053-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Yanayotendwa Katika Swalaah Ya Ijumaa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

053-Yanayotendwa Katika Swalaah Ya Ijumaa 

 

Alhidaaya.com

 

 

· Kiasili Swalaah Ya Ijumaa Ni Rakaa Mbili

 

Si nne zilizopunguzwa. Ni kwa Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khattwaab aliyesema: “Swalaah ya Adhw-haa ni rakaa mbili, na Swalaah ya Fitri ni rakaa mbili, na Swalaah ya Safari ni rakaa mbili, na Swalaah ya Ijumaa ni rakaa mbili kiukamilifu bila kupunguza kwa ulimi wa Nabii wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/232), Ibn Maajah (1063) na Ahmad (1/37). Angalia Al-Irwaa (3/106)].

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba Swalaah ya Ijumaa ni rakaa mbili.

 

· Kilichosuniwa Kusomwa Kwenye Swalaah Ya Ijumaa

 

Imepokelewa toka kwa Raafi’i kwamba Abu Hurayrah aliswalisha Ijumaa, na akasoma baada ya Suwratil Jum-’ah katika rakaa ya pili: (( إذا جاءك المنافقون)) . Akasema: “Nikamwahi Abu Hurayrah wakati alipoondoka nikamwambia: Wewe umesoma Suwrah mbili ambazo ‘Aliy bin Abiy Twaalib alikuwa akiziswalishia huko Kufa”. Abu Hurayrah akasema: “Hakika mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah akiziswalishia Siku ya Ijumaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (877), At-Tirmidhiy (519), Abu Daawuud (1121) na Ibn Maajah (1118)].

 

Na imepokelewa toka kwa An-Nu’umaan bin Bashiyr akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasoma kwenye ‘Iyd Mbili na kwenye Ijumaa: سبح اسم ربك الأعلى na هل أتاك حديث الغاشية  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (878), At-Tirmidhiy (533), Abu Daawuud (1122) na An-Nasaaiy (3/112)].

 

· Aliyetanguliwa Katika Swalaah Ya Ijumaa

 

Atakayefika katika Swalaah ya Ijumaa, atajiunga na imamu katika hali yoyote atakayomkuta nayo. Na kama ataipata rakaa moja pamoja na imamu [kwa mujibu wa makhitilafiano tuliyoyazungumzia kuhusu upatikanaji wa rakaa], basi ataiongezea nyingine baada ya imamu kutoa tasliym. Na kama hakuzipata rakaa mbili kama kuwakuta wako kwenye sijdah au kwenye kikao cha tashah-hud [au kwenye rukuu kwa yule asiyehesabu kwamba rakaa inapatikana kwenye rukuu] katika rakaa ya pili, basi huyo ataswali nne. Hili ndilo walilolifutu Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Mtu akiipata rakaa Siku ya Ijumaa, basi atakamilisha na nyingine moja, na kama atawakuta wako tashah-hud, basi ataswali nne”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5471), Ibn Abiy Shaybah (2/37) na Al-Bayhaqiy (3/204)].

 

Imepokelewa pia toka kwa Ibn Mas-’oud akisema: “ Mwenye kuipata rakaa, basi ameipata Ijumaa, na ambaye hakuipata Ijumaa, basi aswali nne”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5477), Ibn Abiy Shaybah (2/37) na Al-Bayhaqiy (3/204)].

 

Aidha, Sheikh wa Uislamu ameisimulia toka kwa Anas akisema: “Hakuna Swahaba yeyote ajulikanaye kwamba amekwenda kinyume na hili, na ni wengi tu waliosema kwamba hilo ni Ijma’a ya Maswahaba”. Nalo pia ni kauli ya Jamhuri: Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na wengineo.

 

· Kufurika Msikiti Katika Swalaah Ya Ijumaa

 

1- Ikiwa mtu atakosa nafasi kutokana na kujaa Msikiti hadi pomoni, kama ataweza kurukuu na kusujudu kwa namna awezayo, basi atafanya hata kama ni juu ya mgongo wa mwenzake au kwa kuashiria. Hili litamtosheleza kwa kuwa ndio ukomo wa uwezo wake, na halitofautishwi na mtu kushindwa kurukuu au kusujudu kwa sababu ya ugonjwa, au vita na kadhalika. ‘Umar bin Al-Khattwaab kasema: “Msongamano ukizidi, basi na asujudu mmoja wenu juu ya mgongo wa nduguye”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5469), At-Twayalsiy (70), na kwa njia yake Ahmad (1/32) na Al-Bayhaqiy (3/183)].

Hii ni kauli ya Ath-Twawriy, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, Asw-haabu Ar-Raay na wengineo.

 

2- Msikiti ukisongeka, viwanja vyake vikajaa, na safu zikashikana, hapo inajuzu kuswali kwenye vichochoro, au nyumba zilizoshikana na safu, na hata juu ya paa la Msikiti. Na lau kama ukuta utazuia kati ya mtu na imamu au mfano wake, basi haidhuru. Na hili lishaelezwa katika mlango wa Swalaah ya Jamaa.

 

· Sunnah Baada Ya Ijumaa

 

Imesuniwa – baada ya Swalaah ya Ijumaa – mtu aswali rakaa mbili au nne, na kuswalia nyumbani ni bora zaidi. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayekuwa ni mwenye kuswali kati yenu baada ya Ijumaa, basi aswali baada yake rakaa nne [Na kama kitu kitakuharakiza, basi swali rakaa mbili Msikitini, na rakaa mbili ukirejea] )). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (822), Abu Daawuud (1131), At-Tirmidhiy (523), An-Nasaaiy (3/113) na Ibn Maajah (1132)].

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haswali baada ya Ijumaa mpaka aondoke na kuswali rakaa mbili nyumbani kwake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Humaydiy (976), na kutoka kwake Ibn Al-Mindhir (1878). Na asili yake ni katika Al-Bukhaariy (937) na Muslim (882)].

 

Mas-ala Mbalimbali

 

· Idadi Ambayo Kwayo Ijumaa Inaswihi

 

[Angalia Al-Awsatw (4/29), Al Maw-‘idhwat Al Hasanah cha Swiddiyq Khan na Al-Ajwibat Al-Hasanah uk. 76-78.].

 

Swalaah ya Ijumaa ni Faradhi kati ya Faradhi za Allaah Mtukufu, ni alama kati ya alama za Uislamu, na ni Swalaah kati ya Swalaah nyinginezo. Basi yeyote mwenye kushurutisha iwepo ndani ya Swalaah hii idadi zaidi ya ile ya kuruhusu kuswalika Jamaa, basi alete dalili, na dalili hakuna. Na la ajabu ni kuwepo kauli nyingi zilizosemwa katika kukadiria idadi inayotakikana hadi kufikia kauli kumi na tano. [Al-Haafidh amezitaja katika Al Fat-h (2/490)].

 

Katika kauli zote hizi, hakuna hata dalili moja iliyotolewa isipokuwa kauli isemayo: Hufanyika kwa idadi ya zinavyofanyika Jamaa nyinginezo, yaani kwa mtu mmoja pamoja na imamu. Iwaje? Na masharti yamethibiti kwa dalili maalumu zinazoarifu kwamba kama sharti haipo, basi mshurutishwa naye anakuwa hayupo. Kwa hiyo, kuthibitisha masharti hayo kwa kisicho dalili kimsingi, ni kujiingiza vibaya kwenye hatari, na uthubutu wa kumwongopea Allaah, Rasuli Wake na Sharia Yake.

 

Na lau kama Allaah Mtukufu Angelikuwa na muradi katika idadi fulani pasina nyingine, basi Angelibainisha hilo katika Kitabu Chake, au kupitia ulimi wa Nabii Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

· Sunnah Ni Kuwa Zisiswaliwe Ijumaa Kwenye Misikiti Mbalimbali Katika Mji Mmoja Ila Kwa Dharura

 

Dharura ni kama kutotosha Msikiti mmoja kutokana na wingi wa Waumini na mfano wa hilo. Na kama si hivyo, basi hapakukhitilafiwa ya kwamba Ijumaa haikuwa ikiswaliwa katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na katika enzi ya Makhalifa Waongofu isipokuwa katika Msikiti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tu, na haikuwa ikiswaliwa kwenye Misikiti mingine.

 

Ama tuyaonayo leo ya kukithiri kwa wingi Misikiti ambayo Ijumaa zinaswaliwa ikiwemo Misikiti midogo iliyoko barabarani na kwenye vichochoro jirani, huku pakiwepo uwezekano wa kuachana nayo kwa watu kwenda kuswali kwenye Misikiti mikubwa, basi bila shaka hili ni katika jambo lenye kuugawa umma huu mgawanyo wa kusikitisha, na kuitoa Ijumaa toka kwenye kiini chake. [Angalia: Al-Awsatw (4/116), Iswlaahu Al-Masaajid cha Al-Qaasimiy (uk. 60-62), Al-Mughniy (2/92) na Majmu’u Al-Fataawaa (24/208)].

 

· Ijumaa Na ‘Iyd Vikikutana Siku Moja

 

Ikikutana Siku ya Ijumaa na Siku ya ‘Iyd, Maulamaa wana kauli mbili kuhusu aliyeswali ‘Iyd siku hiyo:

 

Ya kwanza: Ni lazima aswali Ijumaa pia

 

Hii ni kauli ya Maulamaa wengi. [Al-Mudawwanah (1/153), Al-Majmu’u (4/320), Tabyiyn Al-Haqaaiq (1/224), At-Tamhiyd (10/272), Al-Awsatw (4/291) na Al-Muhalla (3/303)].

 

Lakini Mashaafi’i wameiondosha kwa wanavijiji tu na si kwa watu waishio mijini. Hoja za kauli hii ni:

 

1- Ujumla wa Kauli Yake Ta’alaa:

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))

(( Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua)). [Al-Jum-‘ah (62:9)].

 

2- Dalili zilizotangulia kuhusu wajibu wa Swalaah ya Ijumaa.

 

3- Kwa vile hizo ni Swalaah mbili za faradhi (juu ya kuwepo makhitalifiano kuhusiana na wajibu wa Swalaah ya ‘Iyd), basi faradhi moja haiwezi kuanguka kwa sababu ya nyingine kama Adhuhuri na ‘Iyd.

 

4- Ruksa ya kuacha Ijumaa kwa aliyeswali ‘Iyd, inawahusu wale tu waliowajibikiwa na Ijumaa katika wakazi wa majangwani na vijijini. Imepokelewa na Abu ‘Ubayd mwachwa huru wa Ibn Azhar akisema: “Niliswali ‘Iyd pamoja na ‘Uthmaan bin ‘Affaan, na hiyo ilikuwa Siku ya Ijumaa. Akaswali kabla ya khutbah, kisha akakhutubu akasema: Enyi watu! Hakika hii ni siku ambayo zimewakusanyikieni ‘Iyd mbili. Basi mwenye kutaka kuisubiri Ijumaa katika watu wa maeneo ya miinuko, basi na asubiri, na mwenye kupenda kurudi, basi nimemruhusu” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5572), Maalik (1/141), na kutoka kwake Ash-Shaafi’iy kwenye Al-Umm (1/239) na ‘Abdul Razzaaq (5732)].

 

Ya pili:

 

Atakuwa hana Ijumaa, lakini imesuniwa kwa imamu kuisimamisha ili aihudhurie mwenye kutaka na yule ambaye hakuwahi kuswali ‘Iyd.

 

Ni kauli ya Jamhuri ya Mahanbali, nayo imesimuliwa toka kwa ‘Umar, ‘Uthmaan, ‘Aliy, Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas na Ibn Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu Anhum). [Al-Mughniy (2/265), Al-Inswaaf (2/403), Kash-Shaaful Qinaa’a (2/41), na Majmu’u Al-Fataawaa (24/211)].

 

Kauli hii katika dalili yake, imetegemea Hadiyth mbili Marfu’u Dhwa’iyf pamoja na baadhi ya athar Swahiyh.

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa Iyaas bin Abiy Ramlah aliyesema: “Nilimshuhudia Mu’aawiyah bin Abiy Sufyaan akimuuliza Zayd bin Arqam akisema: Je, ulihudhuria pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Iyd Mbili zilizokutana siku moja? Akajibu: Ndio. Akauliza: Ni vipi alifanya? Akasema: Aliswali ‘Iyd, kisha akatoa ruksa kwa Ijumaa kwa kusema: ((Mwenye kutaka kuswali, basi aswali)). [Ni Dhwa’iyf mno: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1070), An-Nasaaiy (3/194) Ibn Maajah (1310) na Ahmad (4/372)].

 

2- Yaliyosimuliwa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika zimekusanyika katika siku yenu hii ‘Iyd Mbili. Basi mwenye kutaka itamtosheleza na Ijumaa, na sisi tutaswali Ijumaa)). [Ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1073), Ibn Maajah (1/13) na Al-Haakim (2/288). Maulamaa kadhaa wameitia dosari kama Ahmad, Ad-Daara Qutwniy na Ibn ‘Abdul Barri. Ina Hadiyth mwenza kwa Ibn Maajah (1312) toka kwa Ibn ‘Umar, na Sanad yake ni Dhwa’iyf].

 

3- Ni athar ya ‘Uthmaan iliyotangulia ambapo anasema: “Na mwenye kupenda kurudi, basi nimemruhusu”.

 

Ama kauli ya kundi la kwanza isemayo kwamba hili ni mahsusi kwa watu wa majangwani ambao Ijumaa kwao si wajibu, panaweza kuulizwa: “Ikiwa ni hivyo, basi nini faida ya kauli yake “nimemruhusu”?!

 

4- ‘Atwaa amesema: “ Ibn Az-Zubayr alituswalisha siku ya ‘Iyd katika siku ya Ijumaa mwanzoni mwa mchana. Kisha tukaenda Ijumaa naye hakutokeza, tukaswali peke yetu. Ibn ‘Abbaas alikuwa Taif, na aliporudi tulimwelezea hilo naye akasema: Ameipata Sunnah”. [Ibn Az-Zubayr akalisikia hilo na kusema: Nilimwona ‘Umar bin Al-Khattwaab zinapokutanika ‘Iyd Mbili, hufanya kama hivi]. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1071), toka kwa ‘Atwaa, An-Nasaaiy (3/194) na Ibn Khuzaymah (1465) toka kwa Wahab bin Kaysaan. Katika baadhi ya Sanad, kuna neno “ameipata” tu bila  neno “Sunnah”. Kulithibitisha hili kunahitajia utafiti zaidi. Alaa kulli haal, sisi tunatolea dalili kwa kitendo cha Maswahaba pale ambapo hakuna aliyekwenda kinyume miongoni mwao].

 

Na kauli ya Swahaba: Ameipata Sunnah, ina hukmu ya Umarufu’u kwa kauli yenye nguvu.

 

5- Katika kukitimiza kisa cha Ibn Az-Zubayr kupitia kwa Hishaam bin ‘Urwah toka kwa Wahab bin Kaysaan, Hisham amesema: “Nikalieleza hilo kwa Naafi’i, naye akasema: Lilielezwa kwa Ibn ‘Umar, naye hakulipinga”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/7)].

 

6- Imepokelewa toka kwa Abu ‘Abdul Rahmaan As-Sulamiy akisema: “Zilikutana ‘Iyd Mbili wakati wa ‘Aliy. Akawaswalisha Swalaah ya ‘Iyd, kisha akakhutubu juu ya mnyama wake akasema: Enyi watu! Aliyeswali miongoni mwenu ‘Iyd, basi ameiswali Ijumaa yake bila shaka”. Na katika riwaya nyingine: “Mwenye kupenda kuswali Ijumaa, basi aswali, na anayetaka kukaa, basi akae. [Sufyaan kasema: yaani akae nyumbani kwake]. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/7), ‘Abdul Razzaaq (5731) na Ibn Al-Mundhir (4/290)].

 

7- Wamesema: Hakuna katika Maswahaba hawa, aliyejulikana kwamba amekwenda kinyume na hukmu hii.

 

Jamhuri wamejibu kuhusu athar hizi wakisema kwamba zinachukulika kwa watu wa majangwani ambao Ijumaa kwao si wajibu!!

 

Ibn ‘Abdul Barri kasema: “Athar hizi zikibeba uwezekaniko wa taawiyl tuliyoitaja, basi haitojuzu kwa Muislamu kuipomosha faradhi ya Ijumaa kwa yule ambaye ni wajibu kwake”.

 

Ninasema: “Lenye nguvu ni kwamba Ijumaa hupomoka kwa aliyeswali ‘Iyd kwa mujibu wa athar tulizozitaja za Maswahaba, na kwa kutopatikana athar zenye kukhalifiana na hizi toka kwa yeyote kati yao. Na hii bila shaka inazatiti mwega wa Umarufu’u tukizingatia kwamba kauli ya Ibn ‘Abbaas “Ameipata Sunnah” ina hukmu ya Umarufu’u. Ama kuzibebesha athar zote hizi juu ya yule ambaye Ijumaa si wajibu kwake, basi hiyo ni wazi kuwa ni takilifu. Ikiwa athar ya ‘Uthmaan itakuwa salama, basi kwa mwingine inaweza isiwe salama kama inavyoonekana. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

· Imesuniwa Kwa Imamu Aitishe Ijumaa

 

Na hii ili aswali kwa mwenye kutaka na kwa yule ambaye hakuwahi kuswali ‘Iyd. Hili linapatikana toka kwenye Hadiyth iliyoelezwa nyuma ya An-Nu’umaan bin Bashiyr inayosema kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasoma katika Swalaah ya ‘Iyd na Swalaah ya Ijumaa Suwrat Al-A’alaa na Suwrat Al-Ghaashiyah. Anasema: “Na inapokutana ‘Iyd na Ijumaa katika siku moja, anazisoma Suwrah hizi mbili katika Swalaah mbili”. [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake imeshaelezwa].

 

· Aliyeswali ‘Iyd, Na Asiswali Ijumaa, Je Adhuhuri Kwake Ni Lazima?

 

Imekuja katika athar ya ‘Atwaa – katika kisa cha Ibn Az-Zubayr -: “Akaswali Ijumaa rakaa mbili baada ya Swalaah ya fitr, kisha hakuongeza juu ya Swalaah hizo mpaka akaswali Alasiri. Akasema: Ama Mafuqahaa, wao hawakuzungumza kuhusu hilo. Ama kwa asiye faqihi, yeye kakilaumu alichokifanya Ibn Az Zubayr. Akasema: Mimi hakika nilimlaumu kwa hilo, na nikaswali Adhuhuri siku hiyo, mpaka tulipokuja kujua kwamba ‘Iyd Mbili ilikuwa zinapokutana vile vile, huswaliwa Swalaah moja”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5725) na Abu Daawuud (1072) kwa ufupi].

 

Ash-Shawkaaniy kasema: “Inavyoonyesha ni kuwa hakuswali Adhuhuri, na kwa kuwa Ijumaa inapopomoka kwa njia kati ya njia za kuhalalisha, basi si lazima kuswali Adhuhuri kwa ambaye imempomokea. Ni wazi kwamba wanaosema hivyo ni wale wenye kusema kuwa Ijumaa ndio asili, na wewe unajua fika kwamba Alilolifaradhisha Allaah Mtukufu kwa Waja Wake katika Siku ya Ijumaa, ni Swalaah ya Ijumaa. Hivyo basi, kulazimisha Adhuhuri kwa aliyeiacha kwa udhuru au bila udhuru, kunahitajia dalili, na hakuna dalili ifaayo kuishikilia juu ya hilo kwa ninavyofahamu mimi”. [Naylul Awtwaar (3/336)].

 

Ninasema: “ Ama kuipomosha Adhuhuri kwa yule ambaye hakuswali Ijumaa baada ya kuwa ameswali ‘Iyd, mimi sijui kama kuna Swahaba yeyote aliyelikubali hilo. Na hii pakizingatiwa kuwa imekuja toka kwa ‘Atwaa mwenyewe akisema: “Zilikutana ‘Iyd Mbili katika enzi ya Ibn Az-Zubayr, akawaswalisha ‘Iyd, kisha akawaswalisha Ijumaa Swalaah ya Adhuhuri rakaa nne”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/7)].

 

Roho hairidhiki wala kutulia kwa kuipomosha Adhuhuri. Lililo bora ni mtu kwenda Ijumaa ili aondokane na mvutano huu. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Ijumaa Ikiwafikiana na Siku Ya ‘Arafah

 

Mahujaji hawaswali Ijumaa, bali wanaswali Adhuhuri na Alasiri kwa kukusanya na kupunguza. Na kabla ya hapo, imamu huwakhutubia khutbah ya ‘Arafah kama alivyofanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hayo yatakuja kwenye mlango wa Hijjah Insha Allaah.

 

 

Share