010-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Kuzika Maiti Na Yanayohusiana

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

010-Kuzika Maiti Na Yanayohusiana 

 

Alhidaaya.com

 

 

  • Hukmu Ya Kuzika Maiti

Kuzika maiti ni Fardhi ya Kutoshelezana hata kama maiti ni kafiri:

 

1- Ni kwa Hadiyth ya Abu Twalha: "Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru Siku ya Badr vigogo ishirini na nne wa Kikureshi watiwe kwenye kisima kati ya visima vya Badr". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (3976) na Muslim (2875)].

 

2- Tumezungumza nyuma kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia 'Aliy wakati Abu Twaalib alipokufa – kafiri -: ((Nenda ukamzike)). [Isnadi yake ni Laini: Takhriyj yake ishatajwa].

 

Muislamu hazikwi pamoja na kafiri, wala kafiri pamoja na Muislamu, bali Muislamu huzikwa kwenye makaburi ya Waislamu, na kafiri kwenye makaburi ya washirikina. Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na yakaendelea mpaka enzi yetu ya leo. [Angalia dalili za hilo kwenye mlango wa Hukmu Za Janazah].

 

· Akifa Mwanamke Mjamzito Wa Ahlul Kitaab Na Aliyemtia Mimba Ni Muislamu, Wapi Atazikwa?

 

Imamu Ahmad kasema: " Atazikwa kati ya makaburi ya Waislamu na makaburi ya Ahlul Kitaab. Yeye ni kafiri na hazikwi kwenye makaburi ya Waislamu, kwa kuwa watapata adha kutokana na kuadhibiwa kwake, na hazikwi kwenye makaburi ya makafiri, kwa kuwa mwanaye ni Muislamu atapata adha ya kuadhibiwa kwao. Hivyo atazikwa sehemu yake peke yake".

 

Wamesema: "Mgongo wake utaelekezwa Qiblah kwa kulazwa kwa ubavu ili uso wa mtoto uelekee Qiblah juu ya ubavu wake wa kulia, kwa kuwa uso wa mtoto unaelekea mgongo wa mama yake". [Al-Mughniy (2/563)].

 

· Sunnah, Ni Kuzikwa Kwenye Makaburi

 

[Ahkaamul Janaazah (uk 173 na zinazofuatia)]

 

Hii ni kwa vile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anazika maiti kwenye makaburi ya Al-Baqiy’i kama habari yakini zilivyotangaa kwa hilo kizazi kwa kizazi, na haikunukuliwa kuwa kuna Salaf yeyote aliyezikwa sehemu isiyo makaburi, isipokuwa tu habari yakini zilizotangaa kwamba Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) [na Maswahiba wake wawili] alizikwa kwenye chumba cha 'Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha), na hili ni spesheli kwao.

 

Pia, Mashuhadaa wa vita hawazikwi kwenye makaburi bali huzikwa mahala walipouawa, na hawapelekwi kuzikwa kwenye makaburi. Ni kwa Hadiyth ya Jaabir ya kwamba amati yake alimleta baba yake Jaabir na khali yake – baada ya kuuliwa vitani kishahidi- ili awazike kwenye makaburi. Akashtukiziwa na mtu ananadi: Ee! Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anawaamuruni muwarejeshe maiti muwazike pale walipofia. Akarudi nao, akawazika pale walipouawa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3149), An-Nasaaiy (4/79), At-Tirmidhiy (1771) na Ahmad (3/397)].

 

· Ni Karaha Kumzika Maiti Katika Nyakati Hizi Ila Kwa Dharura

 

1,2,3- Jua linapochomoza, linapokua utosini na linapozama

 

Ni kwa Hadiyth ya 'Uqbah bin 'Aamir aliyesema: "Nyakati tatu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatukataza kuswali au kuwazika maiti wetu: Wakati jua linapochomoza dhahiri bayana mpaka linaponyanyuka, jua linapolingamana sawasawa katikati ya mbingu mpaka lipinduke, na jua linapokurubia kuzama mpaka lizame". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Muslim (831), Abu Daawuud (3176), At-Tirmidhiy (1035) An-Nasaaiy (1/275), Ibn Maajah (1519)].

 

4- Wakati wa usiku bila dharura

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir: " Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaja mtu mmoja katika Maswahaba wake aliyekufa, akavikwa sanda isiyomtosha, akazikwa usiku. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakemea mtu kuzikwa usiku mpaka aswaliwe isipokuwa mtu akilazimika kufanya hivyo".  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Muslim (943), Abu Daawuud (3148) na Ahmad (3/295-329)].

 

Sababu ni kuwa kuzika usiku kuna uhakika mkubwa wa kupatikana idadi ndogo ya wenye kumswalia maiti. Na kwa ajili hiyo, imekatazwa kuzika usiku ili aswaliwe mchana, kwa kuwa mchana watu wanakuwa na uchangamfu wa kumswalia maiti. Ikiwa watalazimika kumzika usiku kutokana na kuchelea kuharibika kutokana na joto au mfano wake, basi itajuzu kumzika hata kwa kutumia taa na kuteremka nayo kaburini. Ni kwa Hadiyth ya Ibn 'Abbaas: "Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimzika mtu kwenye kaburi lake usiku, na taa ikawashwa katika kaburi lake" [Al-Albaaniy kasema ni Hasan: Imefanyiwa "ikhraaj" na At-Tirmidhiy (1064)].

 

· Sifa Ya Kaburi

 

1- Ni vizuri kaburi liwe na kina cha kutosha, pana na zuri

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu maiti wa Uhud: (( Chimbeni, panueni, nendeni chini na tengenezeni vizuri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3199), At-Tirmidhiy (1766) na An-Nasaai (4/8)].

 

2- Inajuzu kuchimba mwanandani au “shaqqu” kwenye kaburi, na mwanandani ni bora zaidi

 

Mwanandani ni mpasuo pembeni ya kaburi mwelekeo wa Qiblah. Na “shaqqu” ni kaburi au shimo lichimbwalo kwenda chini (kama mto).

 

Yote mawili yalifanywa wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na mwanandani ni bora zaidi, nayo ndiyo Allaah Aliomchagulia Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki, Madiynah kulikuwa na mtu anayechimba mwanandani na mwingine shaqqu. Wakasema: Tumtake istikhaarah Mola wetu, na tutume watu wawaite, na yeyote atakayekuja mwanzo, basi tutamwachia. Wakaenda kuitwa, na mwenye kuchimba mwanandani akawahi kuja, nao wakamchimbia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwanandani”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Maajah (1557) na Ahmad (3/99)].

 

Na imepokelewa toka kwa Sa’iyd bin Abiy Waqqaas kwamba amesema: “Nichimbieni mwanandani, na nisimikieni tofali juu ya kaburi langu kama alivyofanyiwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Muslim (966), An-Nasaaiy (1998) na Ibn Maajah (1556)].

 

An Nawawiy kasema: “ Maulamaa wamekubaliana kwamba kuzika kwenye mwanandani na shaqqu kunajuzu. Ikiwa ardhi ni ngumu udongo wake hauporomoki, basi mwanandani ni bora kutokana na dalili zilizotangulia, na kama ni laini unaoporomoka, basi shaqqu ni bora”. [Al-Majmu’u Sharhul Muhadh-dhab (5/287)].

 

· Ni Nani Anayezika?

 

1- Wanawake haifai kuzika wafu:

 

[Kutoka kitabu changu cha Fiqhu As Sunnah Lin Nisaai (uk. 198) chapa ya At-Tawfiyqiyyah].

Lililozoeleka wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na ambalo Waislamu wamekuwa wakilifanya mpaka hivi leo, ni wanaume kusimamia kazi ya kuzika. Wanaume ndio wenye uwezo zaidi wa kulifanya hilo, na kama wanawake watalifanya, basi inaweza kusababisha kufichuka sehemu za mwili wao mbele ya ajanibu, na hili halijuzu. Lililowazi zaidi kuliko haya yote ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtanguliza Abu Twalha ili amzike binti yake – na Abu Twalha si maharimu yake – kama itakavyokuja mbele, na Rasuli hakuwatanguliza wanawake. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

2- Ni nani mwenye haki zaidi ya kuzika maiti?

 

Mawalii wa maiti na akaribu zake ndio wenye haki zaidi ya kumteremsha kaburini. Na hii ni kwa ujumuishi wa Neno Lake Ta’alaa:

((وَالَّذِينَ آمَنُوا مِن بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَـٰئِكَ مِنكُمْ ۚ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ))

((Na wale walioamini baada (ya hijra) na wakahajiri na wakafanya jihaad pamoja nanyi; basi hao ni miongoni mwenu. Na ndugu wa uhusiano wa damu wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (kwa kurithiana), katika shariy’ah ya Allaah. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila kitu)). [Al-Anfaal (8:75)].

 

Na kwa Hadiyth ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Nilimwosha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nikaanza kuangalia uchafu anaokuwa nao maiti, nami sikuona kitu. Alikuwa msafi akiwa hai na maiti. Na waliosimama kumzika na kumteremsha kaburini ni watu wanne tu: ’Aliy, Al-Abbaas, Al-Fadhwl, na Swaaleh mwachwa huru wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli wa Allaah alichimbiwa mwanandani, na alisimikiwa tofali juu ya kaburi lake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Haakim (1/362), na kutoka kwake Al-Bayhaqiy (4/53). Ina Hadiyth wenza].

 

3- Nani wa kumwingiza mwanamke kwenye kaburi lake?

 

(a) Maharimu wake: Ni kwa ujumuishi wa Aayah iliyotangulia, na kwa Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin Abziy: “Kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) alipiga takbiyrah nne kumswalia Zaynab binti Jahsh, kisha akatuma mtu kwenda kuwauliza wake wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni nani atakayemwingiza Zaynab kwenye kaburi. Wakamjibu: Ni yule aliyekuwa akiingia nyumbani kwake bila kizuizi wakati wa uhai wake”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Abiy Shaybah (3/324) na Al-Bayhaqiy (4/53)].

 

(b) Mumewe: Ana haki zaidi kuliko mtu wa kando. Tumetangulia kusema nyuma kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ‘Aaishah: (( Nimependa kwamba hilo liwe nami ni hai, nikakuosha na kukukafini, na nikakuzika)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishatajwa kwenye mlango wa mwanamume kumwosha mkewe].

 

3- Ni sharti kwa anayemzika maiti asiwe amemwingilia mkewe usiku huo

 

Mwanamume wa kando ajnabi atatangulizwa kumzika maiti badala ya maharimu au mume kama alimwingilia mkewe usiku huo. Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “ Tulihudhuria mazishi ya binti ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekaa juu ya kaburi, nikaona macho yake yanatoa machozi, naye akasema: ((Je, kuna yeyote kati yenu hakumwingilia mkewe usiku?)). Abu Twalha akasema: Mimi. Akasema: ((Basi teremka kwenye kaburi lake)). Akateremka kwenye kaburi lake, akamzika”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1342) na Ahmad (3/126)].

 

Imepokelewa toka kwa Anas kwamba: “Ruqayya alipokufa, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Asiingie kaburini mtu aliyemwingilia mkewe usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ahmad (3/370), na Al-Haakim (4/47) kwa Sanad Swahiyh].

 

· Namna Ya Kumlaza Maiti Kaburini

 

1- Sunnah ni kumwingiza maiti kwa upande wa inakolala miguu yake

 

Ni kwa Hadiyth ya Ibn Is-Haaq aliyesema: “Al-Haarith aliusia ‘Abdullah bin Yaziyd amswalie. Alimswalia kisha akamwingiza kaburini kwa upande wa inakolala miguu yake, na akasema: “Hii ni katika Sunnah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3195) kwa Sanad Swahiyh].

 

2- Alazwe maiti katika kaburi lake juu ya ubavu wake wa kulia, na uso wake uelekezwe Qiblah.

 

Haya ndiyo waliyoyafanya Waislamu tokea enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka hivi leo.

 

3- Aseme anayemlaza kwenye mwanandani: “Bismil-Laahi, wa’alaa Sunnat (au ‘alaa millati) Rasuwlil-Laah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3197), At-Tirmidhiy (1051) na Ibn Maajah (1550) kwa Sanad Swahiyh].

 

4- Je kaburi la mwanamke lisitiriwe kwa nguo watu wasione mpaka afukiwe?

 

Kuna Hadiyth Dhwa’iyf iliyosimuliwa kuhusiana na hili, lakini Ibn Qudaamah amesema katika Al-Mughniy (2/501): “Na je mwanamke kaburi lake hufunikwa kwa nguo? Hatujui makhitalifiano kati ya Maulamaa kuhusiana na kusuniwa hili [Kisha akaleta athar kuhusiana na hili toka kwa ‘Umar na Anas, halafu akasema:] Kwa kuwa mwanamke ni uchi, na hakuna dhamana ya kufichuka sehemu yake yoyote wakaiona waliopo…”.

 

5- Ni Sunnah kutupia mateko matatu ya mchanga baada ya kumaliza kuziba mwanandani

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimswalia maiti, kisha akamwendea maiti na akatupia mateko matatu upande wa kichwa chake”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Maajah (1565), na katika Al-Irwaa (751) kapitisha uSwahiyh wake].

 

6- Kaburi inyanyuliwe kidogo toka usawa wa ardhi ili ihifadhiwe, na ifanywe kuwa na mgongo

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichimbiwa mwanandani, na akasimikiwa tofali, na kaburi lake likanyanyuliwa kiasi cha shibri toka usawa wa ardhi”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Hibaan (2160) na Al-Bayhaqiy kwa Sanad safi].

 

Imepokelewa toka kwa Sufyaan At-Tammaar akisema: “Nilioona kaburi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ikiwa na mgongo”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1390)].

 

7- Kaburi itiwe alama kwa jiwe au mfano wake, ili azikwe mbele yake anayekufa katika jamaa wa maiti

 

Ni kwa Hadiyth ya Al-Muttwalib bin Hantwab aliyesema: “ Alipokufa ‘Uthmaan bin Madh-’uwn, jeneza lake lilitolewa akazikwa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru mtu mmoja amletee jiwe akashindwa kulibeba. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaliendea, akaikunja mikono yake…… kisha akalibeba na kuliweka kwenye kichwa chake. Akasema: “ “Unaliwekea kwalo alama ya kaburi ya ndugu yangu, nije kumzika atakayekufa katika jamaa zangu”.  [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa "ikhraaj" na Abu Daawuud (3205) na Al-Bayhaqiy (3/412)].

 

· Inajuzu Kuzika Maiti Wawili Au Zaidi Katika Kaburi Moja Kwa Dharura

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdillah akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anawakusanya wanaume wawili katika nguo moja katika maiti wa Uhud, kisha anauliza: “Ni yupi kati yao aliyehifadhi zaidi Qur-aan?” Anapoonyeshwa mmoja wa wawili hao, humtanguliza kwenye mwanandani na husema: (( Mimi ni shahidi juu ya hawa Siku ya Qiyaamah)), na huamuru wazikwe na damu zao, hawakuoshwa wala hawakuswaliwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1343), An-Nasaaiy (1/277), At-Tirmidhiy (1036), Abu Daawuud (3138) na Ibn Maajah (1514)].

 

Pia yaelezwa kuwa wakizikwa wawili na zaidi, hutangulizwa mbora wao.

 

· Mwanamke Huzikwa Pamoja Na Mwanamume Kwa Dharura

 

Imepokelewa toka kwa Wailah bin Al-Asqa’a (Radhwiya Allaahu Anhu): “ Kwamba ilikuwa wanaume na wanawake wakizikwa pamoja, mwanamume hulazwa kwenye kaburi mwelekeo wa Qiblah, na mwanamke hulazwa nyuma yake kwenye kaburi”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na ‘Abdul Razzaaq (6378). Kuna athar nyinginezo ziangaliwe kwenye Jaami’i Ahkaamun Nisaa (1/556)].

 

Ash-Shaafi’iy kasema kwenye Al-Ummu (1/245): “ Sipendi kabisa mwanamke azikwe pamoja na mwanamume. Lakini kama ni lazima kufanya hivyo na hapana budi, mwanamume atakuwa mbele na mwanamke nyuma yake, na kitawekwa kizuizi cha mchanga kati ya mwanamke na mwanamume kwenye kaburi”.

 

 

Share