026-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Qiyaam Ramadhwaan (Tarawehe)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

026-Qiyaam Ramadhwaan (Tarawehe)

 

Alhidaaya.com

 

 

· Fadhila Yake Na Kuruhusika Kwake

 

Swalaah ya Tarawehe ni Sunnah iliyokokotezwa kwa wanaume na wanawake katika mwezi wa Ramadhwaan, nayo ni moja kati ya alama mashuhuri za dini. [Raddul Mukhtaar (1/472), Haashiyatul ‘Adawiy (1/352) na Al-Majmu’u (4/31)] Na Swalaah hii ndiyo inayokusudiwa na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( من قام إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه))

((Mwenye kusimama hali ya kuwa na iymaan na kutafuta thawabu, husamehewa madhambi yake yaliyopita)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2009) na Muslim (759)].

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliiswali pamoja na Maswahaba wake katika baadhi ya masiku lakini hakuendelea nayo kwa ajili ya kuchelea isije ikafaradhishwa kwao ikawashinda. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Msikitini na watu wakaswali pamoja naye. Kisha akaswali usiku uliofuatia na watu wakakithiri zaidi. Halafu wakakusanyika usiku wa tatu lakini yeye hakutoka kuswali nao. Kulipopambazuka alisema: “Nimeona mlilolifanya, na hakuna lililonizuilia kutoka kuwajieni isipokuwa nimechelea Swalaah hii kufaradhishwa kwenu”. Na hii ni katika Ramadhwaan [Rasuli wa Allaah akafariki na hali ikabaki hivyo] [Hadiyth Swahiyh:Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1129) na Muslim (761)].

 

· Jamaa Katika Tarawehe

 

Tumeeleza katika Hadiyth ya ‘Aaishah iliyopita kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Tarawehe pamoja na Maswahaba wake katika baadhi ya masiku. Na imepokelewa toka kwa Abu Dharri akisema: “Tulifunga Ramadhwaan pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na yeye hakuswali nasi kwa chochote katika mwezi. Zilipobakia siku saba, aliswali nasi mpaka ikamalizika theluthi ya usiku, kisha katika usiku wa nne, hakuswali nasi. Na usiku uliofuatia, aliswali nasi mpaka ikamalizika takriban nusu ya usiku. Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Kwa nini Usituswalishe usiku wetu huu uliobakia ukatupatisha thawabu zaidi? Akasema:

(( إن الرجل إذا قام مع الامام حتى ينصرف حسبت له بقية ليلته ))

((Hakika mtu atakaposimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi huhisabiwa usiku uliobakia)).

Kisha usiku wa sita hakutuswalisha, lakini usiku wa saba alituswalisha. Halafu alikwenda kwa mkewe na watu wakakusanyika. Akatuswalisha mpaka tukaogopa kukosa daku”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1375), At-Tirmidhiy (806), An-Nasaaiy (3/202) na Ibn Maajah (1327)].

 

Mambo yaliendelea hivyo mpaka ilipokuja enzi ya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu). Akawakusanya watu katika Tarawehe ili waswalishwe na imamu mmoja. Katika Hadiyth ya ‘Urwah bin Az Zubayr toka kwa ‘Aaishah anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki na mambo yako hivyo, na yaliendelea hivyo hivyo katika Ukhalifa wa Abu Bakr mpaka mwanzoni mwa Ukhalifa wa ‘Umar. ‘Umar akawakusanya watu pamoja waswalishwe na Ubayya bin Ka’ab, naye akawaswalisha katika Ramadhwaan. Huo ukawa ndio mkusanyiko wa kwanza wa watu wakiswalishwa na imamu mmoja katika Ramadhwaan”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (924), An-Nasaaiy (4/155) na wengineo].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdul Rahmaan bin ‘Abdul Qaadir akisema: “Tulitoka pamoja na ‘Umar bin Al-Khattwaab katika mwezi wa Ramadhwaan kwenda Msikitini. Tukawakuta watu makundi makundi wametawanyika; huyu anaswali peke yake, na mwingine anaswali na kundi la watu linamfuata. ‘Umar akasema: Mimi naona hawa wangelikusanywa waswalishwe na imamu mmoja ingelikuwa bora zaidi. Akapitisha shauri, akawakusanya pamoja waswalishwe na Ubayya bin Ka’ab. Usiku mwingine nilitoka naye tukawakuta watu wanaswalishwa na imamu mmoja. ‘Umar akasema: “Bid-’a njema kabisa hii, na ile wanayoiacha watu wakalala ni bora zaidi kuliko ile wanayoiswali –yaani mwisho wa usiku-, na watu walikuwa wakiswali mwanzoni mwa usiku”. [Hadiyth Swahiyh:Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2010) na Maalik (252) na tamko ni lake].

 

Kisha Swalaah iliendelea kuswaliwa katika hali hii mpaka hivi leo. Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wamekubaliana kwamba inaruhusika Tarawehe kuswaliwa kwa Jamaa.

 

· Idadi Ya Rakaa Za Tarawehe

 

Tumeshaeleza kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hazidishi zaidi ya rakaa kumi na moja au kumi na tatu wakati anaposwali Qiyaamul Layl nyumbani kwake, si katika Ramadhwaan au katika miezi mingine.

 

“Ama masiku aliyoswali Tarawehe pamoja na Maswahaba wake, idadi ya rakaa haikutajwa, na hakuna Hadiyth Swahiyha inayoainisha idadi ya rakaa hizo”. [Al-Maswaabiyh Fiy Swalaat At Taraawiyh (uk 14-15) cha As-Suyuutwiy]

 

Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wametofautiana kwa kauli nyingi katika kuainisha idadi ya rakaa za Tarawehe. Kati ya kauli hizo ni:

 

1- Rakaa kumi na moja

 

(a) Kwa kuwa ndiyo idadi aliyojichagulia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe.

 

(b) As-Saaib bin Yaziyd anasema: “ ’Umar bin Al-Khattwaab alimwamuru Ubayya bin Ka’ab na Tamiym Ad Daariy wawaswalishe watu rakaa kumi na moja. Imamu alikuwa akisoma Suwrah inayozidi Aayah mia moja mpaka tukawa tunaegemea fimbo kutokana na urefu wa kisimamo, na tulikuwa hatuondoki isipokuwa mwanzoni mwa Alfajiri”. [Isnadi yake ni Swahiyh :Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik katika Al-Muwattwaa (1/115)].

 

2- Rakaa ishirini kutoa Witr

 

Hii ni kauli ya Maulamaa wengi kama Ath-Thawriy, Ibn Al-Mubaarak, Ash-Shaafi’iy na Abu Haniyfah na masahibu zake. Na hili limehadithiwa toka kwa ‘Umar, Aliyy na Maswahaba wengineo. [Sharhus Sunnat (4/120), Al-Badaai-’i (1/288), Al-Mughniy (1/208) na Al-Majmu’u (4/32-33)]

 

Dalili yao ni:

 

Yaliyokuja toka kwa As-Saaib bin Yaziyd (vile vile) akisema: “’Umar aliwakusanya watu waswalishwe na Ubayya bin Ka’ab na Tamiym Ad-Daariy kwa rakaa ishirini na moja, wanasoma Suwrah zenye Aayah zaidi ya mia moja, na wanaondoka mwanzoni mwa Alfajiri”. [Sijui kama athar hii na iliyo kabla yake moja inamtia walakini mwenzake, au zinabeba uwezekano wa kuwa ni matukio mawili tofauti]

 

Al-Kaasaaniy kasema: “ ’Umar aliwakusanya Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mwezi wa Ramadhwaan chini ya uimamu wa Ka’ab, naye akawaswalisha rakaa 20. Hakuna yeyote aliyempinga, na kwa hivyo inakuwa ni Ijma’a ya wote juu ya hilo.”

 

3- Rakaa thelathini na tisa pamoja na Witr

 

Ni kauli ya Maalik aliyesema: [Al-Mudawwanah (1/193), na Sharhu Az-Zarqaaniy (1/284)]

“Hilo kwetu ni jambo la tangu zamani”. Hoja yake ni yale yaliyopokelewa toka kwa Daawuud bin Qays anayesema: “Niliwakuta watu wakati wa enzi ya ‘Umar bin ‘Abdul ‘Azizy na Abaan bin ‘Uthmaan wanaswali rakaa thelathini na sita, na wanaswali Witr rakaa tatu.” [Hadiyth Swahiyh:Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/393) na Ibn Nasr katika Qiyaam Ramadhwaan (uk. 60)].

 

4- Rakaa arobaini na Witr rakaa saba

 

Al-Hasan bin ‘Abdullah amesema: “‘Abdul Rahmaan bin Al-Aswad alikuwa anatuswalisha katika mwezi wa Ramadhwaan rakaa arobaini na Witr rakaa saba”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/393)].

 

Pia inaelezewa kwamba Ahmad bin Hanbali alikuwa akiswali katika mwezi wa Ramadhwaan rakaa zisizo na hesabu. [Kash-Shaaful Qinaa (1/425) na Matwaalibu Ulin Nuhaa (1/563)]

 

Ninasema: “Uhakikisho ni yale aliyoyasema Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah (22/272/273):

“Na haya yote ni wasaa na ukunjufu. Idadi yoyote itakayoswaliwa kati ya hizi, inakuwa ni vizuri. Wingi wa idadi ya rakaa hutofautiana kwa mujibu wa hali ya waswaliji. Ikiwa wanaweza kuhimili kisimamo kirefu, basi kuswali rakaa kumi na rakaa tatu za baada yake kama alivyokuwa akiswali Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe katika Ramadhwaan na katika miezi mingineyo itakuwa ni bora. Na kama hawakiwezi kisimamo kirefu, basi kuswali rakaa ishirini ni bora zaidi, nazo ndizo zinazoswaliwa na Waislamu wengi, kwani idadi hii ni kati na kati baina ya kumi na arobaini. Na ikiwa ataswali rakaa arobaini na zaidi, basi itajuzu, na hakuna lolote lililo makruhu katika hilo. Maimamu wengi wamelielezea hili kama Ahmad na wengineo. Na mwenye kudhani kwamba Tarawehe ina idadi maalumu ya rakaa iliyowekwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isiyozidi wala kupungua, basi amekosea”.

 

Ninasema: “Hivi ndivyo Fiqh inavyotakikana iwe. Yako wapi haya kwa baadhi ya ndugu zetu wanaoiwacha jamaa ya Tarawehe katika “Al-Haram” na kwenda zao baada ya kuswali rakaa kumi?!! Allaah Atusamehe sote”.

 

· Mapumziko Baada Ya Kila Rakaa Nne

 

Mafuqahaa wamekubaliana kwamba inaruhusiwa kupumzika baada ya kila rakaa nne, kwani jambo hili limerithiwa toka kwa watangu wema. Wao walikuwa wakirefusha kisimamo katika Tarawehe na wanapumzika baada ya kila rakaa nne. [Fardul Mukhtaar (1/474), Haashiyatul ‘Adawiy (2/321) na Matwaalibu Ulin Nuhaa (1564)]

 

Ninasema: “Huenda asili ya hili ni kauli ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) tuliyoitaja mara kadhaa inayoelezea namna Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiswali: “Anaswali nne, basi usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha anaswali nne, basi usiulize uzuri wake na urefu wake”. Kauli hii inatuarifu kuwepo mapumziko baina ya kila rakaa nne. Katika mapumziko haya, hakuna dhikri maalumu wala dhikri nyingine za aina zozote kama wanavyofanya baadhi ya wasiojua.”

 

· Je, Qur-aan Hukhitimishwa Katika Tarawehe?

 

Hakuna Sunnah yoyote iliyopokelewa toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba ameainisha mpaka wa kisomo katika Tarawehe, bali kisomo hutofautiana kwa mujibu wa hali ilivyo. Imamu atasoma kiasi cha kutowakimbiza watu wakaikacha jamaa. Na lau kama watu wataridhika wenyewe kurefushwa kisomo, basi ni bora kutokana na athar zilizotangulia.

 

Hanafiy na Hanbali wanapendelea Qur-aan Tukufu ikhitimishwe katika mwezi mzima ili watu waisikilize Qur-aan yote katika Swalaah hiyo. [Fat-hul Qadiyr (1/335), Al-Badai’i (1/289) na Al-Mughniy (2/169)]

 

· Kuswali Na Imamu Hadi Mwisho

 

Anayeswali nyuma ya imamu, anatakikana asimwache njiani bali akamilishe naye mpaka mwisho. Katika Hadiyth ya Abu Dharri, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Mwenye kuswali na imamu mpaka akamaliza, huandikiwa thawabu za Qiyaamul Layl)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah].

 

Ikiwa imamu ataswali Witr mwishoni mwa Swalaah, ataswali naye hata kama niya yake ni kuja kuswali Qiyaamul Layl, hili haliharibu kitu kama tulivyotangulia kusema. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

 

Share