071-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Ni Sehemu Ipi Ya Ardhi Inayofaa Kutayamamia?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

071-Ni Sehemu Ipi Ya Ardhi Inayofaa Kutayamamia?

 

Alhidaaya.com

 

 

Maulamaa wana rai mbili kuhusu mchanga unaofaa kutayamamia:

 

Rai ya kwanza

 

Ni uso wowote wa ardhi ikiwa ni changarawe, mlima, mchanga au udongo. Huu ni mwelekeo wa Abuu Haniyfah, Abuu Yuusuf na Maalik. Umekhitariwa na Shaykh wa Uislamu. Pia Ibn Hazm amelikhitari hilo, lakini yeye kashurutisha kuwa endapo kama uso wa ardhi hauna udongo, basi uwe umeshikamana na ardhi. [Al-Istidhkaar (3/157), Al-Mabsuutw (1/108), Majmuu Al-Fataawaa (21/364) na Al-Muhallaa (2/158)].

 

Kati ya hoja zao ni:

 

1- Neno Lake Allaah Mtukufu:

((صعيدا زلقا))

((Ardhi  tupu)) [Al-Kahf (18:40)]
Na Neno Lake Ta’alaa:

((صعيدا جرزا))

((Ardhi kame)) [Al-Kahf (18:8)]

 

Amesema katika “Al-Istidhkaar” (3/158): “Al-Juzur” ni ardhi ngumu isiyootesha kitu.

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((وجعلت لي الأرض مسجدا وطهورا))

((...na ardhi imefanywa kwangu kuwa sehemu ya kuswalia na kitwaharisho)). [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia hivi karibuni].

 

3- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((يحشر الناس يوم القيامة على صعيد واحد))

((Watu watafufuliwa siku ya Qiyaamah juu ya ardhi moja)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4712) na Muslim (472)].

 

4- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((جعلت الأرض كلها لي ولأمتي مسجدا وطهورا، فأينما أدركت رجلا من أمتي الصلاة فعنده مسجده وعنده طهوره))

((Ardhi yote imefanywa kwangu na kwa umati wangu kuwa sehemu ya kuswalia na kitwaharisho, na popote itakapomkuta Swalaah yeyote katika umma wangu, basi hapo ndipo sehemu yake ya kuswalia, na hapo ndipo kitwaharisho chake)). [Hadiyth Hasan: Imetangulia hivi karibuni].

 

5- Hadiyth ya Abuu Al-Juhaym kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipiga juu ya ukuta kwa mikono yake miwili, akatayamamu, kisha akamjibu mtu maamkizi. [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia hivi karibuni].

 

6- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba amesema:

“Uso mzuri zaidi wa ardhi ni konde na ardhi ya konde”. [Isnadi yake ni dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/161)].

 

Rai ya pili

 

Uso wa ardhi ni udongo na kisicho udongo hakifai kutayamamia.

 

Huu ni mwelekeo wa Ash-Shaafi’iy, Hanbali, Abuu Thawr na Ibn Al-Mundhir. [Al-Mughny (1/155), Al-Majmu’u (2/246), Al-Istidhkaar (3/159) na Al-Awsatw (2/43)].

Kati ya hoja zao ni:

 

1- Ni ziada iliyokuja katika Hadiyth isemayo:

((وجعلت تربتها لي طهورا)) 

))na umefanywa udongo wake kwangu ni kitwaharisho)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (522), Ibn Hibaan (1697), Ad-Daara Qutwniy (1/175) na Al-Bayhaqiy (1/213 – 230). Yeye amezungumzia kuhusu ziada, na la sahihi ni kuwa ziada hii ipo].

 

..katika Hadiyth ya

((جعلت لي الأرض مسجدا))

Wamesema: “Riwaya hii imehusishwa na riwaya isemayo:

((جعلت لي الأرض مسجدا وطهورا))

2- Ni Hadiyth iliyopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((أعطيت ما لم يعط أحد من الأنبياء : نصرت بالرعب، وأعطيت مفاتيخ الأرض، وسميت أحمد، وجعل لي التراب طهورا، وجعلت أمتي خير الأمم)).

((Nimepewa mambo ambayo hakupewa Nabii yeyote: Nimenusuriwa kwa kutiwa khofu maadui, nimepewa funguo za ardhi, nimeitwa Ahmad, nimefanyiwa udongo kuwa kitwaharisho, na umma wangu umefanywa umma bora zaidi)). [Hadiyth Munkar: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/98) na Al-Bayhaqiy (1/213)].

 

Ninasema:

 

“Yenye nguvu zaidi kwangu ni kauli ya kwanza. Ni kwamba inafaa kutayammamu kwa kila kile kinachoitwa ardhi, au kila kinachobeba chochote cha ardhini kama vumbi na mfano wake. Ama kauli ya pili, hebu tuitazame kwa pande mbili:

 

Kwanza: Hakuna chochote cha kuthibitisha katika dalili zao kama ulivyoona.

Pili: Wamelichukulia neno “at-turbah” katika Hadiyth kwa maana ya udongo. Na hapa hebu tuangalie. Abuu Hurayrah katika Hadiyth ya Muslim anasema:

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinishika mkono akaniambia:

((خلق الله – عز وجل – التربة يوم السبت، وخلق فيها الجبال يوم الأحد، وخلق الشجر يوم الإثنين ..))

((Allaahu ‘Azza wa Jalla Aliumba udongo (ardhi) siku ya Jumamosi,  Akaumba humo milima siku ya Jumapili, na Akaumba miti siku ya Jumatatu…)).

 

Katika Kamusi ya “Lisaan Al-‘Arab”, mtunzi amesema:

"خلق الله التربة يوم السبت"

“Allaah Ameumba udongo Siku ya Jumamosi”, yaani ardhi.

 

Ninasema: Na maana hii iko wazi katika Hadiyth, Walillaahi Al-Hamd”.

 

Share