001-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Kwanza: Swalaah Tano

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

001-Kwanza: Swalaah Tano

 

Alhidaaya.com

 

 

  • Hukmu Ya Mwenye Kuacha Swalaah

Mwenye kuacha kuswali ana hali mbili: Ima aache akikataa kwamba si fardhi na si wajibu, au aache kwa uzembe na uvivu tu lakini anakubali kwamba ni wajibu kwake kuswali.

 

[1] Anayeacha kwa kupinga:

 

[Al-Majmu’u (3/16), kwa mabadilisho madogo. Angalia vitabu rejea vilivyoashiriwa katika suala linalofuatia]

 

Mwenye kuacha Swalaah akikataa kwamba si lazima, au akakataa ulazima wake lakini akawa anaonekana akiswali, basi huyo ni kafiri murtadi kwa Ijma’a ya Waislamu.

 

Kiongozi atamtaka atubie. Kama atatubia ataachwa, na kama atakataa basi atamwua kwa kuwa ni murtadi, na atafanyiwa hukmu zote za wenye kuritadi. Haya atafanyiwa yule aliyeishi na kukulia katika jamii ya Kiislamu. Lakini ikiwa bado ni mgeni na Uislamu, au aliishi maeneo ya mbali na Waislamu ikawezekana kwamba hakuweza kujua wajibu wa Swalaah, basi huyo hatokufurishwa kwa kukataa, bali tutamweleza wajibu wa Swalaah. Ikiwa atakataa baada ya kuelezwa, basi anakuwa ni murtadi.

 

[2] Anayeacha kwa uvivu na kuzembea tu lakini hakatai kuwa ni wajibu:

 

Waislamu wote wanakubaliana kwamba kuacha Swalaah ya fardhi kwa makusudi (bila ya udhuru wowote wa kisharia), ni moja kati ya makosa mazito na madhambi makubwa, na kwamba kosa hilo mbele ya Allaah ni kubwa kuliko madhambi ya kuua mtu, kupora mali, kuzini, kuiba na kunywa tembo, na kwamba kosa hilo hupelekea kwenye adhabu ya Allaah, hasira Zake na hizaya Yake duniani na aakhirah. [As-Swalaat wa Hukmu Taarikihaa cha Ibn Al-Qayyim (uk. 60). Nyongeza kati ya mabano nimeiweka mimi na umuhimu wake haufichiki]

 

Halafu 'ulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu yake juu ya kauli mbili:

 

Ya kwanza: Mtu huyu ni fasiki, mwasi na mtendaji kosa kubwa kabisa lakini si kafiri. Haya wameyasema Maulamaa wengi, nayo ni rai yenye nguvu ya Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na Masahibu zake, Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad katika moja ya riwaya mbili. [Haashiyat Ibn ‘Aabidiyna (1/235), Al-Fataawaa Al-Hin-diyyah (1/50), Haashiyat Ad-Dusuwqiy (1/189), Mawaahibul Jaliyl (1/420), Mughnil Muhtaaj (1/327) na Al-Majmu’u (3/16 na zinazofuatia). Angalia I’ilaamu Al-Ummat cha Sheikh ‘Atwaa bin ‘Abdillatwiyf (Allaah Amhifadhi)]

 

Ya pili: Ni kafiri mwenye kutoka nje ya Uislamu. Ni rai yenye nguvu ya Sa’iyd bin Jubayr, Ash-Sha’abiy, An-Nakh’iy, Al-Awzaa’iy, Ibn Al-Mubaarak, Is-Haaq, na kauli mbili sahihi toka kwa Ahmad na moja kati ya ijtihadi za Mafuqahaa wa Kishaafi’iy. Kauli hii imesimuliwa na Ibn Hazm toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, Mu’aadh bin Jabal, ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf, Abu Hurayrah na Maswahaba wengineo. [Muqaddimaat Ibn Rushdi (1/64), Al-Muqni-’i (1/307), Al-Inswaaf (1/402), Majmu’u Al-Fataawaa (22/48), As-Swalaat cha Ibn Al-Qayyim na Hukmu Taarikis Swalaat cha Sheikh Mamdouh Jaabir (Allaah Amhifadhi)]

 

 

Share