038-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Muda Wa Kupukusa Unapoanzia

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

038-Muda Wa Kupukusa Unapoanzia

 

Alhidaaya.com

 

 

Imejulikana kwamba muda wa kupukusa kwa mkazi ni siku moja na usiku wake, na kwa msafiri ni siku tatu na masiku yake. Basi ni wakati gani muda huo unaanza kuhesabiwa? Katika hili, Wanachuoni wana kauli tofauti:

 

Ya kwanza

 

Unaanza pale anapopata hadathi ya kwanza baada ya kuzivaa. Hii ni kauli ya Sufyaan Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy, Abu Haniyfa na wenzake. Na hili li wazi katika madhehebu ya Hanbali. [Al-Mabsuwtw (1/99), Al-Majmu’i(1/470), Al-Mughniy (1/291) na Al-Awsatw (1/443)].

 

Wamesema kuwa kipindi cha baada ya  hadathi, ni wakati unaoruhusiwa kupukusa.

 

Ya pili

 

Unaanza kuanzia wakati wa kuzivaa. Ni kauli ya Al-Hasan Al-Baswriy. [Al-Ikliyl Sharh Manaar As-Sabiyl cha Shaykh Wahiyd ‘Abdu Ssalaam (1/136)].

 

Ya tatu

 

Atapukusa Swalaah tano, yaani Swalaah 15 kwa msafiri (3X5), na wala asipukuse zaidi ya hivyo. Ni madhehebu ya Ash-Sha’abiy, Is-haaq, Abu Thawr na wengineo. [Al-Mughniy (1/291), Al-Majmu’u (1/466) na Al-Awsatw (1/444)].

 

Ya nne

 

Unaanza pale inapojuzu kwake kupukusa baada ya hadathi, sawasawa ikiwa alipukusa au hajapukusa na wala hakutawadha kwa namna ambayo lau kama atapukusa baada ya kupita sehemu ya muda, itambidi apukuse ule muda uliosalia basi. Haya ni madhehebu ya Ibn Hazm. Yeye ameyajadili madhehebu mengi. [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (2/95 na kurasa zinazofuatia)].

 

Ya tano

 

Unaanza tokea pukuso la kwanza baada ya hadathi. [Masaail Ahmad cha Abu Daawuud (10) na Al-Muhallaa (2/95)].

 

Ni kauli ya Ahmad bin Hanbali na Al-Awzaa’iy. Pia ni kauli iliyoungwa mkono na An-Nawawiy, Ibn Al-Mundhir na Ibn ‘Uthaymiyn. Na hii ndio kauli yenye nguvu zaidi kutokana na maana bayana ya neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 

((يمسح المسافر))  و ((يمسح المقيم))

((Msafiri hupukusa)) na ((Mkazi hupukusa)).

 

Na haiwezekani kuthibitishwa kwamba mtu anapukusa, ila kwa kitendo cha kupukusa. Na haijuzu kuipiga pande maana hii bayana bila dalili au ushahidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Na kwa haya, ikiwa mtu ametawadha wakati wa Swalaah ya adhuhuri na akavaa khufu zake saa sita kwa mfano, kisha akabakia na utwahara wake hadi saa tisa alasiri, kisha wudhuu ukamtenguka na wala hakutawadha mpaka saa kumi (baada ya Swalaah ya alasiri) na akapukusa, basi  atapukusa mpaka saa kumi alasiri ya kesho yake ikiwa ni mkazi, na mpaka siku ya nne ikiwa ni msafiri.

 

Share