Eda: Hikma Yake, Hukmu Zake, Yanayopasa Na Yasiyopasa

Eda: Hikma Yake, Hukmu Zake, Yanayopasa Na Yasiyopasa

 

Abu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Eda ni kipindi anachokaa mwanamke aliyeachika (Talaka) au aliyefiwa na mumewe, na baada ya kipindi hicho ndoa yake huwa halali. Na imeitwa eda kwa jina hili kutokana na jina la kiarabu ‘iddah’ kwa kukusanya kwake (idadi) ya miezi au quruu[1]   au hedhi au vipindi vya tohara ya hedhi.

 

 

Hikmah Ya Kuhalalishwa Eda:

 

Hapa tunaona baadhi ya mawazo ya ‘Ulamaa ambao wameona hizi ndizo hikmah au sababu za kuwekewa eda Shariy'ah, ingawa hikmah ya mwanzo na ya mwisho ni hiyo ya mwisho hapo chini ya fungu hili:

 

 

 • Kutambua kama mwanamke ni mjamzito au laa.

 

 • Kuweza kubainika nasaba au kizazi ili kuepusha utata wa kutokujulikana nani ndiye baba.

 

 • Kipindi ambacho mke anakaa eda kiwe kifupi au kirefu kinaangaza mwangaza wa kweli kuhusu uzito wa ndoa yao na mkataba mtakatifu walioufunga baina yao.

 

 • Eda ya kufiwa inamwezesha mwanamke kutoa huzuni zake na kupata muda wa kujiliwaza na msiba uliomtokea wa kipenzi chake. Pia inamhifadhi kwa kutokuwa chombo cha kusemwa na kuzungumzwa kila apitapo.

 

 • Kupata nafasi mume na mke kutafakari kwa makini kuhusu mahusiano yao kabla hawajavunja muungano wao wa kifamilia na haswa katika talaka ivunjikayo (ya kwanza au ya pili)

 

 • Ama hikmah ya juu kuliko zote kuhusu eda ni utiifu kwa maamrisho ya Rabb wetu (Subhaanahu Wa Ta'aalaa). Kwani kuna wengi wanaotoa hoja za akilini mwao kama vile kudai kuwa siku hizi kuna utaalam wa kujua kama mwanamke ana mimba kwa vipimo bila haja ya kukaa eda mwanamke n.k. Hoja kama hiyo si ya busara maana ni sawa na kusema ‘siku hizi kuna kinga za mimba kama kondomu n.k, kwa hiyo zinaa iwe halaal!’ Wamesahau kuwa hikmah kuu ni utiifu kwa Muumba na utekelezaji wa maamrisho yake na mengine ni ya ziada na wala si ya msingi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anatujua zaidi kuliko tujijuavyo nafsi zetu.

 

 

Hukmu Za Eda:

 

1-Eda Kishariy'ah

 

Kishariy'ah eda ina maana nyingi, mojawapo: Kupata yakini kwa kile kiumbe chenye kuzaliwa ili kuepukana na mchanganyiko wa nasaba. Na vilevile eda hikmah yake hiyo eda ni kutoa fursa na muda kwa mume na mke baada ya talaka huenda kwa kipindi hicho wakamaliza tofauti zao na kurudiana na kuishi tena kama wanandoa kamili. Na pia sababu nyingine ni kulipa na kutekeleza haki haki zote za mume aliyefariki (ikiwa ni eda ya kufiwa) na kudhihirisha athari za kumpoteza mume, kwa kipindi cha maombolezi, nako ni kujizuia huyo mwenye eda na kujipamba, kujiremba n.k. kama tutakavyoona mbele.

 

 

Na eda ni wajibu kwa mwanamke wakati anapoachana na mumewe, ima kwa talaka au kwa kufiwa na mumewe au ‘faskh’ (kutenguka kwa ndoa) au khulu’[2]  (kujivua na ndoa hiyo). Na ni sharti awe ashaingiliwa na mumewe. Na eda haiwi kwa mwanamme, na anaruhusiwa kuoa mwanamke mwingine bila hata kusubiri kwisha  hiyo eda ya mkewe. Ila tu kama kutakuwa na kizuizi, kama kutaka kumuoa dada ya mkewe, maana hairuhusiwi kishariy'ah kuchanganya baina ya dada wawili kwa wakati mmoja kwani kishariy'ah atakuwa yule mke aliyempa talaka ni wake hadi atakapomaliza muda wa eda yake. Au pia kama ana wake wanne na amempa talaka mmoja kati yao, haitoruhusiwa kwake kuoa mwanamke mwingine hadi eda ya huyo aliyemuacha imalizike vilevile. Kishariy'ah hairuhusiwi kuwa na zaidi ya wake wanne.

 

 

2-Kumalizika Eda:

 

Kunatofautiana muda wa kwisha eda kutokana na sababu au aina za eda yenyewe. Aina zenyewe ni hizi zifuatazo:

 

 

i) Eda ya aliyepewa talaka:

 

Ni ‘quruu’ (vipindi vya hedhi, tohara) tatu, endapo atakuwa keshaingiliwa na mumewe na hakuwa ni mwenye mimba, au aliyekoma hedhi, au mdogo asiyepata hedhi bado. Na haya yamefafanuliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anaposema:

 

وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلَاثَةَ قُرُوءٍ ۚ  

Na wanawake waliotalikiwa wabakie kungojea zipite hedhi (na twahara) tatu.  [Al-Baqarah: 228]

 

 

ii) Eda ya aliyefiwa na mumewe:

 

Ni miezi minne na siku kumi, kama Alivyoipangia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Qur-aan:

 

 وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا ۖ فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا فَعَلْنَ فِي أَنفُسِهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿٢٣٤﴾

Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao (eda) miezi minne na siku kumi. Watakapofikia muda wao, si dhambi kwao katika yale waliyoyafanya katika nafsi zao kwa ada ya shariy’ah. Na Allaah kwa yale myatendayo, ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Al-Baqarah: 234]

 

Kiwango hiki ni endapo atakuwa si mjamzito (mwenye mimba), ama akiwa ni mjamzito basi eda yake itakwisha pale atakapojifungua. Kama tutakavyoeleza zaidi hapo mbele.

 

 

Hakuna tofauti ya huyu aliyefiwa ikiwa mumewe alimwingilia alipokuwa hai au hakumwingilia, yote ni mamoja. Na atakapokufa mume na hali mkewe yuko katika eda ya talaka rejea, itageuka eda hiyo na kuwa ni eda ya kufiwa. Ila endapo mume wa mke aliyeachwa talaka wazi atakuwa amekufa, na kumuacha kwake kulikuwa  wakati akiwa na afya yake nzuri au kwa matakwa ya mwanamke mwenyewe, basi katika hali hiyo mke atakamilisha tu hiyo eda ya talaka na hatokaa eda ya kufiwa.

 

 

 

iii) Eda ya aliyekoma hedhi:

 

 

(Kwa kupindukia miaka) Ni miezi mitatu kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ

Na wale wanawake wanaokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa mna shaka, basi eda yao ni miezi mitatu. [Atw-Twalaaq: 4]

 

Na itakapowarejelea hedhi wakati ashaanza eda yake, basi atakaa eda ya ‘quruu’ badala ya miezi. Ama akiwa amepata hedhi mara moja au mbili tu kisha akawa katika hedhi yake iliyokoma basi arejee kwenye kukaa eda ya miezi mitatu badala ya quruu.

 

 

iv) Eda ya mjamzito (mwenye mimba):

 

Inamalizika kwa kujifungua kama Anavyosema hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ۚ  

Na wenye mimba muda wao (wa eda) watakapozaa mimba zao.  [Atw-Twalaaq: 4]

 

Ama ikiwa mwanamke eda yake ishaanza naye hajui kama ana mimba na baadaye ikadhihiri hiyo mimba, basi atabadili eda yake kutoka kuwa ni eda ya ya mwezi na kuwa ni eda ya mimba (ujauzito). Na ataendelea na eda hadi atakapojifungua.

 

 

 

v) Eda ya msichana ambaye hajafikia kupata hedhi, na eda ya mwanamke aliyevunja ungo ambaye pia hajawahi kupata hedhi na ambaye hakufikia umri wa kukoma hedhi:

 

 

Hawa wote eda yao ni miezi mitatu kutokana na ushahidi wa maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ ۚ

Na wale wanawake wanaokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa mna shaka, basi eda yao ni miezi mitatu, pamoja na wale wanawake wasiopata hedhi. [Atw-Twalaaq: 4]

 

 

Lakini endapo itamtokezea hedhi mmoja kati ya wanawake wa aina hiyo kabla ya kumalizika muda wa eda yake, ataibadili hiyo eda na kuwa ni ya quruu badala ya ile ya miezi iliyokuwa mwanzo.

 

 

vi) Eda ya mwanamke aliyezaa mapacha au zaidi:

 

 

Itaanza baada ya kumzaa pacha wa mwisho, kwani mazingatio katika eda ya ujauzito ni kujulikana kiumbe (baraa-atu rahim), kwa kuondokana kabisa na ujauzito.

 

 

 

vii) Eda ya aliyetowekewa na mumewe:

 

Aliyetoweka ni yule ambaye hajulikani alipo na habari zake hazikusikika tangu alipoondoka au kutoweka pamoja na kutafutwa kwa muda mrefu. Wanazuoni wa Shariy'ah wametenganisha kati ya kupotea kwake kwa aina mbili: kujulikana alipo na kutojulikana. Ikiwa alipo panajulikana na ikiwa yuko salama huko alipo ima kibiashara, kikazi au kimatembezi, na kukakatika habari zake, basi wamesema Wanazuoni kuwa  ndoa yao bado itabaki hadi kuthibitike mauti yake au atoe talaka au kupite muda mrefu ambao si wa kawaida ya yeye kupotea hivyo. Ikifikia hali hiyo, basi mke atakaa eda na kisha itakuwa halali kwake kuolewa tena. Ama ikiwa kupotea kwake kutajulikana kama vile kumesikika kuwa ndege aliyopanda katika safari yake imeanguka na hakupona mtu au gari alilosafiria limepinduka n.k, hapo mke atakaa eda ya mfiwa ya miezi minne na siku kumi. Na ikiwa kupotea kwake kumekuwa kurefu mno na hajulikani kama kapatwa na nini, na kukawa hakuna mawasiliano ya aina yoyote, basi hapo mke atasubiri kipindi cha miaka minne kisha atakaa eda ya mfiwa ya miezi minne na siku kumi. Ila ni vizuri zaidi kabla ya hivyo kuwe kumefanyika majuhudi makubwa ya kumtafuta kwa kutumia njia za kila aina na haswa kwa wakati huu ambapo njia za mawasiliano zimekuwa nyingi na nyepesi mno. Ni vizuri kutolewe taarifa kwenye vyombo vya habari, mitandao, mabalozi n.k.

 

 

Lakini ikiwa kutoweka kwa bwana kukawa hatimaye kumebainika alipo na kukawa na mawasiliano, mathalan kumejulikana kuwa yuko jela na kifungo chake ni miaka mingi, au kasafiri mbali na atakawia sana kurudi, hapo kutatazamwa kama muda huo mrefu utamuathiri mke na watoto wake ima kiuchumi au kimwili au kiusalama, basi hapo mke ana haki ya kusubiri au kudai talaka au kuomba kuachishwa na mume huyo. Qaadhi au Shaykh au Imaam au kiongozi wa Dini ataangalia sababu za pande zote na dharura iliyopo kabla ya kumwachanisha mke na mumewe.

 

 

 

3-Yanayopaswa Kwa Mwenye Eda:

 

‘Ulamaa wengi wa kishariy'ah wamekubaliana kuwa mwenye eda anapaswa kukaa katika nyumba ya ndoa kwa muda wa eda yake yote hadi itakapomalizika. Ikiwa eda hiyo ni ya talaka au ya kuomba kuachwa (kuachishwa) au ya kifo, haitakikani atoke ila kwa haja maalum au nyudhuru za kishari'ah la sivyo atakuwa ametenda dhambi. Na mume anaweza kumkataza asitoke ikiwa eda hiyo ni ya talaka, na mrithi ana haki ya kumzuia kutoka ikiwa eda hiyo ni ya kufiwa. Ila baadhi ya ‘Ulamaa wanasema kuwa katika eda ya kufiwa mke anakaa eda yake atakavyo.

 

Na inapaswa kwa mwenye eda ya kufiwa akae katika maombolezi (al-ihdaad) kwa muda wote wa eda yake. Na kuomboleza ni kuacha yeye kujipamba kwa mavazi ya marembo rembo, kuvaa dhahabu, na kujipaka manukato n.k. Kufanya hivyo kuna maana ya kuchunga na kuheshimu ule uhusiano wa kindoa uliokuwa baina yake na mumewe, nako pia ni kuonyesha utiifu kwa uhusiano wao. Pia kunapatikana katika huo muda wa maombelezi, utulivu wa nafsi ya mwanamke na kufikiria maisha mapya ya ndoa yamkabiliyo mbeleni.  

 

 

Mas-ala Mbalimbali Katika Eda Na Haswa Eda Ya Kufiwa:

 

 

Haya ni baadhi ya mas-ala ambayo ni haraam kwa mwenye eda kuyafanya kishariy'ah:

 

 

 • Kujitia manukato mwilini au nguoni.

 

 • Kujitia rangi za mdomo, rangi za kucha, poda, na aina zote za vipodozi.

 

 • Kujitia wanja wa macho bila dharura ya kuumwa.

 

 • Kuvaa nguo za rangi rangi: au ya rangi moja lakini yenye kuvutia na yenye mapambo. Si lazima hata hivyo kuvaa kaniki kama inavyodhaniwa na wengi au shuka la bafta n.k.

 

 • Kuvaa mapambo ya dhahabu, fedha, lulu, almasi na madini mengine, ikiwa ni pete, mkufu, hereni, bangili na vinginevyo.

 

 • Kujitia hina popote maungoni panapoonekana na watu.

 

 • Kutoka nje pasipo na dharura. Haikatazwi mwenye eda kutoka nje kama hana wa kumtegemea kwa mahitaji yake, mathalan ikiwa inambidi kufanya kazi kwa kupata mahitaji yake, kwenda kununua mahitaji yake ya nyumbani, au kufundisha kama mwalim n.k.

 

 • Kuolewa

 

 • Kuposwa

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida nyenginezo tele:

 

Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Nikaah - كِتَابُ اَلنِّكَاحِ

 

Mambo Ya Uzushi Yanayofanywa Na Wakaa Eda:

 

 

Kuna mambo yafanywayo na baadhi ya wanawake wenye kukaa eda ambayo ni ya kijahili na hayapo katika mafunzo ya Dini yetu hii nyepesi. Mambo hayo ima kwa kutokujua hao wayafanyao, au kwa kufundishwa na maustaadh na masheikh wababaishaji.

 

 

Utakuta baadhi ya wenye eda hawawezi kutoka majumbani mwao sharti wawe wametoka na fimbo au bakora, wengine wakitoka huku wamevaa matambara kama mwendawazimu, na wengine ambao hawajistiri inavyopasa utawaona nywele zao hawazichani wala kuzisafisha kwani wameambiwa hairuhusiwi kuchana wala kuoga kila mara. Hadi mwanamke akimaliza eda yake, si chawa na uvundo unaotoka mwilini mwake kwa kutojisafisha kila mara. Hayo ni matunda ya mafunzo ya waalimu wa Dini wasio na elimu Swahiyh ya kutegemewa.

 

 

Haya ni baadhi ya mambo ya uzushi katika eda yaliyokuwa yakifanyika zamani na yanayofanyika hadi sasa katika jamii yetu:

 

 

 • Kuja mtu kama mwalimu au Sheikh kumnuiza huyo mwenye eda wakati aanzapo eda yake, na kumchagulia saa ya kuianza hiyo eda.  (Eda huanza pale tu akatapo roho mume. Hakutakikani kunuizwa wala kungojea saa maalum ya kuianza).

 

 • Baadhi ya wenye eda huwa na khofu na eda na kuamini kuwa ikiwa hajakaa hiyo eda ipasavyo, basi atafikwa na balaa au wazimu au kifo.

 

 • Kutonyanyua sauti ili isisikike na watu walio nje. Si vizuri mwanamke kunyanyua sauti yake lakini kwenye hili kunakuwa kunatiliwa mkazo mno hata inakuwa vigumu watu kumsikia, hata kama anahitaji kitu au anamuhitaji mtu amjie, matokeo yake anakuwa kama bubu au yuko kifungoni hata baadhi ya mahitajio yake anayakosa kwa kuamini kuwa hapaswi kutoa sauti.

 

 • Kupelekwa chooni kwa kuchukuliwa vyetezo vya ubani, na yeye kubeba fimbo ya mumewe au kisu au kukamata kaa la moto lililozimika, au ndimu, au chumvi.

 

 • Wengine hawaendi chooni usiku kwa kuamini ni vibaya na huwa wanawekewa chombo chumbani cha kujisaidia haja zake. Matokeo chumba kinakuwa hakitamaniki na kuhatarisha pia afya ya mkazi.

 

 • Hata akiwa faragha hawezi kutoa kitambaa cha kichwa akiamini kuwa ni balaa. Kwa maana amefundishwa kuwa akifanya hivyo atatoa nafasi ya wazimu kumuingia kichwani mwake.

 

 • Kutoruhusiwa kulalia kitanda chenye godoro na badala yake alalie kitanda cha kamba au mbao kisicho na tandiko juu yake au jamvini.

 

 • Kuvaa aina fulani ya viatu tu, kama vya mbao na sharti visimtoke mguuni. Na wanaamini kuwa kiatu kikimvuka tu basi na wazimu umemvaa saa hiyo hiyo.

 

 • Kukatazwa kuonana na wanaume hata kama ni maharimu wake.

 

 • Kutoruhusiwa kusema na mtu tokea alasiri ya siku ya Alkhamiys tena baada ya kuogeshwa! Hadi mshuko wa siku ifuatayo ya Ijumaa. Hata akitokewa na hatari hawezi kupiga yowe la kuhitaji msaada!

 

 • Kulazimishwa kufunga Swawm siku hizo za Alkhamyis na Ijumaa na kusoma Qur-aan na nyiradi ndefu ndefu. Haijulikani kama Swawm hiyo ni ya eda au ya nini, na wala haijulikani ilipofundishwa.

 

 • Kuja kusomewa kila Alkhamiys na huyo mwenye kumsomea hupewa chochote. Naam, hayo ndiyo hao masheikh wababishaji wayafundishayo ili waweze kupata chochote. Na mambo mengi ya Dini yamezushwa ili kuwanufaisha hao wayaanzishayo. Allaah Awaongoze.

 

 • Kukatazwa hata kujitazama katika kioo kwa muda wa eda yake yote.

 

 • Kutoamkia au kutoamkiwa kwa kupewa Salaam kama kuambiwa “anakusalimu fulani” bali huambiwa “fulani anakupeni hujambo?”

 

 • Kutojibu neno lolote katika hali ya kusimama. Ila ni sharti akitaka kumjibu mtu, apige magoti ndipo ajibu.

 

 • Kulalia chini ya mto kitu kinachomhusu aliyefariki. Au kulalia ndimu, msumari na wembe.

 

 • Kutokukata kucha za mikono wala za miguu kwa muda wote huo wa eda wa miezi minne na siku kumi. Nako ni kufuga uchafu na kujihatarisha yeye mwenyewe kujidhuru kwa makucha yake.

 

 • Kuzikusanya nywele zote zilizong’ooka ili ziende zikatupwe mbali kabisa kama baharini siku atokapo eda yake pamoja nywele anyolewazo siku hiyo.

 

 • Kuondoshwa hiyo eda katika sehemu za pwani, kwa kuchagua siku maalum na kwenda kuosha nguo pwani na kugonga madebe na vyuma na kukaa siku tatu bila kuonekana na watu.

 

 

Haya ni mambo yaliyokuwa yakifanywa zamani na mengine hadi leo yanaendelea kufanyika katika baadhi ya jamii yetu kutokana na kudanganywa watu na pia kwa kutokuelewa wengi wetu na kwa kutofanya jitihada za kujielimisha. AlhamduliLLaah hivi sasa kutokana na elimu Swahiyh imeenea sehemu nyingi na wengi wanasoma, basi mambo hayo yamepungua sana.

 

 

Mambo yote yaliyopo hapo juu, mengi ni ya kusikitisha na mengine ni ya kuihusisha Dini yetu na ugumu na kuipa picha mbaya kabisa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

 

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ  

Na Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika Dini.  [Al-Hajj: 78]

 

  

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu. [Al-Baqarah: 185]

 

 

Vilevile tumeona mifano mingi ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisisitiza kuhusu kutotia uzito na ugumu katika Dini. Alikuwa akisema:

 

أُرْسِلْتُ بِحَنِيفِيَّةٍ سَمْحَةٍ

Nimetumwa kwa Dini Ya Haniyfah (kuelemea haki tu) na (Dini) ya sahali ya uvumilivu.  [Musnad Ahmad na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Asw-Swahiyhah)

 

 Pia alipowatuma ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na Mu’aadh bin Jabal (Radhiwya Allaahu ‘anhu) kwenda Yemen, aliwausia kufanya wepesi kwa kuwabashiria kheri watu wa huko na kuwavuta katika dini kwa upole bila kuwatilia uzito na kuwakimbiza, akasema:

 

 

يَسِّرَا وَلَا تُعَسِّرَا وَبَشِّرَا وَلَا تُنَفِّرَا وَتَطَاوَعَا وَلَا تَخْتَلِفَا

Rahisisheni mambo kwa watu (kuhusu mambo ya Dini) wala msifanye magumu na toeni habari njema na msiwakimbize, na mtiiane (msikizane) wala msikhitilafiane.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Sasa ni ajabu kuona baadhi ya Masheikh wakiwafundisha watu mambo magumu magumu na yasiyokuwa hata katika mafundisho ya dini yetu hii nyepesi.

 

 

Allaah Atujaalie hima ya kujifunza na kutafuta elimu ya haki na iliyo Swahiyh na atuepushe na uzushi na ya batili. 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

[1] Quruu: 

 

Kuna kutofautiana kwa maoni ya ‘Ulamaa kuhusu hii quruu, je, ni Twahara au ni hedhi?  

Quruu, ni neno linalotumika kwa maana ya hedhi au Twahara kwa vile linaoana na maana zote mbili. Hanafiy na Hanbaliy, wanaona kwamba neno hili lina maana ya hedhi. Hii inamaanisha kwamba mwanamke aliyeachwa atakaa hadi hedhi tatu zimalizike. Ikiwa hedhi itakatika baada ya mara moja tu, basi itakamilishwa na miezi.

Ama Imaam Maalik na Ash-Shaafi'iyy, wao wanaona kwamba neno hili lina maana ya Twahara. Na Twahara hapa ni vile vipindi vinavyokuwa baina ya hedhi mbili.

 

 

[2] Khul'u:

 

Kilugha: Ni neno lenye asili ya Kiarabu lenye kumaanisha kuondosha na kuvua. Ni kama vile mtu anavyoivua nguo kuitoa mwilini.

 

Kishary'ah: Ni kukiondosha kifungo cha ndoa kwa tamko la kuvua au kwa tamko lingine lenye maana kama hiyo kwa mkabala wa mali anayoitoa mke kumlipa mumewe. Na hili bila shaka limeruhusiwa ili kumpa mwanamke uhuru wa kujiengua toka kwenye ndoa na mumewe baada ya maisha kwa upande wake kufikia ukomo wa kutoweza tena kuishi kwa raha na mumewe.

 

Dalili yake: Ni Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ ۗ وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُوا مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلَّا أَن يَخَافَا أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا افْتَدَتْ بِهِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٢٢٩﴾

Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika mlivyowapa wanawake, isipokuwa wote wawili wakikhofu kuwa hawatoweza kusimamisha mipaka ya Allaah. Mtakapokhofu kuwa wote wawili hawatoweza kusimamisha mipaka ya Allaah; basi hakuna lawama juu yao katika ambacho amejikombolea kwacho. Hiyo ni mipaka ya Allaah basi msitaadi. Na atakayetaadi mipaka ya Allaah basi hao ndio madhalimu. [Al-Baqarah: 229]

 

Ama kwenye Hadiyth ni kisa cha mke wa Thaabit bin Qays aliyekwenda kushtaki kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya mumewe, pamoja na kuwa mumewe hakuwa na tatizo la dini wala tabia bali yeye hakumpenda na akawa anakhofia kutotekeleza wajibu wake kama mke. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliwatenganisha lakini kwa kumtaka mke airejeshe shamba aliyokuwa amepewa na mumewe kama ni mahari. Hadiyth ni kama ifuatavyo:

 

عنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ اِمْرَأَةَ ثَابِتِ بْنِ قَيْسٍ أَتَتْ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! ثَابِتُ بْنُ قَيْسٍ مَا أَعِيبُ عَلَيْهِ فِي خُلُقٍ وَلَا دِينٍ، وَلَكِنِّي أَكْرَهُ اَلْكُفْرَ فِي اَلْإِسْلَامِ، قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " أَتَرُدِّينَ عَلَيْهِ حَدِيقَتَهُ؟ "، قَالَتْ: نَعَمْ. قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " اِقْبَلِ اَلْحَدِيقَةَ، وَطَلِّقْهَا تَطْلِيقَةً} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ . وَفِي رِوَايَةٍ لَهُ: {وَأَمَرَهُ بِطَلَاقِهَا}

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa) amesema kuwa: “Mke wa Thaabit bin Qays  alimuendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Thaabit bin Qays simtii kasoro katika tabia wala Dini lakini nachukia kukufuru nikiwa Muislamu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Utamrudishia shamba lake?” Akasema: Ndio. Rasuli wa Allaah akasema: (kumwambia Thaabit): “Kubali shamba lako na umuache talaka moja.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

Katika Riwaayah yake nyingine imesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamrisha ampe talaka.”

 

 

 

 

Share