042-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Safu Na Hukmu Zake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

042-Safu Na Hukmu Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

· Safu Bora Zaidi Kwa Upande Wa Wanaume Na Wanawake

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Safu bora zaidi ya wanaume ni ya kwanza, na ya shari yake zaidi ni ya mwisho, na safu bora zaidi ya wanawake ni ya mwisho, na ya shari yake zaidi ni ya kwanza)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (440), Abu Daawuud (678), At-Tirmidhiy (224), An-Nasaaiy (2/93) na Ibn Maajah (1000)].

 

Ninasema: “Safu ya mwisho ya wanawake kuwa ni bora zaidi mahala pake ni pale wanawake wanapokuwa wanaswali nyuma ya safu za wanaume. Na ikiwa wanaswali nyuma ya mwanamke, au na imamu mwanamume katika mahala palipotenganishwa na wanaume, basi safu yao bora itakuwa ni ya kwanza. Hii ni kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakika Allaah na Malaika Wake Wanazitakia rahma safu za mwanzo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (664), An-Nasaaiy (2/90) na Ibn Maajah (997)].

 

Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Fadhila Za Safu Ya Kwanza

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Na lau wangelijua yaliyoko kwenye safu ya mbele, basi wangelipiga kura)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (720) na Muslim (437-439)].

 

Na katika tamshi la Muslim: ((..ingelifanyika kura)).

 

· Fadhila Ya Upande Wa Kulia Wa Safu

 

Imepokelewa toka kwa Al-Barrai akisema: “Tulikuwa tunaposwali nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tunapenda kuwa kulia kwake akituelekea kwa uso wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (709), Abu Daawuud (615), An-Nasaaiy (2/94) na Ibn Maajah (1006)].

 

Imepokelewa kwa njia Marfu’u toka kwa ‘Aaishah akisema: “Hakika Allaah na Malaika Wake Huwatakia rahma walioko kuumeni mwa safu”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (676) na Ibn Maajah (1005). Al-Bayhaqiy kaitia dosari matni yake (3/103) akisema kwamba haikuhifadhiwa. Al-Albaaniy kaipitisha kwenye Tamaam Al-Minnah (uk. 228), nayo ni kama walivyosema. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi].

 

Lakini Hadiyth hii haikuhifadhiwa kwa tamshi hili.

 

· Wanaosimama Nyuma Ya Imamu

 

Imepokelewa toka kwa Ibn Mas-’oud (Radhwiya Allahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Wasimame nyuma yangu wale wenye akili na wajuzi miongoni mwenu, kisha wale wanaowafuatia (mara tatu). Na jiepusheni na vurugu za sokoni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” Muslim (432), Abu Daawuud (675), na At-Tirmidhiy (228)].

 

Hadiyth hii inatuarifu kwamba wa kuwa nyuma ya imamu ni mtu mweledi zaidi kisha mjuzi zaidi. Kwa kuwa imamu anastahiki zaidi kuwa karibu na mtu huyo, kwani anaweza kumhitajia akamate uimamu badala yake, na pia anaweza kumkumbusha kama atasahau kitu ambacho wengine hawawezi. Aidha, weledi hao wataitoa picha halisi ya Swalaah, wataihifadhi na watu watajifunza kutoka kwao. Na kwa ajili hiyoRasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapenda Muhaajiruwna na Answaar wakae nyuma yake ili wajifunze kutoka kwake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (977), Ahmad (3/100) na wengineo].

 

· Kukamilisha Safu Ya Kwanza Kisha Inayoifuatia

 

Imepokelewa toka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Kamilisheni safu ya kwanza kisha inayoifuatia, na kama kuna upungufu, basi uwe kwenye safu ya mwisho)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/93) na Abu Daawuud (671)].

 

Na imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samrah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea akasema: ((Mbona nawaona mnanyanyua mikono yenu kana kwamba ni mikia ya farasi waliochacharika? Tulieni katika Swalaah)). Akasema: Kisha akatutokea akatuona tumejigawa mafungu mafungu akatuambia: (( Kwa nini msipange safu kama wanavyopanga safu Malaika mbele ya Mola wao?)) Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni vipi Malaika wanapanga safu mbele ya Mola wao? Akasema: ((Wanaikamilisha safu ya kwanza na wanazinyoosha safu zao)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (430), Abu Daawuud (661), An-Nasaaiy (2/92) na Ibn Maajah (992)].

 

· Wajibu Wa Kunyoosha Safu Na Kuziba Mianya

 

Kuna Hadiyth nyingi Swahiyh zinazozungumzia suala hili. Kati yake ni:

 

1- Hadiyth ya An-Nu’umaan bin Bashiyr aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika mtazinyoosha safu zenu, au Allaah Atakhitilafisha kati ya nyuso zenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (717) na Muslim (436)].

 

Maana ya: “Allaah Atakhitilafisha kati ya nyuso zenu”, ni kuwa Ataingiza uadui na chuki kati yenu, na nyoyo zenu zitakhitalifiana. Kwa kuwa kukhitalifiana kidhahiri, ni sababu ya kukhitalifiana kindani. Maana hii inatiliwa nguvu na:

 

2- Hadiyth ya Abu Mas-’oud aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipapasa mabega yetu katika Swalaah na kutuambia: ((Simameni sawa na msikhitalifiane, la sivyo nyoyo zenu zitakhitalifiana)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (432), Abu Dawuud (674), An-Nasaaiy (2/87) na Ibn Maajah (976)].

 

3- Imepokelewa toka kwa Anas toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba kasema: ((Lingamanisheni safu zenu, kwani hakika mimi nawaoneni kwa nyuma yangu)). Mmoja wetu alikuwa akilinatisha bega lake na bega la mwenzake, na unyayo wake kwa unyayo wake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (725) na Muslim (434)].

 

4- Anas anasema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Zinyorosheni sawa safu zenu, ziwekeni karibu karibu, na kuweni sambamba kwa shingo zenu. Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, hakika mimi namwona Shaytwaan anaingia kupitia mianya ya safu kana kwamba ni kondoo wadogo weusi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (667), An-Nasaaiy (2/92), na Ahmad (3/260)].

 

5- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Lingamanisheni safu, yawekeni mabega sambamba, zibeni mianya, kuweni laini ndugu zenu wakiwashika mikono, na wala msiache nafasi wazi kwa Shaytwaan. Na mwenye kuunga safu, Allaah Humuunga, na mwenye kuikata safu, Allaah Humkata)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (666), An-Nasaaiy (2/93) na Ahmad (2/97)].

 

6- Imepokelewa toka kwa Anas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Zisawazisheni safu zenu, kwani kuzisawazisha safu ni sehemu ya kuisimamisha Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” kwa tamko hili na Al-Bukhaariy (723), na kwa jingine Muslim (434), na wengineo].

 

• Imamu anatakiwa yeye mwenyewe azinyoroshe safu au awaamuru maamuma wafanye hivyo, na asihirimie Swalaah ila baada ya safu kulingamana sawa. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Umar alikuwa hahirimii mpaka safu zilingamane sawa, huwapa jukumu kwa hilo watu”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (2439)].

 

· Faida

 

An-Nawawiy kasema kwenye Al-Majmu’u (4/297): “Kama mwenye kuingia kwenye safu atakuta mwanya au nafasi wazi, basi ataingia. Ikiwa safu ya mbele imepwaya, basi anaweza kuipasua safu ya nyuma yake iliyo jaa ili kuziba pengo, kwa kuwa hilo ni kosa la maamuma wa mwanzo”.

 

· Ukaraha Wa Kupanga Safu Kati Ya Nguzo

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdul Hamiyd bin Mahmoud akisema: “Niliswali pamoja na Anas bin Maalik siku ya Ijumaa. Tukasogezwa kwenye nguzo, nasi tukasogea mbele na tukarudi nyuma. Anas akasema: Tulikuwa tukijiepusha na hili katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (673), An-Nasaaiy (2/94), At-Tirmidhiy (229) na Ahmad (3/131). Imeelezwa kama ni Dhwa’iyf kwa vipimo visivyokubalika].

 

Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Mu’aawiyah bin Murrah toka kwa baba yake akisema: “Tulikuwa tukikatazwa kupanga safu kati ya nguzo wakati wa uhai wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na tunafukuzwa tuwe mbali nazo kabisa”.[Isnadi yake ni Laini: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1002), Ibn Khuzaymah (1567), Ibn Hibaan (2219) na Al-Haakim (1/218). Inatiliwa nguvu na Hadiyth ya kabla yake].

 

Na kwa ajili hiyo, ni karaha kwa maamuma kusimama kati ya nguzo za Msikiti kwa kuwa nguzo hizo huzikata safu zao. Lakini ikiwa safu ni fupi ya kuweza kujaza nafasi kati ya nguzo mbili, basi hakuna ukaraha kwa kuwa safu haikatwi. Ibn Mas-’oud, An-Nakh’iy, Ibn Al-Mundhir toka kwa Hudhayfah na Ibn ‘Abbaas wamelikirihisha hilo wakati ambapo Ibn Syriyna, Maalik na Aswhaabu Ar Ra’ay wameliruhusu. Wamesema kwamba hakuna dalili yoyote inayozuia hilo!! [Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (4/181-182)].

 

Na hakuna shaka yoyote kwamba Hadiyth ya Anas ina hukmu ya Umarfu’u, na inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Qurrah bin Qays. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Ama ikiwa ni imamu na maamuma mmoja tu, basi hakuna ukaraha wa kusimama baina ya nguzo mbili kwa sababu tuliyokwishaieleza. Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia nyumbani akiwa pamoja na Usamah bin Zayd, ‘Uthmaan bin Twalha na Bilaal. Akapotea huko kwa muda kisha akatoka. Nilikuwa mtu wa kwanza kuingia baada yake, nikamuuliza Bilaal: Ameswalia wapi? Akasema: Kati ya nguzo mbili za mbele”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (504) na Muslim (1329)].

 

· Anayeswali Peke Yake Nyuma Ya Safu

 

Asili katika Swalaah ya Jamaa ni kuwa maamuma wanatakiwa wawe kwenye safu zilizopangana sawa kama ilivyoelezwa. Na ikiwa maamuma ataswali peke yake nyuma ya safu, basi Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na hukmu ya Swalaah yake katika kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Ni kwamba Swalaah yake haiswihi. Ni kauli ya Ahmad, Is-Haaq, An-Nakh’iy, Ibn Abu Shaybah na Ibn Al-Mundhir. [Al-Awsatw (4/183), Al-Mughniy (2/211) na Al-Mumti’i (4/376)].

 

Dalili zao ni hizi zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya ‘Aliy bin Shaybaan aliyesema: “Tulitoka mpaka tukafika kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tukampa Bay-’ah na tukaswali nyuma yake. Halafu tuliswali nyuma yake Swalaah nyingine, na alipomaliza alimwona mtu mmoja anaswali peke yake nyuma ya safu. Alipomaliza, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama mbele yake na kumwambia:  (( Ielekee Swalaah yako, hakuna Swalaah kwa aliye nyuma ya safu)).  [Hadiyth Swahiyh kwa isnadi nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1003), Ahmad (3/23), na Ibn Hibaan (2202)].

 

2- Hadiyth ya Waabiswah bin Ma’abad ya kwamba mtu mmoja aliswali peke yake nyuma ya safu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru aswali tena upya. [Hadiyth Swahiyh kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (230,231), Abu Daawuud (682), Ibn Maajah (1004) na Ahmad (4/228). Angalia Al-Irwaa (541)].

 

Wamesema: “Lau kama Swalaah yake ingelikuwa imeswihi, basi asingemwamuru aiswali tena. Kwa kuwa kufanya upya ni wajibiko na taklifu katika jambo ambalo limeshafanywa na kumalizika, na lau kama si kuharibika kwake, asingelimkalifisha kulifanya tena upya”.

 

Ya pili:

 

Swalaah yake inaswihi, lakini ni karaha kusimama peke yake bila ya udhuru. Ni kauli ya Abu Haniyfah na Maswahibu zake, Maalik, Al-Awzaaiy na Ash-Shaafi’iy. [Al-Badaai-’i (1/218), Mughnil Muhtaaj (1/247), Jawaahirul Ikliyl (1/80), na Al-Awsatw (4/183)].

 

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Bakrah ambaye alimwahi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa katika rukuu. Akarukuu kabla hajafika kwenye safu. Akalieleza hilo kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Rasuli akamwambia: ((Allaah Akuzidishie pupa, lakini usifanye tena)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (783), Abu Daawuud (683), An-Nasaaiy (2/118) na Ahmad (5/39)].

 

Wamesema: “Abu Bakrah aliifanya nguzo moja ya Swalaah nyuma ya safu lakini hakuamuriwa kuswali tena upya. Alilokatazwa ni kutokifanya tena kitendo hicho, kana kwamba ameelekezwa kwa lile lililo bora zaidi. Wamelitolea dalili hilo ya kwamba agizo la kuiswali tena upya Swalaah kwenye Hadiyth ya Waabiswah ni agizo la Sunnah, ikiwa ni kukusanya kati ya dalili mbili”.

 

Wa mwanzo wamejibu wakisema: Zinaweza kukusanywa kwa njia nyingine. [Fat-hul Baariy (2/314) chapa ya As-Salafiyyah, na Majmu’u Al-Fataawaa (23/397)].

 

Nayo ni kuwa Hadiyth ya Abu Bakrah ni mahsusi kwa ujumuishi wa Hadiyth ya Waabiswah. Mwenye kuanza kuswali peke yake nyuma ya safu, kisha akaingia kwenye safu kabla ya kusimama toka kwenye rukuu, basi si lazima aswali tena kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Abu Bakrah. Na kama si hivyo, basi ni lazima airejeshe tena kwa mazingatio ya ujumuishi wa Hadiyth za Waabiswah na ‘Aliy bin Shiybaan.

 

2- Ni kwamba Ibn ‘Abbaas wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomzungusha toka kushoto hadi kulia – na Hadiyth hii ishazungumzwa mara nyingi - alikuwa ameswali peke yake nyuma yake kwa sehemu ndogo ya Swalaah!! Wanasema: Chenye kuharibu Swalaah hakina tofauti kati ya kingi chake na kichache chake.!!

Wamejibiwa: Kwa mfano wa yaliyotangulia katika Hadiyth ya Abu Bakrah ni kuwa hakuna madhara yoyote kwa picha hii ndogo ya mtu kusimama peke yake nyuma ya safu kabla hajaingia.

 

3- Wameuchukulia ukanushi kwenye neno lake: “Hakuna Swalaah kwa aliye nyuma ya safu”, kama ni ukanushi wa ukamilifu na si ukanushi wa kuswihi.

Hili limejibiwa kwamba asili ni kukanusha uwepo, - na hili haliwezekani - kisha kukanusha uswihifu mpaka dalili ithibitishe kutowezekana kwake, na hapo pataelekewa kwenye ukanushi wa ukamilifu. Na hapa hakuna dalili vile vile. Kisha hili linakataliwa kwa amri yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuswali tena kama ilivyotangulia.

 

4- Kuswali Ummu Sulaym peke yake kwenye safu nyuma ya Anas na yatima wakimfuata Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Limejibiwa kwamba hii ni hoja dhaifu isiyoweza kuipinga hoja ya katazo. Kwani kusimama mwanamke nyuma ya safu ya wanaume ni Sunnah amuriwa. Na lau kama mwanamke atasimama kwenye safu ya wanaume, basi hilo litakuwa ni makruhu, na halifai kwa kipimo. Halafu isitoshe, mwanamke huyo alisimama peke yake nyuma ya safu kwa kuwa hakukuweko mwanamke mwingine wa kusimama naye, na lau kama angelikuweko, basi angelazimika kusimama pamoja naye, na hukmu yake ingelikuwa ni ya mwanamume anayeswali peke yake nyuma ya safu ya wenzake.  [Majmu’u Al-Fataawaa (23/395)].

 

Ya tatu:

 

Ikiwa atasimama peke yake kwa sababu ya udhuru, Swalaah itaswihi na kama si hivyo, itabatilika. Ni kauli ya Al-Hasan Al-Baswriy na Hanafi. Imekhitariwa na Sheikh wa Uislamu na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim, na imetiliwa nguvu na Ibn ‘Uthaymiyn. [Al-Badaai-’i (1/218), Al-Inswaaf (2/289), Majmu’u Al-Fataawaa (23/396), I’ilaam Al-Muwaqqi’iyna (2/41), Tahdhiyb As Sunan (2/266-Al’Awn) na Al-Mumti’i (4/383)].

 

Hoja yao ni dalili za kauli ya pili lakini wamesema kwamba ukanushi wa kuswihi hauwi isipokuwa kwa kitendo kilichoharamishwa, au kwa kuacha wajibu. Na qaaidah inasema: Wajibu haupo kwa kushindwa.

 

Ninasema: “Huenda hii ndio kauli inayokubalika zaidi, kisha kauli ya kwanza. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.”

 

· Rai

 

“Ninalolihisi ndani ya nafsi yangu ni kuwa muradi wa neno lake Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Anayeswali peke yake nyuma ya safu hana Swalaah)), ni kuwa anayekusudiwa ni yule mwenye kuswali nyuma ya safu za watu kivyake, na hapo Hadiyth itakuwa haina mushkil. Lakini sikupata yeyote aliyetangulia mwenye ufahamu huu (ingawa ufahamu huu una nguvu na unakubaliana na Uswuul za Sharia). Hivyo siwezi kuthubutu kulikata hilo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

· Aliyeingia Akakuta Safu Zimejaa, Nini Afanye?

 

[Al-Badaai-’i (1/218), Fat-hul Qadiyr (1/309), Jawaahirul Ikliyl (1/80), Mughnil Muhtaaj (1/248), Al-Majmu’u (4/297), Kash-Shaaful Qinaa (1/490), Al-Inswaaf (2/289), Al-Mughniy (2/216), Al-Awsatw (4/185) na Al-Mumti’i (4/383)].

 

Mtu anatakiwa ajiepushe kuswali peke yake nyuma ya safu kiasi inavyowezekana ili asiingie kwenye ukaraha uliozungumzwa na Jamhuri. Swalaah itafaa kwa mujibu wa kauli ya Hanafi:

 

1- Akikuta nafasi katika safu ya mwisho atasimama hapo.

 

2- Akikuta nafasi kwenye safu ya mbele, atazipasua safu ili aifikie kwa kuwa waliotangulia wamefanya kosa la kutoijaza. Na kama hakupata nafasi isipokuwa kusimama pembeni ya imamu, basi atafanya hivyo. Dalili za hili zishaelezwa nyuma.

 

3- Kama hakuna mtu wa kusimama naye, je atamvuta mtu toka kwenye safu ili asimame naye?

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na hili. Hanafi, Hanbali na Ash-Shaafi’i wamelijuzisha. Pia imepokelewa toka kwa ‘Atwaa na An-Nakh’iy. Hii ni kwa vile kuna udharura wa kufanya hivyo. Ash-Shaafi’iy kalifungamanisha hilo na kuidadisi hali ya mvutwa kama ni mtu wa kukubali au la ili kuepusha mgogoro. Ahmad na Is-Haaq wanaona ni bora kumgusa ili arudi nyuma badala ya kumvuta.

 

Ninasema: “Asili ya kujuzu kumvuta mtu nyuma toka kwenye safu, ni Hadiyth ya Ubayya bin Ka’ab iliyoelezwa nyuma wakati alipomvuta mtu na kusimama mahala pake. Alipomaliza alimwambia: “Hakika hii ni amri toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu ya kwamba tumfuate..” [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa kwenye kipengele cha “Nani anayemfuata imamu?”]

 

Lakini kuna matahadharisho mengineyo yanakuja.

 

Maalik anaona ni makruhu mtu kumvuta mwingine akasema: Ataswali peke yake, na mwenye kuvutwa asikubali, na hili limepokelewa toka kwa Al-Awzaaiy, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. Katika kuvuta huku, kuna matahadharisho ambayo ni:

 

1- Kutamletea tashwishi mvutwaji.

 

2- Mvutwaji atafanyiwa kosa kwa kutolewa sehemu aliyokwishaanza kuizoea.

 

3- Kutaacha nafasi kwenye safu na huenda hili likawa ni mlango wa kuikata safu. Makemeo juu ya hili yashaelezwa nyuma.

 

4- Safu nzima itafanyiwa kosa, kwa kuwa watasogea kwa ajili ya kujaza mwanya.

 

Ninasema: “Ni bora asimvute mtu, bali aswali peke yake kutokana na udhuru. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

 

Share