076-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Hedhi Na Nifasi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

076-Hedhi Na Nifasi

 

Alhidaaya.com

 

Damu za kimaumbile zinazomtoka mwanamke zinagawanyika vigawanyo vitatu:

 

1- Damu ya hedhi

 

2- Damu ya nifasi

 

3- Damu ya istihaadhwah

 

Damu Ya Hedhi

 

[Majina mengineyo ya hedhi ni: الطمث – العراك – الضحك – الإكثار – الإعصار. (Al-Muhadh-dhab 1/341)]

Ni damu nyeusi, nzito na yenye harufu mbaya. Inamtoka mwanamke toka sehemu maalumu katika nyakati maalumu.

 

Hedhi ni jambo ambalo Allaah Amewaumbia  wanawake wote kama Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwambia  ‘Aaishah kama ilivyo katika Swahiyh Mbili:

(( إن هذا أمر كتبه الله على بنات آدم....))

((Hakika hili ni jambo, Allaah Amelihukumia kwa mabinti wa Aadam)).

 

Hawwaa (Amani iwe juu yake), yeye ndiye wa mwanzo kuipata. Imepokelewa kwa isnadi Swahiyh kwa Ibn 'Abbaas akisema:

“ Hawwaa alianza kupata damu ye hedhi baada ya kushushwa toka peponi”.

 

Damu ya hedhi haina mpaka wa uchache wala wingi, bali hilo linategemea maumbile ya mwanamke, kwa vile hakuna dalili yoyote sahihi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayobainisha uchache wake au wingi wake.

 

Shaykh wa Uislamu katika Kitabu cha Al-Fataawa (21/623) anasema:

“Ama wale wanaosema kwamba wingi wa hedhi ni siku kumi na tano na uchache wake ni siku moja kama Ash-Shaafi’iy na Ahmad, au wanaosema kuwa hedhi haina mpaka maalumu kama Maaliki, wao wanasema hayo tu, lakini halijathibiti lolote kuhusiana na hilo toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Maswahaba zake. Na marejeo ya yote hayo yanasimamia juu ya maumbile ya mwanamke kama tulivyosema, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.” [Jaami'u Ahkaamin Nisaa (1/179). Angalia Al-Muhalla (2/191) na Al-Mughniy (1/308)].

   

Share