021-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Yenye Kubatwilisha Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

021-Yenye Kubatwilisha Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Kuwa na uhakika wa kupata hadathi yenye kubatilisha wudhuu

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilalamikiwa kuhusiana na mtu ambaye anaona kana kwamba kimemtoka kitu ndani ya Swalaah yake akasema:

((Asiondoke mpaka asikie sauti, au anuse harufu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (137) na Muslim (361)].

 

2- Kuacha sharti kati ya masharti ya Swalaah au nguzo kati ya nguzo zake bila ya udhuru

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mtu aliyeswali vibaya wakati alipomwona kwamba hatulii katika Swalaah yake na kumwambia:

((Rejea uswali tena, kwani hukuswali)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (793) na Muslim (397)].

 

Nyuma tumekwisha zitaja shuruti na nguzo za Swalaah, unaweza kuzirejea.

 

3- Kula au kunywa kwa makusudi

 

Ibn Al-Mundhir amesema: “Maulamaa wote wamewafikiana kwamba mwenye kula au kunywa katika Swalaah ya faradhi kwa makusudi, basi lazima aswali tena”.

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema pia kuwa hata Swalaah ya Sunnah inabatilika, kwani linalobatilisha faradhi, hubatilisha vile vile Sunnah.

 

4- Kuzungumza makusudi kwa jambo lisilohusiana na maslaha ya Swalaah

 

Imepoekelewa toka kwa Zayd bin Arqam akisema: “Tulikuwa tukizungumza katika Swalaah; mmoja wetu anamzungumzisha swahibu yake pembeni ndani ya Swalaah mpaka ikateremka:

((حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ))

..na hapo tukaamuriwa kunyamaza [tukakatazwa kuzungumza]. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1200) na Muslim (539) na ziada ni yake].

 

·       

Faida

 

Mwenye kuzungumza ndani ya Swalaah kwa kusahau au kutojua hukmu, Swalaah yake haibatiliki. Mu’aawiyah bin Al-Hakam amehadithia kwamba aliswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mtu mmoja alipiga chafya, akamhimidi Allaah, naye akamwambia: “Yarhamukal Laahu”. Watu wakaanza kumwangalia akawaambia: “Ebo!! Mna nini!! Mbona mnanitizama hivyo?!”

 

Hadiyth hii inatuonyesha kwamba alizungumza lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuibatilisha Swalaah yake wala hakumwamuru kuirejesha kwa kuwa alikuwa hajui hukmu, bali alimwambia:

((Hakika Swalaah hii haifai ndani yake chochote katika maneno ya watu, bali ni tasbiyh, takbiyr na kusoma Qur-aan)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (537). Tumeshaieleza nyuma].

 

 5- Kicheko cha sauti

 

Kicheko hiki hubatilisha Swalaah kwa Ijma’a ya Maulamaa kama alivyonukulu Ibn Al-Mundhir. Kicheko ni kibaya kuliko maneno kwa sababu huandamana na dharau na kuichezea Swalaah. Kuna athari nyingi toka kwa Maswahaba (Allaah Awaridhie) zinazoonyesha kwamba Swalaah hubatilika kwa kucheka. [Imepokelewa toka kwa Jaabir na Abuu Muusa kama ilivyo kwa Ibn Abuu Shaybah katika Al-Muswannaf (1/387)].

 

·       

Faida

 

Kutabasamu hakubatilishi Swalaah, lakini kunakuwa makruhu kama kutakuwa bila ya udhuru. Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “Kutabasamu hakuivunji Swalaah, lakini mkoromo huivunja”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (1/387) na ‘Abdul Razzaaq kwa Sanad Hasan].

 

 

Share