013-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Mahala Palipokatazwa Kuswalia

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

013-Mahala Palipokatazwa Kuswalia

 

Alhidaaya.com

 

 

Kiasili, ardhi yote ni sehemu ya kuswalia, na Swalaah inajuzu pahala pake popote kutokana na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((Nimefadhilishwa juu ya Manabii kwa mambo sita…Nimefanyiwa ardhi twahara na mahala pa kuswalia..)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (523), na mahala pa ushahidi kwenye Al-Bukhaariy (335), na Muslim (520) toka kwa Jaabir].

 

Lakini hutolewa ndani ya wigo wa ujumuishi huu, mahala ambapo imethibiti kwa Hadiyth kwamba ni marufuku kuswalia. Kati ya mahala hapo ni:

 

1- Kwenye mapumzikio ya ngamia na kwenye zizi lao

 

Ni sehemu ambapo ngamia husimama wakati wanapofika sehemu ya kunywa maji, au sehemu wanakojihifadhi na kulala. Jaabir bin Samrah anasema kwamba mtu mmoja alimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Je, naweza kuswali kwenye zizi la mbuzi na kondoo?” Akamjibu: “Ndio”. Akamuuliza: “Je, naweza kuswali kwenye zizi au sehemu ya mapumzikio ya ngamia?” Akamjibu: “Hapana”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (360)].  Sababu ya karibu zaidi inayoweza kusemwa kuhusu katazo hilo, ni pale Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

(( Msiswali kwenye zizi au mapumzikio ya ngamia, kwani ni sehemu ya mashaytwaan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (493), Ibn Maajah (769), na Ahmad (5/55)].

 

Uwezekano hauko mbali wa mashaytwaan kuandamana na ngamia, na kuwa maeneo yake ya kupumzikia na kulala ni hifadhi ya mashaytwaan. Na kwa ajili hiyo, imekatazwa kuswalia hapo. Ni kama alivyokataa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali mahala ambapo Swalaah ya Alfajiri iliwapita. Ameeleza sababu ya hilo katika neno lake:

(( Mahala hapo shaytwaan alitujia )). [Hadiyth Swahiyh: Imekuja katika mlango wa “Nyakati za Swalah”]

 

2- Makaburini

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriy akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Ardhi yote ni sehemu ya kuswalia, isipokuwa makaburi na bafu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (492), At-Tirmidhiy (236), na Ibn Maajah (745).  Kuna mvutano kuhusu kama ni ‘Mawswuul” au “Mursal”. La sawa ni “Mawswuul”. Angalia Al-Irwaa (1/320)].

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Murthad kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( Msikae juu ya makaburi, na wala msiswali kuyaelekea )). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (972)].

 

 Na Bi ‘Aaishah anasema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  

((Allaah Amewalaani Mayahudi na Manaswara, waliyafanya makaburi ya Manabii wao Misikiti)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (435) na Muslim (529)].

 

Kana kwamba sababu ya kukataza kuswali kwenye makaburi ni kuzuia njia ya kuyaabudu makaburi au kujishabihisha na makafiri.

 

Makaburi yote ni hali moja hapa, yawe ya Waislamu au ya makafiri. Na ikiwa yatafukuliwa na maiti zikatolewa, basi Swalaah itajuzu hapo.

 

Kumswalia maiti baada ya kuzikwa kwa yule ambaye hakuwahi kumswalia, hutolewa ndani ya wigo wa katazo. Na hii ni kwa Hadiyth ya Ibn 'Abbaas aliyesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali mbele ya kaburi baada ya maiti kuzikwa, na akampigia takbiyr mara nne. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (954)].

 

Aidha, imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuulizia mtu aliyekuwa anasafisha Msikiti. Wakamjibu: "Amefariki ee Rasuli wa Allaah!" Akasema: "Kwa nini msinijulishe?" Wakajibu: " Yeye alikuwa hivi na hivi" (yaani wakamdunisha). Akawaambia: "Nionyesheni lilipo kaburi lake". Rasuli akaenda kwenye kaburi lake, akamswalia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1337) na Muslim (956)].

 

Hadiyth hii inatuarifu kuhusu uhalali wa kumswalia maiti kwenye kaburi, na Jamhuri wamejuzisha hili. Lakini Maalik na Abuu Haniyfah wamelikataa hili. Mengi zaidi yatakuja katika mlango wa "Janaaiz".

 

3- Bafu:

 

Ni mahala pa kuogea (na si pa kukidhia haja) kama wanavyopaita watu. Haijuzu kuswali hapo kutokana na Hadiyth ya Abuu Sa'iyd iliyotangulia: ((Ardhi yote ni sehemu ya kuswalia isipokuwa makaburi na bafu)).

 

Ama mahala pa kukidhi haja kama chooni au msalani, haijuzu kuswali hapo pia kutokana na unajsi wa mahala na kuwa ni makazi ya mashaytwaan. Zayd bin Arqam anasema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakika sehemu hizi za kufanyia haja, ni makazi yaliyokaliwa, basi anapoingia mmoja wenu msalani  aseme: Ninajilinda kwa Allaah na majini wa kiume na majini wa kike)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (6) na Ibn Maajah (296)].

 

·       

Je, Inajuzu Kuswali Juu Ya Shimo La Majitaka?

 

Kiusahihi, sehemu ya juu ya shimo la majitaka haihusiani na shimo lenyewe, na wala sehemu hiyo haiitwi choo. Hivyo inajuzu kuswali juu yake madhali hapo juu hapana najsi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

·       

Nini Hukmu Ya Kuswalia Nguo Ya Wizi Au Iliyoharamishwa, Au Ardhi Ya Kupora?

 

Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na suala hili na mengineyo yanayofanana:

 

Ya kwanza:

 

Swalaah haiswihi. Kauli hii ni mashuhuri katika madhehebu ya Ahmad na Ibn Hazm. Sheikh wa Uislamu ameikubali kauli hii. [Al-Inswaaf (1/194), Al-Muhallaa (4/33) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/89)]

 

Hoja yao ni:

 

1- Yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) ikiwa Marfu’u:

((Mwenye kununua nguo kwa dirham kumi, na katika hizo kuna dirham moja ya haramu, basi Swalaah yake haitokubaliwa madhali dirham hiyo ipo)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/98) kwa Sanad Dhwa’iyf].

 

2- Nguo inafungamana na nguzo na masharti ya ‘ibaadah, hivyo huiathiri kinyume na kama iko nje yake. Ni kama mtu aliyetawadha kwa chombo cha dhahabu, hiki hakiathiri, kwani kiko nje ya Swalaah.

 

Ya pili:

 

Swalaah inaswihi, lakini atapata dhambi kwa kuivaa. Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Maalik na Ash-Shaafi’iy. [Al-Majmu’u (3/180), Al-Mabsuutw (1/206) na Naylul Awtwaar (2/92)]

 

Nayo ndiyo yenye nguvu kwa kuwa hakuna Hadiyth yoyote inayokataza kuswalia kwenye ardhi ya kupora, au nguo ya wizi, au iliyoharamishwa, bali imekuja Hadiyth yenye kukataza kitendo cha uporaji au kuzungumzia vivazi kiujumla. Hivyo Swalaah inaswihi lakini madhambi ya uporaji yapo, na  hili huitwa “Kanuni ya uchangukaji”. [Angalia Qawaa’id Ibn Rajab (uk 11 na 12)] Ama Hadiyth waliyoitolea dalili, Hadiyth hii  haifai, juu ya kwamba kukubaliwa huko hakulazimu kukanusha usahihi wake.

 

Ninasema: “Huenda tuliyoyatilia nguvu, yanathibitishwa zaidi na Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizawadiwa joho la hariri akalivaa, kisha akaswali nalo. Halafu alinyanyuka, akalivua kwa kishindo mno kana kwamba amelichukia. Kisha akasema: “Hili halitakikani kwa wachaMungu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (375) na Muslim 2075)]

 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amelivaa kabla ya kuharamishwa, kisha Jibriyl akamjulisha kuwa ni haramu kuvaa hariri (kama ilivyo kwenye riwaya ya Muslim toka kwa Jaabir) ndani ya Swalaah na nje ya Swalaah. Lakini pamoja na hivyo, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuirudia tena Swalaah.

 

1-    

Kusitiri uchi pamoja na uwezo wa kufanya hivyo

 

Maulamaa wamekubaliana (isipokuwa wachache mno) kwamba kusitiri uchi ni sharti ya kuswihi Swalaah kwa atakayeweza kufanya hivyo kwa dalili zifuatazo:

 

1- Kauli Yake Ta’alaa:

 

 يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ 

 

Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu (ya mavazi ya sitara na twahara) katika kila mahala pa ‘Ibaadah. Na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu. [Al-A’araaf ( 7:31)]

 

Kwa maana kwamba zisitirini nyuchi zenu mnapotaka kuswali, kwani wao walikuwa wakiitufu Ka’abah wakiwa uchi, ndipo ikashuka Aayah hii (kama ilivyoelezwa kwenye Swahiyh Muslim).

 

2- Hadiyth ya Salamah bin Al-Akwa’a aliyesema: “Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Sisi tunakuwa mawindoni. Je, anaweza mtu kuswali na nguo moja? Akajibu: “Ndio, ajifunge nayo chini, na kama hakuweza, basi aifunge kwa mwiba”. [Isnadi yake ni teketeke. Al-Bukhaariy ameifanya ‘Mu’allaq” kwa muundo wa kutothibiti kuwepo (1/553) na akasema kuwa Isnadi yake ichunguzwe. Ninasema: “Hivyo ndivyo ilivyo kutokana na kasoro aliyoieleza Al-Haafidh kwenye Al-Fat-h (1/555). Kisha Hadiyth hii imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (632), na An-Nasaaiy (2/70). Mzingo wake uko kwa mpokezi asiye makini.  Al’Allaamah Al-Albaaniy kwenye Al-Mishkaat (760) na kabla yake An-Nawawiy kwenye Al-Majmu’u (3/164), wanaona kwamba ni Hadiyth Hasan!!”]

 

3- Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Allaah Haikubali Swalaah ya msichana aliyebaleghe ila kwa khimar)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (641), At-Tirmidhiy (377) na wengineo. Baadhi ya Maulamaa wameitia walakini. Katika Al-Irwaa (1/215), Al-Albaaniy ameipasisha kuwa ni Hasan].

 

4- Hadiyth ya Jaabir akisimulia kuswali kwake pembezoni mwa Rasuli  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikihusiana na nguo. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

((Kama ni pana, jizungushie, na kama inabana, jifunge nayo chini)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (361) na Muslim (3010].

 

Haitotosheleza chini ya izari (sitara ya chini ya mwili). Hivyo inaonyesha ulazima wa kusitiri mwili katika Swalaah. Wajibu huu ni katazo la kinyume chake, na kinyume hiki ni uharibifu. Hivyo kujisitiri kunabeba usharuti kwa Jamhuri.

 

5- Ibn ‘Abdul Barri amehadithia kwamba Maulamaa wote kwa ijmai wamekubaliana kwamba Swalaah inakuwa baatwil kwa mwenye kuswali uchi naye ana uwezo wa kujisitiri. Pia Sheikh wa Uislamu amenukuu hivyo. Lakini baadhi ya wafuasi wa Maalik wamenukuu kwamba Swalaah haibatiliki kwa kutositiri uchi. Naye Ash-Shawkaaniy, juu ya msingi wa qaida yake iliyotangulia katika kushurutisha utwahara wa nguo, mwili na mahala,  anasema kwamba ni wajibu.  [At-Tamhiyd, Majmu’u Al-Fataawaa (22/117), Al-Fat-h (1/555), Bidaayatul Mujtahid (1/156) na As-Saylul Jarraar (1/158)]

 

Linaloonekana kwangu ni kuwa suala hapa linatofautiana kwa mwenye kuliangalia kwa mtizamo wa kina.

 

6- Kuusitiri uchi wakati mtu anaposimama mbele ya Allaah Mtukufu, kunaingia katika mlango wa kumtukuza. [Al-Badaai-’i (1/116), Ad-Dusuwqiy (1/211), Mughnil Muhtaaj (1/184) na Kash-Shaaful Qinaa (1/263)]

 

 

Share