037-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Safari

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

037-Swalaah Ya Safari

 

Alhidaaya.com

 

 

Maana ya safari katika lugha ya kawaida ni kukata masafa, na kinyume chake ni kusalia mjini anapoishi mtu. Ama kiistilahi, ni kutoka mtu toka makazi yake kwenda sehemu nyingine yenye umbali wa masafa fulani ambayo Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu urefu kama tutakavyokuja kueleza.

 

Kwanza: Kupunguza Swalaah

 

  • Taarifu Yake:

Kupunguza maana yake ni kuzuia na kutofikia kitu upeo wake na mwisho wake. Ama kiistilahi, ni kuifanya Swalaah ya rakaa nne kuwa rakaa mbili wakati wa safari sawasawa katika hali ya vita au ya amani.

  • Kujuzu Kwake

Kupunguza Swalaah wakati wa safari, kumethibiti katika Qur-aan, Hadiyth na Ijma’a. Dalili zake zitakuja wakati tukiuchambua mlango huu Insha-Allaah.

 

Maulamaa wamekubaliana kwamba inajuzu kupunguza Swalaah safarini. Pia wamekubaliana kwamba Swalaah za Alfajiri na  Magharibi hazipunguzwi, lakini wamekhitalifiana kwa upande wa hukmu ya kupunguza Swalaah kama ni wajibu au si wajibu (ruksa). Aidha, wamekhitalifiana kuhusu masharti ya kupunguza na masuala mengineyo husika. Hebu sasa tujaribu kuyachambua masuala haya.

  • Hukmu Ya Kupunguza Swalaah Safarini

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya kupunguza Swalaah ya rakaa nne kwa kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Kupunguza kumeruhusiwa, nayo ni kauli ya Jamhuri; Maalik, Ash-Shaafi’i na Hanbali. [Ash-Sharhul Kabiyr katika Haashiyat Ad-Dusuwqiy (1/358), Al-Majmu’u (4/337), Kash-Shaaful Qinaa (1/324), Al-Mughniy (2/197), Bidaayatul Mujtahid (1/241), Naylul Awtwaar (3/239) na Al-Haawiy cha Al-Mawruwdiy (2/363-365)]

Kisha hawa wakakhitalifiana juu ya lililo bora kati ya kupunguza, au kuswali kamili, au je mtu anakhiyarishwa?

 

Ya pili:

 

Kupunguza ni wajibu na haijuzu kuswali Swalaah kamili. Ni madhehebu ya Hanafi na Ahlu Adh-Dhwaahir,  na kauli kwa Maalik. [Al-Badaai-’i (1/91), Fat-hul Qadiyr (1/395), Bidaayatul Mujtahid (1/241), Al-Muntaqaa cha Al-Baajiy (1/260), Al-Muhallaa (4/264), Ma’alimu As-Sunan (1/48) Naylul Awtwaar (3/239)]

 

Kisha wakakhitalifiana, je akiswali kamili, Swalaah itabatilika au la?

 

  • Dalili Za Makundi Haya Mawili Na Uhakiki Wake

(a) Dalili za wanaosema kwamba si wajibu

 

Dalili ya kwanza ya Jamhuri:

 

Kauli Yake Ta’alaa:

((وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ إِنْ خِفْتُمْ أَن يَفْتِنَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُوا لَكُمْ عَدُوًّا مُّبِينًا))

((Na mtakaposafiri katika ardhi basi si dhambi kwenu kufupisha Swalaah mkikhofu kwamba waliokufuru watakushambulieni. Hakika makafiri wamekuwa kwenu ni maadui dhahiri)). [An-Nisaa (4:101)]

 

Wanasema kuwa Aayah kueleza kwamba hakuna ubaya kunamaanisha kwamba hakuna dhambi, bali jambo ni mubaaha na si la fardhi wala la kufungiwa niya.

 

Wenye kusema ni wajibu wamewajibu kwa njia tatu:

 

Njia ya kwanza:

 

Haikubaliki tamshi la hakuna ubaya kuwa ni mahsusi kwa jambo la mubaaha tu, bali hutumiwa vile vile katika wajibu. Katika hilo ni Kauli Yake Taa’laa:

((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ))

(( Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya khayr basi hakika Allaah ni Mwenye Kupokea shukurani, Mjuzi wa yote)). [Al-Baqarah (2:158)]

 

Tamshi la hakuna lawama katika Aayah limekuja katika kusa’i kati ya Swafaa na Marwa katika Hajji, nako ni faradhi.

 

Limejibiwa hili kwa kusemwa: Aayah imeshuka kwa ajili ya kubainisha kwamba kusa’i ni katika alama, na hiyo ni pale Waislamu walipoona dhiki ya kuifanya kwa vile Waarabu walikuwa wakiifanya enzi ya ujahili. Hivyo Aayah haikushuka  kwa ajili ya kubainisha hukmu ya kusa’i!!

 

Njia ya pili:

 

Muradi wa kupunguza katika Aayah ni kupunguza umbo la Swalaah wakati wa vita kwa kuacha kusimama na kurukuu.

 

Limejibiwa hili kwa kusemwa: Muradi wa kupunguza ni kupunguza idadi ya rakaa kwa kuzifanya mbili badala ya nne kwa dalili ya Hadiyth ya Ya’alaa bin Umayyah itakayokuja baadaye. Hadiyth hii inaeleza kwamba alitatizikiwa kupunguza idadi ya rakaa safarini katika hali ya amani kama alivyotatizikiwa ‘Umar. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

((Ni swadaqah ambayo Allaah Amewapeni, basi ikubalini Swadaqah Yake)). [Hadiyth Swahiyh: Angalia inayofuatia baada yake].

 

Njia ya tatu:

 

Katika Aayah kuna sharti ya kuwepo vita, basi kwa nini hamkuisema ili kupunguza kujuzu na badala yake mkaijuzisha katika amani?

 

Limejibiwa hilo kwa kusemwa kwamba kupunguza katika safari, kumethibitishwa na Sunnah ya Rasuli.

 

Dalili ya pili ya Jamhuri: 

 

Hadiyth ya Ya’alaa bin Umayyah aliyesema: “Nilimwambia ‘Umar bin Al-Khattwaab:

((فليس عليكم جناح أن تقصروا من الصلاة إن خفتم أن يفتنكم الذين كفروا))

Watu wako kwenye amani!! Akasema: Nimestaajabu kwa hili ulilolistaajabia. Nikaenda kumuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo naye akasema:

((Ni swadaqah ambayo Allaah Amewapeni, basi ikubalini swadaqah Yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (686), Abu Daawuud (1199), At-Tirmidhy (3037) na Ibn Maajah (1065)].

 

Wanasema: “Kuelezewa kupunguza kama ni swadaqah, kunaonyesha kujuzu, kwa kuwa swadaqah ni kitu cha khiyari tu, na si cha lazima”.

 

Wenye kusema ni wajibu wamejibu wakisema:

 

“Hadiyth ni dalili kwetu na si kwenu, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuikubali swadaqah hii, na agizo lake ni la wajibu, na kila ihsani kwetu ni swadaqah”.

 

Wamejibiwa:

 

“Kuna kielelezo zaidi ya kimoja chenye kulibadili agizo toka kwenye ulazima kulipeleka kwenye uzuri na ubora likifanyika!! Kati ya vielelezo hivyo ni kuwa tamshi “swadaqah” linapotolewa, hukusudiwa kwalo swadaqah ya kujitolea na si swadaqah ya lazima”.

 

Dalili ya tatu ya Jamhuri:

 

Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Aaishah aliposema: “Nilitoka pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda ‘Umrah katika mwezi wa Ramadhwaan. Yeye hakufunga nami nikafunga, akapunguza Swalaah nami nikaswali kamili, kisha nilimwambia: Kwa hishma ya wazazi wangu: Wewe hukufunga nami nimefunga, umepunguza Swalaah nami nimeswali kamili. Akaniambia: ((Umefanya vizuri ee ‘Aaishah)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaraqutwniy (2/188) na Al-Bayhaqiy. Ad-daaraqutwniy kaitilia nguvu irsali yake kwenye Al’Ilal].

 

Wenye kusema ni wajibu wamelijibu hili kwa majibu yafuatayo:

 

Kwanza: Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haifai kwa hoja.

 

Pili: Matni yake ina shaka na walakini, kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya ‘Umrah mara nne tu na hakuna yoyote kati ya hizo aliifanya katika mwezi wa Ramadhwaan, bali katika mwezi wa mfungo pili. [Jibu hili linajibiwa kwamba Nabiy alifanya ‘Umrah mbili katika Mwezi wa Ramadhwaan: ‘Umratul Qadhwaa na ‘Umrah ya ukombozi wa mji wa Makkah. Zote mbili zilikuwa katika Ramadhwaan]

 

Tatu: Sheikh wa Uislamu amesema: “Hadiyth hii kazushiwa ‘Aaishah. [Ameinukulu kwenye Zaad Al-Ma’ad (1/472) chapa ya Ar-Risaalah]

 

Haiwezekaniki akaswali kinyume na Swalaah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wengineo huku akiwaona wakipunguza, halafu yeye peke yake aswali kamili bila sababu kinaishi. Vipi liwe hilo na yeye ndiye asemaye: Swalaah imefaradhiwa rakaa mbili? Ataonekana vipi akizidisha faradhi ya Allaah na kwenda kinyume na Nabiy wa Allaah pamoja na Maswahaba wake?!!”

 

Dalili ya nne ya Jamhuri:

 

Yaliyosemwa na ‘Aaishah ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipunguza Swalaah katika safari na kutimiza, na hula na hufunga”. [Hadiyth Munkar: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaraqutwniy (2/242), (2/189), Ash-Shaafi’iy (518) na Al-Bayhaqiy (3/141, 142) na Sanad yake imeharibika. Sheikh wa Uislamu amesema: “Haya kazushiwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. Angalia Al-Irwaa (3/3-9)].

 

Wenye kusema ni wajibu wamejibu wakisema:

 

Hili linachukulika kama yeye alipunguza kivitendo na akatimiza kihukmu. Ni kama kauli ya ‘Umar: “Swalaah ya safari ni rakaa mbili kamili bila kupungua”. Hili linajibiwa kwa kusema: “Ni kuwa kuswali kamili  katika habari ya ‘Aaishah, kunaonyesha kwamba inajuzu kuiswali Swalaah ya rakaa nne kwa rakaa nne katika safari. Ama kutimiza katika habari ya ‘Umar, kunaonyesha utimilifu kwa upande wa malipo. Habari ya ‘Aaishah haibebeshwi juu ya maneno ya ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu)”.

 

Ninasema: “Hadiyth hii ni Munkari na haihitajii taawiyl ya aina yoyote ile”.

 

Dalili ya tano ya Jamhuri:

 

Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin Yaziyd isemayo: “‘Uthmaan alituswalisha Mina rakaa nne. ‘Abdullah bin Mas-’oud akaelezwa hilo, akavuta kumbukumbu yake nyuma na kusema: Niliswali pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Mina rakaa mbili, niliswali pamoja na Abu Bakr As-Siddiyq Mina rakaa mbili, na niliswali pamoja na ‘Umar Mina rakaa mbili. Basi laiti fungu langu lingekuwa rakaa mbili zenye kukubaliwa badala ya nne” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1084) na Muslim (695)].

 

Wamesema: “Yaani, laiti ‘Uthmaan angeliswali rakaa mbili badala ya nne kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakri, ‘Umar na ‘Uthmaan mwanzoni mwa Ukhalifa wake. Na makusudio yake ni ukaraha wa kwenda kwake kinyume na alilokuwa akilifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahibu wake wawili. Lakini pamoja na haya, Ibn Mas-’oud amewafiki kujuzu kuswali kamili, na kama si hivyo, asingelijuzisha kumfuata yeyote anayeswali kamili”. [Sharhu Muslim cha An Nawawiy (5/204)]

 

Wenye kusema ni wajibu wamejibu kwa njia hizi:

 

(a) ’Uthmaan aliswali kamili Minaa kwa kuwa alinuwia kukaa Makkah baada ya Hijjah, na Maswahaba waliyekuwa naye waliswali kamili kwa kuwa nao watakaa Makkah madhali yeye yuko huko.

 

Hili limejibiwa: “Kukaa Makkah kulikuwa ni marufuku kwa Muhaajirina. Imepokewa kwa njia sahihi kuhusu ‘Uthmaan ya kwamba alikuwa hawaagi wanawake isipokuwa akiwa juu ya mnyama wake, na huharakia akichelea kurejea kwenye hijra yake. Na imethibiti kwamba wakati walipomzingira walimwambia: “Panda mnyama wako wende Makkah”. Akawajibu: “Sitoondoka Madiynah nilikohamia”. [Fat-hul Baariy (2/665) chapa ya As-Salafiyyah]

 

(b) Imesemwa kwamba ‘Uthmaan aliswali kamili Mina kwa kuwa alikuwa na mke Makkah, kwa dalili kwamba watu walipopinga yeye kuswali Mina rakaa nne aliwaambia: “Enyi watu! Mimi nimeoa Makkah tokea nije, na mimi nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Mwenye kuoa kwenye mji fulani, basi aswali Swalaah ya mkazi)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraj” na Ahmad (1/62) kwa Sanad Dhwa’iyf. Al-Bayhaqiy kaitia kasoro ya kuweko mkatiko].

 

Hili limejibiwa: “Hadiyth hii imekosolewa kuwa ina mkatiko, haifai kwa hoja.

 

(c) Imesemwa: ‘Uthmaan aliswali kamili kwa kuwa yeye ni imamu wa Waislamu, na sehemu yoyote anaposhukia anazingatiwa kuwa ni mkazi na nyumbani kwake!!”

 

Hili limejibiwa: “Kwamba lililo bora zaidi kwa hukmu hii ni Nabiy wa Allaah. Imethibiti kwamba alikuwa akipunguza katika safari zake zote”.

 

Dalili ya sita ya Jamhuri:

 

Ni kwamba msafiri akiingia kwenye Swalaah ya mkazi, ataswali rakaa nne kwa makubaliano ya Jamhuri. Na lau kama faradhi yake ni ya kupunguza, msafiri asimfuate mkazi.

 

Wenye kusema ni wajibu wamejibu wakisema: “Faradhi ya msafiri ni rakaa mbili, na haibadiliki kwa kumfuata mkazi, lakini rakaa mbili za mwisho zinakuwa ni Sunnah, kwa dalili kwamba ikiwa hatokaa baada ya rakaa mbili za kwanza, Swalaah yake itabatilika kwa kuwa ameacha kikao ambacho ni faradhi kwake”.

 

Hili limejibiwa: “Haikubaliki kuwa rakaa mbili za mwisho kuwa ni Sunnah, na lau kama zingelikuwa ni hivyo, basi isingelikuwa ni wajibu kwake kutimiza nyuma ya imamu mkazi”.

Dalili ya saba ya Jamhuri:

 

Wametumia kipimo cha kufunga kwa msafiri katika mchana wa Ramadhwaan. Wanasema kuwa kufungua ni ruksa kwake lakini si wajibu, na hali ni hivyo hivyo katika kupunguza Swalaah.

 

Wenye kusema ni wajibu wamejibu wakisema: “Hiki ni kipimo kisichoendana, hakifai. Kwa kuwa Swiyaam hulipwa, na mfungaji huiachia badali kinyume na rakaa mbili katika Swalaah ya rakaa nne, kwani msafiri huziacha bila badali”.

 

(b) Dalili za wanaosema kwamba ni wajibu

 

Dalili ya kwanza: Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) aliposema: “Swalaah ilifaradhishwa rakaa mbili mbili katika ukazi na safari. Swalaah ya safari ikapitishwa, na ikazidishwa katika Swalaah ya faradhi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (350) na Muslim (685)].

 

Jamhuri wamelijibu hili kwa njia mbili:

 

(a) Muradi wa kufaradhishwa Swalaah rakaa mbili ni kwa aliyetaka kuzifupisha. Zikaongezwa rakaa mbili katika Swalaah ya ukazi kwa njia ya lazima, na Swalaah ya safari ikapitishwa kuwa inajuzu kwa rakaa mbili.

 

Au muradi mwingine ni kwamba ufaradhi wa Swalaah ulianza kwa rakaa mbili, kisha zikakamilishwa kwa kufanywa nne, na kwa ajili hiyo, ‘Aaishah alikuwa akikamilisha katika safari.

 

(b) Hadiyth hii ni Mawquwf kwa ‘Aaishah. Hivyo basi, si dalili na hususan yeye hakushuhudia zama za kufaradhishwa Swalaah!!

 

Hili limejibiwa: “Hadiyth Mawquwf ikiwa haina nafasi ndani yake ya akili kuweza kuingia, basi itakuwa na hukmu ya urufaisho, na hapa ndivyo ilivyo”.

 

Dalili ya pili: Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas isemayo: ”Allaah Alifaradhisha Swalaah kwa ulimi wa Nabiy wenu rakaa nne kwa mkazi, rakaa mbili kwa msafiri, na rakaa moja vitani”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (687), Abu Daawoud (1247), na An-Nasaaiy (3/169)]

 

Jamhuri wamejibu: “Hadiyth haichukuliwi kwa mwonekano wake, bali makusudio yake ni kwamba Swalaah ya safari ni rakaa mbili katika hali ya kuzipunguza kwa msafiri. Ama akitaka kutimiza, basi hakuna ubaya ikiwa ni kukusanya kati ya dalili!!

 

Dalili ya tatu: Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khattwaab aliyesema: “Swalaah ya safari ni rakaa mbili, Swalaah ya Fitr ni rakaa mbili na Swalaah ya Ijumaa ni rakaa mbili kwa ukamilifu bila kupunguza kwa ulimi wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/118), Ibn Maajah (1064) na Ahmad (1/37)].

 

Jamhuri wamejibu: “Muradi wa ukamilifu ni kuwa malipo ya Swalaah na fadhwla zake yanakuwa kamili bila upungufu. Na taawiyl hii imebidi ije kwa kuwa mwonekano wa Hadiyth unahukumia kwamba Swalaah iwe rakaa mbili katika safari bila kuwa imepunguzwa, na hili linapingana na Qur-aan katika kuiita “Qaswr!!”

 

Dalili ya nne: Neno lake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Ni swadaqah ambayo Allaah Amewapeni, basi ikubalini swadaqah Yake) [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].Hadiyth hii ishazungumziwa.

 

Dalili ya tano: Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Nilisuhubiana na Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) safarini. Hakuzidisha zaidi ya rakaa mbili mpaka alipofariki. Nilisuhubiana na Abu Bakr safarini. Hakuzidisha zaidi ya rakaa mbili mpaka alipofariki. Nilisuhubiana na ‘Umar safarini. Hakuzidisha zaidi ya rakaa mbili mpaka alipofariki. Kisha nilisuhubiana na ‘Uthmaan safarini. Hakuzidisha zaidi ya rakaa mbili mpaka alipofariki. Na Allaah Amesema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (689)] .

 

Ama tuliyoyaeleza nyuma kuhusu kupunguza ‘Uthmaan Swalaah akiwa Mina, linaloonekana ni kuwa hakuwa akiswali kamili isipokuwa Mina basi kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar isemayo: “Nabiy wa Allaah aliswali Mina rakaa mbili, na Abu Bakr baada yake, na ‘Umar baada ya Abu Bakr, na ‘Uthmaan mwanzoni mwa Ukhalifa wake, kisha ‘Uthmaan aliswali baada ya hapo rakaa nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1082) na Muslim (694)].

 

Jamhuri wamejibu: “Kitendo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kudumu kwake hakuonyeshi ulazima”.

 

Dalili ya sita: Rakaa mbili za mwisho inajuzu kuziacha bila kuzifidia, hivyo haijuzu kuzizidisha juu ya rakaa mbili za faradhi, kama lau angezizidisha katika Swalaah ya Alfajiri.

 

Jamhuri wamejibu: Kuchukulia Swalaah ya Alfajiri kama kipimo hakuendani, kwa kuwa Swalaah ya Alfajiri ni rakaa mbili na haikubali ziada kwa hali yoyote kinyume na Swalaah ya safari, kwani inakubali ziada wakati wa kumfuata mkazi.

  • Dalili Yenye Nguvu

Baada ya kuziweka mezani dalili za makundi mawili na kuzijadili, dalili za Jamhuri hazina salama isipokuwa kitendo cha ‘Uthmaan na ‘Aaishah zikilinganishwa na mwonekano wa Hadiyth za ‘Aaishah, ‘Umar na Ibn ‘Abbaas mbali na kudumu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake wawili katika kupunguza Swalaah safarini.

 

Linaloonekana ni kwamba kauli inayosema ni wajibu kupunguza ndiyo yenye nguvu na mwelekeo zaidi. Haingii ndani ya wigo huu aliyemfuata imamu mkazi. Na lau kama mtu atasema kwamba hilo ni Sunnah iliyokokotezwa na haitakikani kuiacha na kwamba kuswali kamili ni makruhu, basi atakuwa hakwenda mbali. Na haya yamenukuliwa toka kwa Sheikh wa Uislamu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

  • Masafa Ya Kupunguza Swalaah

Maulamaa wamekhitalifiana katika kuainisha masafa ambayo inajuzu kupunguza Swalaah katika kauli tatu:

 

Ya kwanza: Ni maili 48 sawa na kilometa 85. Hii ni kauli ya Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas, Al-Hasan Al-Baswriy na Az-Zuhry. Ni madhehebu ya Maalik, Al-Layth, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq na Abu Thawr. [Al-Qawaaniyn (100), Ad-Dusuwqiy (1/385), Al-Majmu’u (4/322), Al-Haawiy (2/361), Al-Mughniy (2/90) na Kash-Shaaful Qinaa (1/504)] Dalili zao ni:

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas  ikiwa Marfu’u: “Enyi watu wa Makka! Msipunguze chini ya “burudi” nne toka Makkah hadi ‘Asqalaan”. Hadiyth hii ni Munkari, haifai. [Hadiyth Munkari: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaraqutwniy (148) na Al-Bayhaqiy (3/137). Angalia Al-Irwaa (565)].

 

2- Yaliyothibiti kwamba Ibn ‘Umar na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhumaa) walikuwa wakipunguza katika masafa ya “burudi” nne sawa na “farsakha” kumi na sita. [Hadiyth Swahiyh: Al-Bukhaariy kasema ni Mu’allaq (2/659) na Al-Bayhaqiy kasema ni Mawsoul. Angalia Al-Irwaa (568)].

 

Al-Burud” ni wingi wa “Al-Bariyd”, nao ni mwendo wa “farsakha” nne, na “farsakha” moja ni sawa na maili tatu, na maili moja ni sawa na takriban kilometa 1.8.

 

3- Umbali wa “burudi” nne unakuwa na mazito ya safari kati ya kupanda na kushuka. Hivyo inajuzu kupunguza katika masafa hayo lakini si chini ya hapo.

 

Ya pili: Ni mwendo wa siku tatu na masiku yake kwa kutumia ngamia. Ni kauli ya Ibn Mas-’oud, Suwayd bin Ghaflah, Ash-Sha’abiy, An-Nakh’iy na Ath-Thawriy. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah. [Ibn ‘Aabidiyn (2/122), Al-Hidaayah (1/80), Naylul Awtwaar (3/246), na Bidaayatul Mujtahid]

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Ibn ‘Umar toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: ((Asisafiri mwanamke siku tatu ila awe pamoja na maharimu yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1086) na Muslim (1338)].

 

2- Hadiyth ya ‘Aliy bin Abiy Twaalib kuhusu kupukusa juu ya khufu mbili isemayo: “Allaah Amezifanya siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa kwenye mlango wa kupukusa juu ya khufu mbili].

 

Wamesema: “Kufungamana hukmu ya msafiri katika Hadiyth mbili kwa aliyesafiri siku tatu, hakufungamani na kupunguza chini ya hapo!!”.

 

3- Ni mantiki kwamba tatu ni uchache wa kingi na wingi wa kichache, na haijuzu kupunguza katika safari ndogo!! Ni wajibu mpaka wake uwe uchache wa kingi (nazo ni tatu)!!

 

Ya tatu: Kupunguza hakuna masafa maalumu, bali mtu hupunguza kwa chochote kijulikanacho kama safari.

 

Ni kauli ya Adh-Dhwaahiriyyah na chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim. [Al-Muhalla (5/10), Majmu’u Al-Fataawaa (24/12-35), Zaad El-Ma’ad, Fat-hul Baariy (2/660) na Al-Mughniy (2/44)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Kauli Yake Ta’alaa:

((وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ إِنْ خِفْتُمْ أَن يَفْتِنَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُوا لَكُمْ عَدُوًّا مُّبِينًا))

(( Na mtakaposafiri katika ardhi basi si dhambi kwenu kufupisha Swalaah mkikhofu kwamba waliokufuru watakushambulieni. Hakika makafiri wamekuwa kwenu ni maadui dhahiri )). 

Mwonekano wa Aayah unaonyesha kwamba kupunguza kunahusiana na safari yoyote ardhini bila ya kuainishwa masafa maalum.

 

2- Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuainisha mpaka maalumu wa kiwakati au kimahala wa kupunguza Swalaah, bali kafungamanisha hukmu na kile kiitwacho safari tu. Hivyo haijuzu kutofautisha kati ya aina na aina bila dalili ya kisharia, bali la wajibu ni kukiainisha kilichoainishwa na sharia, na kutokiainisha kile kisichoainishwa. Mlango wa kukadiria masafa ya kupunguza Swalaah uko kwa Allaah na Rasuli Wake tu, nao hauingiliwi kwa rai hewa.

 

3- Imethibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipunguza chini ya masafa yaliyotajwa nyuma kidogo:

 

(a) Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotoka mwendo wa maili tatu au farsakha tatu, huswali rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (691)].

 

Hii inaonyesha kibayana kwamba kupunguza kunafungamana na safari yoyote ile hata kama itakuwa ni ya maili tatu au farsakha tatu. Al-Haafidh kasema: “Hii ni Hadiyth Swahiyh na bayana zaidi katika hili”.

 

Jamhuri wamelijibu hili wakisema: “Linachukuliwa hili kwa masafa ya kuanzia kupunguza na si kwa mwisho wa safari!!” Al-Haafidh anasema: “Umbali wa uchukulifu huu haufichikani, pamoja na kwamba Al-Bayhaqiy ameeleza katika riwaya yake kwa njia hii kwamba Yahya bin Zayd amesema: Nilimuuliza Anas kuhusu kupunguza Swalaah. Nilikuwa natoka Basrah kwenda Kuufah nikiswali rakaa mbili mbili mpaka ninapotoka. Anas akasema: Akaitaja Hadiyth. Ikaonekana kwamba alimuuliza kuhusiana na kujuzu kupunguza katika safari, na si mahala pa kuanzia kupunguza”.

 

(b) Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Niliswali  Adhuhuri pamoja na Nabiy Madiynah rakaa nne, na rakaa mbili Dhul Hulayfah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1089) na Muslim (690) na nyongeza ya (Alasiri) ni yake].

 

Masafa kati yao ni maili tatu.

 

(a) Imethibiti toka kwa wawili hao kinyume cha mpaka huo kwa Sanad Swahiyh. Aidha, wengine katika Maswahaba wamekwenda kinyume nao.

 

(b) Na lau kama tutakubali kwamba haikuthibiti toka kwao isipokuwa dalili walioitoa Jamhuri, na kwamba hakuna aliyekwenda nao kinyume, basi hapo pia hakuna hoja kwa kuwa kunakhalifiana na yaliyothibiti toka kwa Nabiy kama ilivyotangulia.

 

5- Ama katika Hadiyth: ((Asisafiri mwanamke siku tatu…)), hakuna kinachosema humo kwamba ili safari iwe ni safari ni lazima iwe ya siku tatu, bali maana yake ni kuwa haijuzu mwanamke kusafiri safari hii maalumu bila kuwa na maharimu yake. Kuna Hadiyth Swahiyh Marfu’u toka kwa Abu Hurayrah isemayo: (( Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho kusafiri mwendo wa siku moja na usiku bila kuwa na mahramu yake)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1088) na Muslim (1939)].

Katika Hadiyth hii, hakuna mpaka wa safari.

  • Kauli Yenye Nguvu

Ni kauli ya tatu isemayo kwamba Swalaah hupunguzwa kwa chochote kijulikanacho kama safari sawasawa ikiwa ni ndefu au fupi, na safari hiyo haina mpaka maalumu katika lugha. Hili linarejeshwa kwa watu wenyewe kwa mujibu wa ada na desturi, na linatofautiana kwa kutofautiana zama kimaendeleo kwa upande wa vyombo vya usafiri. Kidhibiti chake ni kusema mtu: “Mimi nasafiri kwenda mji fulani”, na si kusema: “Ninakwenda”, na huko anakokwenda kujulikane kiada kama ni safari kama kuchukua masurufu ya safari na kadhalika. Allah Ndiye Mjuzi Zaidi.

  • Je, Ni Sharti Kwa Safari Ya Kupunguza Iwe Ya Lengo La Halali?

Jamhuri ya Maulamaa; Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanasema kwamba hairuhusiwi kupunguza isipokuwa katika safari ya wajibu au ya halali, na haijuzu katika safari ya maasia kama ujambazi na mfano wake. [Bidaayatul Mujtahid, (1/244), Al-Majmu’u (4/201), Al-Mughniy (2/101) na Kash-Shaaful Qinaa (1/324)]

 

Na hili linajengewa juu ya kauli yao kwamba kupunguza ni ruksa, na makusudio yake ni kumpumguzia uzito msafiri, na kwamba ruksa ya kupunguza imetolewa ili imsaidie msafiri kufanikisha malengo yake ya safari. Hivyo haiwi isipokuwa kwa msafiri halali, si kwa msafiri wa safari ya kwenda kumkasirisha Allaah.

 

Lakini Maulamaa wenye kusema kwamba ni wajibu kupunguza Swalaah ya safari kama Abu Haniyfah, Ibn Hazm, Ibn Taymiyah na wengineo, wanasema kwamba mtu atapunguza katika safari yoyote ile hata kama ni ya maasia, kwa kuwa faradhi yake ni rakaa mbili tu na si nne. Na hii ni kauli kwa Maalik. [Fat-hul Qadiyr (1/47), Al-Kharshiy (1/57), Al-Muhalla (4/267) na Majmu’u Al-Fataawaa (24/110)]

 

Ninasema: “Kwa yule ambaye kupunguza kwake ni ruksa, haruhusiki kupunguza katika safari ya maasia. Ama mwenye kusema kuwa ni wajibu kupunguza, hatofarikisha kati ya safari halali au safari ya maasia, na hili ndilo lenye nguvu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

  • Sehemu Anapoanza Msafiri Kupunguza Swalaah

Maulamaa kwa kauli moja wanasema kwamba inajuzu kwa msafiri aanze kupunguza Swalaah baada ya kuyaacha majumba ya mji wake. [Al-Ijma’a cha Ibn Al-Mundhir (39) na Al-Mughniy (2/260)]

 

Kisha wakakhitalifiana kuhusiana na kujuzu kupunguza kabla ya hilo katika kauli mbili. Kauli sahihi zaidi kati ya mbili ni kuwa haijuzu kupunguza kabla ya kuyaacha majumba. Ni kauli ya Jamhuri. [Ibn ‘Aabidiyn (2/121), Adh-Dhahiyrah (2/365), Al-Majmu’u (4/202) na Kash-Shaaful Qinaa (1/325)]

 

Nayo inathibitishwa na Hadiyth ya Anas aliyesema: “Niliswali  Adhuhuri pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah rakaa nne, na Dhul Hulayfah rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma].

 

Hadiyth hii yaonyesha wazi kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akianza kupunguza Swalaah mara baada tu ya kutoka Madiynah.

  • Muda Wa Kupunguza Anapowasili Kwenye Mji Aliokwenda

Msafiri ataendelea kupunguza Swalaah madhali yuko safarini vyovyote muda urefukavyo. Lakini anapowasili kwenye mji alioukusudia, ni muda gani anaoruhusiwa kupunguza?

Jambo hili limenyamaziwa, halikuzungumzwa. Hakuna Hadiyth yoyote iliyopokelewa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayoeleza wazi kuhusu hilo. Aidha, kipimo cha kuainisha muda huo hakina nguvu kwa Maulamaa. Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na suala hili kwa kauli takriban kumi na moja. Zilizo mashuhuri zaidi ni kauli nne ambapo wenye kauli hizi wamejaribu kutolea dalili kupitia matukio ya kupunguza yaliyonukuliwa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kauli mashuhuri zaidi ni hizi zifuatazo:

 

Ya kwanza: Akipanga kukaa zaidi ya siku nne hatopunguza

 

Hii ni kauli ya Jamhuri; Maalik, Ash-Shaafi’iy na Hanbali, isipokuwa Maalik na Ash-Shaafi’iy wamesema: Ni siku nne zikitolewa siku ya kuingia na ya kutoka. Hanbali wamewekea mpaka Swalaah ishirini na moja. [Ad-Dusuwqiy (1/364), Al-Majmu’u (4/361), Al-Haawiy (2/372), Al-Mughniy (2/132) na Kash-Shaaful Qinaa (1/330)]

Na wametoa dalili kwa haya yafuatayo:

 

1- Ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia Makkah asubuhi ya tarehe nne ya mfungo tatu, kisha akakaa Makkah tarehe nne, tano, sita na saba. Siku ya pili aliswali Alfajiri, kisha akatoka kwenda Mina, na alikuwa akipunguza Swalaah katika siku hizi nailhali ameazimia kukaa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” kwa maana yake (1564), na Muslim (1240) katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas, na Muslim (1218) toka Hadiyth ya Jaabir].

 

Hili limejibiwa: Kwamba hakuna linaloashiria katika Hadiyth hii kwamba muda huu ndiyo muda mdogo zaidi wa kukaa, kwani imethibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa zaidi ya muda huo huku akiendelea kupunguza kama itakavyokuja kubainishwa.

 

2- Hadiyth ya Al-‘Alaa bin Al-Khadhwramiy asemaye: “Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mhamiaji atakaa Makkah siku tatu baada ya kumaliza amali ya Hijjah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1352)].

 

Wanasema kwamba hili linaonyesha kuwa mwenye kukaa siku tatu hayuko katika hukmu ya mkazi, bali yuko kwenye hukmu ya msafiri.

 

Wamejibiwa: “Maana ya Hadiyth ni kwamba aliyehama toka Makkah kabla ya ukombozi, ni marufuku kwake kulowea hapo isipokuwa akae siku tatu tu baada ya kumaliza amali zake za Hijjah, asizidishe. Ama msafiri, si karaha kwake kuongeza zaidi ya siku tatu Makkah, lakini vipi kipimo chake kitakuwa? Halafu, katika Hadiyth hakuna ishara yoyote juu ya muda ambao msafiri akikaa atapunguza!!

 

Isitoshe, Hadiyth inaashiria kwamba zikizidi siku tatu kwa mhamaji, basi ataingia kwenye hukmu ya msafiri na si mkazi, wakati wao wanasema kwamba zikizidi siku tatu kwa msafiri, basi ukaazi wake ni sahihi. Na lau mmoja angelipimiwa kwa mwingine, basi ingelikuwa ni wajibu kwa msafiri apunguze zikizidi siku tatu na si aswali kamili kinyume na kauli yao. [Al-Muhalla (5/24)]

 

3- Athar ya ‘Umar bin Al-Khattwaab isemayo: “Mayahudi, Wakristo na Majusi waliwekewa muda wa siku tatu Madiynah za kununua na kukidhi mahitajio yao, na haruhusiwi yeyote kati yao kukaa humo kwa zaidi ya siku tatu”. [Isnadi yake ni ya watu madhubuti: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/147-9,209) kwa Sanad ambayo wapokezi wake ni watu madhubuti isipokuwa wamezungumzia kusikia Yahya bin Bakiyr toka kwa Maalik].

 

Wamesema: “Athar inaonyesha kwamba siku tatu ni mpaka wa safari, na zaidi ya hapo ni mpaka wa ukazi.

 

Wamejibiwa: “Siku tatu hazionyeshi mpaka wa safari kama tulivyobainisha katika kipengele kilichotangulia”.

 

4- Ugeni wa msafiri ni siku tatu na baada ya hapo huhesabiwa ni mkazi!!

 

Wamejibiwa: “Hakuna chenye kuonyesha muda mdogo zaidi wa ukazi kama ilivyo wazi”.

 

Ya pili: Akipanga kukaa zaidi ya siku kumi na tano hatopunguza

 

Ni kauli ya Abu Haniyfah, Ath-Thawriy na Al-Muzaniy. [Al-Badaai-’i (1/97,98), Al-Hidaayah (1/81) na Al-Majmu’u (4/364)]

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya Anas isemayo: “Tulitoka Madiynah kwenda Makkah pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akiswali rakaa mbili mbili mpaka tuliporejea Madiynah. Akaulizwa: “Je, mlikaa Makkah siku zozote?” Akajibu: “Tulikaa siku kumi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1081) na Muslim (693) na tamko jingine ni lake].

 

Na katika tamshi: “Tulikaa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku kumi tukipunguza Swalaah”. Hili linajibiwa kwa yale yale yaliyotangulia katika Hadiyth ya Jaabir na Ibn ‘Abbaas.

 

2- Yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa Makkah mwaka wa ukombozi siku kumi na tano akipunguza Swalaah”. [Ni Dhwa’iyf kwa tamko hili: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1231) na Ibn Maajah (1076). Imekuwa  Swahiyh kwa tamko la “kumi na tisa” na litakuja kuelezewa karibuni].

 

3- Yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar kwamba wamesema: “Ukisafiri ukafika kwenye mji, na huku umejipangia kukaa siku kumi na tano, basi swali Swalaah kamili. Na kama hujui ni lini utaondoka, basi punguza Swalaah”. [Kalitaja At-Tirmidhy toka kwa Ibn ‘Umar baada ya Hadiyth (548) bila isnadi yake].

 

Wanasema: “Uainisho huu hausemwi kwa rai ya mtu, bali una hukmu ya Hadiyth Marfu’u!!”.

 

Wamejibiwa: “Hiyo na kauli ya Swahaba iliyokhalifiwa na wengineo, hivyo haiwezi kuwa dalili. Isitoshe, yaliyothibiti toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar ni kinyume chake. Ibn ‘Abaaas kasema: “ Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa siku kumi na tisa akipunguza, na sisi tukisafiri siku kumi na tisa tunapunguza, na kama tukizidisha tunaswali kamili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1080)].

 

 Ya tatu: Msafiri ataendelea kupunguza madhali hakupanga kukaa moja kwa moja

 

Ni kauli ya Al-Hasan, Qataadah na Is-Haaq, na imechaguliwa na Ibn Taymiyah. [Al-Majmu’u (4/365), Majmu’u Al-Fataawaa (24/18) na Al-Muhalla (5/23)]

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyosema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa siku kumi na tisa akipunguza, nasi tunaposafiri tunakaa siku kumi na tisa tunapunguza, lakini tukizidisha tunaswali kamili”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeielezea nyuma kidogo].

 

2- Hadiyth ya Jaabir aliyosema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa Tabuk siku ishirini akipunguza Swalaah”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/295) na Abu Daawuud (1236). Hadiyth hii imetiwa kasoro. Angalia Al-Irwaa (574)].

 

3- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Imraan bin Haswiyn aliyesema: “Nilishiriki vitani pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na nilikuwa naye katika ukombozi wa Makkah. Akakaa Makkah masiku kumi na nane haswali isipokuwa rakaa mbili akisema: ((Enyi wenyeji! Swalini nne, sisi ni wasafiri)). [Hadiyth Dhwa’iyf: “Takhriyj” yake tushaielezea].

 

Wanasema: “Hadiyth hizi zinaonyesha kwamba uhakika wa msafiri haufungamani na muda maalumu, bali tunaloona ni kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipunguza katika siku kumi na nane, kumi na tisa na ishirini, kwa kuwa alikuwa ni msafiri”.

  • Faida

Kwa wenye madhehebu matatu yaliyotangulia ni kuwa msafiri anapokaa kwenye mji bila kuwa na nia ya kuendelea na ukaaji huo, halafu asijue ni lini atasafiri au lini atamaliza mambo yake, basi huyo atapunguza Swalaah siku zote. Kigezo chao ni kuwa Masalaf walifanya hivyo.

 

(a) Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba alikaa Azerbaijan miezi sita baada ya theluji kuwazingira. Alikuwa akiswali rakaa mbili.  [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/152) na Ahmad (2/83,154) kwa mfano wake kwa mapana kwa Sanad Hasan. Angalia Al-Irwaa (577)].

 

(b) Imepokelewa toka kwa Abu Al-Minhaal Al-‘Anziy akisema: “Nilimwambia Ibn ‘Abaas: Mimi ninakaa Madiynah mwaka mzima sisafiri”. Akaniambia: “Swali rakaa mbili”. [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/207)]..

 

(c) Imepokelewa toka kwa Al-Hasan kwamba Anas bin Maalik alikaa Nisabuor mwaka mmoja au miwili. Alikuwa akiswali rakaa mbili, kisha hutoa tasliym, kisha huswali rakaa mbili, na wala hakusanyi. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj" na Ibn Abu Shaybah (5099), na kutoka kwake Ibn Al-Mundhir (1736)].

 

(d) Imepokelewa toka kwake kwamba ‘Abdur Rahmaan bin Samurah kilimpitia kipindi kimoja au viwili vya baridi kali huko Kabul. Hakuwa akikusanya, na huswali rakaa mbili. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj" na Ibn Abu Shaybah (2/13)].

 

(d) Imepokelewa toka kwa Anas akisema: "Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikaa Ram Hormuz miezi tisa wakipunguza Swalaah". [Isnadi yake ni Dhwa’iyf Imefanyiwa “ikhraaj" na Al-Bayhaqiy (3/152). Angalia Al-Irwaa (576)].

 

(d) Imepokelewa toka kwa Abu Waael akisema: "Tulikuwa pamoja na Masruwk huko Silsilah miaka miwili. Alikuwa na kibarua huko na alikuwa akituswalisha rakaa mbili mpaka alipoondoka". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj" na Ibn Abu Shaybah (2/208), na ‘Abdu Ar Razzaaq (4357)].

Athar hizi zote zinathibitisha asili hii.

 

Ya nne: Msafiri atapunguza siku ishirini na masiku yake, kisha baada ya hapo ataswali kamili sawasawa akipanga kuendelea kukaa au bila kupanga

 

Ni kauli ya Abu Muhammad bin Hazm. Ash-Shawkaaniy kamfuata lakini yeye amepambanua kati ya aliyenuwia kukaa akisema: "Hapunguzi zaidi ya siku nne. Ama yule ambaye hakupanga na hajui lini ataondoka, basi huyo atapunguza siku ishirini, kisha ataswali kamili baada ya hapo. Na hii ni kauli ya Ash-Shaafi'iy". [Mughnil Muhtaaj (1/262)]

Maulamaa wenye kauli hii, wametoa dalili za Maulamaa wa kauli ya tatu isipokuwa wao wameangalia mambo mawili:

 

La kwanza: Nia ya kukaa haizingatiwi hapa, kwa kuwa nia haziingii katika amali ambazo Allaah Hakuziamuru kama kusafiri na kukaa sehemu, bali nia zinakuwa wajibu katika amali ambazo Allaah Ameziamuru, na hizo hazifai kufanywa bila nia. [Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah amekubaliana nao juu ya hili. Angalia Al-Muhalla (5/29) na Majmuu Al-Fataawaa (24/41)]

 

La pili: Kuchunga asili, nako ni kuswali kamili. Wanasema: "Kiukweli ni kuwa asili ni mkazi kuswali kamili, kwa kuwa kupunguza Swalaah kumewekwa kwa msafiri tu. Na mkazi si msafiri, na lau kama si kuthibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alipunguza Makkah na Tabuk alipokuwa mkazi, basi kuswali kamili ingelikuwa ni wajibu. Hivyo, asili hiyo haiachwi ila kwa dalili, na dalili inaonyesha kupunguzwa Swalaah hadi siku ishirini kama ilivyo katika Hadiyth ya Jaabir. Na hakuna kauli yoyote sahihi inayoeleza kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipunguza akiwa mkazi zaidi ya hivyo mtu akapata kupunguza kwa idadi hiyo. Na hakuna shaka kwamba kupunguza kwake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika muda huo hakukanushi kwamba alipunguza zaidi ya hapo. Lakini pamoja na hayo, angalizo la asili iliyotajwa ndilo lenye kuhukumia hilo". [Naylul Awtwaar (3/251)]

  • Lenye Nguvu Katika Suala Hili

Hakuna katika Qur-aan Tukufu wala Hadiyh za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa mkazi na msafiri. Ama mlowezi katika nchi ya kigeni, huyu hakosi moja ya hali mbili: Kwanza, ima atakuwa ametua hapo, akatafuta nyumba yake binafsi, akaitia fenicha na samani, na akaishi hapo raha mustarehe. Huyu atakuwa ni mkazi na haruhusiwi kupunguza, si siku nne wala zaidi ya hapo, na halirejewi kwa hili kupunguza Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah huko Makkah siku nne nailhali yeye anajua kwamba atakaa huko muda huo. Na hii ni kutokana na yale tuliyoyaeleza nyuma kwamba kinachozingatiwa katika safari na ukazi ni mazingira ya ukaaji na utulivu, na si muda. Pili, au ashukie sehemu ambapo hahisi uhuru wala utulivu. Huyu atakuwa ni msafiri wa kupunguza madhali mambo yako hivyo hata zaidi ya siku ishirini.

 

Kwa mfano mtu anaweza kusafiri toka Mansourah hadi Cairo (Misri) kwa ajili ya haja ambayo anajua kwamba itachukua mwezi mmoja. Akawa wiki moja analala kwa jamaa yake, wiki nyingine kwa rafiki na kadhalika. Huyu hahesabiwi kama mkazi bali msafiri, na anaweza kupunguza apendavyo mwenyewe mpaka arejee kwake au apate sehemu ya kutulia kabisa kama nyumba yake binafsi.

 

Hii ndiyo kauli yenye nguvu kwa upande wetu katika mas’ala haya, nayo ndiyo yenye kukusanya dalili zote zilizotangulia, nayo iko karibu zaidi na kauli ya tatu ya Maulamaa ambayo inafuatiwa katika nguvu na kauli ya nne. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

  • Faida: Kuishi Kwenye Hosteli Ya Wanafunzi

Hairuhusiwi kwa mwanafunzi kupunguza Swalaah akiwa hostelini kwake ikiwa atatulia hapo vyema kwa mujibu wa tuliyotangulia kuyasema kuhusiana na mazingira ya ukazi. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

  • Si Lazima Niya Ya Kupunguza

Hili ndilo sahihi kwa mujibu wa mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akipunguza anapowaswalisha Maswahaba wake na wala hawajulishi kabla ya kuingia kwenye Swalaah kwamba anapunguza, au hata kuwaamrisha kutia niya ya kupunguza. Na haya ndiyo madhehebu ya Abu Haniyfah, Maalik na moja ya kauli mbili katika madhehebu ya Ahmad. [Majmu’u Al-Fataawaa (24/16-21), Al-Hidaayah (1/81), Ash-Sharhu As-Swaghiyr (1/174-na Bughyat As-Saalik) na Al-Mughniy (2/105)]

 

Na haya tushayaeleza katika mlango wa “Kutofautiana niya kati ya imamu na maamuma”.

  • Swalaah Ya Msafiri Nyuma Ya Imamu Mkazi

Ikiwa msafiri atamfuata imamu mkazi katika Swalaah ya rakaa nne, basi hakosi moja ya mambo matatu:

 

La kwanza: Ni kuzipata rakaa tatu au nne pamoja na imamu

 

Hapo itamlazimu amfuate imamu na akamilishe rakaa nne nyuma ya imamu wake. Hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Ibn Hazm. [Al-Mughniy (2/151), Al-Muhalla (5/31), na Fat-hul Maalik Bitartiyb At-Tamhiyd (3/132)]

Dalili za Jamhuri ni hizi zifuatazo:

 

1- Ujumuishi wa kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakika si jinginelo, imamu amewekwa ili afuatwe, basi msende kinyume naye)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishaelezwa].

 

2- Hadiyth ya Muusa bin Salamah Al-Hadhliy aliyesema: “Nilimuuliza Ibn ‘Abbaas vipi niswali kama niko Makkah ikiwa sikuswali nyuma ya imamu?” Akajibu: “Rakaa mbili, Sunnah ya Abal Qaasim (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (688), An-Nasaaiy (3/119) na Ibnu Khuzaymah (951)].

 

Na katika tamko: “Sisi tukiwa nanyi, tunaswali rakaa nne, na tunaporejea kwenye nyumba tulizofikia, tunaswali rakaa mbili. Akasema: “Hiyo ni Sunnah ya Abal Qaasim (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/216), Ibnu Khuzaymah (952) na Al-Bayhaqiy (3/153) kwa njia tofauti].

 

3- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba yeye alikuwa akikaa Makkah siku kumi akipunguza Swalaah. Lakini akiswali pamoja na watu, huswali kama wanavyoswali. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (196) na ‘Abdul Razzaaq (4381)]

 

Katika tamshi jingine: “Alikuwa anaposwali na imamu huswali rakaa nne, na kama anaswali peke yake huswali rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (694)].

 

La pili: Ni kuipata rakaa moja au mbili pamoja na imamu. Hapa Maulamaa wana kauli mbili.

 

Ya kwanza: Ni lazima akamilishe nne. Ni madhehebu ya maimamu wanne na wengineo, na ni kauli ya Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas na Taabi’iyna. Wametoa dalili zilizotangulia na kwa Hadiyth ya Abu Mujlaz aliyesema: “ Nilimwambia Ibn ‘Umar: “Ikiwa msafiri atazipata rakaa mbili za Swalaah ya wakazi, je zitamtosheleza au itabidi akamilishe nao? Akacheka kisha akasema: “Atakamilisha pamoja nao”. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/157). Angalia Al-Irwaa (3/22)].

 

Ya pili: Rakaa mbili tu zitamtosheleza. Ni kauli ya Is-Haaq, Twaawuus, Ash-Sha’abiy na Tamiym bin Hadhlam (Swahibu yake Ibn Mas-’oud) na Abu Muhammad Ibn Hazm.

 

Ninasema: “Huenda kuswali kamili ni sahihi zaidi kwa kuwa hii ndio kauli ya Ibn ‘Umar na Ibn ‘Abbaas. Hakuna Swahaba yeyote aliyekwenda kinyume nao, na kwa kuwa yeye kaipata jamaa pamoja na imamu mkazi, hivyo itambidi aswali kamili. Lakini panaweza kuja swali: “Ikiwa amenuwiya kupunguza nyuma ya mwenye kuswali kamili na akazipata rakaa mbili – bila kushurutisha mwoano kati ya niya ya imamu na maamuma kama ilivyotangulia- je zitamtosheleza?”

 

Ninasema: “Hapa ni mahala pa ijtihaad, na madhehebu ya Maswahaba ni bora zaidi kufuatwa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

La tatu: Ni kupata chini ya rakaa pamoja na imamu

 

Al-Hasan, An-Nakh’iy, Az-Zuhriy, Qataadah na Maalik wanasema kwamba atapunguza kinyume na Jamhuri. Dalili zao ni:

 

1- Neno Lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenye kuipata rakaa moja katika Swalaah, basi kaipata Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake imeelezwa nyuma kidogo].Na huyu anakuwa hakuipata hukmu ya jamaa.

 

2- Mwenye kuipata rakaa moja ya Swalaah ya Ijumaa, basi ataikamilisha. Ama apataye chini ya hapo, faradhi yake haimwajibikii bali ataswali rakaa nne kama tutakavyokuja kueleza katika mlango wa Swalaah ya Ijumaa.

 

Ninasema: “Mwelekeo wa hili una nguvu, na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

  • Mkazi Kumfuata Msafiri

Ikiwa mkazi anaswali Swalaah ya rakaa nne nyuma ya msafiri, basi ni lazima akamilishe rakaa zote nne baada ya imamu wake kutoa tasliym kwa mujibu wa Maulamaa wote. [Al-Mughniy (2/152)]

Na imesuniwa kwa imamu awajulishe baada ya kutoa tasliym kwa kuwaambia: “Kamilisheni Swalaah yenu, sisi ni wasafiri”.

 

1- Imepokelewa na Ibn ‘Umar kwamba ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) alikuwa anapokwenda Makkah, huwaswalisha watu rakaa mbili kisha husema: “Enyi watu wa Makka! Kamilisheni Swalaah yenu, sisi ni wasafiri”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (195), Ibn Abi Shaybah (1/419), ‘Abdul Razzaaq (4369) na Al-Baghawiy (1029)].

Imesimuliwa mfano wake Hadiyth Marfu’u ya ‘Imraan bin Huswayn kuhusiana na kisa cha ukombozi wa Makka lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf.  Lakini ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) alikifanya kitendo hicho mbele ya Maulamaa Maswahaba na hakuna yeyote aliyempinga. Isitoshe, hakuna aliyekhalifiana naye, na hilo lilikuwa likifanyiwa kazi.

 

2- Kwa kuwa ni wajibu kwake kuswali rakaa nne, isingeliwezekana aache rakaa yoyote kama lau asingelimfuata msafiri.

  • Faida:

Msafiri akiwaswalisha watu wakiwemo wasafiri na wakazi, kisha wudhuu ukamtenguka baada ya rakaa, halafu mkazi akakamata mahala pake, nini kifanyike?

[Fat-hul Maalik Bitabwiyb At-Tamhiyd ‘Alaa Muwattai Maalik (3/133)]

 

(a) Pamesemwa: “Mkazi atakamilisha Swalaah ya imamu wa kwanza, kisha atawaashiria wanaomfuata wakae, halafu atasimama peke yake ili akamilishe rakaa nne. Baadaye atakaa tasha-hudi, na maamuma wasafiri walio nyuma yake watatoa tasliym. Halafu maamuma wakazi nao watasimama wakamilishe Swalaah peke yao. Hii ni kauli ya Maalik”.

 

(b) Pamesemwa: “Imamu wa pili atakamilisha Swalaah ya imamu wa kwanza, halafu atarudi nyuma, atamtanguliza msafiri ili amalize Swalaah na wasafiri watatoa tasliym pamoja naye, kisha wakazi watasimama kukamilisha rakaa zao zilizobakia kila mmoja peke yake. Hii ni kauli ya Abu Haniyfah na Maswahibu zake pamoja na Ath-Thawriy”.

 

(c) Pamesemwa: “Wote watakamilisha Swalaah ya mkazi”. Ni kauli ya Shaafi’iy, Al-Awzaaiy na Al-Layth.

  • Je, Swalaah Za Sunnah Huswaliwa Safarini?

Maulamaa wamekhitalifiana katika mas’-ala haya. Hii ni kutokana na kukhitalifiana mwonekano wa athari zenye kugusia aliyoyafanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) safarini. Wamekhitalifiana juu ya kauli tano:  [Fat-hul Baariy (2/674), Naylul Awtwaar (3/261), Zaad Al-Ma’ad (4738) na Al-Furu’u cha Ibn Muflih (2/59)]

 

1- Hairuhusiwi kabisa Swalaah za Sunnah safarini

 

Dalili yake ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Niliandamana na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), sikumwona akiswali Sunnah za Rawaatib safarini. Na Allaah Anatuambia:

((لقد كان لكم في رسول الله أسوة حسنة))

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1-11) na Muslim (689)].

Ibn ‘Umar alikuwa anasema anapowaona watu wakiswali Sunnah safarini: “Ningelikuwa ni mwenye kuswali Sunnah, ningeliswali kamili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (689) na At-Tirmidhiy (544)].

 

2- Inaruhusiwa Sunnah zote

 

Waliosema hivi ni Jamhuri. Wametoa dalili kwa Hadiyth zenye kusunisha kiujumla Swalaah zote za Sunnah na za Rawaatib, kuswali Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Dhuhaa siku ya ukombozi wa Makkah na rakaa mbili za Alfajiri wakati walipolala mpaka jua likachomoza.

 

3- Sunnah zote zinaruhusika lakini za Rawaatib haziruhusiwi

 

Ni chaguo la Sheikh wa Uislamu na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim, na kauli ya Ibn ‘Umar. Kigezo chao ni Ibn ‘Umar kukanusha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali Sunnah za Rawaatib pasina zinginezo isipokuwa rakaa mbili kutokana na yaliyothibiti toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah za Sunnah juu ya mgongo wa mnyama wake kule alikokuwa akielekea na kuashiria kwa kichwa chake. Ibn ‘Umar alikuwa akilifanya hilo. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1105) na Muslim (700) kwa mfano wake].

 

4- Za mchana haziruhusiwi lakini za usiku zaruhusiwa

 

Dalili ni Hadiyth ya ‘Abdullah bin ‘Aamir kwamba baba yake alimweleza kuwa alimwona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaswali Sunnah usiku safarini juu ya mnyama wake kule anakoelekea. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1104) na Muslim (689) kwa mfano wake].

 

Pia, ni kwa kutoacha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali Swalaah ya Witr akiwa nyumbani au safarini.

 

Ninasema: “Lakini kauli hii inachafuliwa na Swalaah ya Dhuhaa aliyoiswali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya ukombozi wa Makkah”.

 

5- Hairuhusiwi Sunnah baada ya Faradhi lakini inajuzu kabla yake na kwa Sunnah zozote

Ni kauli ya Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake. Al-Haafidh kaitilia nguvu akisema: “Tofauti kati ya Sunnah za kabla ya Faradhi na baada yake ni kuwa zile za kabla haziingii katika dhana kwamba ni sehemu ya Faradhi kwa kuwa zimejitenga nayo kwa iqaamah, kumngojea imamu na mfano wa hivyo, kinyume na za baada ya Faradhi ambazo aghlabu huhusiana nayo, na zinaweza kuwekwa katika dhana kwamba ni sehemu ya faradhi”.

 

Ninasema: “Asili ya hili ni kuthibiti kuswali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) rakaa mbili kabla ya Alfajiri katika safari”.

 

 

Pili: Kukusanya Kati Ya Swalaah Mbili

  • Taarifu Yake

Kukusanya kati ya Swalaah mbili ni kuswali Adhuhuri na  Alasiri, au  Magharibi na  ‘Ishaa kwa pamoja katika wakati wa moja ya Swalaah mbili kwa mkusanyo wa kutanguliza au mkusanyo wa kuchelewesha.

  • Kujuzu Kwake

Kukusanya kati ya Swalaah mbili kunajuzu kwa kauli ya Maulamaa wote lakini wamekhitalifiana upande wa miundo ya kukusanya na sifa yake kama tutakavyokuja kuchambua baadaye.

 

1- Kukusanya safarini:

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na hukmu ya kukusanya Swalaah mbili safarini juu ya kauli mbili:

 

Ya kwanza: Haijuzu kukusanya isipokuwa katika Siku ya Arafah na usiku wa kuweko Mahujaji Muzdalifah. Hii ni kauli ya Abu Haniyfah na riwaya toka kwa Maalik, Al-Hasan na Ibn Syriyn. Dalili yao ni: [Al-Mabsuwtw (1/235), Sharhul Ma’aaniy (1/162), Al-Mudawwanah (1/116) na Al-Mughniy (2/200)]

 

1- Kauli Yake Ta’alaa:

((إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا))

((Hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu)). [An-Nisaa (:103)]

Nyakati za Swalaah zimethibiti kwa “Tawaaturi”, hivyo haijuzu kuziacha kwa habari ya “Aahaad”.

 

2- Hadiyth ya Ibn Mas-’oud aliposema: “Sikumwona Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali Swalaah yoyote katika wakati usio wake isipokuwa Swalaah mbili: Alipokusanya  Magharibi na  ‘Ishaa Muzdalifah, na aliposwali Alfajiri siku ile kabla ya wakati wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1682) na Muslim (1289)].

 

3- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Kupoteza jambo hakupatikani mtu anapolala, lakini kupoteza ni mtu anapokuwa macho)).

Wanasema: “Kitovu cha kulipoteza jambo au kutolipoteza, kimefanywa katika hali ya kuwa macho au usingizini, na hayo hayahusishwi na ukazi au safari, na mkazi na msafiri wako sawa.

 

Ya pili: Inajuzu kukusanya kati ya  Adhuhuri na  Alasiri, na kati ya  Magharibi na  ‘Ishaa. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Ath-Thawriy, Is-Haaq, Abu Thawr, na Ibn Al-Mundhir. Imesimuliwa na kundi la Maswahaba akiwemo Mu’aadh, Abu Musa, Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar. [Al-Mudawwanah (1/116), Bidaayatul Mujtahid (1/248), Al-Majmu’u (4/225), Al-Mughniy (2/200) na Naylul Awtwaar (3/253)]

Dalili yao ni:

 

1- Hadiyth ya Anas aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposafiri kabla jua halijapinduka, huchelewesha  Adhuhuri hadi wakati wa  Alasiri, kisha huteremka na kukusanya Swalaah mbili. Na ikiwa limeshapinduka kabla hajasafiri, huswali  Adhuhuri, kisha hupanda mnyama wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1111) na Muslim (704)].

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakusanya kati ya  Magharibi na  ‘Ishaa mwendo ukiwa mrefu kwake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1106) na Muslim (45)].

 

3- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakusanya Swalaah ya  Adhuhuri na  Alasiri akiwa safarini, na hukusanya kati ya  Magharibi na  ‘Ishaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1107)].

 

Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal aliyesema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakusanya kati ya  Adhuhuri na  Alasiri, na kati ya  Magharibi na  ‘Ishaa katika vita vya Tabuk. [Akaichelewesha Swalaah siku moja, kisha akatoka, akaswali  Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja. Kisha akaingia, halafu akatoka, akaswali  Magharibi na ‘Ishaa kwa pamoja]”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (706), Ibn Maajah (1070) bila nyongeza, Abu Daawuud (1201) na An-Nasaaiy (1/285)].

 

Hadiyth hizi na nyinginezo zinaonyesha kwa mwonekano wake na ujumuishi wake kwamba inajuzu kukusanya kati ya Swalaah mbili katika safari, sawasawa ikiwa ni “Jam-’u Taqdiym” au “Jam-’u Taakhiyr”.

 

Wenye kauli ya kwanza wamezichukulia Hadiyth hizi kama ni “ukusanyaji wa kipicha”, nako ni kucheleweshwa Magharibi kwa mfano mpaka mwisho wa wakati wake na kuharakishwa  ‘Ishaa mwanzoni mwa wakati wake!!

 

Hili limetolewa neno lisemalo:” Kukusanya ni ruksa. Na kama kutakuwa kama walivyoeleza, basi ingelikuwa ni dhiki zaidi kuliko kuiswali kila Swalaah katika wakati wake, kwa kuwa mianzo ya nyakati na miisho yake hawaidiriki wajuzi wengi sembuse watu wa kawaida. Aidha, Hadiyth zimekuja zikibainisha wakati mmoja wa Swalaah mbili, na hili ndilo linalofahamika katika tamko la kukusanya”. [Fat-hul Baariy (2/675) chapa ya As-Salafiyyah]

Ama neno lao: “Hatuachi habari “Mutawaatir” kwa Hadiyth hizi, basi sisi tunasema:”Hatuziachi, bali tunazikhusisha nazo, na kuihusisha Mutawaatir na khabar Swahiyh, kunajuzu kwa Ijma’a ya Maulamaa”. [Al-Mughniy (2/201)]

 

Ama Hadiyth ya Ibn Mas-’oud, inavyoonekana ni kuwa haikusudii Ijma’a kwa pande mbili: Ni kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikusanya baina ya  Adhuhuri na  Alasiri Arafah, hivyo uainisho huo si sahihi. Halafu hakuna yeyote aliyesema kwamba Alfajiri iliswaliwa kabla ya wakati wake, bali makusudio ni kuharakia zaidi kuiswali.

Isitoshe, kuna wengineo zaidi ya Ibn Mas-’oud walioshuhudia kwa macho yao kukusanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah safarini kwingineko kusiko Arafah na Muzdalifah. Na bila shaka, mwenye dalili hutangulizwa kabla ya asiye nayo, naye amekanusha na wengine wamethibitisha, na mthibitishaji hutangulizwa kabla ya mkanushaji pakizingatiwa kwamba Ibn Mas-’oud kasema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakusanya kati ya Swalaah mbili safarini.  [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Ya’alaa (5413), At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (10/39) na At-Twahaawiy katika Sharhul Ma’aaniy (1/160)].

 

2- Kukusanya mjini anakoishi mtu

 

Kukusanya Swalaah mbili hakuhusishwi na safari tu, bali inajuzu kukusanya mtu akiwa mjini kwake kwa sababu hizi zifuatazo:

 

(a) Mvua

 

Inajuzu kukusanya  Adhuhuri na  Alasiri, au  Magharibi na  ‘Ishaa kutokana na mvua kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri. Lakini Maalik amekuhusisha kujuzu huko kwa usiku tu na si mchana!! Dalili zao ni hizi zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikusanya baina ya  Adhuhuri na  Alasiri, na  Magharibi na  ‘Ishaa Madiynah bila kuweko vita wala mvua”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (705). Angalia Al-Irwaa (579)].

 

Hili linatufahamisha na kutuhisisha kwamba kukusanya Swalaah kutokana na mvua kulikuwa kunajulikana wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na lau kama isingelikuwa hivyo, kusingelikuwa na faida ya kukanusha mvua kama ni sababu ya kuruhusu kukusanya Swalaah. [Irwaaul Ghaliyl (3/40)]

 

2- Imepokelewa toka kwa Naaf’i akisema kwamba Ibn ‘Umar alikuwa anapowakusanya viongozi baina ya  Magharibi na ‘Ishaa wakati wa mvua, hukusanya Swalaah hizo pamoja nao. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (333) na Al-Bayhaqiy kutoka kwake].

 

3- Imepokelewa toka kwa Hishaam bin ‘Urwah kwamba baba yake ‘Urwah, Sa’iyd bin Al-Musayyib na Abu Bakr bin ‘Abdul Rahmaan bin Al-Haarith bin Hishaam bin Al-Mughyrah Al-Makhzoumiy, walikuwa wakikusanya baina ya  Magharibi na ‘Ishaa katika usiku wa mvua, na hawalioni hilo kama tatizo. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/168). Angalia Al-Irwaa (3/40)].

 

4- Imepokelewa toka kwa Muusa bin ‘Uqbah ya kwamba ‘Umar bin ‘Abdul Aziyz alikuwa akikusanya baina ya  Magharibi na ‘Ishaa ya mwisho kama kuna mvua. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/168). Angalia Al-Irwaa (3/40)].

 

(b) Haja ya dharura

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja Madiynah bila kuwepo vita au mvua”. Abu Kurayb au Sa’iyd akamuuliza: “Kwa nini alifanya hivyo?” Akajibu: “Ili asiusumbue na kuutaabisha umma wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (705) na Ahmad (1/223)].

 

Katika hili, pana ruksa kwa wenye nyudhuru ili kuwaondolea tabu na mashaka kinyume na wale wasio na nyudhuru kama hizi. Hii ni kauli ya Ibn Syriyna na Ash-hab mfuasi wa karibu wa Maalik. Al-Khattwaabiy ameisimulia toka kwa Al-Qaffaal Ash-Shaasiy mfuasi wa karibu wa Ash-Shaaf’iy toka kwa Is-Haaq Al-Marouziy toka kwa jumuiko la Maulamaa wa Hadiyth. Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah wamelikhitari. [Majmu’u Al-Fataawaa (24/25), Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (2/3509), Al-Qawaaniyna (75) na Ma’aalim As-Sunan (2/55)]

 

Sheikh wa Uislamu amesema: “Ikiwa itakuwa uzito kwa wazalishaji viwandani na wakulima wakati wa Swalaah unapoingia kama maji kuwa mbali nao, au kama watayaendea ili kujitwaharisha kazi yao itasimama, basi wanaweza kuswali katika wakati mmoja kwa kukusanya Swalaah mbili”. [Majmu’u Al-Fataawaa (21/458)]

  • Mgonjwa

Mgonjwa ambaye inakuwa uzito kwake kuiswali kila Swalaah katika wakati wake, anaruhusiwa kukusanya kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia na kwa kuchukulia kipimo cha mwanamke mwenye damu ya Istihaadhwah. Inasimuliwa kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru Hamnah bint Jahsh ambaye alikuwa akisumbuliwa sana na damu ya Istihaadhwah kwa kumwambia:

((Ikiwa utahimili kuichelewesha  Adhuhuri na kuiwahisha  Alasiri, kisha ukaoga wakati unapotwaharika ukaswali Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja, halafu ukaichelewesha Magharibi na kuiwahisha isha, kisha ukaoga na kuzikusanya Swalaah mbili, basi fanya)). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (287), At-Tirmidhiy (128) na Ibn Maajah (627). Angalia Al-Irwaa (188). Inaonekana kama kuipitisha kama Hadiyth Hasan kuna angalizo].

 

 

 

Maalik na Ahmad wamejuzisha mgonjwa kukusanya Swalaah. Sheikh wa Uislamu kalikhitari hilo, lakini Ash-Shaafi’iy kakataa. [Al-Qawaaniyn (75), Al-Mughniy (2/112) na Al-Majmu’u (4/370)]

 

Kauli ya kujuzu hilo iko wazi, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

  • Je, Ni Sharti Kuandamisha Kati Ya Swalaah Mbili Zinazokusanywa?

[Al-Kharshafiy (2/70), Al-Majmu’u (3/375), Al-Inswaaf (2/342), Al-Mughniy (2/132) na Majmu’u Al-Fataawaa (24/54-56)]

 

1- Akiziswali katika wakati wa Swalaah ya pili (jam’u taakhiyr), basi si sharti kuandamisha baina ya Swalaah mbili zinazokusanywa, bali anaweza kuachanisha kati yao. Kwa mfano, anaweza kuswali  Adhuhuri mwanzo wa wakati wa  Alasiri, kisha akaichelewesha  Alasiri kidogo akaja kuiswali kabla  wakati wake haujatoka. Hii ni kauli ya Jamhuri kinyume na baadhi ya Mahanbali.

 

2- Akiziswali katika wakati wa Swalaah ya kwanza (Jam-’u Taqdiym), Jamhuri wanasema kwamba ni lazima aziswali bila kuziachanisha. Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah amekhalifiana nao kwa kusema kwamba hilo halishurutishwi. Ni riwaya toka kwa Ahmad, na kauli ya Ash-Shaafi’iy, na hili lakubalika zaidi.

 

Ibn Taymiyah kasema: “Si sharti kuandamisha kati ya Swalaah mbili, si katika wakati wa Swalaah ya kwanza wala ya pili. Hilo halina mpaka katika sharia, na kulichunga kunaangusha makusudio ya ruksa. Na Sunnah imekuja kwa upana zaidi ya hivyo, kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikusanya mwanzo wa wakati kama alivyofanya ‘Arafah, na wakati mwingine alikusanya katika wakati wa Swalaah ya pili kama alivyofanya Muzdalifah na katika safari zake nyinginezo. Pia, wakati mwingine alikusanya katikati ya nyakati za Swalaah mbili, na katika hali hii zinaweza kuwa mwishoni mwa wakati wa Swalaah ya kwanza, au mwanzoni mwa wakati wa Swalaah ya pili”.

 

Swalaah ya pili inaweza kuswaliwa wakati wa Swalaah ya kwanza, na ya kwanza wakati wa Swalaah ya pili, yote yanajuzu. Hii ni kwa vile asili ya suala hili ni kuwa wakati unakuwa ni mmoja ikitokea haja, na kutanguliza na kuweka kati ni kwa sababu ya maslaha.

  • Kukusanya Kwa Adhana Moja Na Iqama Mbili

Imesuniwa wakati wa kukusanya Swalaah mbili kutosheka na adhana moja tu na kuqimu kwa kila Swalaah. Katika Hadiyth ya Jaabir, anasema kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah mbili Arafah kwa adhana moja na iqama mbili. Akaenda Muzdalifah, akaswali hapo Magharibi na ‘Ishaa kwa adhana moja na iqamah mbili. Hakuswali Sunnah kati yake, kisha akalala kwa ubavu mpaka ilipochomoza Alfajiri. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja kamili na “takhriyj” yake katika Mlango wa Hijjah InshaAllaah].

 

Imepokelewa na Ibn Mas-’oud akisema: “Tukafika Muzdalifah wakati inaadhiniwa ‘Ishaa au muda kidogo kabla yake, akamwamuru mtu mmoja aadhini na kuqimu kisha akaswali  Magharibi. Baada yake aliswali rakaa mbili, halafu aliagiza mlo wake wa usiku akala, kisha akamwamuru Uraa aadhini na kuqimu, halafu akaswali  ‘Ishaa rakaa mbili….”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1675) na Muslim 1289) kwa mfano wake].

 

Huu ni mwelekeo wa Ash-Shaafi’iy katika madhehebu yake ya zamani, na riwaya toka kwa Ahmad na Ibn Hazm. Lakini Ath-Thawriy, Ahmad katika riwaya nyingine na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya, wanaona kwamba atakusanya Swalaah mbili kwa iqaama mbili tu. Wameishikilia Hadiyth ya Usaamah anayesema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuja Muzdalifah aliteremka, akatawadha, akaufanya vyema wudhuu wake. Halafu Swalaah ikaqimiwa, akaswali  Magharibi na kisha kila mtu alimtua ngamia wake nyumbani kwake. Halafu ‘Ishaa ikaqimiwa akaswali, na wala hakuswali Swalaah yoyote baina ya Swalaah mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1672), Muslim (1280) na Ahmad (5/263)].

 

La sawa ni hayo waliyoyasema hao wa mwanzo kwa kuwa Hadiyth ya Jaabir imejumuisha ziada ya adhana, nayo ni ziada isiyo kanushi, hivyo ni lazima kuikubali. [Naylul Awtwaar (3/263) chapa ya Al-Hadiyth]

Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

  • Kufatanisha Kati Ya Swalaah Mbili Zinazokusanywa

Ni sharti kuwepo mpangilio kati ya Swalaah mbili zinazokusanywa, kwa kuwa sharia imekuja na mpangilio maalumu wa nyakati za Swalaah zote. Hivyo, ni wajibu kila Swalaah iwe katika mahala pake ilipopangiwa na sharia kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)).

Lakini, lau kama mtu atasahau, au akawa hajui, au akawakuta watu wanaswali ‘Ishaa huku yeye kanuwia “Jam-’u Taakhiyr”, akaswali nao ‘Ishaa halafu akaswali  Magharibi, je itamtosheleza? Mafuqahaa wanasema kwamba haitofaa, Swalaah yake ya ‘Ishaa itakuwa ni batili, na itambidi aswali tena ‘Ishaa baada ya  Magharibi. [Sharhul Mumti’i (4/576)]

 

Share