034-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sijdah Ya Kisomo

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

034-Sijdah Ya Kisomo

 

Alhidaaya.com

 

 

· Taarifu Yake:

 

Sijdah ya kisomo ni sijdah ambayo mtu husujudu kwa kusoma au kusikia Aayah ya Qur-aan Tukufu kati ya Aayah za sijdah.

 

· Fadhila Yake:

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwanadamu anaposoma Aayah ya sijdah akasujudu, shaytwaan hujitenga kando akilia huku akisema: Ee maangamivu yangu! Ameamuriwa kusujudu akasujudu, naye ataipata Pepo, nami niliamuriwa kusujudu nikakataa, nami nitaupata moto)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (81), Ibn Maajah (1052) na Ahmad (9336)].

Kuna Hadiyth nyingi zilizothibiti zinazozungumzia kiujumla kuhusiana na fadhila za sijdah hii. Kati ya hizo ni:

 

- Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusiana na kufufuliwa na shifaa isemayo: ((Mpaka Atakapotaka Allaah rahma kwa Awatakao kati ya watu wa motoni, Atawaamuru Malaika wawatoe wale waliokuwa wakimwabudu Allaah. Watawatoa na watawajua kutokana na athari za sijdah, kwani Allaah Ameuharamishia moto kuila athari ya sijdah. Watatoka motoni, na mwili wote wa mwanadamu utaliwa na moto isipokuwa athari ya sijdah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (806) na Muslim (182)].

 

- Hadiyth ya Thawbaan mwachwa huru wa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambapo alimuuliza Nabiy kuhusu amali ambayo Allaah Atamwingiza kwayo Peponi. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Jilazimishe kukithirisha sijdah, kwani wewe hupati kusujudu sijdah moja kwa ajili ya Allaah, isipokuwa Allaah Hukunyanyulia kwayo daraja moja na Hukupomoshea kwayo kosa moja)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (488), At-Tirmidhiy (388), An-Nasaaiy (2/238) na Ibn Maajah (1423)].

 

- Hadiyth ya Rabiy’ah bin Ka’ab Al-Aslamiy ya kwamba alimwomba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awe pamoja naye peponi, Nabiy akamwambia: ((Jisaidie mwenyewe kwa kukithirisha sijdah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (489), Abu Daawuud (1320), An-Nasaaiy (2/227) na Ahmad (4/59)].

 

· Hukmu Yake:

 

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa sijdah ya kisomo ipo kisharia kutokana na Aayah na Hadiyth zinazolizungumzia jambo hilo kama Hadiyth ya Ibn ‘Umar asemaye: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitusomea Suwrah yenye Aayah ya sijdah, kisha yeye husujudu nasi tunasujudu pamoja naye mpaka mmoja wetu anakosa sehemu ya kuweka paji lake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1075) na Muslim (575)].

 

Kisha Maulamaa hao wamekhitalifiana kuhusiana na wajibu wake juu ya kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Ni wajibu. Hii ni kauli ya Ath-Thawriy, Abu Haniyfah, riwaya toka kwa Ahmad na chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah. [Fat-hul Qadiyr (1/382), Ibn ‘Aabidiyn (2/103), Majmu’u Al-Fataawaa (23/139-155) na Al-Inswaaf (2/193)]

 

Ya  pili:

 

Ni Sunnah, na si wajibu. Ni kauli ya Jamhuri; Maalik, Ash-Shaafi’iy, Al-Awzaa’iy, Al-Layth, Ahmad, Is-Haaq, Abu Thawr, Daawuud na Ibn Hazm. Pia katika Maswahaba ni pamoja na ‘Umar bin Al-Khattwaab, Salmaan, Ibn ‘Abbaas, na ‘Imraan bin Haswiyn. [Al-Majmu’u (4/61), Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/445), Al-Mawaahib (2/60), At-Tamhiyd (19/133) na Al-Muhallaa (5/105)]

 

Wenye kusema ni wajibu wameleta hoja zifuatazo:

 

1- Kauli Yake Ta’alaa:

((فَمَا لَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ وَإِذَا قُرِئَ عَلَيْهِمُ الْقُرْآنُ لَا يَسْجُدُونَ))

(( Basi wana nini hawaamini? ●  Na wanaposomewa Qur-aan, hawasujudu)). [Al-Inshiqaaq (84:20 na 21)].

 

Wanasema kwamba mtu halaumiwi isipokuwa kwa kuacha la wajibu.

 

2- Kauli Yake Ta’alaa:

((فَاسْجُدُوا لِلَّـهِ وَاعْبُدُوا))

((Basi msujudieni Allaah na mwabuduni Yeye)). [An-Najm 53:62)]

 

3- Kauli Yake Ta’alaa:

((كَلَّا لَا تُطِعْهُ وَاسْجُدْ وَاقْتَرِب))

(( Laa hasha! Usimtii; na sujudu na kurubia (kwa Allaah) )). [Al-‘Alaq (96:19)].

 

Wanasema kuwa agizo katika aya mbili ni la wajibu.

 

4- Yaliyomo kwenye Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyopita: ((Mwanadamu ameamuriwa kusujudu akasujudu, naye ataipata Pepo)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo katika mlango huu].

 

5- Kauli ya ‘Uthmaan: “Hakika sijdah ni wajibu kwa mwenye kusikiliza”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (4220), ‘Abdul Razzaaq (5906) na Al-Bayhaqiy (2/324)].

 

Jamhuri wamewajibu:

 

1- Kulaumiwa katika Aayah ya Suwrat Al-Inshiqaaq kunafungamana na kuacha sijdah kwa kugomea na kibr. Hivyo kunamgusa mwenye kuacha ambaye haamini fadhila yake wala uwepo wake.

 

2- Kutoa dalili kwa Aayah mbili za mwisho kutazingatiwa ikiwa agizo kwenye Aayah hizo ni la wajibu, na makusudio ya sijdah yawe ni sijdah ya kisomo, na yote mawili hayaingii hapo. [Tuhfat Al-Ahwadhiy (3/172)]

 

Ninasema: “Imepokelewa toka kwa Zayd bin Thaabit akisema: “Nilimsomea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Wan-Najm”, naye hakusujudu.” Na katika riwaya nyingine: “Hakusujudu yeyote kati yetu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1072) na Muslim (577)].

 

“Agizo katika Aayah mbili za mwisho linachukuliwa ima ni la Sunnah, au muradi wake ni sijdah ya Swalaah, au ni la wajibu katika Swalaah ya faradhi, au kwa mujibu wa qaaidah ya Ash-Shaafi’iy ni Sunnah kwa kuzingatia maana zake mbili kwa pamoja”. [Fat-hul-Baariy (2/648) kwa mfanowe]

 

3- Imehadithiwa kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab alisoma siku ya ijumaa juu ya mimbari Suwrat An-Nahl. Alipofika Aayah ya sijdah, aliteremka akasujudu na watu nao wakasujudu. Ijumaa iliyofuatia, aliisoma sura hiyo hiyo na alipofika Aayah ya sijdah alisema: “Enyi watu! Hakika sisi tunaipita sijdah, mwenye kusujudu basi kafanya la sawa, na asiyesujudu, basi hana makosa”. Na ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) hakusujudu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1077)].

 

Aliyasema hayo mbele ya hadhira ya Maswahaba, na hakuna yeyote aliyepinga, na ikawa ni Ijma’a kwao wote.

 

Ninasema: “Sheikh wa Uislamu ana minakasha ya kuzijadili dalili za Jamhuri ya Maulamaa na anayependa anaweza kuipitia. Lililo sahihi zaidi ni kauli ya Jamhuri. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Inavyofanyika:

 

1- Mafuqahaa wamekubaliana kwamba sijdah ya kisomo ni sijdah moja tu.

 

2- Sijdah inakuwa kwa muundo ule ule wa sijdah ya Swalaah kwa kuweka chini mikono miwili, magoti mawili, miguu miwili, pua na paji la uso. Pia, kwa kuweka mbali vifundo vya mikono na mbavu, na tumbo na mapaja mawili, mbali na kuelekeza vidole Qibla na mengineyo yaliyotangulia.

 

3- Kwa mujibu wa kauli iliyo sahihi zaidi, haikatazwi kupiga takbiyr ya kuhirimia wala kutoa tasliym. Sheikh wa Uislamu amesema katika Al-Fataawaa (23/165): “Hii ndio Sunnah ijulikanayo toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Masalaf wote wameishika, na Maimamu mashuhuri wameielezea”.

 

Ninasema: “Ibn ‘Abdul Barri katika At-Tamhiyd (19/134) amenukuu toka kwa Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Abu Haniyfah wakisema kwamba tasliym hakuna. Kisha akasema (23/166): Lililohadithiwa kuhusiana na hilo toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni takbiyr moja, kwani mtu haguri kutoka ‘ibaadah moja kwenda nyingine”.

 

Ninasema: “Anaashiria Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitusomea Qur-aan. Akipita Aayah ya sijdah hupiga takbiyr na husujudu sijdah mbili”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1413), Al-Bayhaqiy (2/325) na ‘Abdul Razzaaaq (5911). Angalia Al-Irwaa (472)].

 

Lakini, dalili ya kujuzu kupiga takbiyr wakati wa kusujudu na kunyanyuka toka kwenye sijdah inaweza kupatikana kwenye Hadiyth ya Waail bin Hujr aliyesema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akinyanyua mikono yake miwili pamoja na takbiyr, na hupiga takbiyr kila anapokwenda chini na kila anaponyanyuka. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (4/316), Ad-daaramiy (1252) na At-Twayaalsiy (1021). Angalia Al-Irwaa (2/36)].

 

Jamhuri wanaona ni vyema kupiga takbiyr wakati wa kusujudu na kunyanyuka toka kwenye sijdah.

 

Ninasema: “Inajuzu kunyanyua mikono miwili pamoja na takbiyr vile vile. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

4- Mwenye kutaka kusujudu sijdah ya kisomo naye hayuko kwenye Swalaah, ni bora zaidi kwake asimame kwanza, kisha apomoke kwenda kwenye sijdah. Hii ni kauli ya Mahanbali, baadhi ya Mahanafi waliofuatia, inakubalika kwa Ash-Shaafi’iy, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Al-Badaai-’i (1/192), Matwaalib Ulin Nuhaa (1/586) na Majmu’u Al-Fataawaa (23/173)]

 

Wamesema: الخرور “Al-Khuruwr” ni kuporomoka toka kwenye kisimamo. Allaah Amesema:

(( قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا ۚ إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا ))

(( Sema: “Iaminini au msiamini. Hakika wale waliopewa elimu kabla yake wanaposomewa (Qur-aan) wanaporomoka kifudifudi wanasujudu”)). [Al-Israa (17:107)]

 

Na ikiwa hakufanya na akasujudu bila kusimama, basi hakuna ubaya. Ash-Shaafi’iy na wafuasi wake wengi wanasema kwamba hakuna chochote kinachotegemewa chenye kuthibitisha kusimama huko, bali ni bora kuacha. [Al-Majmu’u (4/65)]

 

· Je, Ni Sharti Kuwa Twahara Na Kuelekea Qiblah Kwa Ajili Ya Sijdah Ya Kisomo?

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba yenye kushurutishwa kwenye Swalaah, hushurutishwa vile vile kwenye sijdah ya kisomo. Wanasema ni lazima mtu awe twahara, aelekee Qiblah pamoja na masharti mengineyo. [Ibn ‘Aabidiyn (2/106), Ad-Dusuwqiy (1/307), Al-Majmu’u (4/63) na Al-Mughniy (1/650)]

 

Lakini Ibn Hazm na Sheikh wa Uislamu hawakushurutisha hayo kwa kuwa sijdah si Swalaah, bali ni ‘ibaadah. Ni maarufu kwamba kiini cha ‘ibaadah yenyewe haishurutishiwi twahara. Ni kauli ya Ibn ‘Umar, Ash-Shu’abiy na Al-Bukhaariy, nayo ndiyo sahihi.

Linaloonyesha hilo ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas asemaye kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisujudu aliposoma An-Najm, akasujudu, na wakasujudu pamoja naye Waislamu, washirikina, majini na watu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1071) na At-Tirmidhiy (575)].

 

Al-Bukhaariy amesema kwenye Fat-h (2/644): “Mshirikina ni najisi, hana wudhuu”.

Ash-Shawkaaniy amesema: “Katika Hadiyth zenye kuzungumzia kuhusu sijdah za kisomo, hakuna chochote chenye kuonyesha kwamba mwenye kusujudu ni lazima awe na wudhuu. Waliokuwepo kwenye kisomo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakisujudu pamoja naye, na wala haikunukuliwa kwamba alimwamuru yeyote kati yao kutawadha, na haiwezekani wawe wote na wudhuu. Aidha, washirikina walikuwa wakisujudu pamoja na Nabiy kama ilivyotangulia, nao ni najisi na wudhuu wao haufai. Ama kusitiri uchi na kuelekea Qiblah pamoja na kuweza, hilo limesemwa kuwa linazingatiwa kwa itifaki”. [Naylul Awtwaar (3/125) chapa ya Al-Hadiyth]

 

Ninasema: “Madhali sijdah si Swalaah, basi si lazima kuelekea Qiblah kama walivyosema Ibn Hazm na Ibn Taymiyah. Lakini hakuna shaka ya kwamba kusujudu mtu akiwa na twahara na akaelekea Qiblah, inakuwa ni bora na ukamilifu zaidi, na haitakikani kuliacha hilo bila ya udhuru. Ama kushurutisha, hilo halitakikani na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Namna Anavyosujudu Mtembeaji Kwa Miguu Na Aliye Kwenye Kipando

 

Anayesoma au anayesikia Aayah ya sajdah na akawa anatembea kwa miguu au yuko kwenye kipando, kisha akataka kusujudu, basi huyo ataashiria kwa kichwa chake upande wowote ule. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar ya kwamba aliulizwa kuhusiana na sijdah mtu akiwa juu ya mnyama akajibu akisema: “Sujudu na ashiria”. Hili limesimuliwa na Ibn Abi Shaybah (4210) kwa Sanad Swahiyh. Kundi la Masalafi katika masahibu wa Ibn Mas-’oud na wengineo wamepitisha kwa njia sahihi kwamba mtembeaji huashiria kwa kichwa.

 

· Yasemwayo Kwenye Sijdah Ya Kisomo

 

1- Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) akisema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema mara nyingi katika sijdah za Qur-aan usiku: ((Sajada wajhiy lil-ladhiy Khalaqahu wa Swawwarahu wa Shaqqa sam-’ahu wa baswarahu bihawlihi wa quwwatihi)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1414), At-Tirmidhiy (580) na An-Nasaaiy (2/222). Kuna mvutano kuhusu Sanad yake, nayo kwa hali zote ni Dhwa’iyf. Angalia Fat-hur Rahmaan cha Sheikh wetu Abu ‘Umayr uk. 99. Ninasema: “Kuna Hadiyth mwenza Marfu’u Swahiyh iliyopokelewa toka kwa ‘Aliy kuhusiana na sijdah za Swalaah ambayo imesimuliwa na Muslim”]

 

2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Alikuja mtu mmoja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ee Nabiy wa Allaah! Nilipolala usiku, nilijiona kana kwamba naswali nyuma ya mti, kisha nikasujudu na mti nao ukasujudu kama nilivyosujudu, halafu nikausikia ukisema: Ee Allaah! Niandikie kwayo Kwako thawabu, na Uniondoshee kwayo makosa, na Uniwekee Kwako akiba, na Uitakabalie kwangu kama Ulivyoitakabali kutoka kwa Mja Wako Daawuud”. Ibn ‘Abbaas anaendelea kusema: “Hapo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasoma Aaya ya sajdah akasujudu, kisha nikamsikia anasema mfano wa aliyomwelezea mtu yule kuhusiana na matamshi ya mti”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (5790), Ibn Maajah (1053) na wengineo. Ina Hadiyth mwenza ambayo haiiongezei hii ila udhwa’iyf zaidi. Lakini pamoja na hivyo, Sheikh Abul Ashbaal (Rahimahul Laahu) amesema kwamba ni Hadiyth Swahiyh. Angalia Fat-hur Rahmaan uk. 100]

 

Ninasema: “Hadiyth hizi mbili ni Dhwa’iyf kwa mujibu wa kauli yenye nguvu zaidi. Kuhusu Hadiyth ya kwanza, ipo Hadiyth nyingine mwenza inayohusiana na sijdah za Swalaah. Imam Ahmad ameashiria kutothibiti hilo aliposema: “Ama mimi, nitasema: Subhaana Rabbiyal A’alaa”. Ikiwa mambo ni hivi, basi adhkaari za sijdah ya kisomo zitakuwa ni zile tulizozitaja nyuma katika sijdah ya Swalaah. Kati ya hizo, ni zile za Bibi ‘Aaishah zilizotajwa nyuma kidogo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

·Ni Nani Mlengwa Wa Hukmu Ya Sijdah Ya Kisomo?

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba hukmu ya sijdah ya kisomo inamkusudia msomaji wa Aayah yoyote ya sijdah sawasawa akiwa ndani ya Swalaah au nje ya Swalaah. Halafu wakakhitalifiana kuhusiana na msikiaji, je itampasa kusujudu au la? Wamekhitalifiana juu ya kauli mbili: [Al-Badaai-’i (1/192), Ad-Dusuwqiy (1/307), Bidaayatul Mujtahid (1/329) Al-Majmu’u (4/72) na Matwaalib Ulin Nuhaa (1/582)]

 

Ya kwanza:

 

Atasujudu tu hata kama msomaji hakusujudu. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Maalik.

 

Ya pili:

 

Hatosujudu isipokuwa tu kama atakusudia kusikiliza na msomaji ambaye anafaa kuwa imamu akasujudu. Ni kauli ya Ahmad na riwaya toka kwa Ahmad. Hoja zao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliposema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitusomea Suwrah yenye Aaya ya sajdah, akasujudu nasi tukasujudu mpaka baadhi yetu wakakosa sehemu ya kuweka paji la uso”. [Hadiyth Swahiyh: Imeshatajwa kwenye mlango wa hukmu ya sijdah ya kisomo].

 

2- Yaliyosimuliwa ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliambiwa: “Fulani alisoma kwako Aayah ya sajdah ukasujudu, nami nimesoma kwako hukusujudu?” Akasema: ((Wewe ulikuwa imamu, na lau ungelisujudu, nasi pia tungesujudu)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi’iy katika Musnadi yake (359) na Al-Bayhaqiy amepokea toka kwake (2/324). Angalia Al-Irwaa (473)].

 

3- Ibn Mas-’oud alimwambia Tamiym bin Hadhlam – naye ni kijana mdogo- aliposoma Aayah ya sijdah: “Sujudu, wewe ndiye imamu wetu hapo”. [Hadiyth Hasan kwa Sanad zake: Al-Bukhaary ameifanya Hadiyth Mu’allaq (2/648). Na Sa’iyd bin Mansour pamoja na Al-Bukhaariy kwenye At-Taariykhul Kabiyr, wameifanya kuwa Hadiyth Mawswuwl kama ilivyo kwenye At-Taghliyq (2/210). Ina Hadiyth mwenza kwa Al-Bayhaqiy na ‘Abdul Razzaaq ambayo Sheikh wetu amesema kuwa ni Hadiyth Hasan kwenye Fat-hur Rahmaan uk 114]

Hoja hizi zote zinaonyesha kwamba ni Sunnah kwa msikilizaji asujudu kama msomaji atasujudu, na kama hakusujudu, basi haki ya yeye kusujudu haina nguvu ingawa itakuwa bora kusujudu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Sijdah Ya Kisomo Katika Nyakati Zisizoruhusiwa Kuswali

 

Sijdah ya kisomo inajuzu katika nyakati zisizoruhusiwa kuswali bila ukaraha kwa mujibu wa kauli yenye nguvu zaidi. Tushaeleza nyuma kuwa sijdah si Swalaah, na kwamba Hadiyth zinazozungumzia umarufuku zinahusiana na Swalaah pekee. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad. Ibn Hazm kayasema haya haya. [Al-Mughniy (1/623), Al-Muhallaa (5/105) na Bidaayatul Mujtahid (1/328)]

Imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar akisema kwamba ni karaha lakini Sanad yake ni Dhwa’iyf. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Kukariri Kisomo Au Kuisikia Aayah Ya Sajdah Zaidi Ya Mara Moja

 

Kama akisoma, au akaisikiliza Aayah ya sajdah zaidi ya mara moja, anaweza kuakhirisha sijdah akaja kusujudu mara moja tu. Ikiwa atasujudu, kisha akasoma tena Aayah ya sijdah, basi itakuwa bora zaidi kwake asujudu mara nyingine tena. Na hii ni kauli ya Jamhuri kinyume na Abu Haniyfah. [Fat-hul Qadiyr (2/22), Ad-Dusuwqiy (1/311), Mughnil Muhtaaj (1/446) na Al-Inswaaf (2/196)]

 

· Kupitwa Na Sijdah Ya Kisomo

 

Imesuniwa kwa msomaji na msikilizaji kusujudu moja kwa moja baada ya Aayah ya sajdah hata kama watachelewa kidogo. Lakini kitambo kikirefuka kati ya sajdah na sababu yake, basi hawatosujudu kwa kuwa mahala pake pashapita. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali. [Al-Majmu’u (4/71-72) na Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/445)]

 

· Sijdah Ya Kisomo Ndani Ya Swalaah

 

Imepokelewa toka kwa Abu Raafi’i akisema: “Niliswali pamoja na Abu Hurayrah Swalaah ya ‘Ishaa akasoma إذا السماء انشقت kisha akasujudu. Nikamwambia: Unafanya nini hivi? Akasema: Nilisujudu kwa Aayah hii nyuma ya Abul Qaasim (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nami nitaendelea kusujudu kwayo mpaka nikutane naye”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (766) na Muslim (578)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “’Umar alisujudu kwenye “An-Najm” akasimama, kisha akaiunganishia Suwrah”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5880) na At-Twahaawiy (1/355)].

 

Katika matukio haya mawili, inaonyesha kwamba imesuniwa kusujudu kwa anayesoma Aayah ya sijdah katika Swalaah yake bila ya kubagua kati ya Swalaah ya Faradhi au ya Sunnah, ni sawa akiwa peke yake au katika Jamaa, au Swalaah ya kimya au ya sauti. Hii ndiyo kauli ya Jamhuri. [Al-Badaai-’i (1/192), Kash-Shaaful Qinaa (1/449) na Mawaahibul Jaliyl (2/65)]

 

Lakini kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri, ni karaha kwa imamu kuisoma katika Swalaah ya kimya ili asije kuwakanganya maamuma. Ash-Shaafi’iy anasema si karaha, bali imesuniwa aikawize sajdah mpaka atakapoimaliza Swalaah ili asiwakanganye maamuma kwa sharti kwamba kitambo kisirefuke.  [Al-Majmu’u (4/72) na Nihaayatul Muhtaaj (2/95)]

 

· Je, Inajuzu Kuiruka Aayah Ya Sijdah Katika Swalaah?

 

Ni makruhu kwa mwenye kuswali kusoma Aayah nyinginezo na kuiruka Aayah ya sajdah ili asipate kusujudu. Hili limenukuliwa toka kwa kundi la Masalafi kama Ash-Sha’abiy, Ibn Al-Musayyib, Ibn Siyriyn, An-Nakh’iy na Is-Haaq. Jamhuri ya Maulamaa wamelikirihisha hili pia, nalo huitwa: “Katiza sajdah”. [Al-Badaai-’i (1/192), Kash-Shaaful Qinaa (1/449) na Ad-Dusuwqiy (1/309)]

 

· Faida

 

Imekirihishwa vile vile mtu kuzikusanya Aayah za sijdah, halafu akazisoma na kusujudu. [Al-Kaafiy cha Ibn Qudaamah (1/160), Al-Mudawwanah (1/111-112) na Rawdhwat At Twaalibiyna (1/323)]

 

· Ikiwa Sijdah Ni Mwisho Wa Suwrah, Atafanya nini?

 

Ikiwa Aayah ya sijdah iko mwisho wa Suwrah, mtu atachaguzwa kati ya mambo matatu:

 

1- Asujudu kisha asimame, halafu aiunganishe na Suwrah nyingine kisha arukuuu. Hili alilifanya ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu). Alisoma Suwrat Yuwsuf katika Swalaah ya Alfajiri, akarukuu, kisha katika rakaa ya pili akasoma Suwrat An-Najm akasujudu, halafu akasoma إذا السماء انشقت . [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (2882) na At-Twahaawiy (1/355)]..

Na hili ndilo bora zaidi.

 

2- Arukuu, na rukuu itamtosheleza na sajdah.

 

(a) Imepokelewa toka kwa Naafi’i kwamba Ibn ‘Umar alikuwa anasujudu anapoisoma An Najm katika Swalaah, na kama hakusujudu hurukuu. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5893).

 

(b) Ibn Mas-’oud aliulizwa kama mtu atarukuu au atasujudu kwenye Suwrah inayoishilia na Aayah ya sajdah akasema: “Kama hakuna kati yako na kati ya sajdah isipokuwa kurukuu, basi ndiyo iliyo karibu”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Shaybah (4371)

 

Ninasema: “Mahala pa hili ikiwa mtu anaswali peke yake, au akawa ni imamu na akajua kwamba hatowakanganya maamuma. Kama atahofia kuwakanganya, baadhi yao wakasujudu na wengine wakarukuu, basi asifanye hilo. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

3- Asujudu, kisha apige takbiyr asimame, halafu arukuu bila ya kusoma Suwrah nyingine.

 

· Akisoma Aayah Ya Sajdah Juu Ya Mimbari

 

[Al-Kaafiy cha Ibn Qudaamah (1/160), Al-Mudawwanah (1/111-112) na Rawdhwat At Twaalibiyna (1/323)]

 

Akipenda anaweza kuteremka akasujudu chini na watu watasujudu pamoja naye, na kama hakusujudu, basi hakuna ubaya kutokana na kitendo cha ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu). [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa katika mlango wa hukmu za sijdah].

 

Na lau kama ataweza kusujudu juu ya mimbari, basi atasujudu hapo hapo, na watu watasujudu pamoja naye. Na ikiwa khatibu hakusujudu, maamuma hawaruhusiki kusujudu.

 

·       

Mwahala Pa Kusujudu (Aayah za sajdah)

 

Mwahala (Aayah) pa kusujudu ni 15 katika Qur-aan Tukufu. Hili limeelezewa katika Hadiyth Marfu’u lakini Dhwa’iyf toka kwa ‘Amri bin Al-‘Aaswiy ya kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsomea Aayah 15 za sijdah katika Qur-aan, tatu katika hizo zipo katika Suwrah fupi (Mufasswal), na mbili katika Suwrat Al-Hajj. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1401), Ibn Maajah (1057), Al-Haakim (1/223) na Al-Bayhaqiy (2/214)].

 

Kati ya Aayah hizi 15, zipo kumi kati yake ambazo Maulamaa wamezipitisha bila hitilafu yoyote, na zipo nne ambazo Maulamaa wamehitalifiana ingawa zimeelezewa katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh, na kuna Aayah moja ambayo haikuthibitishwa kwa Hadiyth Swahiyh lakini baadhi ya Maswahaba walikuwa wakisujudu wanapoisoma jambo ambalo linatutuza nyoyo juu ya uhalali wake.

 

(a) Aayah Za Sijdah Ambazo Maulamaa Hawakukhitilafiana

 

[Sharhul Ma’aaniy cha At-Twahaawiy (1/359), At-Tamhiyd (19/131) na Al-Muhalla (5/105)]

 

1- Al-A’araaf katika Neno Lake Ta’alaa:

((إِنَّ الَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيُسَبِّحُونَهُ وَلَهُ يَسْجُدُونَ))

[Aayah 206]

 

2- Ar-Ra’ad katika Neno Lake Ta’alaa:

(( وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ))

[Aayah 15]

 

3- An-Nahl katika Neno Lake Ta’alaa:

(( وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مِن دَابَّةٍ وَالْمَلَائِكَةُ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ • يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ))

[Aayah 49 na 50]

 

Imethibiti kwamba ‘Umar aliisoma juu ya mimbari siku ya ijumaa, kisha akateremka akasujudu. [Hadiyth Swahiyh: Tumeielezea kwenye mlango wa Hukmu ya kusujudu].

 

4- Al-Israa katika Neno Lake Ta’alaa:

(( قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا ۚ إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا • وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِن كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولًا • وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا))

[Aayah 107-109 ]

 

5- Maryam katika Neno Lake Ta’alaa:

((أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ مِن ذُرِّيَّةِ آدَمَ وَمِمَّنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ وَمِن ذُرِّيَّةِ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْرَائِيلَ وَمِمَّنْ هَدَيْنَا وَاجْتَبَيْنَا ۚ إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُ الرَّحْمَـٰنِ خَرُّوا سُجَّدًا وَبُكِيًّا))

[Aayah 58]

 

6- Al Hajji katika Neno Lake Ta’alaa:

((أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ ۖ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ ۗ وَمَن يُهِنِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّكْرِمٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ))

[Aayah 18]

 

7- Al-Furqaan katika Neno Lake Ta’alaa:

((وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اسْجُدُوا لِلرَّحْمَـٰنِ قَالُوا وَمَا الرَّحْمَـٰنُ أَنَسْجُدُ لِمَا تَأْمُرُنَا وَزَادَهُمْ نُفُورًا))

[Aayah 60]

 

8- An-Naml katika Neno Lake Ta’alaa:

((أَلَّا يَسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي يُخْرِجُ الْخَبْءَ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُخْفُونَ وَمَا تُعْلِنُونَ • اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ))

[Aayah 25 na 26]

 

9- As-Sajdah katika Neno Lake Ta’alaa:

((إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ))

[Aayah 15]

 

10- Fusswilat katika Neno Lake Ta’alaa:

((وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ • فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا فَالَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ يُسَبِّحُونَ لَهُ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُمْ لَا يَسْأَمُونَ))

[Aayah 37 na 38]

 

(b) Aayah ambazo Maulamaa wamekhitalifiana kusujudu zinaposomwa na ambazo dalili za uthibitisho wake ni swahiyh

 

11- Swaad katika Neno Lake Ta’alaa:

((قَالَ لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِ ۖ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْخُلَطَاءِ لَيَبْغِي بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَقَلِيلٌ مَّا هُمْ ۗ وَظَنَّ دَاوُودُ أَنَّمَا فَتَنَّاهُ فَاسْتَغْفَرَ رَبَّهُ وَخَرَّ رَاكِعًا وَأَنَابَ ))

[Aayah 24]

Wanaosujudu wakiisoma Aayah hii ni Abu Haniyfah, Ath-Thawriy, Ahmad, Is-Haaq na Abu Thawr. [At-Tamhiyd (19/131), Al-Badaai-’i (1/193), Ad-Dusuwqiy (1/308), Al-Majmu’u (4/60) na Al-Mughniy (1/618)].

 

Dalili yao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Swaad si katika mahala palipothibiti na kukokotezewa kusujudu, lakini mimi nilimwona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisujudu hapo”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1069), Abu Daawuud (1409) na At-Tirmidhiy (577)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Mujaahid –kuhusiana na sijdah ya Swaad – akisema: “Nilimuuliza Ibn ‘Abbaas: Ni wapi ilisujudiwa? Akasema: Je, hukusoma:

(( وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ كُلاًّ هَدَيْنَا وَنُوحاً هَدَيْنَا مِن قَبْلُ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَى وَهَارُونَ وَكَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ • وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَى وَعِيسَى وَإِلْيَاسَ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ • وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطاً وَكُلاًّ فَضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ • وَمِنْ ءابَائِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ وَإِخْوانِهِمْ وَاجْتَبَيْنَاهُمْ وَهَدَيْنَاهُمْ إِلَى صِراطٍ مُّسْتَقِيمٍ• ذلِكَ هُدَى اللَّهِ يَهْدِى بِهِ مَن يَشَآءُ مِنْ عِبَادِهِ وَلَوْ أَشْرَكُواْ لَحَبِطَ عَنْهُمْ مَّا كَانُواْ يَعْمَلُونَ • أُوْلَـئِكَ الَّذِينَ ءَاتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ فَإِن يَكْفُرْ بِهَا هَـؤُلاءِ فَقَدْ وَكَّلْنَا بِهَا قَوْماً لَّيْسُواْ بِهَا بِكَافِرِينَ • أُوْلَـئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّهُ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ قُل لاَّ أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْراً إِنْ هُوَ إِلاَّ ذِكْرَى لِلْعَالَمِينَ))

 Na Daawud amekuwa ni katika wale ambao Nabiy wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuriwa kumfuata, naye alisujudu hapo, na Nabiy wa Allaah alisujudu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4807), Ahmad (3215) na Al-Bayhaqiy (2/319)].

 

3- Imepokelewa na Mujaahid ya kwamba alimuuliza Ibn ‘Abbaas: “Je, ipo sajdah kwenye Swaad? Akajibu: “Ndio, kisha akasoma ووهبنا mpaka akafikia فبهداهم اقتده . Akasema: Yeye ni miongoni mwao. Na Ibn ‘Abbaas akasema: Nilimwona ‘Umar akisoma Swaad juu ya mimbari, akateremka na kusujudu hapo, kisha akapanda tena mimbari”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (4267), ‘Abdul Razzaaq (5864) na Al-Bayhaqiy (2/319)].

 

4- Imepokelewa na As-Saaib bin Yaziyd akisema: “Nilimwona ‘Uthmaan akisujudu katika Swaad”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (4257), ‘Abdul Razzaaq (5864) na Al-Bayhaqiy (2/319)].

 

· Sajdah Tatu Za Suwrah Fupi (Al-Mufasswal)

 

Hizi ni Aayah tatu za kusujudu kwa Abu Haniyfah, Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [At-Tamhiyd (19/131), Al-Badaai-’i (1/193), Al-Majmu’u (4/62) na Al-Mughniy (1/617)]

 

12- An-Najm Aayah ya 62:

((فَاسْجُدُوا لِلَّـهِ وَاعْبُدُوا))

Dalili ya kuthibiti hili ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Mas-’oud ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Suwrat An-Najm akasujudu, na hakubaki yeyote katika watu ila alisujudu”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1070) na Muslim (576)].

Hadiyth kama hii iliyopokelewa na Ibn ‘Abbaas tushaitaja nyuma.

 

2- Kitendo cha ‘Umar cha kusujudu kwenye Suwrah hiyo kama ilivyoelezewa nyuma, na Sanad yake ni Swahiyh.

 

· Faida:

 

Kadhalika, imethibiti kuachwa sajdah kwenye Suwrah hiyo. Imepokelewa toka kwa Zayd bin Thaabit ya kwamba alimsomea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) An-Najm lakini hakusujudu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1072) na Muslim (577)].

 

13- Al-Inshiqaaq Aayah 20 na 21:

((وَإِذَا قُرِئَ عَلَيْهِمُ الْقُرْآنُ لَا يَسْجُدُونَ • بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا يُكَذِّبُونَ)) 

Dalili ni:

 

1- Ni kusujudu Abu Hurayrah hapo na kauli yake: “Nilisujudu kwa Aayah hii nyuma ya Abul Qaasim (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na nitaendelea kusujudu ikisomwa mpaka nitakapokutana naye”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (766) na Muslim (578)]

 

2- Pia kasema: “Abu Bakr na ‘Umar walisujudu katika إذا السماء انشقت naإ قرأ باسم ربك الذي خلق , na ni nani aliye bora zaidi kuliko wao?” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (1037), At-Twayaalisiy (2499) na Abul Razzaaq ( 5886)].

 

3- Imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Umar, Ibn Mas-’oud na ‘Ammaar. [Angalia athari zilizopokelewa toka kwao katika “Fat-h Ar-Rahmaan Biahkaami Wa Mawaadhi’i Sujuudil Qur-aan” cha Sheikh wetu Abu ‘Umayr (Allaah Amhifadhi) (69,70)]

 

14- Al-‘Alaq Aayah ya 19:

((كَلَّا لَا تُطِعْهُ وَاسْجُدْ وَاقْتَرِب))

Imetangulia kabla yake Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kuthibiti hilo toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr na ‘Umar.

 

(c) Aayah ambayo Maulamaa wote wamekhitalifiana na hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh inayothibitisha

 

15- Al-HajjiAayah ya 77:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ))

 Ni Aayah ambayo Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanasujudu wanapoisoma. [At-Tamhiyd (19/131), Al-Majmu’u (4/62) na Al-Mughniy (1/618)]

 

Kuna Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir kuhusiana na hili ambapo ‘Uqbah alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama kwenye Al-Hajji kuna sajdah mbili. Nabiy akasema: ((Ndio, asiyesujudu anapoisoma, basi asiisome)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1402), At-Tirmidhiy (578) na Ahmad (4/151)]

 

Ni Hadiyth Dhwa’iyf iliyofanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1402), At-Tirmidhiy (578) na Ahmad (4/151) ingawa Maswahaba wote wameisema wakiwemo ‘Umar bin Al-Khattwaab, ‘Aliy, Ibn ‘Abbaas, Ibn Mas-’oud, Abu Muusa, Abud Dardaai, na ‘Ammaar bin Yaasir (Radhwiya Allaahu Anhum).

 

Kadhalika, Abu ‘Abdul Rahmaan As-Sulamiy, Abul ‘Aaaliyah na Zurri bin Jaysh. Ibn Qudaamah amesema: “Hatujasikia yeyote aliyeikataa katika enzi yao”.

 

Ninasema: “Hili linatutuza nyoyo juu ya kuswihi kwake, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Share