080-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Mambo Yanayoruhusiwa Kwa Mwenye Hedhi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

080-Mambo Yanayoruhusiwa Kwa Mwenye Hedhi

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Kusoma nyiradi na Qur-aan

 

Kama ilivyotangulia nyuma, inajuzu kwa mwenye hedhi au janaba kufanya hivyo kwa kauli yenye nguvu zaidi. Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na mashuhuri katika madhehebu ya Ash-Shaaf'iy na Ahmad. [Yamenukuliwa haya na Shaykh wa Uislamu katika Al-Fataawaa (21/459)]

 

Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (1/77, 78) anasema:

"Kusoma Qur-aan, kusujudu kwenye Aayah ya sajdah, kuugusa Msahafu na kufanya nyiradi, hayo ni matendo ya kheri, yaliyosuniwa na yenye thawabu. Basi mwenye kudai kwamba hayo hayafai, basi alete dalili".

 

2- Kusujudu kama atasikia Aayah ya sajdah

 

Hakuna ubaya mwanamke mwenye hedhi kusujudu anaposikia Aayah ya sajdah, kwani sajdah si Swalaah, na wala si lazima awe na twahara.

 

Imethibiti katika Swahiyh Al-Bukhaariy (4862) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Suwrat An-Najm, akasujudu yeye, kisha wakasujudu pamoja naye Waislamu, washirikina, majini na wanaadamu.

 

Ni mbali kusema kuwa wote walikuwa na wudhuu, kisha sajdah ya kisomo si Swalaah. Az-Zuhriy na Qataadah wamesema hayo hayo kama ilivyo katika Muswannaf wa ‘Abdur-Raaziq. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/174) kwa maana yake]

 

3- Kugusa Msahafu

 

Hatuijui dalili yoyote ya wazi inayomzuia mwenye hedhi kugusa Msahafu ijapokuwa Maulamaa wengi wanasema kuwa haijuzu kwa mwenye hedhi kugusa Msahafu. Na haya yashaelezewa kwa urefu nyuma.

 

4- Mume kusoma Qur-aan akiwa kwenye  paja la mkewe  mwenye hedhi

 

Ni kwa Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) aliyesema:

"Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiisoma Qur-aan na kichwa chake kipo kwenye paja langu nami niko hedhini" [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7549) na Muslim (uk. 246) na wengineo].

 

5- Kuhudhuria Swalaah za ‘Iyd Mbili

 

Hili halina ubaya, bali ni jambo mustahabu kwa wenye hedhi watoke ili kuhudhuria Swalaah ya ‘Iyd, lakini watakaa kando ya uwanja wa Swalaah.

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((يخرج العواتق وذوات الخدور والحيض وليشهدن الخير ودعوة المؤمنين، ويعتزل الحيض المصلى))

((Watoke wazee wakongwe, waliotawishwa na wenye hedhi, ili waishuhudie kheri na du’aa za Waumini, lakini wenye hedhi wawe kando ya uwanja wa Swalaah)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika sehemu tofauti, kati yake ni nambari (324)].

 

6- Kuingia Msikitini

 

Suala hili lina mvutano mkubwa kati ya Maulamaa, nalo limeshachambuliwa hapo kabla. [Ni mwisho wa Mlango wa Kuoga]

 

Tunachoweza kusema ni kuwa sisi hatujagundua dalili yoyote sahihi na ya wazi inayomzuia mwenye hedhi kuingia Msikitini. Na asili ya jambo lolote ni uhalali mpaka liwepo la kuliharamisha. Lakini pamoja na hayo, kila mmoja aendelee kufanya istikhaarah kwa Allaahu Ta'alaa kuhusu suala hili.

 

7- Kulishana na kunyweshana na mumewe

 

Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akisema:

"Nilikuwa nikinywa huku niko hedhini, kisha nampa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye anaweka kinywa chake mahala nilipoweka kinywa changu, kisha anakunywa. Na ninang'ata mnofu wa nyama nikiwa hedhini, kisha ninampa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye anaweka kinywa chake mahala pa kinywa changu.” [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (300), Abuu Daawuud (259), An Nasaaiy (1/59) na Ibn Maajah].

 

8- Kumtumikia mumewe

 

Ni kama kumwosha kichwa au kumchana nywele. Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akisema:

"Nilikuwa nikimchana Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nywele nami niko hedhini". [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (295) na Muslim (297)].

 

9- Kulala na mumewe ndani ya shuka moja

 

Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akisema:

"Wakati nikiwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tumelala katika shuka, nilipata hedhi, kisha nilijichomoa nikachukua nguo yangu ya hedhi. Akaniuliza: Je, umepata hedhi? Nikamjibu: Ndio, halafu akaniita nikalala naye ndani ya qatifa". [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (298) na Muslim (296)].

 

Katika Sharh Muslim (1/954) An-Nawawiy anasema: "Inajuzu kulala  na mwenye hedhi katika blanketi moja."

 

 

Share