078-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nini Hukmu Ya Unjano Na Rangi Yenye Kumili Weusi Baada Ya Kutwaharika Na Hedhi?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

078-Nini Hukmu Ya Unjano Na Rangi Yenye Kumili Weusi Baada Ya Kutwaharika Na Hedhi?

 

Alhidaaya.com

 

 

Unjano na rangi yenye kumili weusi ni maji anayoyaona mwanamke mithili ya usaha. Maji haya yanakuwa si damu ya hedhi kama yatamtoka mwanamke baada ya kukatika damu au baada ya kukauka. Atazingatiwa yu twahara, ataswali, atafunga na mumewe atamwingilia.

Dalili ya hili ni Hadiyth ya Ummu 'Atwiyyah aliposema:

“Tulikuwa - baada ya kujitwaharisha - hatushughulishwi chochote na rangi yenye kumili weusi au unjano”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (307), An-Nasaaiy (1/186), Ibn Maajah (647) na wengineo. Al-Bukhaariy ameikhariji bila ziada (326)].

 

Faida

 

1- Damu inapokatika na mwanamke akawa twahara lakini maji ya kuogea yakakosekana, itambidi atayamamu na mumewe anaruhusika kumwingilia. Hili ndilo tamko la Maulamaa wengi. [Majmu’u Al-Fataawaa (1/625), Al-Muhallaa (2/171), Sharhu Muslim (1/593) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/152)]

 

2- Damu ikiendelea kutoka zaidi ya muda wake wa kawaida, nini atafanya?

Ikiwa kwa mfano damu yake kwa kawaida hutoka kwa muda wa siku sita kila mwezi, kisha ikazidi ikawa siku saba, au nane, au tisa, nini atafanya?

 

Tunasema: “Hali ya mwanamke huyu haiachani na moja ya mawili:

 

·       

Ima atakuwa anaweza kupambanua na kutofautisha kati ya damu ya hedhi na damu nyingineyo.

 

Mwanamke huyu ataiangalia damu hii. Ikiwa rangi yake, harufu yake na maumbile yake yako sawa na damu ya hedhi, basi ataendelea kuacha Swalaah, Swaum na kuingiliwa kama alivyokuwa, kwa kuwa hakuna mpaka maalumu wa muda wa kutoka damu hii kama tulivyotangulia kusema. Na kama ataiona inatofautiana na damu ya hedhi, basi ataoga na kuswali.

 

·       

Au atakuwa hawezi kupambanua na kutofautisha kati ya damu ya hedhi na nyingineyo (kuna baadhi ya wanawake wako hivi).

 

Huyu ataendelea kubakia bila kuswali, wala kufunga, wala kuingiliwa na mumewe mpaka atakapotwaharika, kwa kuwa hakuna mpaka wa upeo wa mwisho wa kutoka damu ya hedhi.  [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/215), na kitabu cha Fataawaal Mar-at cha Ibn ‘Uthaymiyn].

 

3- Ikiwa damu katika siku zake za mwezi inakuja siku mbili kwa mfano, kisha inakatika siku ya tatu, halafu inarudi tena siku ya nne na kadhalika.

 

Jibu sahihi la hali hii ni kuwa kukatika damu ndani ya masiku ya hedhi yanayojulikana, hakuzingatiwi bali huhesabiwa ni hedhi. Kinachozingatiwa ni kuonekana alama ya utwahara, nayo ni majimaji meupe ambayo akina mama wanayajua. [Fataawaal Mar-at, Jam’u Muhammad Al-Musnad (uk. 26)].

 

4- Je, mjamzito hupata hedhi?  [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/208)]

 

Maulamaa wana mielekeo miwili katika suala hili. Kundi la kwanza ambalo ni la wengi, wanasema kwamba mwanamke mjamzito haingii hedhini. Dalili yao ni Hadiyth ya Abuu Sa’iyd Al Khudriyyi (Radhwiya Allaahu Anhu) isemayo:

(( لا توطأ حامل حتى تضع ولا غير حامل حتى تحيض حيضة ))

((Mjamzito haingiliwi mpaka ajifungue, wala asiye mjamzito mpaka aingie hedhini)). [Hadiyth Hasan Lighayrih. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2157), na Ahmad (3/62). Kuna Hadiyth nyingine kama hii kwa Ad Daar Qutwniy (3/257)]. 

 

Wanasema:”Linalothibitisha kwamba mwanamke hana kitu katika tumbo lake la uzazi, ni kutokwa na damu ya hedhi, na lau kama mjamzito anapata hedhi, basi hedhi hii haiwezi kuthibitisha kuwa hana kitu tumboni”.

 

Ama kundi la pili akiwemo Ash Shaafi’iy, wao wanasema kwamba mjamzito hupata damu ya hedhi.

 

Jibu sahihi kuhusiana na kauli yao hii ni kuwa asili na kaida kuu ya wingi ni kwamba mja mzito hapati hedhi. Lakini inaweza ikamtokezea mwanamke fulani katika hali isiyo ya kawaida akatokwa na damu wakati wa ujauzito. Damu hii itaangaliwa; ikiwa iko sawa na damu ya hedhi kwa rangi, harufu na maumbile, na ikamjia wakati uleule anaopata hedhi, basi itazingatiwa kuwa ni damu ya hedhi. Hapo ataacha Swalaah, Swaum na mumewe hatoruhusiwa kumwingilia. Lakini damu hii haitoingizwa katika hisabu ya eda, kwa kuwa Allaah Anasema:

(( وأولات الأحمال أجلهن أن يضعن حملهن))

(( Wenye mimba muda wao ni kuzaa mimba zao)). [At-Twalaaq (65:4)]

 

Ama ikiwa damu inayomtoka inatofautiana na sifa za damu ya hedhi na imekuja katika wakati usio wa hedhi, basi si damu ya hedhi na wala haibebi hukmu za hedhi. Itakuwa ni kama damu ya istihaadhwah.

 

 

Share