Maamrisho Ya Kuisoma Qur-aan Na Kuifanyia Kazi

 

 

Maamrisho Ya Kuisoma Qur-aan Na Kuifanyia Kazi

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Allaah ('Azza wa Jalla) Alimuamrisha kwanza Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hivyo ni amri kwa Waumini wote pia:     

 

 

Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾

Soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. Na bila shaka kumdhukuru Allaah ni kubwa zaidi. Na Allaah Anajua yale mnayoyatenda. [Al-‘Ankabuwt: 45]

 

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا﴿٤﴾

na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali.  [Al-Muzzammil: 4]

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِن كِتَابِ رَبِّكَ ۖ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ وَلَن تَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا ﴿٢٧﴾

Na soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyofunuliwa Wahy katika Kitabu cha Rabb wako. Hakuna yeyote atakayeweza kubadilisha Maneno Yake; na wala hutopata kamwe makimbilio isipokuwa Kwake.  [Al-Kahf: 27]

 

 

Na pia Alimuamrisha Rasuli Wake  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aseme:

 

إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَـٰذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٩١﴾

 “Hakika nimeamrishwa nimwabudu Rabb wa mji huu Ambaye Ameufanya mtukufu, na ni Vyake Pekee vitu vyote. Na nimeamrishwa kwamba niwe miongoni mwa Waislamu.

 

وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴿٩٢﴾

Na kwamba nisome Qur-aan.” Hivyo anayeongoka, basi hakika anaongoka kwa ajili ya manufaa ya nafsi yake. Na anayepotoka, basi sema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji.” [An-Naml: 91-92]

 

 

Na wameamrishwa wake zake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuisoma Qur-aan majumbani mwao na kuifundisha. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا ﴿٣٤﴾

Na kumbukeni yale yanayosomwa majumbani mwenu katika Ayaat za Allaah na Hikmah (Sunnah), hakika Allaah daima ni Mwenye kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika [Al-Ahzaab: 34]

 

 

Jinsi umuhimu wa kuisoma Qur-aan ulivyokuwa adhimu, umekuwa hadi kwamba Waumini wanapokuwa vitani au wakiwa wagonjwa wanapaswa waisome kwa kadiri ya uwezo wao.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَيِ اللَّيْلِ وَنِصْفَهُ وَثُلُثَهُ وَطَائِفَةٌ مِّنَ الَّذِينَ مَعَكَ ۚ وَاللَّـهُ يُقَدِّرُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ ۚ عَلِمَ أَن سَيَكُونُ مِنكُم مَّرْضَىٰ ۙ وَآخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِي الْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِن فَضْلِ اللَّـهِ ۙ وَآخَرُونَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ ۚ

 

Hakika Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Anajua kwamba unasimama (kuswali) karibu na thuluthi mbili za usiku au nusu yake, au thuluthi yake; na kundi miongoni mwa wale walio pamoja nawe. Na Allaah Anakadiria usiku na mchana. Anajua kwamba hamuwezi kuukadiria wakati wake na kusimama kuswali, basi Amepokea tawbah yenu. Basi someni kile kilicho chepesi katika Qur-aan. (Allaah) Anajua kwamba watakuweko miongoni mwenu wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wanatafuta fadhila za Allaah, na wengineo wanapigana katika njia ya Allaah. Basi someni kile kilicho chepesi humo. [Al-Muzzammil: 20]

 

 

Basi hebu jiulize ee ndugu Muisamu ambaye huna nyudhuru kama hizo  je, unaisoma Qur-aan hata kidogo? Je unaisoma kwa kiasi cha kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)?

 

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaamrisha kutadaburi (kuzingatia) Aayah Zake na kwamba Al-Qur-aan imejaa baraka Zake Allaah ('Azza wa Jalla). Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾

Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili. [Swaad: 29]

 

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akatahadharisha kuihama Qur-aan; kwa maana kuipuuza na kutokuisoma na kutokuifanyia kazi amri na makatazo Yake. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا ﴿٣٠﴾

Na Rasuli akasema: “Rabb wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan yenye kuhamwa. [Al-Furqaan: 30]

 

Aayah ifuatayo ambayo imekariri mara kadhaa katika Suwratul-Qamar, ni bishara ya kuwa Qur-aan ni nyepesi kujifunza, kuisoma na kuihifadhi.   

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾

Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika? [Al-Qamar: 17]

 

 

Amrisho la kuisoma  Qur-aan kwa haki ipasavyo kwa maana; kuisoma, kuifahamu, kuifanyia kazi maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٢١﴾

Wale Tuliowapa Kitabu wanakisoma kwa haki ipasavyo ya kusomwa kwake; hao ndio wanaokiamini, na atakayekikanusha basi hao ndio waliokhasirika.    [Al-Baqarah:121]

 

 

Imaam Hasan Al-Baswriy amesema: “Wanaifanyia kazi shariy’ah (hukmu) zake na wanaamini mutashaabih zake (mutashaabih: zilizofanana) na wanapeleka yanayowatatiza kufahamu kwa ‘Ulamaa wake.”

 

 

Na  baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa: Ni kuisoma kwa hukmu zake za tajwiyd, kufahamu maana yake, kuifanyia kazi maamrisho na makatazo yake, kujifundisha na kuifundisha.”   Hii kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن عثمانَ بن عفانَ رضي الله عنه أنَّ النبيَّ صلى الله عليه وسلّم قالَ: ((خَيرُكُم مَنْ تعَلَّمَ القُرآنَ وعَلَّمَه)) صحيح البخاريِّ

Imepokelewa kutoka kwa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mbora wenu ni yule mwenye kujifunza Qur-aan kisha akaifundisha)) [Al-Bukhaariy] 

 

 

Ili kupata faida na manufaa zaidi, tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo:

 

 

Aayaat Kuhusu Fadhila Za Qur-aan Na Umuhimu Wake

 

Fadhila Za Kusoma Na Kuhifadhi Qur-aan Katika Hadiyth Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

 

Share