046-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kupaka Juu Ya Soksi Na Viatu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

046-Kupaka Juu Ya Soksi Na Viatu

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Kupaka Juu Ya Soksi

 

Soksi ni kile anachokivaa mtu miguuni sawasawa zikiwa zimetengenezwa kwa sufi au pamba au katani au mfano wa hivyo.

 

Maulamaa wana kauli tatu kuhusu hukmu ya kupukusa juu ya soksi:

 

Ya kwanza:

 

Haijuzu kupukusa juu yake ila tu kama zitafunikwa na viatu vya ngozi.

 

Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah (ambaye baadaye aliachana na msimamo huu), Maalik na Ash-Shaafi'iy. [Al-Mabsuwtw (1/102), Al-Mudawwanah (1/40), Al-Ummu (1/33) na Al-Awsatw (1/465)].

 

Wao wanasema kuwa sababu ni kuwa soksi haiitwi khufu, na kwa hivyo haichukui hukmu yake, na wala hakuna Hadiyth yoyote inayothibitisha kupukusa juu ya soksi!!

 

Ya pili:

 

Inajuzu kupukusa juu ya soksi lakini kwa sharti ziwe nzito na zenye kusitiri mahala penye kulazimu kuoshwa.

 

Haya ni madhehebu ya Al-Hasan, Ibn Al-Musayyib na Ahmad. Pia Mafuqahaa wa Hanafi, Shaafi'iy na Hanbali. [Masaail Ahmad ya Ibn Haaniy (1/21), Al-Awsatw (1/464), Al-Majmu'u (1/540) na Fat-h Al-Qadiyr (1/157)].

 

Ya tatu:

 

Inajuzu kupukusa kwa hali yoyote hata kama ni nyepesi.

 

Ni madhehebu ya Ibn Hazm na Ibn Taymiyah kama inavyojulikana. Kauli hii pia imekhitariwa na Ibn 'Uthaymiyn na Al-'Allaamah Ash-Shanqiytwiynayo ndiyo yenye nguvu. [Al-Muhalla (2/86), Al-Masaail Al-Maardiyniya (uk.58), Majmuu Al-Fataawaa (21/184), Al-Mumt'i (1/190) na Adhwaau Al-Bayaan (2/18,19) ambayo ina utafiti murua kabisa].

 

Maulamaa wenye kauli mbili za mwisho wamejuzisha kupukusa juu ya soksi kwa dalili zifuatazo:

 

1- Ni Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu'ubah aliyesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya soksi zake na viatu vyake. [Al-Albaaniy amesema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (159), At-Tirmidhiy (99) na Ahmad (4/252), naye ndiye mzungumzaji. Angalia katika Al-Irwaa (101)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Al-Azraq bin Qays akisema: "Nilimwona Anas bin Maalik ametengukwa na wudhuu, akaosha uso wake, mikono yake miwili na akapukusa juu ya soksi zake za sufi. Nikamuuliza: Je, wapukusa juu yake? Akasema: Hakika hizi ni khufu mbili, lakini ni za sufi". [Ahmad Shaakir amesema kuwa ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-Duwlaabiy katika Al-Kunaa (1/181)].

 

Anas Allaah Amridhie akaeleza hapa kuwa khufu si lazima iwe ni ya ngozi tu, bali ni zaidi ya hivyo, naye ni Swahaba anayeijua vyema lugha.

 

3- Ni kwamba kuna Maswahaba 11 waliozungumzia kuhusu kujuzu kupukusa juu ya soksi mbili. Kati yao ni 'Umar na mwanawe ‘Abdullaah, 'Aliy, Ibn Mas'uud, Anas na wengineo. Na hakuna yeyote katika enzi yao aliyekwenda kinyume, na hilo likawa limekubaliwa na wote.

 

Kisha Jamhuri ya Maulamaa ikaja kupiga marufuku kupukusa juu ya soksi nyepesi kwa vile hazisitiri mahala panapolazimu kuoshwa. Tumekwisha eleza nyuma kuwa hili si sharti – kwa mujibu wa utafiti – kwa kuchukulia kipimo cha khufu iliyotoboka. Na kwa vile siku hizi zinazovaliwa zaidi ni soksi nyepesi, tutaona kwamba kushurutisha mfano wa masharti kama haya, kunakwenda kinyume na makusudio ya sharia iliyotufanyia ukunjufu kwa kuwabana watu na kuwatia uzito. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Faida

 

Inaingia katika maana ya soksi bendeji, plasta na matambara anayofungwa mtu mguuni kwa udhuru, kwani hizo ni vigumu kuzifungua. Yeye atapaka tu juu yake kama alivyolikhitari hilo Shaykh wa Uislamu.

 

Na hukmu za kupukusa juu ya soksi mbili ni hukmu zile zile za kupukusa juu ya khufu mbili.

 

Anapovaa Soksi Juu Ya Nyingine

 

Hili lina hali mbalimbali:

 

1- Akitawadha kisha akavaa soksi juu ya nyingine (mbili), basi atapukusa soksi ya juu tu endapo kama atatengukwa na wudhuu.

 

Na haya ni madhehebu ya Hanafiy. Na ni kauli yenye nguvu kwa Maalik na Hanbali. Aidha ni kauli ya zamani ya Ash-Shaafi'iy aliyetofautiana nao katika kauli yake mpya. [Haashiyat Ibn 'Aabidiyn (1/179), Jawaahir Al-Ikliyl (1/24) na Rawdhat At-Twaalibiyn (1/127). Mengi wameyazungumzia hapa kuhusu khufu, lakini hukmu ni moja].

 

2- Akitawadha akavaa soksi juu ya nyingine, kisha akapukusa juu yake, halafu akaivua ya juu baada ya kupukusa, basi inajuzu kwake kuukamilisha muda kwa kuzipukusa soksi za ndani, kwa kuwa cha msingi hapa ni kuwa yeye alizivaa miguu yake ikiwa twahara.

 

3- Akitawadha akavaa soksi, kisha akaivaa nyingine juu yake kabla ya kutengukwa na wudhuu, basi atapukusa juu ya soksi zozote azitakazo (za ndani au za nje. [Mahanbali wamelielezea hili katika Kash-Shaaf Al-Qina'a (1/117-118)].

 

4- Akitawadha akaivaa soksi moja, akapukusa juu yake kisha akaivaa nyingine hali ya kuwa ana twahara, itajuzu kwake kupukusa ya juu, kwa vile kimsingi ameiingiza miguu yake ikiwa ni twahara. Na kama alitengukwa na wudhuu kisha akaivaa nyingine, haitojuzu kwake kupukusa ya juu, bali itajuzu ya chini. [Imeelezwa katika Kash-Shaaf Al-Qina'a (1/117-118) kwamba hapukusi. Amesema: "Kwa vile khufu iliyopukuswa ni badala ya kuosha ile iliyo chini yake. Na badali haijuzu kuwa na badali nyingine, bali atapukusa ya chini kwa vile ruhusa imefungamana nayo!!].

 

2- Kupaka Juu Ya Viatu

 

Imetangulia katika Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu'ubah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya soksi zake na viatu vyake. [Tumeitaja nyuma kidogo]

 

Hadiyth hii tukisema kuwa ni Swahiyh, inaweza kubeba mambo mawili:

 

1- Ni kuwa alivaa viatu na soksi na akapukusa juu yake, na hukmu ya viwili hivyo ni moja kama ilivyotangulia katika kuvaa soksi juu ya soksi au khufu juu ya khufu.

 

2- Ni kuwa Al-Mughiyrah alimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa mara juu ya soksi na mara nyingine juu ya viatu. Na hii inakuwa ni dalili kuwa inajuzu kupukusa juu ya viatu ijapokuwa bila ya soksi. Na hili ingawa liko mbali kidogo, lakini linaweza kutolewa dalili juu ya kujuzu hilo kutokana na yaliyotangulia katika Hadiyth ya Abuu Dhwabyaan kwamba "Aliy bin Abi Twaalib alitawadha, akapukusa juu ya viatu vyake, kisha akaingia Msikitini, akavua viatu vyake, kisha akaswali…" Na hapa hakutaja soksi. [Tumeitaja nyuma kidogo]

 

Na pengine kujuzu kupukusa juu ya viatu kunatilika nguvu vile vile kwa kutoshurutishwa kuwa chenye kupukuswa kiwe ni chenye kusitiri mahala pa lazima kuoshwa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Share