Vazi Lipi Lililo Bora Mbele Ya Allaah?

 Vazi Lipi Lililo Bora Mbele Ya Allaah?

 

Imekusanywa Na: Bint Ahmadah

 

Alhidaaya.com

 

 

Amri kuu aliyopatiwa mwanamke wa Kiislamu inayomtofautisha na ndugu yake wa kiume ni kauli ya Allaah (Aliyetukuka): 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

  Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59]

 

 

Vipi kuvaa nguo leo hii imekuwa viroja kwa Waislam? Kwani wamesahau mavazi yao, leo imekuwa watafuta kila mavazi kisha tunasema yetu, kisa tumejisahau lipi lililotulazimu kwetu na lililo muhimu kwetu na kwa Rabb wetu?

 

Kwani kuiga mavazi yaliyokuwa si yetu Waislam hayajatuhusu kabisa. Lakini kwa mtizamo wa leo ndio tunakwenda na wakati. Ati kuvaa nguo kwenye magoti ndio kustaarabika kwa ulimwengu wa leo, kumbe kinyume chake ni kupotoka kimaadili. Ustaarabu wa kweli tunaotakiwa kujinasibisha nao ni ule uliokuwepo zama za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum).

 

Wanawake katika zama hizo walikuwa ni wastaarabu wa maneno, vitendo na hata mavazi. Kwani akisimuliwa Bibi Faatwimah binti wa Rasuuli-Llaah vipi alivyokuwa mstaarabu si kwa watu wake tu, bali hata kwa ndugu zake wa kike pia anawagusa. Alijichunga ulimi wake, mwili wake, mpaka vitendo vyake hadi akawa mmoja kati ya wanawake bora duniani.

 

Pia tukitizama maana ya ustaarabu ni kuelimika kutokana na kitu fulani. Je wewe mwenzangu kuvaa mavazi yasiyostahiki mbele za watu ndio kustaarabika wakati dini yetu ya Kiislam imekwisha weka mavazi yanayotakiwa yavaliwe kwa mwanamke wa Kiislam. Elimu ya Qur-aan ndio ustaarabu wetu na tunalazimika kuitekeleza. Sio kuvaa kimini wala kijinzi. Je ikiwa wewe ni mama unavaa mavazi hayo mtoto naye avae vipi? Japo kuna baadhi yao huona fakhari kumuona mtoto wao amevaa jinzi na kitopu mbele ya watu. Na huwaonyesha marafiki zake kwa ufakhari.

 

Aayah za Allaah tunazigeuza tunavyotaka sisi kwa kujitupia kitandio kichwani ukiambiwa useme si ushajisitiri. Kuna wengine wakiwa hawana vyeo huvaa vizuri tu, wakipata vyeo ndio huvua hijabu mpaka inafika wakati hata ule wa kujitupia haukai kichwani. Kwa hiyo Allaah ulimjua ulipokuwa na dhiki, wakati wa raha Hajulikani. Umesahau kwa kupata 'chako' kwenye dunia hii 'nzuri' iliyojaa starehe hatimaye ukamsahau Allaah. Je huu ndio uungwana tuliofunzwa na Uislamu? Tunashindwa na paka au mbwa anayefugwa na mwanaadamu. Paka au mbwa aliyefunzwa na akafunzika wanapoamrishwa na bwana wake hakaidi. Hata kama paka akifunzwa kukataa kula samaki asiyepikwa hatakula na atakula aliyepikwa tu.

 

Lakini wewe dada yangu unasahau kwamba kuna mafunzo maalum ya Qur-aan uliyopatiwa kuyafuata na kwamba hapa ulimwenguni umeletwa kwa lengo la kumuabudu Allaah tu. Lakini leo wasema unakwenda na wakati. Ole wako kwa kuifanya dunia ni yako kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Qur-aan tukufu:

 

 وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

Na wala usifuatilie usiyo na elimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa: 26]

 

 

Ni juu yetu kina dada wenzangu kujikamata vilivyo kwenye mafunzo sahihi ya Uislam wetu. Tusione hayaa kumrekebisha dada mwenzetu anayeporomoka kimaadili. Msimamo unahitajika kwenye kivazi hasa kwa wale wanawake wanaofanya kazi. Kibarua kisiwe ndio sababu ya kumuasi Rabb Mtukufu. Vazi la Uislam kwa mwanamke ndio heshima yake na yetu sote kwa ujumla. Shime tukamatane masikio dada zangu!

 

 

 

 

Share