha Rasuli husema:

((هكذا أمرني ربي عز وجل))

((Hivi ndivyo Mola wangu Ázza wa Jalla Alivyoniamuru)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrih. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (145), Al-Bayhaqy (1/54) na Al-Haakim (1/149). Angalia Al-Irwaa (92).

 

Na jambo hili linageuzwa kuwa Sunnah kutokana na Hadiyth iliyotangulia hapo kabla ya Rifa’a bin Raafi’i inayozungumzia kisa cha mwenye kuswali vibaya.

 

 

9- Kusugua viungo:           

                                                      

Ni kwa Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zubayr aliyesema: “Nilimwona Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha, na kisha akaingia kuisugua mikono yake miwili”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Hibaan (1082) na Al-Bayhaqy (1/196)].

 

 

10- Kuasulia vidole vya mikono na miguu:

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((أسبغ الوضوء، وخلل الأصابع، وبالغ في الاستنشاق إلا ان تكون صائما))

((Tawadha wudhuu kamili, asulia vidole, na ubalighishe katika kupaliza maji, isipokuwa kama umefunga)).[Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].

 

Na kama vidole na sehemu za kati yake haviosheki ila kwa kuasulia, basi wakati huo itakuwa ni lazima kufanya hivyo kama tulivyotangulia kusema.

 

 

11- Kuosha zaidi ya mpaka wa faradhi:

 

Imesuniwa kutawadha kikamilifu, kurefusha kuosha uso hadi katika ncha ya utosi, na kuosha juu zaidi ya vifundo viwili na visigino. Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

 ((إن أمتي يأتون يوم القيامة غرا محجلين من آثار الوضوء))

((Hakika umati wangu utakuja siku ya Qiyaama hali ya kuwa nyuso zao, mikono yao na miguu yao inang’ara kutokana na athari za wudhuu)). 

 

Abu Hurayrah anasema: “Basi yeyote kati yenu atakayeweza kurefusha kuosha uso, basi na afanye”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (36) na Muslim (246)].

 

Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba alitawadha, akaosha mikono yake hadi akaingia kuosha vipanya vyake, akaosha miguu yake miwili hadi akaingia kuosha miundi yake. Kisha alisema: “Hivi ndivyo nilivyomwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha”.[ Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (246).

 

Na imepokelewa tena toka kwake akisema: Nimemsikia kipenzi changu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

((تبلغ الحلية من المؤمن حيث يبلغ الوضوء))

((Nuru ya Muumini inafikia pale wudhuu unapofikia)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (250)].

 

 

 

12- Kutumia maji kwa uangalifu:

 

Ni kwa Hadiyth ya Anas aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiogea maji ya lita 2 hadi lita 2½, na akitawadha kwa maji ya ½ lita”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (198) na Muslim (325)].

 

 

13- Du’aa baada ya kutawadha: 

 

Imepokelewa toka kwa ‘Umar amesema: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((ما منكم من أحد يتوضأ فيسبغ ثم يقول: أشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له، وأشهد أن محمدا عبده ورسوله إلا فتحت له أبواب الجنة الثمانية يدخل من أيها شاء))

((Hakuna yeyote kati yenu anayetawadha akautimiza vilivyo wudhuu wake, kisha akasema: “Nashuhudia ya kwamba hapana mola mwingine isipokuwa Allaah Aliye Peke Yake na Asiye na mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mja Wake na Rasuli Wake, isipokuwa hufunguliwa milango minane ya pepo aingie wowote autakao)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (234)].

 

 

Imepokelewa na Abu Sa‘iyd kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((من توضأ فقال: سبحانك اللهم وبحمدك، أشهد أن لا إله إلا أنت، أستغفرك وأتوب إليك، كتب فى رق ثم طبع بطابع فلا يكسر إلى يوم القيامة))

((Mwenye kutawadha akasema: “Umetakasika ee Mola na kwa Himdi Yako, ninashuhudia ya kwamba hapana mola mwingine ila Wewe, nakuomba maghfirah na ninatubia Kwako”, huandikwa katika karatasi nyeupe, kisha hutiwa chapa, halafu haichanwi mpaka Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa ”Ikhraaj” na An Nasaaiy katika kitabu cha Al-Kubraa (9909), na Al-Haakim (1/564). Kuna Hadiyth kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine].

 

 

14- Kuswali rakaa mbili baada ya kutawadha:

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Uthmaan aliyesema: “Nilimwona Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha kama hivi ninavyotawadha akasema”:

 

((من توضأ نحو وضوئي هذا، ثم صلى ركعتين لايحدث فيهما نفسه، غفر له ما تقدم من ذنبه))

((Mwenye kutawadha kama wudhuu wangu huu, kisha akasimama akaswali rakaa mbili haizungumzishi nafsi yake, basi husamehewa madhambi yake yaliyotangulia)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (6433) na Muslim (226)].

 

 

Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal wakati wa Swalaah ya alfajiri:

 

(( يا بلال! حدثني بأرجى عمل عملته فى الاسلام، إني سمعت دف نعليك بين يدي في الجنة)). قال : ماعملت عملا أرجى عندي من أني لم أتطهر طهورا في ساعة من ليل أو نهار إلا صليت بذلك الطهور ما كتب لي أن أصلى))                                                                                                          

((Ee Bilaal! Nielezee amali yenye matarajio zaidi uliyoifanya katika Uislamu, kwani mimi nimesikia mtaharuki wa viatu vyako mbele yangu huko peponi)).

Bilal akasema: “Sikufanya amali yoyote yenye matarajio makubwa kwangu zaidi ya kuwa sikupata kujitwaharisha wakati wowote wa usiku au mchana, ila huswali kwa twahara hiyo kile nilichoandikiwa kukiswali”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (1149) na Muslim (2458)].

 

 

 

Inajuzu Kukausha Viungo Baada Ya Kutawadha Kwa Kutopokelewa Lolote La Kuzuia Hilo

 

Na asili ni kufaa hilo. Na kama itasemwa kuwa imethibiti kwamba Maymuunah (Allaah Amridhie) alimletea Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kitambaa cha kujifutia baada ya kuoga, na yeye hakujifutia nacho, na akaondoka na ilhali anakung’uta mikono yake miwili.. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (270)]…..basi tunasema: “Tukio hili lina mwelekeo wa kuwa na mambo kadhaa. Inawezekana kuwa alikirejesha kitambaa hicho kutokana na sababu inayohusiana nacho kama kutokuwa kisafi, au kuhofia kukilowesha na maji au sababu nyingine. Kisha Bi Maymuunah kumletea Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kitambaa hicho, inaonyesha kuwa ilikuwa ni mazoea yake. [Faida zaidi zipo kwenye Ash Sharhul Mumti’i (1/181). Angalia Kitabu cha Zaadul Maad (1/197)].

 

 

Kujuzu huku kunatiliwa nguvu na  yaliyopokelewa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akaligeuza juba la sufi alilokuwa nalo, kisha akajifuta nalo.” [Isnadi yake iko karibu na Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (468, 3564)].

 

 

At-Tirmidhiy (54) anasema: “Baadhi ya Maswahaba wasomi wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wa baada yao, wameruhusu kujifuta kwa kitambaa baada ya kutawadha. Na mwenye kulifanya hilo kuwa makruhu, basi amefanya hivyo kwa yale yaliyosemwa kuwa “wudhuu hupimwa”.

 

 

Wudhuu Haufai Kwa Aliyepaka Kucha Rangi[Yamenukuliwa kutoka kitabu changu cha Fiqhus Sunnah Lin Nisaa (uk 39)].

 

Kwa vile hilo huzuia maji kupenya na kufika sehemu ya faradhi. Ama rangi nyingine ya kawaida kama vile hina na mfanowe, hiyo haiathiri. Lakini hata hivyo ni vizuri kuiondosha kabla ya kutawadha na kuswali kwa kauli ya Ibn ‘Abbaas: “Wake zetu hujipaka hina bora kabisa. Hujipaka baada ya Swalaah ya ‘Ishaa na huiondosha kabla ya Alfajiri”. [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibnu Abi Shaybah (1/120)].

 

Na imepokelewa kuwa Ibraahiym An-Nakh’iy aliulizwa kuhusu mwanamke anayepaka mikono yake hina bila ya kuwa na wudhuu kisha wakati wa Swalaah ukafika. Alijibu akisema: “Ataondosha vilivyomo mkononi mwake kama atataka kuswali”. [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqy (1/77, 78)].

 

 

 

 

 

Share