001-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Wanayoyafanya Waliopo Kwa Aliyekaribia Kukata Roho

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

001-Wanayoyafanya Waliopo Kwa Aliyekaribia Kukata Roho

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Wamkumbushe Shahaadah

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wakumbusheni watu wenu waliokaribia kukata roho “Laa ilaaha illa Allaah”)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (916), Abu Daawuud (3117), An-Nasaaiy (4/5), At-Tirmidhiy (976) na Ibn Maajah (1445)].

 

Makusudio ya Hadiyth ni kwamba mkumbusheni aliyekaribia kufa "لا إله إلا الله" ili liwe neno lake la mwisho. Ni kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Anas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwa mtu wa ukoo wa Bani Najjaar ili kumzuru. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Ee khali! Sema "لا إله إلا الله")). Akasema: Je, ni khali mimi au ami? Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Hapana, bali ni khali)). Akamwambia: ((Sema "لا إله إلا الله" )). Akasema: Je, ni bora  kwangu? Akasema: ((Na’am)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/152, 154, 268)].

 

 Na hii ni kwa matarajio ya kuwa neno lake la mwisho liwe "لا إله إلا الله" kabla ya kufa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtu ambaye neno lake la mwisho limekuwa "لا إله إلا الله" ataingia Peponi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3100)].

 

Maulamaa wote kwa pamoja wamekubaliana juu ya ukumbushaji huu. Ukumbushaji huu unatakikana ufanywe kwa upole na taratibu, na wala usikaririwe ili asidhikike. Akidhikika anaweza kulichukia hilo kwa moyo wake kisha akatamka yasiyofaa. Ikiwa atalitamka mara moja, basi asikaririwe tena isipokuwa tu kama atazungumza baada yake jambo jingine. Hapo atakumbushwa tena ili neno lake la mwisho liwe "لا إله إلا الله" . [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (2/580), Al-Majmu’u (5/110) na Al-Mughniy (2/450)].

 

· Zindusho

 

Maulamaa wamependezesha kuisoma Suwrat Yaasiyn kwa aliyekaribia kukata roho [Ibn ‘Aabidiyn (2/191), Ad-Dusuwqiy (1/423), Mughnil Muhtaaj (2/5) na Kash-Shaaful Qinaa (2/82)], wakitegemea yaliyosimuliwa kwa njia Marfu’u: ((Wasomeeni watu wenu waliokaribia kukata roho Suwrat Yaasiyn)), lakini ni Dhwa’iyf. Hivyo haiwezi kuruhusu hilo, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

2- Wamwelekeze Qiblah

 

Zimehadithiwa jumla ya Hadiyth Mursal zenye kutiliana nguvu kwa ujumla wake na kupanda kufikia ngazi ya Hasan ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowasili Madiynah, alimuulizia Al-Barraa bin Ma’aruur na watu wakamwambia kwamba ameshafariki, na kwamba aliamuru theluthi ya mali yake apewe Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na aelekezwe Qiblah wakati alipokuwa karibu kukata roho. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ameipata fitwrah, nami nimeirejesha theluthi yake kwa mwanaye)). Kisha akaenda akamswalia akasema: ((Ee Allaah! Mghufirie na Mrehemu, na Mwingize Pepo Yako, na hakika Ushafanya)). [Hadiyth Hasan kwa Sanad zake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/353) na Al-Bayhaqiy (3/384). Sheikh wetu katika kitabu cha Al-Ghuslu wal Kafan amesema ni Hadiyth Hasan katika ukurasa wa 22].

 

Na katika riwaya ya kisa hiki toka kwa ‘Abdul Rahmaan bin ‘Abdullaah bin Ka’ab bin Maalik amesema: “Al-Barraa bin Ma’aruwr alikuwa mtu wa mwanzo kuelekea Qiblah akiwa hai na maiti”.

Kuelekezwa huku Qiblah ni jambo linalopendeza kwa Jamhuri ya Maulamaa, bali An Nawawiy amenukulu Ijma’a juu ya jambo hili, lakini Sa’iyd Al-Musayyib (Allaah Amrehemu) amelikataa. Walipotaka kumwelekeza Qiblah alighadhibika na kusema: “Je, siko Qiblah mimi?” [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq katika Al-Muswannaf (3/391)].

 

Ingawa alipinga, lakini wengine walilikubali. Isitoshe, yeye hakupitisha kwa kukata kauli kwamba talqiyn kwa maiti ni bid-’a au ni haramu!! Kisha walichotaka kukifanya kwa Sa’iyd, ni dalili kwamba hilo lilikuwa mashuhuri kwao likifanywa na Waislamu wote kwa wafu wao. [Al-Mughniy (2/451), na Al-Ghuslu wal Kafan uk. 25].

 

· Namna Ya Kumwelekeza Qiblah

 

Maulamaa wana njia mbili kuhusiana na namna hii:

 

1- Alazwe chali miguu yake ikielekea Qiblah, na kichwa chake kinyanyuliwe kidogo ili kiwe mwelekeo wa Qiblah.

 

2- Alazwe kwa ubavu wake wa kulia uso ukielekezwa Qiblah. [Al-Majmu’u (5/116)].

 

Namna hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Linaloitilia nguvu ni pale Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Al-Barraa bin ‘Aazib: ((Ukienda kulala, basi tawadha kama unavyotawadha kwa ajili ya Swalaah, halafu lalia ubavu wako wa kulia. Ukifa, basi utakufa juu ya fitwrah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (244) na Muslim (2710)].

 

Ninasema: “Hili linatolewa ushahidi vile vile na Hadiyth ya Ummu Salamah kuhusu kisa cha kufariki Faatimah (Radhwiya Allaahu Anhaa). Inasema: Akalazwa kwa ubavu na akaelekezwa Qiblah, naye akaweka mkono wake chini ya shavu lake. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6/461). Sanad yake ina udhwa’iyf].

 

Na hii haiwi isipokuwa amelala kwa ubavu. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

 

Share