052-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nguzo Ya Kuoga

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

052-Nguzo Ya Kuoga

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni kukieneza kiwiliwili chote kwa maji. Uhalisia hasa wa kuoga ni kububujisha maji kwenye kiwiliwili chote na kufika maji hayo katika kila unywele na ugozi. Na hili limethibiti katika Hadiyth zote zinazoelezea kuhusu picha ya namna alivyokuwa akikoga Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam). (Hadiyth hizi nitazielezea hivi karibuni). Na kati ya Hadiyth hizo ni Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie):

((..kisha anamimina maji juu ya kiwiliwili chake chote)). [Hadiyth Swahiyh: Matni na takhriyj yake zitakuja karibu].

 

Al-Haafidh amesema katika Al-Fat-h (1/361):

“Usisitizo huu (wa kusema “kiwiliwili chake chote”) unaonyesha kwamba yeye alieneza kiwiliwili chake chote kwa josho”.

 

Na katika Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-‘am kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam)  amesema:

((أما أنا، فآخذ ملء كفي ثلاثا فأصب على رأسي، ثم أفيض بعد ذلك على سائر جسدي))

((Ama mimi, huchukua ujazo wa kiganja changu mara tatu, kisha namimina juu ya kichwa changu, kisha nabubujisha baada ya hapo juu ya kiwiliwili changu chote)). [Hadiyth Swahiyh: Ahmad ameikhariji kwa tamko hili (4/81), na katika Al-Bukhaariy (254) na Muslim (327) kwa ufupisho].  

 

Lingine linaloonyesha kuwa nguzo pekee ya kukoga ni kukieneza kiwiliwili chote kwa maji, ni Hadiyth ya Ummu Salamah aliyesema:

“Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke ninayesuka sana nywele, je, nizifumue wakati wa kukoga janaba?” Akasema:

(( لا، إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات، ثم تفيضين عليك الماء فتطهرين))

(( Hapana, bali yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu, kisha utajimiminia maji utwaharike)).

 

Ama kusugua viungo, kusukutua na kupaliza maji wakati wa kukoga, kauli yenye nguvu inasema kuwa hayo yote ni Sunnah kama tutakavyoeleza mbeleni. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri.

 

 

Share